SHEREHE YA UTATU MTAKATIFU
1. Kut
34: 4b -6. 8-9
|
2. 2 Kor 13: 11 -13
|
3. Yn 3: 16 -18
|
Mungu wetu ni mkubwa. Yuko katika
nafsi tatu: Baba Mwana na Roho Mtakatifu. Ana nguvu. Nakubaliana na Andrew
Guzalds aliyesema: “Kuna nguvu zaidi katika neno moja kutoka kwa Mungu kuliko
maneno yote ya adui yakiwekwa pamoja.” Ukiwa na Mungu huko upande wa wengi. Sala
yako iwe hii: “Nakuomba ee Bwana wangu, ufuatane nasi” (Kutoka 34:9). Tafakari hadithi hii: Binti alimuaga mama
yake, “naenda matembezi na marafiki zangu.” Mama yake akamwambia: “Mungu awe
nawe katika Safari yako.” Kwa dharau na kiburi binti akajibu “mh mama gari
imejaa labda huyo Mungu akae kwenye buti kama anaweza. Kwa kasi akawasha gari
wakaondoka. Njiani wakapata ajali mbaya wote wakafa walitambuliwa tu kwa mavazi
waliyovaa! Polisi walipofungua buti wakakuta mayai trey 2 yakiwa salama kabisa!
Unajua kwa nini? Wewe Mungu umemweka wapi?
Kuna methali ya Wahaya wa Bukoba
isemayo: “Fanya urafiki na mkubwa anamaliza kabisa tatizo la kukosa kitoweo.”
Mungu mmoja katika nafsi tatu ni mkubwa fanya urafiki naye. “Kuna utupu au
ombwe lenye sura ya Mungu katika kila mtu ambalo linaweza kujazwa na Mungu,”
alisema Blaise Pascal.
Mungu wetu Mkubwa hata siku moja
usimwambie kuwa dhoruba yako ni kubwa, tatizo lako ni kubwa bali iambie
dhoruba: Mungu wangu ni mkubwa ni nafsi tatu, Mungu mmoja. Ukiwa na imani kwa Mungu
mmoja nafsi tatu, utaiondoa milima. Lakini ukiwa na hofu milima itakuondoa. Uwe
mwondoaji wa milima kwa kuamini katika Utatu Mtakatifu na kwa kusali hivi: “Nakuomba
ee Bwana wangu, ufuatane nasi” (Kutoka 34:9).
Mafiga mawili hayaivishi
chungu.Ni methali ya Kiswahili. Mafiga mawili hayawezi kukiivisha chungu;
lazima yawe matatu. Tutakapo kufanikiwa lazima tuwe tayari kushirikiana na
wenzentu. Katika mtazamo huu wazee wetu
walituachia busara: kidole kimoja hakivunji chawa. Jiwe moja haliinjiki chungu.
Kuna kitendawili cha Wafipa wa Tanzania kisemacho: Tatu tatu mpaka Ulaya. Jibu
ni mafiga. Haya ni mawe matatu. Ndoa inahitaji watatu: mme, mke na Mungu. Kwa
kumuungiza Mungu kwenye ndoa, ndoa inadumu. Ni katika msingi huu tunasema:
Familia inayosali pamoja hudumu pamoja. Umoja huu wa Utatu ni muhimu. “Kwa kuungana tunasimama; kwa kugawanyika
tunaanguka,” alisema John Dickson. Tafakari methali ya Tanzania isemayo: Mkono
mmoja haulimi shamba.
Siku zilizopita nilipokea ujumbe
katika simu wenye maneno haya: “Kuna siri gani katika namba 3? Shetani
alimjaribu Yesu mara 3. Yesu alianguka na msalaba mara 3. Petro alimkana Bwana
Yesu mara 3. Jogoo aliwika mara 3. Yesu alifufuka si ku ya 3. Wanawake walienda
kaburini siku ya 3 nao walikuwa 3. Matanga huanuliwa siku ya 3. Mafiga ya
kupikia huwa 3. Mashindanoni namba za ushindi ni 3. Nyakati zinagawanyika mara
3: wakati uliopita, uliopo na ujao. Wazo, neno na tendo vinakamilisha uwezo wa
binadamu navyo ni vitatu. Kuna nafsi 3 katika sarufi: Mimi, Wewe na Yeye. Nafsi
za Mungu ni 3: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Nini maana ya 3? Namba tatu ni
namba ya ukamilifu na utimilifu. Namba tatu inawakilisha kitu kizima, cha kweli
na kamilifu. Inadokeza uimara, uthabiti, uhakika.
Jumapili ya leo wakatoliki kote
duniani wanasherehekea Sherehe ya Utatu Mtakatifu. Inahusu imani kuwa Mungu ni
mmoja katika nafsi tatu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Ni kama mafiga matatu. Wakatoliki
hubatizwa kwa jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu na wala sio kwa
majina ya Baba na Mwana na Roho Mtakatifu. Hapa hakuna suala la hesabu za kujumlisha
ambapo moja kujumlisha na moja kujumlisha na mojo ni tatu. Ikumbukwe kuwa moja
kuzidisha na moja kuzidisha na moja ni
moja. Hapa hatuingizi hoja ya mahesabu. Ieleweke hivi mimi ukisoma makala yangu
kwenye gazeti unaniita mwandishi wa makala maalum (columnist), kanisani waumini
wananiita padre, chuoni wanafunzi wananiita mwadhiri. Hatuko watatu ni mmoja.
