Saturday, April 19, 2014

WEMA HAUOZI NA UKWELI UTAFUFUKA


 

                                                       JUMAPILI YA PASKA

1. Matendo 10: 34; 37 - 43
 
2. Kol 3: 1-4
 
3. Yohane 20: 1-9
 

 

 WEMA HAUOZI

Leo ni Jumapili ya Paska. Hauchi hauchi unakucha. Hayawi hayawi yamekuwa. Hii ndiyo siku aliyoifanya Bwana tufurahi na kushangilia. Siku hazilingani Jumamosi hailingani na Jumapili. Kama wema unapewa hadhi ya kuwa mtu Yesu Kristu ni wema wenyewe. Walipomzika walijitahidi kuzika na mema yote aliyoyafanya. Lakini alifufuka na mema yake yalifufuka yameandikwa katika Biblia. Wema hauozi. “Mfanya mazuri huvuna chuki.” Ni methali ya kiafrika. Yesu Kristu alifanya mazuri lakini walimsulubisha siku ya Ijumaa Kuu. Ni shukrani ya punda ambayo ni mateke. Mtu ambaye yeye yote ni asali inzi watamla. Ni methali ya Jamaica. Yesu Kristu alikuwa ni mwema na alitenda mema. Wenye wivu na kijicho walimtundika msalabani na kumuua. “Wema ni uwekezaji pekee ambapo hakuna kufilisika,” alisema Henry David Thoreau.

Baada ya Yesu kufufuka Mtume Petro alihubiri jinsi Yesu alivyokuwa akitenda mema: “Na jinsi alivyozunguka katika nchi yote akitenda mema…Naye walimtundika  mtini na kumwua. Mungu lakini alimfufua siku ya tatu na kumjalia kutokea waziwazi” (Matendo ya Mitume 10: 38-40). Yesu aliishi kwa ajili ya wengine. “Maisha ni shughuli ya kusisimua na inasisimua zaidi pale mtu anapoishi kwa ajili ya wengine,” alisema Helen Keller. Tutende wema, wema hauozi. Mgeni mmoja katika familia fulani alimuuliza mtoto wa miaka saba: “Unafanya tendo la wema kila siku, Tommy?” Kijana huyo alijibu: “Jana nilimtembelea nyanya yangu yaani mama yake mama yangu huko kijijini. Alifurahi nilipofika. Leo nimeondoka alifurahi sana kuona ninaondoka.” Ukisoma katikati ya hadithi hii huenda mtoto huyo alisababisha usumbufu mkubwa kwa nyanya yake badala ya kutenda wema. Kila tendo jema halisauliki. Ndiyo maana wanajenga minara kuwakumbuka watu wema. Watoto wanakumbushwa somo la paska kutenda wema, wema hauozi.

Wazazi wanapowatendea watoto wao wema, wema huo hauozi. Kuna mtoto aliyesali hivi: “Mpendwa Mungu husiwape wazazi wangu watoto wengine. Hawajui kumtendea mema huyu mmoja waliye naye.” Sala hii inabainisha mengi katika malezi. Huenda mtoto huyu akutendewa mema kweli au huenda mtoto huyu alikuwa mchoyo anajifikiria yeye peke yake. Yote yakishasemwa wazazi hawana budi kujifunza somo la paska wema hauozi.

Tukumbuke kuwa Yesu Kristu alifufuka akiwa na makovu ya vidonda. Kwa kutumia mantiki hii Mwenye heri Tereza wa Calcutta alisema: “Tunaposafisha vidonda vya masikini, tunasafisha vidonda vya Kristu.”  Yesu mwenyewe alisema mliyomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.  “Usihuunike au kulalamika kwamba ulizaliwa katika wakati ambao hukuweza tena kumuona Mungu katika mwili. Hakuutoa upendeleo huu kutoka kwako. Kwani anasema: Chochote mlichokitenda kwa kaka zangu wadogo, mmenitendea mimi,” alisema Mtakatifu Augustino wa Hippo. Ishi ukijua kuwa Yesu yuko hai na anaishi katika watu.

Kuna hadithi juu ya Peter Newness ambaye alikuwa hajawahi kutoa mchango wowote katika shirika lolote.Katibu la shirika la upendo alimjia kumuomba atoe mchango wake. Alimwambia kuwa kadiri ya rekodi zake hajawahi kutoa mchango wowote licha ya kupata mamilioni kila mwezi. Bwana Newness alimjibu: “Je unajua kuwa mama yangu ni mgonjwa na bili zake ni nusu ya mapato yangu? Je unajua kuwa kaka yangu ni kipofu na hana kazi? Je, unajua kuwa mme wa dada alikufa katika ajali akimwacha bila pesa na wakati ana watoto watatu?” Katibu alimjibu: “Sikujua, samahani ningejua hayo yote nisingekujia.” Peter Newness alimwambia katibu huyo: “Sasa, niambie, kama hawa wote siwapi hata shilingi nitakupaje wewe pesa.” Licha ya Newness kutaja jamaa zake wenye matatizo hakuwasaidia. Hakujua kuwa wema hauozi. Tusifanye hayo ya Peter Newness. Somo la Paska ni kuwa wema hauzoi.

