JUMAPILI YA 6 YA PASKA
1. Mdo 8: 5-8, 14 -17
|
2. 1 Pet 3: 15-18
|
3. Yn 14: 15-21
|
“Mwe tayari sikuzote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za
tumaini lililo ndani yenu” (1 Pet 3: 15).
Kuna aliyekuwa anagonga jiwe kwa nyundo ili alivunje vipande vipande.
Aligonga mara mia moja jiwe halikunjika akakata tamaa. Mwenzake waliyekuwa
wanafanya kazi hiyo pamoja alikuja na kugonga jiwe mara moja liwe lilivunjika.
Iliitajika mara ya mia na moja jiwe livunjike lakini mgongaji wa kwanza alikata
tamaa. Kukata tamaa ni mwisho wa matumaini. Mtume Petro anatutaka tuikie wito
huu: “Mwe tayari sikuzote kumjibu kila
mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu” (1 Pet 3: 15). Tumaini
lililo ndani yetu ni hili: Maisha pamoja
na Yesu ni matumaini yasiyo na mwisho, bila yeye, ni mwisho usio na matumaini. Tumaini
letu ni hili: “Sitawaacha ninyi yatima” (Yn
14: 15-21). “Matumaini hayamuui yeyote.” Hii ni methali ya Kongo. Ingawa
matumaini hayaliwi kama chakula hatuwezi
kuishi bila matumaini. “Matumaini ni
nguzo ya dunia.” Ndivyo isemavyo methali ya Kiafrika. Matumaini ni kumpokea
Roho Mtakatifu. “nao wakampokea Roho Mtakatifu” (Mdo 8: 17). Kukata tamaa ni
kumkataa Roho Mtakatifu.
MATUMAINI NI MTAZAMO CHANYA
Watu wanapokwambia, “Kata tamaa,”
matumaini yanasema, “jaribu tena.” Watu
wanapokwambia, “nusu glasi haikujaa,”
matumaini yanasema, “nusu glasi imejaa.” Watu wanapokwambia, “matatizo
ni mengi,” matumaini yanasema, “yana
mwisho” Watu wanapokwambia, “mlango wa kazi umefungwa,” matumaini yanasema, “Mungu anafungua mlango
mwingine.” Siku moja nilikutana na msichana niliyesoma naye Chuo Kikuu. Alikuwa
na mimba. Aliniambia Mungu amemfungulia mlango, dirisha na madirisha madogo.
Niliuliza namna gani aliniambia kuwa baada ya kumaliza masomo chuo kikuu
alipata kazi. Pili alimpata mme bora. Tatu alikuwa na mimba. Mungu wetu si kuwa
anaweza kukufungulia mlango tu bali anaweza kukufungulia milango na madirisha.
Endelea kuvumilia na endelea kuamini ukitafuta suluhisho la shida. Endelea
kutumaini.
MATUMAINI NI SILAHA
Shetani alitumia mateso, misiba,
balaa, na mikosi kumkatisha Ayubu tamaa. Lakini ayubu hakukata tamaa. “Hapo
Shetani akaondoka mbele ya Mwenyezi Mungu, akamtesa Ayubu...Mkewe akamwambia,
‘Bado tu ungali ukishikilia unyofu wako? Mtukane Mungu, ufe? Ayubu akamjibu
mkewe, “...Tukipokea mema kutoka kwa Mungu, kwa nini tukatae kutoka pia mabaya
kutoka kwake?” (Ayubu 2: 7-10). Ayubu alitumia silaha ya matumaini kwa Mungu
katika mapambano yake na shetani. Matumaini yamebeba uvumilivu. Mvumilivu hula
mbivu. Kupata pancha sio mwisho wa safari.
Matumaini yamebeba subira. Subira yavuta heri.
YESU NI SHUJAA WA MATUMAINI
Maisha pamoja na Yesu ni matumaini yasiyo na mwisho, bila yeye, ni
mwisho usio na matumaini. Yesu alipokuwa msalabani alivumilia sababu
alikuwa na matumaini katika ufufuko na katika ushindi. Makuhani wakuu,
waandishi, na wazee walimcheka wakisema, “Aliwaokoa wengine, kujiokoa mwenyewe
hawezi. Kama ni mfalme wa Israeli, basi ashuke
sasa msalabani, nasi tutamsadiki” (Mathayo 27: 42). Yesu hakushuka toka
msalabani. Ni kama unamwambia askari atoke uwanja wa vita ili umwamini kuwa ni
askari. Ni kama unamwambia mwanandoa atoke kwenye ndoa ili umwamini kuwa
ameolewa. Ni kama unamwambia mwanafunzi aache shule ili umwamini kuwa yeye ni
mwanafunzi. Yesu hakushuka toka msalabani alivumilia. Matunda yake ni kwamba
kwa uvumilivu wake alituonyesha njia.Hakuna Jumapili ya Paska bila Ijumaa Kuu.
