Saturday, May 28, 2016

EKARISTI NI MAISHA



                                

                NAMNA YA KUIISHI EKARISTI TAKATIFU
                      
                   SHEREHE YA MWILI NA DAMU TAKATIFU YA BWANA WETU YESU KRISTU

1. Mwa 14: 18-20
2.  1 Kor 11: 23-26
3. Luka 9: 11-17

 UTANGULIZI
v  Tangia kuzaliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristu aliishi maisha ya kiekaristi. Alizaliwa na kuwekwa kwenye chombo cha kulishia mifugo ishara ya kuwa yeye atakuwa ni chakula cha roho zetu, yeye ambaye ni mchungaji wakati huo huo ni malisho. Picha ya hori inahusianishwa na chombo cha kulishia kondoo ambao Luka anawaeleza katika Mdo 20: 28-29 kama kanisa la Mungu. Hori inayafunua maisha ya Yesu, uwepo wa mafundisho yake kama chakula cha uhai kwa kanisa.
v  Bethlehemu alipozaliwa maana yake ni nyumba ya mkate. Ukweli huu unaashiria ekaristi. Unabii juu ya Ekaristi unaonekana tendo la Melkisedeki mfalme wa Salemu kuleta mkate na divai (Mwanzo 14: 18). Utamaduni wa kikristo unamwona kama mfano wa Kristo kwa sababu alitolea sadaka kwa Mungu wake mkate na divai kama Kristo alivyojitoa sadaka katika maumbo ya mkate na divai.

v  “Hapa yupo mkubwa zaidi ya Solomon.” Hapa yupo mkubwa zaidi ya wachezaji wa Manchester United. Hapa yupo mkubwa zaidi ya Rais. Hapa yupo mkubwa zaidi ya Prime Minister. Hapa yupo mkubwa zaidi ya Papa. Hapa yupo mkubwa zaidi ya mwana ndondi Tyson. Hapa yupo mkubwa zaidi ya Mwanandondi Conjestina. Hapa yupo mkubwa zaidi ya Mbunge wako. Hapa yupo Bwana wetu Yesu Kristo. Tumsifu. Tumtukuze. Tumwabudu. SIKIO HALIZIDI KICHWA. SIKIO HALIPITI KICHWA. SAKARAMENTI YA EKARISTI NI SAKRAMENTI AMBAPO YUMO BWANA YESU KRISTU YEYE MZIMA MWILI WAKE, ROHO YAKE, MOYO WAKE, UMUNGU WAKE NA DAMU YAKE KATIKA MAUMBO YA MKATE NA DIVAI.

NAMNA YA KUIISHI EKARISTI TAKATIFU

  1. KUABUDU
Kuabudu ni kufanya ibada, ni kuomba. Kuabudu ni kusali. Ni kutukuza. Ni kustahi kwa namna ya hali ya juu. Heshima tunayotoa kwa Ekaristi Takatifu ni zaidi ya heshima. Tunaabudu. Heshima hiyo ya hali ya juu inaitwa “Latria.” Tunamwabudu Yesu Kristu. Kuna namna nyingi za kuabudu: Unaweza kujilaza kifudifudi yaani tumbo chini, mgongo juu. Tunaimba katika wimbo wa  “Sakramenti Kubwa Hiyo.” (Tantum Ergo)- “Sakramenti kubwa hiyo twaheshimu kifudi.” Tunaabudu kwa kupiga goti kama tusomavyo katika barua ya Mt. Paulo kwa Wafilipi, “Ili kwa heshima ya jina la Yesu, viumbe vyote mbinguni, duniani na kuzimu, vipige magoti mbele yake, na kila mtu akiri kwamba Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.” (Wafilipi 2: 10-11). Tunapiga goti mbele ya Tabernakulo kwa maana yuomo Bwana wetu Yesu Kristo. Kuna Ibada mbali mbali za Kumwabudu Yesu Kristo: Sala za binafsi mbele ya Sakramenti Takatifu, Kuwa na Maandamano ya Ekaristi, Sherehe ya Mwili na Damu ya Yesu, Kuwa na Kongamano la Ekaristi, Kuwa na Masaa ya kuabudu: Saa Takatifu. Tunasoma hivi katika Injili ya Mathayo, “Akawaendea wale wanafunzi akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, “Ndiyo kusema hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? Kesheni na kusali ili msije mkaingia katika majaribu.” (Mathayo 26: 40-41) Hatuna budi kuonyesha heshima kwa wenzetu maana wanampokea Yesu.