Yesu alipokuwa msalabani Ijumaa Kuu mawazo yake yalikuwa juu yako. Wema huanzia kwenye mawazo.   Wema huu haukuoza. Fikiria mema juu ya wengine. Paska ni ushindi wa wema dhidi ya ubaya. Paska ni ushindi wa ukweli dhidi ya uongo.  Paska inatia matumaini. “Pale ambapo binadamu anaona majani yaliyokauka, Mungu anaona maua mazuri yanayochipuka,” alisema Albert Laighton. Ijumaa Kuu Yesu Kristu alipokufa msalabani ulionekana ni mwisho usio na matumaini. Lakini Mungu Baba alimfufua siku ya tatu.  Ikawa matumaini yasiyo na mwisho.

 

 UKWELI UTAFUFUKA

Palipo na ukweli uongo ujitenga. Yesu ni ukweli. Kufufuka kwake ukweli ulifufuka. Kwa hiyo ukweli utafufuka. Ukweli ukiutundika msalabani kwa kusema uongo, ukweli utafufuka. Ukweli ukiuzika kwa kuonga na rushwa, ukweli utafufuka. Hakuna haja ya kukutaka tamaa.  Kwa mtu ambaye anakumbuka kuwa Mungu wetu ni Mweza yote hawezi kukata tamaa. Jumapili hii tunapoadhimisha Sikukuu ya Paska tunajifunza mengi katika kufufuka kwa Yesu. Mojawapo ukweli utafufuka.

Inavyoonekana kusema ukweli ni biashara yenye ushindani mdogo. Kuna askari aliyeomba ruhusa kwenda kumsaidia mke wake aliyedai ni mgonjwa. Mkubwa wake kazini alimwambia askari huyo, “Nimepokea barua kutoka kwa mke wako. Anasema hata usipoenda wewe hausaidii chochote.” Askari kwa hasira alijisahau na kusema. “Bosi unasema uongo.” Mimi sina mke. Mark Twain alisema kweli, “Unaposema ukweli, hakuna haja ya kukumbuka.” Mtu anayesema uongo inabidi awe na akili ya kukumbuka. Vinginevyo njia ya muongo ni fupi.

“Ukweli utapanda na kuwa juu ya uongo kama mafuta yanavyokuwa juu ya maji,” alisema Miguel de Cervantes. Ukweli ni ukweli hata kama hakuna mtu anayesema ukweli. Uongo ni uongo hata kama watu wote wanasema uongo. Yesu alifufuka. Tunasoma hivi katika Biblia, “ Mungu lakini alimfufua siku ya tatu na kumjalia kutokea wazi wazi, si kwa watu wote, ila kwa mashahidi waliokuwa wamechaguliwa na Mungu” (Matendo 10: 40). Alimtokea Maria Magdalena. Aliwatokea wafuasi wake.

Mtume Thomasi aitwaye Pacha alipoambiwa tumemwona Bwana alisema, “Nisipoona matundu ya misumari mikononi mwake, na kutia kidole changu sehemu za misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, sisadiki hata kidogo” (Yohane 20: 25). Yesu alipowatokea tena Thomasi alikuwepo na alitia kidole chake sehemu za misumari na kutia mkono wake katika ubavu wake. Papa Gregori Mkuu (540 -604) alikuwa na haya ya kusema, “Kutokuamini kwa Thomasi kumeleta faida zaidi kwenye imani yetu kuliko imani ya wafuasi wengine. Anavyomshika Kristo na kusadikishwa, kila mashaka yanaondolewa na imani yetu inaimarishwa. Hivyo mfuasi aliyekuwa akitia mashaka, aligusa madonda ya Yesu na kugeuka kuwa shahidi wa ukweli wa ufufuko.” Ukweli wa ufufuko wa Yesu ulifanyiwa utafiti na mtume Thomasi. Ni msimamizi wa wenye kufanya utafiti.

