Saturday, January 21, 2017

MAKUNDI



                                      Jumapili ya 3 ya Mwaka

 

1. Isa 9: 1-4
2. 1 Kor 1: 10-13, 17
3. Mt 4: 12-23

 

“Kila mtu wa kwenu husema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Petro, na, Mimi ni wa Kristo. Je! Kristo amegawanyika?” (1 Wakorintho 1:12-13). opi

Tukiungana tutasimama, tukigawanyika tutaanguka. Maelfu ya nati yanashirikia vipande vingi vya gari pamoja lakini nati moja inaweza kutawanya vipande vya gari. Kupotea kwa nati moja au kutofanya kazi vizuri kwa nati moja kunaweza kuleta kasoro katika gari zima. Mgawanyiko waweza kuleta kasoro katika umoja. Umoja wetu wakristu unatoka katika umoja pomoja na Kristu. Kristu hakugawanyika? Mtume Paulo aliandika, “Kila mtu wa kwenu husema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Petro, na, Mimi ni wa Kristo. Je! Kristo amegawanyika?” (1 Wakorintho 1:13).

Wakristo wa Korintho ambao Mtume Paulo aliwaandikia barua walikuwa na tatizo la kubaguana.Kubaguana huku ni kama moto uliongezewa petroli ya maneno na majungu. Palikuwepo na kauli mbiu nne: Mimi ni wa Paulo, Mimi ni wa Apolo, Mimi ni wa Petro na Mimi ni wa Kristo. Waliwashabekia wahubiri mbalimbali lakini wote walikuwa wanamhubiri Kristu. Hatuna budi kuwa na kauli mbiu moja: Mimi ni wa Kristo. Naweza kusema: Umtafute Kristu: umpate Kristu:umpende Kristu. Kinachotakiwa ni kuwa na moyo wa umoja. “Usijali maneno ya watu wakisema kwamba una moyo wa umoja. Wanataka nini? Uwe Chombo cha kuvunjika vipandevipande mara tu kinaposhikwa?” Alihoji Josemaria Escriva (1902-1975) wa Hispania.

Mfano wa msumari unaonesha umuhimu wa umoja. Msumari usipokazwa sana au ulegeapo na kutoka ulipotiwa. Sehemu kubwa pia ulegea ama magurudumu ya mtambo huathirika au kuvunjika. Kazi hucheleweshwa. Pengine mtambo mzima huingiwa na ubovu. Josemaria Escriva alisema, “Usisahu kwamba umoja ndio alama ya uzima: kupotea umoja kuna maana ya kuoza, ishara dhahiri ya kuwa maiti.”

Jambo lingine la kuzingatia ni katika kuleta umoja ni kuvumiliana. Kuna hadithi ya wayahudi inayomhusu mzee wa miaka themanini aliyekutana na Abrahamu. Abrahamu alikuwa amekaa karibu na mlango wa nyumba yake. Mgeni huyo alimuomba Abrahamu akae kwake walau siku moja. Abrahamu alimuuliza mzee huyo, je wewe ni mtu anayeamini? Mzee huyo alijibu, naamini na kuabudu jua. Abrahamu alimfukuza na kusema kuwa hauwezi kulala hapa na kumuita mbwa mchafu. Usiku alipolala Abrahamu Mungu alimtokea katika ndoto na kumwambia: Abrahamu haukuweza kumvumilia mzee huyo walau kwa usiku mmoja. Mimi nimemvumilia miaka themanini. Katika dunia hii watu wana imani tofauti. Kinachohitajiwa ni kupendana, kuvumiliana na kueleweshana polepole bila kuleta mfarakano maana sisi ni wanadamu yaani watoto wa Adamu. Mungu ni Baba yetu sote. Biblia yasema, “Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wanchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao” (Matendo 17: 16).