  1. KUGAWANYA
“Kisha akatwaa kikombe, akamshukuru Mungu, akawapa; wote wakanywa katika kikombe hicho” (Marko 14: 23). Wakatoliki wanashiriki Meza ya Bwana, meza ya kugawanya. Kugawanya ni changamoto kwa Wakristu kunawakumbushwa kuwa kugawanya huku haukuishii na sherehe ya kula pamoja bali wagawanye mali maishani. Wakiishi ukweli huu kutakuwa na fundisho kwa wengine. Watagawanya ardhi walau na wengine wapate. Watagawanya walichonacho. Kugawanya raslimali na mali ni msingi wa amani. Kugawanya kusiishie kwenye mlango wa Kanisa na si suala la maandamano tu bali liguse hao wanao andamana kuonyesha imani yao lakini ni imani katima matendo. “Ndugu zangu, kuna faida gani mtu kusema ana imani, lakini haionyeshi kwa vitendo?” (Yakobo 2: 14)

Jirani ya Abrahamu Lincoln Rais wa zamani wa Amerika alisikia mtu akilia nje ya nyumba akatoka nje kuangalia kuna nini? Alimuona Lincoln akipita na watoto wake wawili ambao walikuwa wakilia kwa sauti ya juu. “Kuna tatizo gani Abrahamu Lincoln?” “Tatizo walilo nalo watoto ni tatizo katika dunia nzima. Nina matunda matatu na kila kijana anataka kuchukua mawili,” alisema Abrahamu Lincoln. Chanzo cha kutokuwa na amani ni baadhi ya watu kutaka kula kiasi kikubwa mgawo wa samba. Sherehe ya leo inawafundisha wakristu kutokula mgawo wa samba bali kugawanya ili pawepo na amani.

  1. KUSHUKURU
Kuna methali isemayo, “Hasiyeshukuru kwa jambo dago apewalo hatashukuru kwa jambo kubwa.” SHUKURU KWA KILA JAMBO. Sherehe ya Leo ya wakatoliki inahusu utamaduni wa kushukuru. “Walipokuwa wanakula Yesu alitwaa mkate, akashukuru, akaumega na kuwapa wanafunzi wake akisema, Twaeni; huu ni mwili wangu” (Marko 14: 22). Waluhya wana methali isemayo, “Nyama choma haiwezi kuwa tamu ukamsahau aliyeichoma.” Methali hii inakazia kuwa na utamaduni wa kushukuru. Leo hii wakatoliki sehemu wanaandamana kusherehekea sherehe inayojulikana kama “Mwili na Damu ya Kristu.” Kwa jina lingine sherehe hii inajulikana kama “Sherehe ya Ekaristi Takatifu.” Neno “Ekaristi” linatokana na neno la Kigiriki ambalo linamaanisha shukrani. Ni sherehe inayohusu kumshukuru Mungu na utamaduni wa kushukuru. Kushukuru ni kitovu cha sherehe hii. Kama umepewa sio siri. Watu wanaona jinsi Mungu alivyokubariki na hivyo kwa mantiki hii wakatoliki wanaandamana hadharani kuonyesha shukrani yao


Suala la sherehe ya leo na shukrani lina msingi wake katika Biblia. “Saa ilipotimia, Yesu akakaa kula chakula pamoja na mitume wake…Kisha akatwaa kikombe akashukuru, akasema, ‘Pokeeni, mgawanyiane…halafu akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa akisema, “Huu ni mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa kunikumbuka.” (Luka 22: 14-19) Yesu alishukuru alipochukua mkate na divai. Ekaristi inamaanisha shukrani na mkate na divai hutumika. Wakristu ambao wanashiriki kumbukumbu ya Karamu ya Mwisho ya Yesu kwa kuandamana leo wanakumbushwa kuwa na utamaduni wa kushukuru maana ndio kiini cha sherehe ya leo.