Pesa inatumika kuficha ukweli. Pesa ilitumika kuficha uweli wa kufufuka kwa Yesu. “Walipokuwa bado njiani, baadhi ya walinzi walienda mjini, wakawapasha makuhani wakuu habari za mambo yote yaliyotendeka. Nao wakakusanyika na wazee. Na baada ya kushauriana na kupatana, wakawapa askari fedha nyingi, wakawaagiza, “Semeni, ‘Wafuasi wake walikuja usiku, wakamwiba sisi tulipokuwa tunalala usingizi.’ Na kama gavana akisikia neno, sisi tutamshauri, ili msipatwe na matatizo.” Nao wakapokea fedha, wakafanya kama walivyoagizwa.” (Mathayo 28: 11-15) Kwa vyovyote iwavyo, kitendo hiki cha kutoa hongo ni ushahidi mkubwa kwamba Yesu amefufuka kwa sababu hongo hutolewa ili kuuzima ukweli uliopo kusudi badala ya kilichotukia kieleweke kinyume chake. Aidha , kwa hali hii ya mambo, mashahidi wa kuona ndio hao walinzi. Wao walishihudia moja kwa moja kwamba Yesu hakuwa kaburini. Laiti wao wangepata ushujaa wa kufunua vinywa vyao na kutueleza. Ukweli ni kuita kila kitu kwa jina lake. Jina la Mungu ni Ukweli. Ni methali Kihindu. Ukweli utafufuka kama si leo ni kesho.

HAKUNA PASKA BILA IJUMAA KUU

Mtaka cha uvunguni sharti ainame. Ili Yesu atukumboe ilibidi kufa msalabani. Lakini hiyo ndiyo siri ya mafanikio katika maisha. Hakuna Jumapili ya Paska bila Ijumaa Kuu. Baada ya dhiki faraja. Ndiyo dira katika kila nyanja iwe katika michezo, biashara, udaktari, ualimu, siasa, dini, familia, kutaja machache. “Hakuna  maumivu hakuna ushindi, hakuna miiba, hakuna kiti cha enzi; hakuna kidonda, hakuna utukufu: hakuna msalaba, hakuna taji,” alisema William Penn (1644-1718) mwingireza aliyekuwa mwandishi wa habari, kiongozi wa kidini, kisiasa na mwanasheria. Unapokuwa na Ijumaa Kuu katika maisha yako usikate tamaa. Paska hipo njiani inakuja. “Pale binadamu anapoona majani yamekauka, Mungu anaona maua mazuri yamechanua,” alisema Albert Laighton (1829-1887) mshairi wa Amerika.

Wazazi wetu wa kwanza walipotenda dhambi ya kwanza yaani kutaka kuwa kama Mungu ambayo ni majivuno na kiburi palikuwepo na pande tano. Kwanza palikuwepo Adamu. Pili palikuwepo Eva. Tatu palikuwepo bustani ya Edeni. Nne palikuwepo roho mbaya akiwa katika sura ya nyoka. Tano palikuwepo mti ambapo walikula tunda. Ili kuondoa dhambi ya asili palihitajika pande tano. Adamu wa kwanza akaja Adamu wa Pili Yesu Kristu. Eva wa kwanza akaja Eva wa Pili Bikira Maria Mama wa Yesu. Bustani pakuwepo bustani ya Kalvari au hata ya Gethsemane. Roho mbaya pakawepo na Roho Mtakatifu. Mti walipokula tunda pakawepo na Mti wa msalaba. Yesu akawa ameshinda kwa kufa msalabani. Mtume Petro anatukumbusha: “Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa!” (1 Petro 2: 24).

 

 “Siku ya kuhuzunisha sana duniani na siku ya kufurahisha sana duniani zilikuwa umbali wa siku tatu,” alisema Sarah Chauncey Woosley (1835-1905) mwandishi wa vitabu vya watoto na jina la uandishi ni Susana Coolidge. Siku hizo mbili ni Ijumaa Kuu na Jumapili ya Paska. Kama una siku ya kuhuzunisha sana ni Ijumaa Kuu yako kuwa na matumaini kuwa siku ya kufurahisha sana yaani Paska yako inakuja. Hali ya hewa ya kiroho ya Paska ni hali ya kutia matumaini, furaha na upendo. Nakutakia heri ya Paska.  Kama unateseka sababu ukweli umezimwa. Sikiliza maneno ya Clarence W. Hall (1925-2011) mwamerika: “Paska inasema unaweza kuuweka ukweli kaburini, lakini hautakaa huko.” Ukweli utafufuka. Kaburi haikuweza kumshikilia Yesu zaidi ya siku tatu. Ukweli hauwezi kuwekwa gerezani. Ukweli hauwezi kufichwa. Hata jiwe kubwa likiwekwa juu ya ukweli. Ukweli utatoka. Hata kama jiwe lisingeondolewa Yesu angetoka kaburini. Maana baada ya kufufuka aliweza kuingia kwenye nyumba milango imefungwa. Sasa kwanini mitume na Maria Magdalena walikuta jiwe limeondolewa. Peter Marshall (1902-1949) mhubiri wa kiamerika analo jibu: “Jiwe liliondolewa kutoka mlango wa kaburi, si kumruhusu Yesu atoke bali kuwawezesha mitume waweze kuingia.”

