SIKUKUU
YA PETRO NA PAULO MITUME
1. Mate 12: 1-11
|
2. 2 Timotheo 4: 6-8, 17-18
|
3. Mathayo 16: 13 -19
|
Hayati Nelson Mandela aliwahi
kukiri hivi: “Mimi sio mtakatifu, isipokuwa kama unamfikiria mtakatifu kuwa ni
mdhambi ambaye anajaribu kila mara.” Kuna aliyesema baada ya kuungama dhambi
zake kwa Mungu kuwa kabla ya kuungama alikuwa ni mdhambi anayeikimbilia dhambi
sasa ni mdhambi anayeikimbia dhambi. “Kanisa sio Jumuiya ya wakamilifu, bali
Jumuiya ya wadhambi,” alisema Papa Benedict XV, Kiongozi wa ngazi ya juu ya Kanisa
Katoliki aliyestaafu. Ukweli huu unasemwa kwa namna nyingine na Billy Graham
mhubiri maarufu: “Sote ni wadhambi. Kila mtu unayekutana naye popote duniani ni
mdhambi.” Wadhambi sio watu wakuchukia. “Chukia
dhambi, mpende mdhambi,” alisema Mahatma Gandhi. Kumchukia mdhambi badala ya dhambi ni jambo
linaloshangaza. Lucius Annaeus Seneca alisema: “Watu wengi wana hasira, na sio
dhidi ya dhambi, bali dhidi ya mdhambi,”
Mchungaji alimwambia mwana Kwaya:
“watu hamsini wameniambia kuwa haujui kuimba hivyo nakufukuza kutoka kwenye
kwaya.” Naye mwana kwaya alimjibu mchungaji: “Watu zaidi ya hamsini wamesema
haujui kuhubiri hivyo nawe ufukuzwe kanisani.” Kuhubiri ni kipaji au karama.
Kuimba ni kipaji au karama. Kinachotufanya watakatifu si kipaji au karama bali
fadhila. Je kuna ukarimu katika kutumia hivyo vipaji? Je kuna unyenyekevu
katika kutumia hivyo vipaji? Je kuna imani katika kutumia hivyo vipaji? Kuna
upendo katika kutumia hivyo vipaji? Je kuna ujasiri katika kutumia vipaji
hivyo. Bikira Maria mama wa Yesu alimpendeza Mungu kwa ubikira wake, lakini alibeba
mimba kwa unyenyekevu wake. Mtakatifu Petro Kiongozi wa kwanza wa Kanisa
alikuwa na kipaji cha uongozi, kipaji cha kuandika lakini kilichomfanya
mtakatifu ni: ujasiri, upendo, unyenyekevu na ukarimu. Mtume Paulo alikuwa na
kipaji cha kuhubiri, kuandika lakini kinachomfanya mtakatifu ni imani. Alisema
mwenyewe: “imani nimeitunza.” Hawa watakatifu walikuwa watu wachangamfu. Kununa
si sifa nzuri kwa watakatifu mtakatifu: “Mungu anilinde na watakatifu
walionuna,” Mtakatifu Tereza wa Avila.
Mchungaji Hudson Taylor alisema: “Watu
maarufu wote wa Mungu walikuwa watu wadhaifu.” Lakini Mungu aliwabadili wakawa
watakatifu. Kanisa Katoliki Katika
kitabu cha Maombi wakati wa sikukuu ya Mitume Watakatifu Petro na Paulo tarehee
29 Juni, hukiri udhaifu wa mtume Petro : “Ndugu wapenzi, Mungu alionyesha nguvu ya neema
yake alipomwita Petro, mvuvi dhaifu, awe mwamba ambao juu yake alijenga kanisa
lake..." Petro baada ya kujitazama alimwambia Yesu, “Ondoka
kwangu mimi mdhambi.” (Luka 5:8) Nabii
Isaya alijitazama, Basi, mimi nikasema, “Ole wangu! Mimi nimeangamia, maana,
midomo yangu ni najisi, na watu ninaoishi nao ni najisi kama
mimi.” (Isaya 6:5) Mtume Paulo alipojitazama, alisema, “Maana mimi ni mdogo
kabisa miongoni mwa mitume, na wala sistahili kuitwa mtume, kwa sababu
nililidhulumu kanisa la Mungu.” (1 Wakorintho 15:9). Tunaposoma maisha ya hawa
wadhambi waliogeuka kuwa watakatifu tutafakari ukweli huu: Biblia haikuandikwa
ili kutufanya wasomaji bali watakatifu.