Kushukuru ni kumsifu Mungu. Mungu kama amekujalia watoto, akili, utajiri, amani moyoni, jina jema, mke, mme, mshukuru ukimsifu. Zingatia maneno haya, “Mtukuzeni Bwana  pamoja nami, na tuliadhimishe jina lake pomoja.” (Zaburi 34:3) Mkumbuke Mungu. Hakuna haja ya kujidai sana sote ni “CHAKUPEWA.” “Nani amekupendelea wewe? Una kitu gani wewe ambacho hukupewa? Na ikiwa umepewa, ya nini kujivunia kana kwamba hukupewa?” (1 Wakorintho 4:7).   Kuna methali isemayo, “Aliyekupa wewe kiti ndiye aliyenipa mimi kumbi.” Na aliye na kidogo akitumie kupata kikubwa.

Kushukuru ni kuthamini zawadi uliyopewa. Kama Mungu ametupa zawadi ya amani, kushukuru ni kuthamini zawadi hiyo. Kama Mungu amekupa zawadi ya mke, kushukuru ni kuthamini zawadi hiyo. Kama Mungu amekupa zawadi ya mme, kushukuru ni kuthamini zawadi  yaani mme. Kama unamshukuru Mungu kwa kuwa Mkenya, basi itendee Kenya mambo mazuri.

Kushukuru ni kuomba tena. Ukipata shukuru. Kuna Baba mmoja ambaye alikuwa anatembea kando ya Bahari ya Indi na mtoto wake wa kiume. Mara wimbi likamchukua mtoto wake wa kiume lakini akaokolewa na mvuvi Msamaria mwema. Badala ya kushukuru Baba huyo alimuuliza mvuvi, “Mtoto wangu alikuwa na kofia umeiweka wapi?” Huo ni ukosefu wa shukrani. Sherehe ya Ekaristi ambayo inamaanisha shukrani ni changamoto kwa wakristu wote kuwa na moyo wa shukrani na sio na moyo wa punda. Shukrani ya punda ni mateke.


  1. KUKUMBUKA
Kwa kukumbuka kukumbuka tunaiishi Ekaristi Takatifu. Yesu alipokula Karamu ya mwisho na wanafunzi wake alisema, “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.” (Luka 22: 19) Sherehe ya leo ni ya ukumbusho huo lakini inafundisha utamaduni wa kukumbuka. Ili kushukuru ni lazima kukumbuka. Lakini tuwe na utamaduni wa kukumbuka mazuri na sio mabaya. Kumbuka walimu wako wa zamani. Kumbuka wazazi wako waliozeeka lakini walikutendea mengi mazuri. Kuna methali ya kiafrika isemayo, “Aneyeona mama yake ameezeeka husema mahali waliyolipa kwa sura hii iliharibika.” Lakini mama alikuwa mzuri ni uzee. Tukiona wazazi wamezeeka hawana nguvu lakini walitusaidia sana lazima tukumbuke na tulipe hisani kwa wema. Tumesikia katika somo la kwanza, “Msiwe na kiburi na kumsahau Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliyewatoa katika nchi ya Misri, mahali mlipokuwa watumwa.” (Kumbukumbu la Sheria 8: 14) Kiburi kinaweza kutufanya tusahau. Mtakatifu Augustini alisema hivi juu ya Bikira Maria, “Maria alimchukua Mimba Neno kwanza katika akili yake kabla ya kumchukukua mamba katika mwili wake.” Nasi baada ya kumpokea Yesu katika mwili wetu tumpokee katika akili zetu. Tumfirie. Tumkumbuke. Maneno ya Mtunga zaburi yatusaidie katika hili, “ Niwapo kitandani ninakukumbuka, usiku kucha ninakufikiria; maana wewe umenisaidia daima kivulini mwa mbawa yako nitashangilia.” (Zaburi 63: 6) TUFANYE MAMBO MAZURI AMBAYO WATU WANAWEZA KUKUMBUKA.

