JUMAPILI YA 4 YA
PASKA
JUMAPILI YA MCHUNGAJI MWEMA NA
KUOMBEA MIITO
“Vijana
wenu wataona njozi” (Matendo ya Mitume 2:17
Mdo 2: 14a. 36-41
|
1 Pet 2: 20b-25
|
Yn 10: 1-10
|
Picha ina thamani zaidi ya maneno 1000.
Bwana wetu Yesu Kristu alikuwa fundi wa kupiga picha akilini, wa kufundisha kwa
kuleta picha. Picha ya mchungaji: Yesu ni mchungaji. Si mchungaji tu ni
mchungaji mwema. Anatoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Yesu ni mlango. (Yohane
10:7). Wachungaji huko Uyahudi walilala mlangoni mwa pango walimo wanyama ili
kuzuia wanyama kama kondoo wasitoke pangoni na kuzuia wanyama wakali wasiingie
pangoni. Yesu ni lango kuelekea kwa Baba.
Mtume Petro naye alikuwa bingwa
wa kupiga picha akilini na kutumia lugha ya picha. “Maana mlikuwa kama kondoo
waliopotea, lakini sasa mmemrudia mchungaji na msimamizi wa roho zenu” (1 Petro
2:25). Tunaona picha ya mchungaji na msimamizi. Tumuuige Bwana Yesu Kristu na
mtume Petro tuwe mafundi wa kupiga picha ya wito tunaoutamani.
Piga picha akilini unataka kuwa
nani. Kupiga picha akilini ni namna ya kufikiria. “Namna yetu ya kufikiri
inatengeneza matokeo mazuri au mabaya,” alisema Stephen Richards. Wito wowote unaoutamani lazima uupigie picha.
Unatamani kuwa padre au mchungaji piga picha unahubiri, piga picha unaendesha
ibada. Unataka kufunga ndoa, piga picha unavikwa pete, piga picha ya arusi.
Unataka kuwa daktari, piga picha unatibu mgonjwa, piga picha umevalia kama
daktari. Tunasoma hivi katika Biblia: “Vijana wenu wataona njozi” (Matendo ya
Mitume 2:17). Ni vizuri vijana kuwa na njozi, kuwa na ndoto. Kuna kitendawili
kisemacho: usiku mzima nimetazama filamu. Jibu ni ndoto. Vijana hawana budi
kuota ndoto za mchana. Ni kupiga picha ya kile unachokitaka, na unachokitamani.
Alfred A. Montapert alikuwa na haya ya kusema:
“Kufanya mambo makubwa lazima kwanza kuota ndoto, halafu piga picha,
halafu panga…amini…tenda!”
Suala la kuota ndoto na kupiga picha si la
vijana tu hata wazee. Tunasoma hivi katika Biblia: “Na Wazee wenu wataota ndoto”
(Matendo ya Mitume 2:17). Nakubaliana na Jack Youngblood aliyesema: “Napiga picha akilini ya mambo
kabla ya kuyafanya. Ni kama kuwa na karakarana akilini.” Kupiga picha akilini ni kuangalia ambavyo
havipo na havionekani. Tunaaswa hivi: ““Tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana”
(2 Wakorintho 4:18). Kardinali Polycarp Pengo wa Tanzania alipokuwa bado kijana
mdogo alienda Kanisani kusali. Siku hiyo ilikuwa ni kumbukumbu ya Mtakatifu
Polycarp Askofu na Shahidi. Baada ya kutoka Kanisani alimwambia mama yake kuwa
anapenda naye kuwa Askofu na shahidi. Mama yake alimwambia kuwa hawezi kuwa
Askofu kabla ya kuwa padre. Yeye alizidi kusisitiza kuwa Kanisani walisema
Polycarp alikuwa Askofu hawajazungumzia suala la padre. Kilichotokea ni
historia. Kijana huyo amekuwa Askofu na sasa ni Kardinali Polycarp Pengo. Huu
ni ushahidi wa hoja ninayoijenga: unavyofikiria ndivyo utakavyokuwa. Nakubaliana
na Robert Collier aliyesema: “Tazama
mambo kwa namna ambayo ungependa kuwa nayo badala ya jinsi yalivyo,” alisema.