Kuna mambo mengi yanatufundisha kuwa hakuna Paska bila Ijumaa Kuu. “Mungu wetu ameandika ahadi ya ufufuko, si katika vitabu tu, bali katika kila jani majira ya majani kuchipuka baada ya kiangazi,” alisema Martin Luther. Kwa hiyo usikate tamaa , kama maisha yako yamejaa Ijumaa Kuu. Ijumaa Kuu inadokeza shida, mateso, maumivu, majonzi, huzuni, sononeko. Haya yote yana mwisho. Lakini tuchukue ushauri wa Henry Knox Sherrill (1890-1980) mchungaji wa kiamerika: “Habari Njema kuwa amefufuka haibadilishi ulimwengu wa sasa. Bado mbele yetu kuna kazi, nidhamu, na sadaka. Lakini ukweli wa Paska unatupa nguvu ya kiroho kufanya kazi, kukubali nidhamu, na kutoa sadaka.” Usikate tamaa Ijumaa Kuu itaisha katika maisha yako. Mungu alipokuwa anaumba Biblia inasema, ikawa jioni ikawa asubuhi siku ya pili. Haisemi siku ya kwanza ilkaa sana. Siku ya Ijumaa Kuu haitakaa sana. Hayati Papa Yohane Paulo II, alisema, “Usijiachilie na kukata tamaa. Sisi ni watu wa Paska na wimbo wetu ni Aleluya.” Furaha ya Paska ituletee matumaini.Itutoe katika upweke, udhaifu, nakukata tamaa. Itutie nguvu na furaha. Jumapili hii ya Paska msamehe aliyekukosea. Mwambie mwenzako, rafiki yako, adui yako kuwa unampenda. Sambaza matumaini ya Paska.

                                                                       AU

 TUWE WAUZAJI WA MATUMAINI

1. Matendo 10: 34; 37 - 43

2. Kol 3: 1-4

3. Yohane 20: 1-9

 

Utangulizi: Maisha pamoja na Yesu ni matumaini yasiyo na mwisho, bila yeye, ni mwisho usio na matumaini. Tuitazame Pasaka kupitia dirisha la matumaini. Kufufuka kwa Yesu kulifufua matumaini ya mitume. Kufufuka kwake kufufue matumaini yetu. “Usikate tamaa mpaka hapo utakapojaza nafasi ya kaburi kwa mwili wako.” Ndivyo isemavyo methali ya Uganda. Hakuna kukata tamaa.

 

 

 

 MISINGI YA KUUZA MATUMAINI

Moto huteketeza nyasi lakini hauchomi mizizi. Hiyo ni methali ya Ewe. Walipomuua Yesu waliteketeza nyasi lakini hawakuteketeza mizizi ya uwezo wake wa kufufuka. Tuuze matumaini. Inasikitisha kwamba mwanzoni Maria Madgalena hakuuza matumaini. Ili tuuze matumaini misingi hii ni muhimu. 

1.KUONA CHANYA KATIKA KILA JAMBO

Mwalimu wa hesabu alikuwa anawafundisha wanafunzi wa darasa la tano mahesabu ya kutafuta thamani ya X. Baada ya kufanya hesabu muda wa dakika ishirini ubaoni alisema, “Sasa tumepata jibu la thamani ya ‘X’ ni sawa sawa na Zero.” Mwanafunzi kwa sauti ya kukata tamaa. “Mwalimu kazi yote tuliyofanya zaidi ya robo saa jibu ni zero.” Mwanafunzi huyu hakuona chanya katika kazi nzima.

Mwalimu aliwauliza wanafunzi, “Je mnaweza kuniambia jambo lolote kuhusu wanasayansi wa kemia wa karne ya kumi na saba.” Mwanafunzi mmoja akajibu, “Mwalimu wote wamekufa.” Mwanafunzi hakuweza kutaja ugunduzi waliofanya aliona upande wa hasi yaani kifo,

Mwanzoni Maria Magdalena hakuona mazingira ya matumaini. Aliona jiwe limeondolewa kaburini. Alifikiria mambo mawili: Kwanza alifikiria kuwa askari wameendelea kuadhibu mwili wa marehemu. Wameutoa kwenda kuufanyia maovu zaidi. Maana nani huwa anaogopa marehemu akisha kufa? Pili alifikiri kuwa walozi au waibaji miili ya marehemu wameuiba. Macho ya Maria Magdalena hayakuona mazingira ya matumaini. Aliyevumbua miavuli ya mvua aliitwa mchawi. Watu walioona hasi katika katika miavuli.