Simoni Petro baada ya kumkiri
Yesu kuwa ni Masiya na Mwana wa Mungu baadaye Yesu alipoweka wazi mpango wake
na sera yake ya kutufia msalabani Petro alimkemea Yesu naye Petro alikemewa
akiambiwa rudi nyuma yangu shetani. Simoni Petro alishinda mtihani wa nadharia
lakini hapa mtihani wa vitendo ulimshinda. Kuwa Masiya kivitendo ni kuwafia
wengine. Mfalme alikuwa na shida ya moyo.
Walitaka kumbadilishia moyo na kumpa moyo wa mtu mwingine. Lakini hapakuwepo na
mtu aliyepata ajali. Hivyo akaitisha mkutano. Akaomba watu kama
kuna anayeweza kunisaidia yaani kuwa tayari kufa kwa ajili yangu atoe moyo
wake. Watu wote wakaamusha mikono. Akasema sasa nimchague nani. Akurusha unyoya
wa ndege na kusema ukimwangukia mmoja wenu huyo ndiye atanipa moyo. Kila
ulipokuwa unamkaribia mtu anaupuliza kwa hewa ya mdomoni unazidi kupaa angani.
Walimpenda kwa maneno na sio kwa matendo.
Ng’ombe licha ya kuwa na miguu
minne huanguka. Ni methali ya wanandi. Kama
mambo ni hivyo itakuwaje mtu mwenye miguu miwili. Methali hii inatufundisha
kuwa binadamu hukosea. Lakini upo uwezekano wa kusahihisha makosa. Kuanguka
chini si kushindwa. Kushindwa ni kutoamka toka chini, “Kwa maana mwenye haki
huanguka mara saba akaondoka tena” (Mithali 24:16). Mtakatifu ni yule
anayeanguka mara 99 na kuamka mara 100. Mwana mpotevu alianguka lakini aliamka
toka chini, “Utukufu wetu wa juu haupo katika kutoanguka kamwe, bali kuamka ghyflukila
tunapoanguka” (Oliver Goldsmith).
Lakini tuna adui anayefurahi
tunapoanguka. Adui huyo ni shetani tusimfurahishe. “Usifurahie maafa yangu ewe adui yangu! Nikianguka, nitainuka tena;
nikiwa gizani, Mwenyezi – Mungu ni mwanga wangu” (Mika 7: 8). Sio shetani
anayecheka na kufurahi tunapoanguka hata adui zetu wengine ambao ni mawakala na
mawikili wake. Hata watakatifu walikuwa na adui kama hao wakawashinda kwa
kushirikiana na neema za Mungu kama tusomavyo katika misale ya waumini: “Watakatifu
tunaowaheshimu leo walikuwa binadamu kama
sisi, na pengine wapo tuliowaelewa. Wao walishinda adui za roho zetu kwa
kutumaini neema za Mungu.”
Binadamu huanguka. Hoja si
kuanguka hoja ni kuinuka. Maneno haya yazame moyoni mwako. “Nikianguka
nitainuka.” Unapoanguka, unapotenda dhambi unakuwa gizani. Lakini Mungu ni
mwanga wako. Mwanga wa Mungu ni neema ya utakaso tunayopata tukitubu. Kumbuka
hoja si namna unavyoanza hoja ni namna unavyomaliza. Mwanampotevu alianza
vibaya akamalizia vizuri. Biblia yasema, “Mtu mwema huanguka mara nyingi lakini
huinuka, lakini mtu mwovu huangamizwa na janga” (Methali 24:16).
Ni kweli mtakatifu ni yule
anayeanguka mara 99 na kuinuka mara 100. Udhaifu wa Musa ulikuwa hasira. Lakini
Mungu alimgeuza kuwa “mtu mpole kuliko wote duniani” (Hesabu 12:3). Udhaifu wa
Ibrahimu ulikuwa ni woga. Mara mbili alidai mke wake alikuwa ni dada yake.