Alitukumboa. Fikiria stampu kwenye barua. Manufaa yake yapo katika uwezo wake wa
kubaki kwenye bahasha mpaka bahasha imfikie mlengwa. Huo ni mfano wa
nguvu ya uvumilivu wa kulishughulia jambo kwa muda mrefu bila kuliacha.
MATUMAINI NI HITAJI LA BINADAMU
Matumaini yetu yawe kama nywele na
kucha. Haijalishi unazikata mara ngapi haziachi kuota. Hata ukiwa kwenye
matatizo kuwa na matumaini. Matatizo ni giza la kukusaidia kuona nyota. Katika giza la matatizo uwe na matumaini.
Ukitembea usiku wenye giza unaona nyota.
Katika mtazamo huo Stephanie Meyer
alisema: “Napenda usiku. Bila giza tusingeona nyota.” Katika matatizo unahitaji kuwa na matumaini.
Usikatishwe tamaa na giza la maneno ya kukukatisha tamaa. Baba wa Uchimbaji
mafuta Edwin L. Drake aliambiwa mwaka 1859: “Unataka kuchimba mafuta?
Unamaanisha kuchimba ardhi ukitafuta mafuta utakuwa umerukwa na akili!”
Kilichofuata ni historia bwana huyo hakusikiliza maneno ya kukatisha tamaa.
Katika yote unahitaji matumaini. Ni kweli alivyosema Louise Phillipe:
“Giza linapokuwa giza nene, nyota inaangaza sana.”
Biblia yasema: “Kabila lililotembea
gizani limeona nuru kuu” (Isaya 9:2). Katika kutembea gizani unaweza kuona
nyota. Wana wa Israel waliogandamizwa na kuteswa katika giza la mateso waliona
nuru kuu. “Nyakati za balaa mbaya sana
na machafuko zimekuwa nyakati za uzalishaji kwa watu wanaofikiri sana. Chuma
kisichokuwa na uchafu kinatolewa penye joto jingi sana. Radi inayoangaza sana
inatokana na wingu na dhoruba jeusi sana,” alisema Charles Caleb
Colton. Kumbe matatizo ni giza la
kusaidia kuona nyota. Vitu vingi vimevumbuliwa kutokana na matatizo. Waisraeli
katika matatizo makubwa ya ukame wamegundua kilimo cha umwagiaji kwenye shina
la mche tu. Wanazalisha matunda na kuuza nchi za nje nchi yenye ukame. Katika
matatizo ya giza umeme umevumbuliwa. Tulizoea kusema barua nu nusu ya kuonana.
Katika matatizo ya kutoonana sasa kumevumbuliwa namna ya kuonana kupitia Skype. Sio vizuri kuwa na matatizo
ukabweteka. Pengine si vizuri sana kuongejea giza ili uone mwanga. Methali ya
Kifaransa inasema: “Yeye anayengojea
kuvaa viatu vya marehemu anaweza kutembea pekupeku kwa muda mrefu.”
Katika matatizo makubwa tunaweza
kutambua uwepo wa Mwenyezi Mungu. Tunaweza kumwona Mungu. Biblia yasema:
“Usifurahi juu yangu, ewe adui yangu, maana nikianguka, nitasimama tena,
nikikaa katika giza, Bwana ni mwangaza wangu” (Mika 7:8). Katika giza utamwona
Bwana mwangaza wako. Matatizo uliyonayo ni mwaliko wa kuwa na matumaini. Geuza
hasi iwe chanya. Badili sumu iwe dawa. Badili jangwa liwe msitu. Badili mlima
uwe tambarare. Penye giza washa mshumaa. Penye chuki panda upendo. Katika mto
usiopitika jenga daraja.