Kuna mtoto aliyekuwa anatembea na mama yake sokoni. Mtoto huyo alipewa chungwa na muuza machungwa bure. Baada ya kupewa mtoto chungwa mtoto huyo alimrudishia aliyempa akimwambia, “Limenye,” badala ya kusema, “Asante, nashukuru.” Mtoto huyo alisahau kushukuru. Hakuwa na msamiati wa shukrani mtoto huyo. Wazazi hawana budi kuwafundisha watoto wao kushukuru ili tuwe na utamaduni wa shukrani.

  1. KUWA KIMYA
Tuna nyakati za kuwa kimya katika adhimisho la Ekaristi: Baada ya masomo ya misa na kabla ya Sala ya Mwisho. Ukimya unamaliza magomvi. Ukimya unahitaji kutulia, “TULIA MBELE YA MWENYEZI-MUNGU.” (ZABURI 37: 7)

  1. KUFURAHI
“Nyumba ambayo inasherehekea haikosi kucheka.” (Methali ya Kiafrika) Leo tunasherehekea. Jumapili tunasherehekea hatuombolezi. “Furaha siyo kutokuwepo kwa matatizo bali ni kuwepo kwa Yesu Kristo,” alisema, William Vander Haven Mazingira ya Ekaristi Takatifu ni mazingira ya furaha. Mazingira ya Adhimisho la Misa ni Mazingira ya Furaha. Nyimbo za Utukufu, Mtakatifu ni nyimbo za furaha. Alipo Yesu kuna furaha.

  1. KUTOA SADAKA
“Mtaka cha uvunguni sharti ainame.” Ili Yesu atuinue alijitoa sadaka. Ekaristi Takatifu ni sadaka. Ili tuiishi Ekaristi Takatifu hatuna budi kuinama uvunguni ili tuwainue wengine.

  1. KUJIANDAA
MTOTO ALIYEOSHA MIKONO VIZURI HULA NA WAFALME. SAMAKI MKUNJE ANGALI MBICHI. MTOTO UMLEAVYO NDIVYO AKUAVYO. Methali zote zinahusu maandalizi. Kuna watu wawili waliokuwa wanaongea. Mmoja akamwambia mwenzake, “Jana nilikuwa na mawazo mabaya juu ya adui yangu?” Mwenzake akamuuliza, “Je uliyafurahia mawazo hayo.” Yeye akajibu, “Mawazo yalifurahisha maana yalihusu kushidwa kwake katika biashara  na magari yake kupata ajali.” Mawazo ya namna hiyo ni dhambi hauwezi kumpokea Bwana Yesu bila kujiandaa. “…Kila aulaye mkate huo au kunywa kikombe cha Bwana bila kustahili, atakuwa na hatia dhidi ya mwili na damu ya Bwana. Basi, kila mtu ajichunguze mwenyewe kwanza, ndipo ale mkate huo na anywe kikombe hicho; maana anayekula na kunywa bila kutambua maana ya mwili wa Bwana, anakula na kunywa hukumu yake yeye mwenyewe.” (1 Wakorintho 11: 27-29) Unaptunza dhambi moyoni bila kuiungama, unamkaribisha shetani. Ni kama ukiwa na uchafu chumbani unawakaribisha mende. Wakati wa vita vya Napoleon kuna mtu aliyekuanapeleleza kwa ajili ya maadui wa Napoleon. Alipokamatwa aliulizwa na alikataa kutoa habari yoyote. Aliwekwa kwenye gilotini-bamba la kukata kichwa (kwa wahalifu ufaransa.) Upanga uliachiwa ukaanza kukata ulikuwa umekata nusu ya shingo, akaanza kusema, “Nitawaambia, nitawaambia, nitawaambia!” Alikuwa amechelewa. Tusichelewe kuungama.