Katika kufanikisha mambo kuna
nguvu ya wingi au nguvu ya namba. Tunaona nguvu ya wingi katika uumbaji. “Mungu
akasema: Tumfanye mtu kwa mfano wetu, afanane nasi” (Mwanzo 1:26). Ni Utatu Mtakatifu uliosema “tumfanye mtu,” katika
kitabu cha Mwanzo. Inavyoonekana hata mwanzoni mwa Injili Utatu Mtakatifu
ulisema, “tumkumboe mtu.” Ili kufanikisha mambo. Ili kufanikiwa lazima
kufikiria katika msingi wa “sisi.” Nafsi
tatu zinafikiria katika msingi wa sisi. Nakubaliana na Ralph Chaplain Yusufu
aliyesema: “Hauwezi ukawa na usalama, hata ukijaribu namna gani; kama haufikiri
kwa msingi wa “sisi” badala ya mimi.” Lorii Myers alikuwa na mawazi hayo
aliposema: “Sisi ni sawa na nguvu.”
Kutatua tatizo la kutozaa la
Abrahamu na Sara palikuwepo na nguvu ya namba au nguvu ya umoja. “Mgeni
akamwambia, ‘Nitarudi kwako mwaka ujao, wakati huu; na hapo mkeo Sara atakuwa
na mtoto wa kiume” (18: 10). Sara na Abrahamu walikuwa wamezeeka lakini kwa
Mungu hakuna lisilowezekana. Abrahamu alitembelewa na utatu mtakatifu. Tafakari
vizuri haya hizi: “Bwana akamtokea Abrahamu” (Mwanzo 18: 1); “Akainua macho
akaona watu watatu wamesimama mbele yake” (Mwanzo 18:2). Ni Bwana mmoja halafu
watu watatu. Kutatuliwa tatizo la kutozaa ni ufunuo wa uwepo wa Mungu katika
nafsi tatu. Tunahitaji nguvu ya Utatu Mtakatifu tufanikiwe ambayo inaelezwa
katika somo la pili: “Neema ya Bwana Yesu Kristo, na upendo wa Mungu Baba, na
Ushirika wa Roho Mtakatifu viwe nanyi nyote” (2 Kor 13:13).
NEEMA YA BWANA YESU KRISTU
Mt. Gregory wa akizungumzia juu
ya ubatizo alisema ni: “Neema: kwani hutolewa hata kwa wahalifu.” Ukweli
kuwa neema hutolewa hata kwa waalifu ni ukweli ambao tunauona msalabani. Neema
ya Bwana wetu Yesu Kristo ilitolewa kwa mwizi Dismasi. Tunahitaji neema ili
kufanikiwa. George W. Bush aliwahi kusema: “Naamini katika neema, kwa sababu
nimeiona; katika amani kwa sababu nimeionja; katika msamaha, kwa sababu
nimehuitaji.” Neema ya Bwana Yesu inaonjeka. Ili kuonja neema ya Bwana wetu
Yesu lazima kushirikiana nayo. Kuna ambaye alitaka kushinda bahati nasibu ya
Kampuni ya Simu ya Tigo. Kila mara aliomba kushinda. Alisali kwa Bwana wetu
Yesu Kristu. Usiku alitokewa katika ndoto. Yesu alimwambia: nataka ushinde
lakini nunua vocha. Alitaka naye atoe mchango wake. Ni lazima kushirikiana na
neema ya Mungu.
UPENDO WA MUNGU BABA
Kilichojaa hufurika. Ni methali
ya Watanzania. Mungu Baba amejaa upendo na unafurika. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata
akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amsadikiye asipotee, bali awe na uzima
wa milele (Yn 3:16). Martin Luther aliita haya hii: “Injili katika mfano mdogo.”
Upendo wa Mungu unajieleza katika kumtuma Mwana wake wa Pekee. Kutoa ni matokeo
ya upendo. Unaweza kupenda bila kutoa. Lakini hauwezi kupenda bila kutoa.
Hata katika matatizo kuna upendo
wa Mungu. Methali ya Kiyiddishi inasema yote: “Yule ambaye Mungu anampenda anamwaadhibu.” Mateso yanaweza kuwa
sehemu ya upendo wa Mungu. “Mungu alikuwa na Mwana mmoja bila dhambi, lakini
hakuwa na yeyote bila mateso,” alisema Mt. Augustini. Kuna kijana mdogo ambaye
alimuua bata wa baba yake. Mkubwa wa kijana huyo akasema: Chochote ninachotaka
unifanyie utanifanyia, vinginevyo nitakushitaki kwa Baba kuwa uliua bata. Siku
ilifuata kijana mkubwa alikuwa na zamu ya kuosha vyombo. Akamwambia mdogo aoshe
vinginevyo alisema: nitakushitaki kuwa ulimuua bata. Alikuwa na zamu ya kuosha
nguo akamwambia mdogo asipoosha nguo atamshitaki kwa baba yake. Mambo yaliendelea hivyo mpaka mtoto mdogo
alipoamua kwenda kuripoti kwa baba yake kuwa alimuua bata. Baba alimwambia
nilikuona ulipofanya tendo hilo. Nilingoja uje kwangu usiwe mtumwa wa kaka
yako. Niliishakusamehe. Huu ni mfano wa upendo wa Mungu Baba.
USHIRIKA WA ROHO
MTAKATIFU
Kama hewa ilivyo kwa mwili wa binadamu ndivyo Roho Mtakatifu
alivyo katika maisha ya kiroho. Roho Mtakatifu yupo nyuma ya pazia anafanya
mambo. Anaunganisha pointi, matukio anapanga kalenda. Omba kuwa na ushirika
naye. Tutumie mafiga haya matatu: Neema, Upendo na Ushirika.
HITIMISHO
Tunahuitaji Utatu Mtakatifu. Tuuiige. Tujifunze kufanya
mambo kwa pamoja. “Sala usafiri kwa haraka tunaposali pamoja.” Ni methali ya
Kilatini.