SHEREHE
YA MWILI NA DAMU TAKATIFU YA BWANA WETU YESU KRISTU
1. Kumb. 8: 2-3, 14-16
|
2. 1 Wakorintho 10: 16-17
|
3. Yn 6: 51 – 58
|
Ingawa tuna mioyo midogo lakini
inaweza kubeba jambo kubwa nalo ni shukrani. “Tunapotoa kwa furaha na kupokea
kwa shukrani, kila mtu anabarikiwa,” alisema Maya Angelou. Kuna methali isemayo, “Hasiyeshukuru kwa jambo
dago apewalo hatashukuru kwa jambo kubwa.” Leo hii wakatoliki sehemu zote
duniani wanaandamana kusherehekea sherehe inayojulikana kama “Mwili na Damu ya
Kristu.” Kwa jina lingine sherehe hii inajulikana kama “Sherehe ya Ekaristi
Takatifu.” Neno “Ekaristi” linatokana na neno la Kigiriki ambalo linamaanisha
shukrani. Ni sherehe inayohusu kumshukuru Mungu na utamaduni wa kushukuru.
Kushukuru ni kitovu cha sherehe hii. Shukuru kwa kila jambo. Sherehe ya Leo ya
wakatoliki inahusu utamaduni wa kushukuru. Waluhya wana methali isemayo, “Nyama
choma haiwezi kuwa tamu ukamsahau aliyeichoma.” Methali hii inakazia kuwa na
utamaduni wa kushukuru. Kama umepewa sio siri. Watu wanaona jinsi Mungu
alivyokubariki na hivyo kwa mantiki hii wakatoliki wanaandamana hadharani
kuonyesha shukrani yao
Sherehe hii inapata nguvu kutoka katika maneno
ya Biblia, “ Ndipo Wayahudi wakaanza kubishana kati yao: “Anawezaje huyu kutupa
mwili wake, tule?’ Yesu akaambia, ‘Kweli nawaambieni, msipokula mwili wa mwana
wa Mtu na kunywa damu yake, hamtakuwa na uhai ndani yenu.” (Yohane 6: 52-53)
Jambo hili la kula mwili na kunywa damu ya Yesu lilizua utata mkubwa katika
historia ya Kanisa Katoliki. Mwanzoni wakristu walishitakiwa kuwa ni watu wala
watu. Ni kama Wayahudi waliojiuliza, “anawezaje huyu kutupa mwili wake?”
Jambo hili linaeleweka hivi.
Kama maji na madini yangekuwa na uwezo wa
kusema yangeiambia mimea usipokunywa maji na kula madini hamtakuwa na uhai
ndani yenu. Kama nyasi na maji vingekuwa na uwezo wa kusema vingewaambia
wanyama kama ng’ombe na mbuzi msipokula majani
na kunywa maji hamna uhai ndani yenu. Katika msingi huu kwa vile binadamu ana
mwili na roho Yesu alisema msipokula mwili wangu na kunywa damu yangu hamtakuwa
na uhai ndani yenu. Kushiriki katika
karamu ya Bwana ni muhimu.
Leo hii tunapewa changamoto ya kushiriki. Katika neno kushiriki
tunapata neno ushirikiano. “Tunapomshukuru Mungu kwa kiokombe kile cha baraka,
je, huwa hatushiriki damu ya Kristo? Na tunapoumega mkate, je, huwa hatushiriki
mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate huo ni mmoja, sisi, ingawa ni wengi, tu mwili
mmoja; maana sote twashiriki mkate huohuo.” (1 Wakorintho 10: 16-17) Basi
kushiriki kwetu kusiishie Kanisani tushiriki katika Jumuiya Ndogo Ndogo.
Tushiriki katika maendeleo ya Taifa.
Suala la sherehe ya leo na
shukrani lina msingi wake katika Biblia. “Saa ilipotimia, Yesu akakaa kula
chakula pamoja na mitume wake…Kisha akatwaa kikombe akashukuru, akasema,
‘Pokeeni, mgawanyiane…halafu akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa
akisema, “Huu ni mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa
kunikumbuka.” (Luka 22: 14-19) Yesu alishukuru alipochukua mkate na divai.
Ekaristi inamaanisha shukrani na mkate na divai hutumika. Wakristu ambao
wanashiriki kumbukumbu ya Karamu ya Mwisho ya Yesu kwa kuandamana leo
wanakumbushwa kuwa na utamaduni wa kushukuru maana ndio kiini cha sherehe ya
leo.
Hellen Keller ambaye alikuwa kipofu
na kiziwi aliandika hivi: “Kila mara nimefikiria ingekuwa baraka kama kila mtu
angekuwa kipofu na kiziwi kwa siku chache wakati wa siku zake za kwanza za utu
uzima. Giza lingemfanya akiri uzuri wa mwanga; ukimya ungemfundisha furaha ya
sauti.” Kuna vitu ambavyo tunavyo lakini
hatukiri uzuri wake na umuhimu wake mpaka tumevipoteza. “Hatuna budi kupata
muda wa kutulia na kushukuru watu ambao wameleta tofauti katika maisha yetu,”
alisema John F. Kennedy.