Tuone Chanya Katika Kila Jambo. Katika milima tuuone uwepo wa mabonde, katika Ijumaa Kuu tuuone uwepo wa Jumapili ya Pasaka, katika ugonjwa tuwepo uwepo wa afya, katika kushuka tuone kuwepo kwa kupanda. Ukiwa unaendesha gari ukakwama kwenye msongamano wa magari, mshukuru Mungu kwa kuwa una gari. Ukiwa unalalamika baada ya kula chakula kwa kuosha sahani nyingi, mshukuru Mungu kwamba una aina nyingi za vyakula na una watu wengi wa kula chakula. Kama una nguo nyingi za kufua badala ya kulalamika kwamba ni chafu sana Mshukuru Mungu kwa sababu una nguo nyingi. Kuna ambaye ana shati moja analiita, “Kauka nikuvae.” Kama hujapata viatu vizuri sana usilalamike mshukuru Mungu kwamba una miguu.

2.KUTEGEMEA MAZURI YATOKEE

Kuna watu ambao huwa hawategemei mazuri yatokee. Kuna Baba mmoja ambaye aliiulizawa na Padre, kwa nini huwa haendi Kanisani. Alijibu, “Mara ya kwanza nilienda Kanisani, wakanimwagia maji wanaiita ubatizo, mara ya pili nilipoenda walifunga kwa pingu na mke wangu tangia siku hiyo tuko kama wafungwa hatuachani. Naogopa kwenda mara ya tatu uenda wakaniweka kwenye jeneza na kuomba watu watoe heshima ya mwisho. Baba huyu hakutegemea mazuri alitegemea mabaya.

Maria Madgalena alikuwa ameenda kuupaka mwili wa Yesu manukato. Alienda kumtafuta Yesu katika wafu. Maria Madgalena alienda kumtafuta Yesu aliyesulubiwa na sio Yesu aliyefufuka kadiri ya Injili ya Mathayo, “Lakini yule malaika akawaambia wale wanawake, ‘Nyinyi msiogope! Najua kwamba mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa.” (Mathayo 28: 5)

Maria Magdalena hakutegemea Yesu afufuke. Askari waliolinda mwili wa Yesu walitegemea kuwa Yesu anaweza kufufuka “Kesho yake, yaani siku iliyofuata ile ya Maandalio, makuhani wakuu na Mafarisayo walimwendea Pilato, wakasema, ‘Mheshimiwa, tunakumbuka kwamba yule mdanganyifu alisema kabla ya kufa ati, ‘Baada ya siku tatu nitafufuka.’ Kwa hiyo amuru kaburi lilindwe mpaka siku ya tatu …”(Mathayo 27: 66)

Hali ya kutotegemeea mazuri imewapata watu wenye majina makubwa katika Biblia. Ilimpata Eliya alilia kwa huzuni na mfadhaiko aliomba afe, “Imetosha! Siwezi tena. Ee Mwenyezi-Mungu, sasa utoe uhai wangu. Mimi si bora kuliko wazee wangu.” (1 Wafalme 19: 4)

Kuna hadithi ambayo inamhusu malaika aliyetumwa na Mungu kumharifu shetani kuwa mbinu zake zote anazotumia kupambana na ukristu zitachukuliwa kutoka kwake. Shetani alimsihii malaika walau abaki na mbinu mojawapo ya mfadhaiko. Malaika alifikiri hilo ni ombi dogo akakubali. Shetani alicheka na kufurahi sana na kujisemea, “Kwa hiyo mbinu moja nimehifadhi mbinu zote.” Mfadhaiko una mambo haya: huzuni na  kukata tamaa. “Kama bado kichwa chako hakijakatwa bado kuna kuna matumaini kwako.” Ni methali ya Haiti. Hamna haja ya kukata tamaa.  Tukumbuke yaliyotendeka na yaliyosemwa.

3.KUONA NA MACHO YA MWILI NA MACHO YA IMANI

Maria Magdalena aliona na macho ya upendo. Hakuingia kaburini kuona kitambaa na sanda. Hakufanya utafiti. Angeona kitambaa na sanda angeamini, kama Yohane alivyoamini. “Kisha yule mwanafunzi mwingine aliyetangulia kufika kaburini, akaingia pia ndani, akaona, akaamini.” (Yohane 20: 8) Alipenda sana sababu aliondololewa mzigo mkubwa wa dhambi. Mtu aliyesamehewa deni la shilingi tano na yule ambaye amesamehewa deni la shilingi milioni tano. Yule aliyesamehewa deni la shilingi milioni tano atapenda sana. Tuone na macho ya mwili na kuona na macho ya imani. Yohane aliingia ndani ya kaburi. Alifanya utafiti. Aliamini.