Ukiwa
unaelekea mahali fulani ingawa haujafika unapiga picha kukoje. Ukiomba piga
picha Mungu atakupatia. Ili kupiga picha unahitaji macho ya imani. Biblia ina
mifano mingi kuhusu jambo hili. Walau tuuone mfano mmoja: Mungu akamleta nje
Abramu, akasema: “Utazame mbinguni,
uhesabu nyota, kama waweza kuzihesabu. Akamwambia: Ndivyo uzao wako
utakavyokuwa. Abramu akamwamini Bwana” (Mwanzo 15: 5-6). Mungu alimtaka
Abramu apige picha. Kuamini maana yake
ni mtu kuweka matumaini kwa Mungu hata kama hakuna ushahidi kwamba Mungu
atafanya kitu. Kwa macho Abramu hakuwa na mtoto. Kwa macho Abramu alikuwa
amezeeka. Kwa macho Sarah alikuwa amezeeka. Kwa imani uzao wao utakuwa kama
nyota.
Juu ya kisa cha Abramu Joel
Osteen alikuwa na haya ya kusema: “ Mungu alijua kuwa Abrahamu alihitaji picha
ya ahadi katika akili yake. Abarahamu na Sarah walikuwa wamezeeka na bila
mtoto, katika maumbile, ilikuwa hali ambayo haiwezekani. Lakini kila mara
Abrahamu alipotozama nyota, alikumbushwa ahadi ya Mungu. Alianza kuona ahadi
kupitia macho ya imani. Huwezi kuzaa
ndoto ambayo kwanza hujaiwazia. Lazima
huiwazie ndani mwako kupitia macho ya imani kabla ya kuitoa nje. Badili kile
unachokiona, utabadili kile unachozalisha.”
Omba “kama” kwamba”
Umepata
Yesu akawaambia,
Waketisheni Watu” (Yohane 6:
10). Yesu aliwataka watu wakae mkao wa
kula chakula “kama kwamba” chakula kimeishapatikana. Muujiza wa kuongeza mikate
ulikuwa haujafanyika lakini Yesu alitenda kama kwamba. Kuna wakristu katika
parokia moja hapa Tanzania walimuomba padre Jumapili iliyokuwa inafuatia iwe
siku ya kuomba kupata mvua. Wakristu hao walishangazwa na padre aliposema
hayuko tayari kufanya maombi ya kuomba mvua kwa vile wakristu hawakwenda na
miavuli ya kujikinga na mvua. Suala la kuwa na miavuli linadokeza maana ya
“kama kwamba.” Yesu aliwambia wakoma kumi waende wajioneshe kwa makuhani kama
kwamba wamepona. Bikira Maria aliwaambia watumishi: lolote atakalowambieni
fanyeni “kama kwamba” Yesu amekubali.
Piga picha ya kile unachokitaka.
Bila shaka Bwana Yesu Kristu alipiga picha ya muujiza, picha ya ongezeko la
samali wawili na mikate mitatu. Suala la
kupiga picha ni muhimu ili ufanikiwe. “Akamleta (Abramu) nje akasema:Utazame
mbinguni, uhesabu nyota, kama waweza kuzihesabu.Akamwambia: Ndivyo uzao wako
utakavyokuwa” (Mwanzo 15:5). Mungu alisisitiza umuhimu wa kupiga picha.
Linda vizuri mawazo yako, mawazo yako
yanasikika Mbinguni. Ukifikiria kuwa tajiri, na mwaminifu, mawazo hayo
yanasikika mbinguni. Ukifikiria kuwa maskini na myonge, mawazo hayo yanasikika
mbinguni. Ukifikiria kuwa mtakatifu au kutenda dhambi, mawazo hayo yanasikika
mbinguni. Mtu anayefanikiwa maishani ni mshindi. Mtu ambaye anashindwa maishani
ni mshinde. Mshindi anasema ni jambo gumu lakini linawezekana. Mshinde anasema,
linawezekana lakini ni jambo gumu sana . Mshindi anaona jibu kwa kila swali.
Mshinde anaona swali katika kila jibu. Mshindi ni sehemu ya jibu. Mshinde ni
sehemu ya tatizo. Mshindi anaona jambo zuri katika kila shida. Mshinde anaona
shida katika kila jambo zuri. Marehemu Edward Cole alipokuwa meneja wa Kampuni
General Motors aliulizwa swali, “Jambo gani linakufanya uwe tofauti na watu
wengine – kwa nini umefanikiwa kuliko maelfu ya watu na kupata kazi ya juu sana
katika General Motors?” Bwana Edward
Cole alifikiri kwa muda na kujibu, “Napenda matatizo!” Katika matatizo aliona
jibu. Uwe na ndoto kubwa hata kama kuna matatizo kama Yozefu wa Agano la Kale.