Mwanga wa umoja una nguvu unaweza kuangaza, taifa zima na dunia nzima na kufukuza giza la kutoelewana na utengano.Tukumbuke kuwa kidole kimoja hakivunji chawa. Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu. Kitaifa umoja ni uhai, utengano ni kifo. “Bwana aliweka wengine sabini na wawili, aliowatuma wawili wawili wamtangulie katika miji na vijiji vyote alivyotaka kuvitembelea mwenyewe” (Luka 10:1).

 “Peke yetu tutafanya machache, pamoja tutafanya mengi,” alisema Helen Keller. Nguvu kubwa ya uongozi wowote ni umoja, na hatari kubwa kwa uongozi wowote ni utengano. Katika kuungana uongozi unasimama, katika kutengana uongozi unaanguka. Uongozi unahitaji moyo wa ushirikiano. Yesu kama kiongozi wa kuigwa hakufanya kazi peke yake. Tunasoma hivi katika Biblia, “Bwana aliweka wengine sabini na wawili, aliowatuma wawili wawili wamtangulie katika miji na vijiji vyote alivyotaka kuvitembelea mwenyewe” (Luka 10:1). Kifungu hiki cha Biblia kinabainisha ukweli kuwa macho mawili huona vizuri kuliko moja. Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.

 

Viongozi wazuri lazima washirikiane katika kugawana baraka na kugawana lawama, kugawana mema na kugawana shutuma. Anayefunga gori ni mmoja lakini timu yote husherekea. Wachezaji wote wanagawana furaha ya ushindi. Hivyo hivyo timu ikishindwa wachezaji wote wanagawana majonzi ya kushindwa. Ushirikiano katika mambo muhimu ni jambo muhimu. Yesu aliwataka wafuasi wake wasiwakatishe tamaa wale ambao walikuwa wanafanya miujiza kwa jina lake ingawa hawakuwa katika kundi moja. Kumbuka maneno ya Marko mwinjili katika Biblia, “Mwalimu, tulimuona mtu akiwafukuza pepo wabaya kwa jina lako, hata baada ya kuwa haandamani nasi, hivyo tukamkataza. Msimkataze, Yesu akanena, kwani hakuna anayeweza kutenda miujiza kwa jina langu akarudi kunisema vibaya. Kwa sababu asiye mpinzani wenu yu upande wenu.”

 

Yale yanayotuunganisha kama ndugu na binadamu ni ya muhimu kuliko yale yanayotutenganisha. Kuwa na lengo moja kama kuboresha maisha ya watu ni jambo ambalo halina budi liunganishe viongozi. Kwamba viongozi wanamhudumia mtu yule yule ni jambo la kuwaunganisha viongozi. Yesu alishirikiana na watu wa aina yote. Alishirikiana na matajiri waliomwazima mwanapunda. Alishirikiana na maskini wengine aliwatibu kama wakoma kumi. Alishirikiana na wenye dhambi kama Zaccheus na alishirikiana na watu wasio kuwa na hila kama Nathanaeli. Uongozi wake ulijumuisha wavuvi kama Simoni Petro na watoza ushuru kama Mathayo.

 

Vidole siku moja vilikuwa na ugomvi. Kidole gumba kilisema mimi ni bora sana, bila mimi hauwezi kushika kalamu, pili ni mnene na mfupi. Kidole cha shahada nacho kilianza kujisifu na kusema, mimi ni bora sana, bila mimi mzazi hawezi kuonya. Bila mimi walimu hawawezi kufundisha na kuonya. Kidole cha kati kilisema, tujipange mstari nani mrefu zaidi. Mimi ni bora. Kidole cha pete kilinyamazisha vidole vingine na kusema, mimi ni bora. Bila mimi maaskofu pete zao hawataziweka wapi? Bila mimi Bwana na Bibi arusi pete zao wataziweka wapi? Kidole cha mwisho kadogo kikasema, sisi vidole vidogi viwili ni bora. Mtu akiwa anasali na viganja viko kifuani sisi tunakuwa tumekaribia altare. Vidole kwa kawaida vinafanikiwa vinapounagana na si pale vinaposhindwa kushirikiana. 