Matumaini yawe mtaji wako na raslimali
yako kwamba inawezekana. Matumaini
yatakuletea furaha katika giza la matatizo. “Kwa tumaini,mkifurahi katika
dhiki, mkisubiri” (Warumi 12:12). Matumaini yetu yaendane na hali halisi
yasionekane kama kichekesho. Kuna mpagaji
aliyeulizwa: “Lini utalipa malimbikizo ya kodi ya chumba?” Alijibu: “Muda mfupi
baada ya kupokea cheki ambayo
mchapishaji wa kitabu changu atanipa nitakulipa. Hii itategemea kama
atakubali kuchapisha kitabu hicho
ambacho napanga kuandika nitakapapata jambo la kuandika juu yake na wazo
fulani.” Ndoto zifanyiwe kazi. Kama una ndoto ya kujenga ghorofa angani
anza kujenga msingi kuanzia chini. “Si kwamba mambo ni magumu ndio maana
hatuthubutu, ni kwa sababu hatuthubutu ndiyo maana mambo ni magumu,” alisema
mwanafalsafa Seneca.
“Namna tunavyoona tatizo ni tatizo,”
alisema Stephen R. Covey. Unaweza kuona tatizo ni giza tu. Namna hiyo ya kuona
ni tatizo. Lakini unaweza kuona tatizo kama giza la kukusaidia kuona nyota.
Kumbe tatizo si tatizo. Tatizo ni namna tunavyoliona tatizo. Nchi zilizoendelea
zimekabiliana na matatizo makubwa kwa mtazamo ambao si tatizo. Tunaweza kusema
matatizo makubwa maendeleo “makubwa”. Mateso mengi na neema nyingi. Kumbuka
kuwa penye matatizo kuna neema. Penye hasi kuna chanya. Penye kivuli kuna
mwanga. Painapo ndipo painukapo.
USIKATE TAMAA PANCHA
SIO MWISHO WA SAFARI
La kuvunda halina ubani. Maji
yakimwagika hayazoeleki. Ni methali za kukatisha tamaa. Methali hizi zina
maana kuwa jambo likiharibika haliwezi
kurekebishwa. Harufu mbaya ya uozo wa tabia haizuiwi. Kwa shetani la kuvunda
halina ubani. Kwa Mungu la kuvunda lina ubani. Kwa shetani maji yakimwagika
hayazoeleki, kwa Mungu maji yakimwagika yanazoeleka. “Hakuna jambo
lisilowezekana kwa Mungu.” (Luka 1: 37) Mbinu ya nne ambayo shetani huitumia
kuwafanya watu washindwe kutenda mazuri wengine wajiue ni kukata tamaa.
Shetani alitumia mbinu hii ya
kukata tamaa kwa Yuda Iskarioti ambaye alimuuza Yesu baadaye Yuda Iskarioti
alijiua. Tunasoma hivi katika Biblia, “Shetani akamwingia Yuda aitwaye Iskarioti...akaenda,
akajadiliana na makuhani wakuu na walinzi wa hekalu kuhusu atakavyomsaliti Yesu
kwao.” (Luka 22: 2-4) Maandiko haya yanasema Shetani alimuingia Yuda. Shetani
alitumia mbinu yake ya kukata tamaa. “Yuda...alipoona kwamba wamekwisha mhukumu
Yesu...akazitupa zile pesa hekaluni, akatoka nje, akaenda akajinyonga.”
(Mathayo 27: 3-5) Yuda Iskarioti aliona kuwa mipango yake imeharibika alikata
tamaa. Tatizo la dhambi ni kuwa mtu anaweza kuchukia hata zile pesa ambazo
hakupata kwa njia ya halali. Yuda alichukia zile pesa. Kama Yuda Iskarioti
angeomba msamaha tungekuwa na historia nyingine labda ya Mtakatifu Yuda
Iskarioti Msimamizi wa Benki, Msimamizi wa watunza pesa na Msimamizi wa Taasisi za Pesa. Alikata
tamaa na kukosa matumaini ya kusamehewa.
Kuna methali ya wamaasai isemayo,
“matumaini sio sawa na kukuta tamaa.” Mtu ambaye amekata tamaa hamlilii Mungu. Yuda
hakumlilia Mungu. Mtu aliyekata tamaa hatafuti na haombi msamaha. Maisha
yakikosa malengo yanakosa na maana. Namna hiyo sababu ya kuishi inaweza
kuponyoka toka mikononi mwa mtu. Matumaini ni kinyume cha kukata tamaa.