Kuna mgonjwa mmoja aliyemuuliza daktari, “Daktari nikiamini kuwa nitapona, je nitapona kweli.?” Daktari akamjibu, “Ndiyo ukiamini utapona kweli.” Mgonjwa akauliza tena, “Je kama imani inafanya kazi namna hiyo, ukiamini kuwa nitakulipa utakuwa umelipwa kweli?” Daktari akajibu,  “Sio lazima.” Mgonjwa alishangaa, “Kwa nini imani inakuwa tofauti upande wa malipo ukilinganisha na upande wa ugonjwa.” Daktari akajibu, “Kuna tofauti kati ya imani kwa Mungu na imani kwako.”  Tuna imani kwa Mungu na Imani kwa Yesu sababu Mungu wetu ni wa kutimiza ahadi. Yesu alisema naweza kulibomoa hekalu nikalijenga siku tatu alibomoa na kulijenga. Siku ya tatu alifufuka. Pasaka inatutaka tuwe wafanya biashara wa matumaini. Tuuze matumaini. Kuna ishara, alama na vielelezo maarufu vya Pasaka vinavyogusia matumaini.

HITIMISHO

“Matumaini hayamuui yeyote.” Hii ni methali ya Kongo. Ingawa matumaini hayaliwi kama chakula hatuwezi kuishi bila matumaini. “Matumaini ni nguzo ya dunia.” Ndivyo isemavyo methali ya Kiafrika. Nyinyi wauzaji matumaini, yaliyopita si ndwele tugange yaliyopo. Leo ni leo liwezekanalo leo lisingoje kesho. Matumaini ni yako yahimarishe. Jana ni yako ikufundishe. Leo ni yako timiza ndoto zako. Kesho ni yako tegemea mazuri. Ukabila upo umalize. Udini upo utupilie mbali. Watu ni wako wapende. Ukweli ni wako, ujue. Ugonjwa unaokusumbua upatie kwa heri ya kutoonana. Kifo sio koma kicheleweshe. Maisha ni yako yaongeze. Ushindi ni wako jitwalie. Usiogopeshwe na kitu chochote umeumbwa katika mfano na sura ya mwenyezi Mungu.

Kama una kinyogo, kidondoshe. Kama unataka kulipiza kisasi, samehe. Kama una kishawishi, kishinde. Kama una chuki ipanguse. Kama una uchungu ukung’ute. Kama una kilema, nenda juu yake. Kama hakuna mapatano patana. Kama unafitina moyoni, ifukuze. Kama una mlima wa matatizo uondoe kwa imani. Kama una ubaya, ushinde kwa wema. Kama kifo kinakuogopesha kicheleweshe. Kama una msalaba, ubebe. Kama una changamoto, ikabili. Wakikuangusha inuka. Wakikucheka wape tabasamu. Wakikusema vibaya, waombee. Wakikuchukia wapende. Wakikuua fufuka.

 

 

Thursday, April 17, 2014

MATENDO SABA YA YESU ALHAMISI KUU




“Kila tendo la Neno aliyetwaa mwili ni fundisho kwetu,” alisema Mt. Augostino. Alhamisi Kuu ya Kwanza Yesu alifanya matendo saba katika kuwaosha miguu mitume wake. Matendo saba hayo ni somo la kujifunza. Bwana Yesu na mitume wake walikuwa katika chumba cha Karamu ya mwisho kinachoitwa Cenaculum. Hiki kilikuwa ni chumba cha kulia chakula cha jioni (cena) kilichokuwa orofani katika nyumba. Kwa kawaida matendo makuu yanayokumbukwa Siku ya Alhamisi Kuu ni kuwekwa Sakramenti ya Ekaristi, Daraja Takatifu na amri ya Bwana ya Mapendo ya kidugu. Lakini kuna utajiri mwingine uliojificha katika matendo saba ya kuwaosha miguu mitume kama tunavyosoma katika Injili ya Yohane: “…aliinuka kutoka mezani, akaweka kanzu  yake kando, akatwaa kitambaa cha kitani, akajizungushia kiuononi. Kisha akatia maji katika chombo, akaanza kuiosha miguu ya wafuasi na kuifuta kwa kitambaa alichojizungushia” (Yohane 13: 3-5).

ALIINUKA KUTOKA MEZANI

Mazuri huachwa kwa ajili ya mazuri zaidi. Ni fundisho la kwanza tunalolipata katika tendo la kwanza la Yesu Alhamisi Kuu ya Kwanza. Bwana Yesu na wafuasi wake walikuwa hawajamaliza mlo wa jioni. Aliacha mazuri mezani. Fundisho alilotaka kulitoa lilikuwa zuri zaidi. Fundisho kuhusu ukuu wa huduma. Ilikuwa ni fursa nyingine ya kumtafakarisha Yuda Iskarioti ajue kuwa tunda la huduma ni amani na pia hasilipe wema kwa ubaya. Lakini yote kwa Yuda Iskarioti ilikuwa kama kupiga ngoma ikiwa imezamishwa majini. Ukweli unabaki kuwa mazuri yanaachwa kwa ajili ya mazuri zaidi. Kama unaweza kumsaidia mtu muda wa kupumzika baada ya chakula sio muhimu kiasi cha kutotoa huduma muhimu kwa wenye shida. John Wesley alisema: “Fanya mazuri yote kadiri uwezevyo, kwa vitendea kazi vyote uwezavyo, kwa njia zote uwezavyo, mahali pote uwezavyo, kwa watu wote uwezavyo, kwa kiasi uwezacho.” Mazuri huachwa kwa ajili ya mazuri zaidi. Kuna methali ya Tanzania isemayo: Jambo linalomfanya mwanamwali alie huwa halipo kwa mme wake bali nyumbani anakotoka. Inabidi kuwaacha wazazi na kuambatana na mme wake. Anaacha mazuri kwa ajili ya mazuri zaidi. Anawaacha wazazi ili naye awe mzazi awe na familia yake.