Saturday, January 14, 2017

KATIKA MATATIZO MTAZAME YEYE


                                        

                                       DOMINIKA YA 2 YA MWAKA  “A “

1. Isa 49: 3, 5-6
2. 1 Kor 1: 1-3
3.  Yn 1: 29-34

 

“Tazama, Mwanakondoo wa Mungu” (Yohane 1: 29)

Akiwa amestaajabia mwanga wa mwezi guru mmoja aliwapeleka wanafunzi wake na kunyosha kidole chake kuwaonesha mwezi (guru ni mtu mwenye maarifa makubwa au mtaalamu wa jambo fulani) . Wafuasi wake ambao walikuwa hawajaelewa mambo vizuri walifurahishwa na kidole cha mwalimu wao. Baadaye wanafunzi wake walikuwa na mdahalo juu ya kidole cha mwalimu wao. Mwanafunzi wake mwenye hekima alibaki kimya akiutazama mwezi. Kama guru akionesha kidole. Yohane Mbatizaji aliwaambia wanafunzi wake “Tazama, Mwanakondoo wa Mungu” (Yohane 1: 29). Yeye alikuwa ni kama kidole cha guru. Wanafunzi hawakupaswa kumtazama Yohane bali Bwana wetu Yesu Kristo. Katika matatizo usitazame ukubwa wa tatizo bali ukubwa na ukuu wa Yesu Kristo.

Injili ya leo ina maneno: ona, tazama, kujua, shuhudia. Neno “kuona” limerudiwa mara nne. Neno “tazama” limerudiwa mara moja. Lakini linajitokeza tena katika mistari miwili inayofuata.

SIMAMA UMTAZAME YESU: “Yohane alikuwa amesimama pamoja na wawili katika wanafunzi wake. Akamtazama Yesu akitembea” (Yohane 1: 36). Yohane Mbatizaji alisimama. Alisimama kumpisha Yesu. Mwenye nguvu mpishe. Yohane Mbatizaji alisimama  akiwakilisha kusimama kwa Sheria ili Yesu aikamilishe na kuleta neema ya Injili. Sio sauti tu inamtangaza Yesu Kristo hata macho ya Yohane Mbatizaji. Alimtazama. Tumtazame Yesu. Tusimamishe shughuli zetu siku ya Jumapili tumtazame Yesu. Tusimamishe shughuli zetu za asubuhi sana twende kanisani tumtazame Yesu wa Ekaristi. Tukitoka kanisani tusimame mbele ya ombaomba tumtazame Yesu. Tusimame mbele ya mwenye njaa, tumtazame Yesu. Tusimame mbele ya mwenye kiu, tumtazame Yesu. Tusimame mbele ya mgonjwa tumtazame Yesu. Mtume Petro alishindwa kusimama kwenye maji na kumtazama Yesu. Alitazama mawimbi akaanza kuzama.

UNAPOTUKANWA MTAZAME YESU: “Jamaa zake walipopata habari, walitoka wamkamate, maana walisema, “Amerukwa na akili” (Marko 3:21). Walimtukana Yesu sembuse Yesu.  Unaposema, “Nimetukanwa.” Yesu anasema, “Na mimi.” Jamaa zake walisema, “Amerukwa na akili.” Ukiwa mkristo si kwamba umekingiwa kutakanwa. Walimtukana Kristo mwenyewe. Yesu alikutana na watu wenye majungu, uzushi na fitina. Tukumbuke hawajawahi kujenga mnara katika historia ya dunia ya kuwaenzi wazushi na waongo. Anayekutukana huenda anajitukana yeye mwenye.  Kuna mtu ambaye aliingia kwenye studio ya sanamu ya mtu. Alianza kusema vibaya juu ya sanamu. “Sanamu hii ya mwanaume imevalishwa nguo chafu. Ndevu zimechakaa. Viatu havikupakwa rangi. Mikono ni michafu.” Mke wa mwanaume huyo alimvuta kando na kumwambia. “Unajisema vibaya maana unachokiona ni sura yako katika kioo.” Huyo mtu alijaribu kumtukana mtengenezaji sanamu lakini alikuwa anajitukana.