  1. KUSHIRIKI
Leo hii wakatoliki sehemu nyingi duniani wanasherekea Sherehe ambayo inajulikana kama Sherehe ya Mwili na Damu ya Yesu Kristu. Sherehe hii inapata nguvu kutoka katika maneno ya Biblia, “ Ndipo Wayahudi wakaanza kubishana kati yao: “Anawezaje huyu kutupa mwili wake, tule?’ Yesu akaambia, ‘Kweli nawaambieni, msipokula mwili wa mwana wa Mtu na kunywa damu yake, hamtakuwa na uhai ndani yenu.” (Yohane 6: 52-53) Jambo hili la kula mwili na kunywa damu ya Yesu lilizua utata mkubwa katika historia ya Kanisa Katoliki. Mwanzoni wakristu walishitakiwa kuwa ni watu wala watu. Ni kama Wayahudi waliojiuliza, “anawezaje huyu kutupa mwili wake?”

Jambo hili linaeleweka hivi. Kama maji na madini yangekuwa na uwezo wa kusema yangeiambia mimea usipokunywa maji na kula madini hamtakuwa na uhai ndani yenu. Kama nyasi na maji vingekuwa na uwezo wa kusema vingewaambia wanyama kama ng’ombe na mbuzi msipokula majani na kunywa maji hamna uhai ndani yenu. Katika msingi huu kwa vile binadamu ana mwili na roho Yesu alisema msipokula mwili wangu na kunywa damu yangu hamtakuwa na uhai ndani yenu.  Kushiriki katika karamu ya Bwana ni muhimu.

Leo hii tunapewa changamoto ya kushiriki. Katika neno kushiriki tunapata neno ushirikiano. “Tunapomshukuru Mungu kwa kiokombe kile cha baraka, je, huwa hatushiriki damu ya Kristo? Na tunapoumega mkate, je, huwa hatushiriki mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate huo ni mmoja, sisi, ingawa ni wengi, tu mwili mmoja; maana sote twashiriki mkate huohuo.” (1 Wakorintho 10: 16-17) Basi kushiriki kwetu kusiishie Kanisani tushiriki katika Jumuiya Ndogo Ndogo. Tushiriki katika maendeleo ya Taifa.

  1. KUAMINI
Tunaamini kuwa Yesu yumo katika Ekaristi. Tunapokomunika tunasema, “Amina.” Tunaamini. Neno AMINA lina maana ya “Ni kweli.” “Ninaamini.”  Amina ni sala. Amina ni matendo. Kuna methali isemayo, “Sikusikii matendo yako yananipigia Kelele.” Amina yako haitisikika kama matendo yanapiga Kelele.


  1. UPENDO
“Akupendaye anakupenda na uchafu wako wote.” Yesu alitupenda na uchafu wetu wote. Sakramenti ya Ekaristi Sakramenti ya Upendo. Yesu alitupenda zaidi ya upeo. Upeo maana yake hadi anayoweza mtu kuona. Alitupenda na uchafu wetu wote. Upendo ni kama tabasamu. Tabasamu halina maana mpaka umelitoa. “Upendo unatibu watu-wote wanautoa na wale wanaupokea,” alisema Karl Menninger. “Ukipenda boga penda na ua lake.”

  1. KUWEPO
“Hasiyekuwepo na lake halipo.” Yesu yupo hapa lake lipo. Yesu yupo katika Ekaristi Takatifu. Yeye alisema, “Nami nipo pamoja nanyi siku zote; naam, mpaka mwisho wa nyakati.” (Mathayo 28: 20).  Tujifunze kuwepo kwa ajili ya Mungu, kuwepo kwa ajili ya wenzetu, kuwepo kwa ajili yetu sisi. Kutukuwepo ni tatizo katika mambo muhimu. Ukienda katika mikutano ya siasa utasikia mwanasiasa anauliza, “Vijana mpo?” Vijana wanaitikia, “Tupo.” Wakina “Baba mmpo?” wanaitikia, “Tupo.” “Wakina mama mmpo?” Wanaitikia, “Tupo.” Je tukiuliza hivyo katika mikutano ya Jumuiya ndogo ndogo makundi yote yataitikia hivyo.

Counter

You are visitor since April'08