Katika hadithi za Aesop kuna hadithi juu ya mtumwa aliyeitwa
Androcles ambaye alitoroka toka kwa Bwana wake na kukimbilia msituni. Alipokuwa
akitangatanga alikutana na simba ambaye alikuwa amelala chini akinguruma na
kutoa sauti ya uchungu. Mwanzoni alitaka kukimbia lakini aligundua simba
hakumfukuzia. Alirudi nyuma na kumwendea. Alipomkaribia, simba alionyesha kwato
zake au mguu wake ambao ulikuwa umevimba na ukitoa damu. Androcles aligundua
palikuwepo na mwiba mkubwa ambao ulikuwa umeingia ndani na ulikuwa
unamsababishia maumivu makali. Aliutoa mwiba huo na kuufunga vizuri mguu wa
simba ambaye aliweza kusimama na kulambalamba mkono wa Androcles kama mbwa.
Simba alimpeleke Androcles kwenye pango lake na kila siku alimletea nyama ya
kula na kuweza kuishi. Lakini baadaye Androcles na Simba walikamatwa. Androcles
alipewa adhabu ya kutupwa kwenye kibanda cha simba huyo ambaye siku nyingi
aliwekwa kwenye kibanda bila chakula. Mfalme na watu wa ikulu ya mfalme
walikuja kushuhudia simba akimrarua Androcles. Simba aliachiliwa kutoka katika
kibanda chake na kumwendea huyo binadamu akinguruma. Alipomkaribia Androcles
alimtambua na kuanza kulamba lamba mikono yake kama mbwa rafiki. Mfalme
alishangaa alimuomba Androcles amueleze maana ya hayo yote. Androcles alimweleza
mfalme kila kitu. Mtumwa alisamehewa na kuachwa huru na simba aliachiliwa arudi msituni. Hayo ni
matunda ya kutenda wema kwa Androcles na kushukuru kwa simba. Shukrani ni
mtaji. Shukrani ina malipo.
Hata unapokosewa unajifunza kitu
fulani. “Msamaha wa kweli ni pale unapoweza kusema, ‘Nashukuru wa uzoefu huo,’”
alisema Oprah Winfret. Biblia inatwaambia: “Shukuruni katika kila jambo; maana
hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu” (1 Wathesalonike 5: 18).
Rick Warren katika kitabu chake Maisha
Yanayoongozwa na Malengo alikuwa na haya ya kusema juu ya haya hiyo: “Mungu
anakutaka umshukuru kwamba atatumia matatizo yako kutimiza malengo yake.” Kusema
kweli kutomthamini mwenzako ni kukufuru maana kushukuru ni kuthamini.
Kutoshukuru ni kosa kubwa kuzidi kulipa kisasi. “Kutoshukuru ni kosa la
kudharauliwa zaidi ya kulipa kisasi, ambacho ni kulipa baya kwa baya, wakati
kutoshukuru ni kulipa baya kwa wema,” alisema
Kushukuru ni kumsifu Mungu. Mungu
kama amekujalia watoto, akili, utajiri, amani moyoni, jina jema, mke, mme,
mshukuru ukimsifu. Zingatia maneno haya, “Mtukuzeni Bwana pamoja nami, na tuliadhimishe jina lake
pomoja .” (Zaburi 34:3) Mkumbuke Mungu. Hakuna haja ya kujidai sana sote ni
“CHAKUPEWA.” “Nani amekupendelea wewe? Una kitu gani wewe ambacho hukupewa? Na
ikiwa umepewa, ya nini kujivunia kana kwamba hukupewa?” (1 Wakorintho
4:7). Kuna methali isemayo, “Aliyekupa
wewe kiti ndiye aliyenipa mimi kumbi.” Na aliye na kidogo akitumie kupata
kikubwa.
Kushukuru ni kuthamini zawadi
uliyopewa. Kama Mungu ametupa zawadi ya amani, kushukuru ni kuthamini zawadi
hiyo. Kama Mungu amekupa zawadi ya mke, shukuru ni kuthamini zawadi hiyo. Kama
Mungu amekupa zawadi ya mme, shukuru ni kuthamini zawadi yaani mme. Kama unamshukuru Mungu kwa kuwa
Mkenya, basi itendee Kenya mambo mazuri. Kama unamshukuru Mungu kwa vile wewe
ni mtanzania itendee Tanzania mambo mazuri.
Kushukuru ni kuomba tena. Ukipata shukuru. Kuna Baba mmoja
ambaye alikuwa anatembea kando ya Bahari ya Indi na mtoto wake wa kiume. Mara
wimbi likamchukua mtoto wake wa kiume lakini akaokolewa na mvuvi Msamaria
mwema. Badala ya kushukuru Baba huyo alimuuliza mvuvi, “Mtoto wangu alikuwa na
kofia umeiweka wapi?” Huo ni ukosefu wa shukrani. Sherehe ya Ekaristi ambayo
inamaanisha shukrani ni changamoto kwa wakristu wote kuwa na moyo wa shukrani
na sio na moyo wa punda. Shukrani ya punda ni mateke.