WAKATI UNAPOKUWA NA HASIRA MTAZAME YESU: Sifa ya mwanakondoo ni upole. Tazama upole wa Yesu. Alirudisha sikio la Malchus, uvumilivu wake kwa Mt. Petro baada ya kumkana, aliwavumilia na kuwasemehe wauaji. Namna ya Yesu ya kujibu ilikuwa ya upole.   Yuda alipomsaliti Yesu kwa busu,  Yesu alimwambia, “Rafiki, fanya ulichokuja kufanya.” Mlinzi alipompiga kofi aliuliza kwa upole, “Mbona wanipiga?” Yeye amesema: “Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu, kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu”(Mt 11:29). Upole ni muhimu kwetu kwa sababu mbili. Kwanza sisi ni viumbe wanaofikiri: Hasira mbaya inazuia kufikiri vizuri. Kufikiri kunatutofautisha na wanyama. Pili, tuna Roho wa upole. Katika maandiko matakatifu tunaaswa hivi: “Hamjui ni Roho ya namna gani mliyo nayo; kwa maana Mwana wa Mtu hakuja kuyaangamiza maisha ya watu, bali kuyaokoa.”  . Baba mmoja alimfokea mtoto wake aliyeiba nyama toka mezani bila kupewa na kabla ya saa ya kula. “Rudisha nyama mezani wewe mhuni. Muone kichwa kama gari la Hummer.”Mtoto alijibu, “Baba sema kwa sauti ya chini na kwa upole watu walioko nje wasijue ulivyonilea vibaya.”

UNAPOSEMWA VIBAYA MTAZAME YESU: “Ana Beelzebuli! Tena, anawafukuza pepo kwa nguvu ya mkuu wa pepo” (Mk 3:22). Yesu alikumbana na upinzani. Usiogope upinzani, kumbuka tiara huruka angani dhidi ya upepo na si pamoja na upepo. Mtu akiwa mkarimu, wanasema anajitangaza. Akiwa mchoyo wanasema ana gundi kwenye vidole, ni myinmi, ni bahili. Mtu akitoa hotuba fupi sana wanasema hakujiandaa. Akitoa hotuba ndefu sana wanasema hatunzi muda. Akiwa motto wanasema ni malaika. Akiwa mtu mzima wanasema achana na Yule shetani. Akiwa mcha Mungu wanasema ni mkatoliki zaidi ya papa. Asipokuwa mcha Mungu wanasema shetani amemweka mfukoni. Waalimu wa sheria walisema Yesu ana Beelzebuli. Kwa tafsiri sisisi Beelzebuli maana yake bwana wa nzi. Beelzebuli ni mkuu wa pepo wabaya. Yesu alitumia mfano kuwajibu. Kadiri ya Baba wa Kanisa Theophylact mfano huo una maana hii: Shetani ni mtu mwenye nguvu, mali yake ni watu ambao amewapokea; mtu asipomshinda kwanza Shetani atamyanganyaje mali yake, ambayo ni watu anaowamiliki, kwanza mmalize shetani harafu uwashinde wengine, na mimi ni adui zao. Namna gani wanaweza kusema nina Beelzebuli .