“Usiku mmoja, Yozefu aliota ndoto, lakini alipowasimulia ndugu zake, wao
wakazidi kumchukia” (Mwanzo 37: 5). Ukiwa na ndoto kubwa utachukiwa lakini
usikate tamaa. Yozefu alifanikiwa. Kwa Mungu hakuna lisilowezekana. Ulivyo sasa
ni matokeo ya mawazo na fikira zako. Juhudi ukijumlisha na ndoto kubwa
ukajumlisha na Mungu ni sawasawa na mafanikio.
Mafanikio yako ya kesho yanategemea jambo unalolifikiria leo.
Nakubaliana na James Allen aliyesema, “Leo
upo pale ambapo mawazo yako yamekuleta; kesho utakuwa pale ambapo mawazo yako
yatakupeleka.”
Usitazame pale tu ulipo tazama na
pale unapoweza kuwa. Usitazame chini ulipo tazama na juu unapoweza kuwa.
Usifikirie jinsi ulivyo, fikiria unavyoweza kuwa. Yesu alimwambia Simoni mwana
wa Yohane, “Wewe ni Simoni mwana wa Yohane. Sasa utaitwa Kefa” (Yohane 1: 42).
Kefa ni Petro, yaani Mwamba. Yesu
alimtia moyo Simoni awe na picha ya mwamba. Alimtia moyo afikirie kuwa yeye ni
mwamba. “Watu wana namna ya kuweza
kubadilika wakawa unavyowatia moyo wawe na sivyo unavyowasumbua wawe,”
alisema Scudder N. Parker.
“Mtu anavyofikiria katika akili yake anakuwa hivyo, na anavyochagua
anakuwa hivyo” (Methali 23: 7). Zig ziglar alisema, “picha unayochora katika akili yako, akili yako itaifanyia kazi ili
kuifanikisha. Unapobadili picha zako unabadili na utendaji.” Kila kitu ambacho unaongeza na kufungia kwa
maneno haya “mimi ni ....” Utageuka kuwa hivyo. Jibariki kwa maneno haya: Mimi
ni mwema. Mimi ni mwaminifu. Mimi ni tajiri. Mimi ni mvumilivu. Mimi ni
mchapakazi. Mimi ni mcha mungu. Mimi ni mwamba. Mimi ni mzuri. Mimi ni mwenye
busara. Mimi ni mwenye heshima. Mimi ni mpole. Mimi ni mtoto wa Muungu.Mimi ni
kisura, Mungu haumbi takataka. Mungu haumbi mtumba.
Mtu ni watu. Watu wanatujenga au
wanatubomoa. Picha tuliyonayo, tunavyojiona uenda imetoka kwa watu wengine,
imetoka kwako, imetoka kwa neno la Mungu, imetoka kwa wazazi, imetoka kwa
shetani. Lakini Yesu ana picha yake, Yesu anaona uwezekano, yanayowezakana,
unayoweza kufanya. Mwanamke alikuwa anamuuliza mme wake, “Sijui huko mbinguni
patakuwepo na nguo za gharama sana za wanawake?” Mme wake akajibu, “ Unataka
kuniambia tukiwa mbinguni nitaangaika kutafuta pesa za kukununulia nguo.”
Mwanamke akamjibu, “Usiwe na wasiwasi, usiogope, wewe hautakuwa huko.” Maneno
kama hayo hayamuinui mwanaume.
Afadhali adui mzuri kuliko rafiki
mbaya. Niambie rafiki yako nitakwambia tabia yako. Simoni Petro alikuwa na
ndugu yake Andrea. Hawa hawakuwa tu ndugu bali walikuwa marafiki. Andrea
alimleta Simoni Petro kwa Yesu. Andrea alimpa Simoni Petro picha nzuri. Kuna
picha inayotoka kwa marafiki zetu. Wanavyotuona na sisi inatujengea picha tunavyojiona.
Andrea alimuona Simon Petro kama mtu anayeweza kuwa mfuasi mzuri wa Yesu
akamleta kwa Yesu. Katika maisha ungekuwa juu lakini marafiki zako wanapicha ya
kukuweka chini. Ungekuwa mbali lakini picha kutoka kwa marafiki zako ni ya
puani. Picha ya Andrea ilikuwa ya juu.
Marafiki ambao hawakusaidii kuwa
kama Yesu anavyotaka uwe, marafiki ambao hawakuinui wakiamua kukuacha waache
waende: “WATU HAO WAMETOKEA KATI YETU LAKINI HAWAKUWA WA KWETU NA NDIYO MAANA
WALITUACHA; KAMA WANGALIKUWA WA KWETU, WANGALIBAKI NASI. LAKINI WALIONDOKA,
WAKAENDA ZAO, KUSUDI IONEKANE WAZI KWAMBA HAWAKUWA KAMWE WA KWETU” (I Yohane 2:
19).