Mungu alimgeuza jasiri na kumfanya baba wa imani. Daudi mzinzi alifanywa kuwa
mtu aupendezaye myo wa Bwana. Yohane mwenye majivuno mmojawapo wa wana wa
ngurumo akawa mtume wa upendo. Udhaifu wa Gidioni ilikuwa ni kutojiamini akawa
mtu shujaa. Saulo muuaji aligeuzwa kuwa mtangazi Injili akawa Paulo. Simoni
dhaifu akawa Petro mwamba. Nakubalina na maneno ya Mtakatifu Yohane Paulo II: “Sisi
sio jumla ya udhaifu wetu na kushindwa kwetu. Ni jumla ya upendo wa baba kwetu
na uwezo wetu wa kweli wa kuwa sura ya mwanawe.”
Kadili tumbili anavyopanda juu
ndivyo makalio yanazidi kuonekana. Binadamu kadili anavyopanda katika ngazi vya
vyeo vya jamii kasoro zake ndogo zinaonekana haraka. Mfalme Daudi naye aliingia
katika kapu hilo hilo . Alitenda kosa na Bathsheba, baada ya
kukemewa na nabii Nathani aliomba msamaha. Zaburi yote ya 51 katika Biblia ni
Zaburi ya kuomba msamaha. “Nihurumie, Ee Mungu, kadiri ya fadhili zako;
ufutilie mbali makosa yangu, kadiri ya wingi wa huruma yako” (Zaburi 51:1).
Baada ya kutubu na kumgeukia Mungu na kuishi maisha mazuri aligeuka na kuwa mtakatifu. Mifano hiyo ni ushahidi tosha kuwa
mtakatifu ni mdhambi aliyeanguka lakini akainuka na kumgeukia Mungu. Lakini
ukweli huo si tiketi ya kumkosea Mungu na kusema nitainuka. Haujui utakufa
namna gani? Ajali huenda isikupe muda wa kumgeukia Mungu. Kumbe wakati
uliokubalika ni sasa. Amua, inuka, achia.
Wenye afya hawamhitaji daktari
bali wagonjwa. Yesu alikuja kuwaita wenye dhambi wapate kutubu. Ukweli huu utufanye tutubu, tujute. “Wafuate watakatifu, kwa sababu wale ambao
uwafuata watakuwa watakatifu,” alisema Papa Mtakatifu Clement I. Orodha ya
watakatifu ambao ni mifano ya kuigwa haifanyi kanisa liwe jumba la makumbusho
la watakatifu bali ni mwaliko wa kuishi vizuri na kuwaiga. “Kanisa ni hospitali
ya wadhambi na sio nyumba ya makumbusho
ya watakatifu,” alisema Pauline Phillips. Mwaliko wa kujitakatifuza ni mwaliko
ambao unavuka ubinafsi. Mbinguni hauendi peke yako. “Jitakatifuze na
utaitakatifuza jamii,” alisema Francis wa Assis. Leo Kanisa Katoliki linafanya
Sikukuu ya Mitume Petro na Paulo. “Tunawaenzi, kuwaheshimu, na kuwapenda mitume
zaidi ya watakatifu wengine, kwa sababu walimtumikia Mungu kwa uaminifu zaidi
na kwa sababu walimpenda kwa ukamilifu zaidi,” alisema Mtakatifu Ignatius. Yote yakishasemwa ukweli unabaki. Tukianguka
tusimame.
Kama utakavyokumbuka Mtakatifu
Paulo alikuwa ameshikilia nguo za Stefano akitazama alivyokuwa anapigwa mawe.
Stefano aliwaombea wote na Paulo akiwemo wakati huo ni Saulo. Sala hizo
zilikuwa na nguvu. Baadaye, Saulo akawa
Paulo. Muuaji akawa Mchungaji. Mwangamizaji akawa Muuokoaji. Adui wa Kanisa
akawa rafiki wa Kanisa. Alitubu. Kila mdhambi ni mtakatifu mtarajiwa ambaye
hajasimamishwa kwenye barabara iendayo Damascus. Kuna Askofu aliyetoa
kichekesho kuwa Mitume Petro na Paulo walishindwa kuishi vizuri pamoja duniani
Kanisa likawaunganisha pamoja katika Sikukuu ya Leo kwa vile wanaishi pamoja
vizuri huko mbinguni. Tukumbuke hawa mababa ni nguzo za imani yetu. Tuwaige
katika mazuri yao ambayo ni mengi kuliko kasoro zao. Kila mtu ni dhahabu inayohitaji
kusafishwa. Kweli mtakatifu ni yule anayeaanguka mara 99 na kuinuka mara 100
tunamuita mtakatifu.