Pili kuinuka kwa Yesu toka mezani ni muhitasari  wa umwilisho wake. Alitoka mbinguni na kuacha mazuri ambayo sikio halijawahi kusikia. Aliacha mazuri ambayo jicho halijawahi kuona. Neno alitwaa mwili. Tunaalikwa tuinuke. Maneno yetu yageuke kuwa matendo. Yachukue mwili. Yasibaki maneno tu.

Tatu kadiri ya rejeo chini ya ukurasa katika Biblia ya Kiafrika, kuinuka kwa Yesu  kutoka mezani ni dokezo la ufufuko. Kuinuka ni fursa ya kuvuta watu kwake. Alisema: “nitakapoinuliwa nitawavuta watu wengi kwangu.”

AKAWEKA KANZU YAKE KANDO

Bwana wetu Yesu Kristu aliweka kando vazi la utukufu wake. Mtume Paulo anaweka wazi ukweli huu: “Muwe nao moyo aliokuwa nao Kristo Yesu, ambaye ijapokuwa alikuwa namna ya Mungu, hakuchukulia kwamba kuwa sawa na Mungun lilikuwa jambo la kushikamana nalo. Bali alijishusha mwenyewe” (Wafilipi 2: 6-7). Kumbuka vazi lake walilipigia kura. Bila shaka lilikuwa vazi zuri. Lilikuwa vazi la heshima. Aliliweka kando. Aliweka cheo chake kando. Ni mwaliko wa kuweka cheo kando na utukufu kando ili kutumikia.Palikuwepo na mwandishi mashuuri wa Kihindi aliyeitwa Suryakant Thripathi. Jina lake maarufu aliitwa Nirala kwa sababu maandishi yake yote yalikuwa na jina Nirala. Nirala alipenda sana kucheza na watoto. Siku moja alikuwa anacheza na watoto mitaani. Watu ambao walikuwa hawajawahi kumuona uso kwa uso walimtembelea. Walimuuliza Nirala mwenyewe bila kumjua: “Tafadhali unaweza kutuonesha nyumba ya Nirala. Tumekuja kumtembelea.” Nirala aliwaambia wangoje atawaonesha nyumba yake baadaye kidogo. Aliendelea kucheza na watoto na baada ya kumaliza aliwaambia kuwa yeye ndiye Nirala. Wageni walishangaa na kumuuliza: “Kwa nini ukutwambia mapema tulipokuuliza.” “Wakati huo sikuwa Nirala mwandishi,bali mcheza na watoto.” Unapocheza na watoto kuwa kama mtoto. Cheo chako kibadilike kulingana na mazingira. Tunasoma katika Biblia: “Kwa wanyonge nalikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu (1 Wakorintho 9:22). Kuna wimbo unasema: “Nimefufuka nab ado ningali pamoja nanyi..”

AKATWAA KITAMBAA CHA KITANI

Alitwaa umbo la mtumishi. Watumwa na watumishi huko Uyahudi enzi za Yesu walijulikana kama:  Watu wa Taulo.” Alichukua cheo cha mtumishi. Tendo hilo lilikuwa ni utabiri wa mateso na kifo chake. “Kabla ya kusulubiwa msalabani alivuliwa nguo Zake, na alipokufa aliwekwa kwenye nguo ya kitani,” alisema Mtakatifu Augustino. Tunaposhawishiwa kufikiria juu ya jina letu, shahada zetu, nafasi yetu, haki zetu, ubora wetu, hadhi yetu, ukuu wetu, mafanikio yetu, sifa zetu, fahari yetu, uwezo wetu tupige picha ya Bwana Yesu anachukua taulo. Katika taasisi na mashirika matatizo yanaweza kujitokeza kwa vile mtu fulani hakupewa nafasi yake. Watu wakubwa ukubwa wao unaweza kutotambuliwa vizuri. Lakini kuna ukubwa wa aina moja, ukubwa wa utumishi. Papa anaitwa “Mtumishi wa Watumishi.” Usijiulize watumishi wangapi wanakutumikia bali jiulize watumishi wangapi wanakutumukia. Ibn Batuta, Mwanafalsafa na mfanyabiashara wa Afrka Magharibi alisema: “Tukifa msitutafute katika makuburi yaliyopakwa chokaa na marumaru, bali mtutafute katika mioyo ya watu tuliowatumikia.”  