WAKATI RAFIKI ANAPOKUSALITI MTAZAME YESU: Bwana Yesu alikuwa rafiki mwaminifu kwa mitume wake. Aliwaita rafiki. Lakini Yuda Iskarioti hakuwa rafiki mwaminifu alimsaliti Yesu kwa busu. Tunasoma katika Biblia hivi: “Lakini Yesu akamwambia, “Yuda! Je, unamsaliti Mwana wa Mtu kwa kumbusu?” (Luka 22: 47). Mama Tereza wa Calcutta alikuwa na haya ya kusema: “Ona huruma ya Kristu kwa Yuda. Bwana aliyetunza ukimya mtakatifu hasingemsaliti kwa mitume wenzake. Yesu angesema hadharani na kuwaambia watu malengo yaliyojifichwa na matendo ya Yuda. Badala yake alionyesha huruma badala ya kulaani. Alimuita Yuda ‘rafiki.’ Na kama Yuda angetazama kwenye macho ya Yesu, leo Yuda angekuwa rafiki wa huruma ya Mungu.” Mbwa ni mfano wa rafiki aliye mwaminifu. Kuna tajiri mmoja aliyekuwa anasafiri akiwa amempanda farasi. Mbwa wake alijaribu kumfuata Bwana wake kwa nyuma lakini Bwana huyo alimfukuza. Lakini mbwa aliendelea kuwafuata kwa nyuma. Katikati ya safari mfuko wa fedha uliokuwa juu ya farasi ulidondoka bila bwana huyo kujua. Mbwa kuona hivyo alikimbia na kuwapita na kuanza kubweka mbele yao. Bwana huyo alikasirika na kumpiga risasi. Baada ya kumpiga risasi mbwa alichechemea na kwenda kujilaza juu ya mfuko wa bwana wake. Bwana wake alipofika hotelini na kutazama vitu vyake aligundua mfuko wa fedha hauonekani. Akaanza kurudi nyuma amempanda farasi wake akitafuta mfuko huo. Alimkuta mbwa amelala juu ya mfuko wa pesa amekufa. Mbwa alikuwa rafiki mwaminifu. 

UNAPOKUTANA NA WENYE MAJIVUNO YA MALI: Mtazame Yesu. Kuna watu ambao wakiona simu yako wanajivuna, sababu ya kwao ni ya bei kubwa. Mtazame Yesu.“Mwana wa mtu hana mahali pa kulaza kichwa.”

UNAPOKUTANA NA WENYE MAJIVUNO YA WALIPOZALIWA NA TABAKA LAO. Mtazame Yesu. Tunasoma katika Biblia, “Kuna zuri linaloweza kutoka Nazareti? Baraka Obama alitokea Kisumu Kijiji cha Kogero akaingia Ikulu ya Marekani si kuitembelea bali kukaa kama Rais.

UNAPOKUTANA NA WENYE MAJIVUNO YA HESHIMA WALIYO NAYO. Mtazame Yesu. Tunasoma katika Biblia, “Huyu si mwana wa seremala?” Yesu alikuwa zaidi ya mwana wa Seremala. Ni Mungu mtu. Wewe ni zaidi ya kazi unayoifanya. Wewe ni mpendwa wa Mungu.

UNAPOKUTANA NA WANAOJIVUNIA UMBO LAO. Mtazame Yesu. Biblia inatwaambia juu ya Yesu wa Ijumaa Kuu: Hana umbo wala uzuri.

UNAPOKUTANA NA WENYE MAJIVUNO YA KISOMO: Mtazame Yesu. Tunasoma hivi katika Biblia, watu walimshangaa Yesu, wakisema, huyu ameyapata wapi haya? na, “Ni hekima gani hii aliyopewa huyu?”

UNAPOKUTANA NA WENYE MAJIVUNO YA KUWA BOSI. Mtazame Yesu. Yesu alisema, “Basi, ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi.”

UNAPOKUTANA NA WENYE MAJIVUNO YA MAFANIKIO. Mtazame Yesu.  Tunasoma hivi katika Biblia, “alikuja kwa walio wake, walio wake hawakumpokea. Hata jamaa zake hawakumwamini. Ni mtu aliyekataliwa na kudharauliwa. Lakini tusisahau kwake kila goti linapigwa.

UNAPOKUTANA NA WENYE MAJIVUNO YA KUSEMWA VIZURI. Mtazame Yesu. Baadhi ya watu walimsema Yesu vibaya: “ rafiki wa watoza ushuru na wa dhambi.”

UNAPOKUTANA NA WENYE MAJIVUNO YA AKILI. Mtazame Yesu. Tunasoma hivi katika Biblia: Nazungumzia mambo haya kama Baba alivyonifundisha.

 

Counter

You are visitor since April'08