AKAJIZUNGISHIA KIUNONI

Bwana Yesu Kristo aliuzungushia Umungu wake taulo ya ubinadamu aliouchukua toka kwa Bikira Maria.  Kuzungusha taulo kiunoni kunadokeza utayari na wepesi wa kufanya kazi. Kumbuka bahati huwaendea walio tayari. Giuseppe Garibaldi  alisema: “Nipe mkono ulio tayari badala ya ulimi ulio tayari.” Yesu hakuwa tayari kwa maneno alikuwa tayari kwa matendo. Matendo yana kauli kuliko maneno. “Safari ya kwenda mbinguni ni kazi ngumu ambayo kila mmoja hana budi kujifunga mkanda ili aitekeleze, kwani kinyume na hapo ipo hatari ya kuishia mlangoni tu,” alisema Samweli Waiti Ndugwa. Jifunge mkanda utumikie.

 KISHA AKATIA MAJI KATIKA CHOMBO

“Kanisa lina maji na machozi, maji ya ubatizo na machozi ya kutubu,” alisema Mtakatifu Ambrose. Maji ni kimiminiko. Kutia maji chomboni kutukumbushe vimiminiko viwili: maji yatakasayo na machozi ya toba. Kadiri duniani panavyokuwepo na dhambi ndivyo tunavyohitaji kufanya toba. Mapdre ni vyombo vya kutakasa watu katika Sakramenti ya Upatanisho. Machozi ya toba yana nguvu: “Machozi kama ya Daudi huzima hata moto wa Jehanumu,” alisema Mtakatifu Chrysostomu. Sikitiko timilifu ni sifa ya toba ya kweli. “Lakini hata sasa, asema BWANA, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuomboleza” (Yoeli 2: 12). “ Kama ukiwa mbele ya mahakama ya kibinadamu baada ya hukumu kupitishwa, ukilia na kuomboleza, kwa kulia kwako hautabadili hukumu kamwe, lakini mbele ya baraza la kimungu utabadili hukumu kama kutoka ndani ya moyo wako utalia kwa ajili ya kupata huruma,” alisema Mtakatifu Chryosostomu.

 AKAANZA KUIOSHA MIGUU YA WAFUASI

Kuna aliyesema kuwa: “Kukaa majini si kutakata.” Yesu alipoosha miguu ya wafuasi wake si wote walitakatata. Nanyi mmekuwa safi lakini si nyote. Ni maneno ya Yesu. Yuda Iskarioti hakuwa safi. Alikuwa na mpango wa kumsaliti Yesu. Kukaa majini si kutakata. Samaki anakaa majini lakini ngozi yake si safi. Samaki anakaa majini lakini lazima kumuosha kabla ya kumla. Tunalazimika kutumia Sakramenti ya Upatanisho ili tupate neema ya utakaso. Kusali sala kunatupa neema ya msaada si neema ya utakaso. Tunahitaji neema hizo zote. Kuna methali ya Kidachi isemayo: “Rafiki akimuosha rafiki yake wote hutakata.” Ni vizuri marafiki wakasahishashana. “Kila mtu anapaswa kutunza kaburi la usawa wa kadiri ambalo ndanimo atazika makosa ya marafi wake. Tukumbuke kuwa: “Urafiki ni kama pesa, rahisi kuzipata kuliko kuzitunza,” alisema Samuel Butler. Yuda Iskarioti hakutunza urafiki wake na Yesu. Alimsaliti Yesu. Kutenda dhambi ni kumsaliti Yesu kwa vipande thelathini vya fedha.  Wanandoa hawana budi kusahihishana. Kuna methali ya Tanzania isemayo: “Viganja viwili ni kwa ajili ya kuoshana.”

NA KUIFUTA KWA KITAMBAA ALICHOJIZUNGUSHIA

 Yesu alitumia raslimali zake za kibinadamu kuwahudumia wengine. Tutumie raslimali tulizonazo kuwatumikia wengine. “Upendo una mikono kuwasaidia wengine. Upendo una miguu kuharakisha kuwasaidia masikini na wahitaji. Upendo una macho kuona mahangaiko na shida za wengine. Upendo una masikio kusikiliza kilio na sauti za huzuni za watu. Namna hiyo ndivyo upendo ulivyo,” alisema Mt. Augustino wa Hippo.

Huduma ni gharama ya ufuasi. Tulipe huduma hiyo. Upendo ni gharama ya ufuasi tulipe gharama hiyo. Yesu ametupa mfano wa unyenyekevu, mfano wa upendo, mfano wa huduma, mfano wa undugu na mfano wa utume.


Counter

You are visitor since April'08