Saturday, January 21, 2017

MAKUNDI



                                      Jumapili ya 3 ya Mwaka

 

1. Isa 9: 1-4
2. 1 Kor 1: 10-13, 17
3. Mt 4: 12-23

 

“Kila mtu wa kwenu husema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Petro, na, Mimi ni wa Kristo. Je! Kristo amegawanyika?” (1 Wakorintho 1:12-13). opi

Tukiungana tutasimama, tukigawanyika tutaanguka. Maelfu ya nati yanashirikia vipande vingi vya gari pamoja lakini nati moja inaweza kutawanya vipande vya gari. Kupotea kwa nati moja au kutofanya kazi vizuri kwa nati moja kunaweza kuleta kasoro katika gari zima. Mgawanyiko waweza kuleta kasoro katika umoja. Umoja wetu wakristu unatoka katika umoja pomoja na Kristu. Kristu hakugawanyika? Mtume Paulo aliandika, “Kila mtu wa kwenu husema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Petro, na, Mimi ni wa Kristo. Je! Kristo amegawanyika?” (1 Wakorintho 1:13).

Wakristo wa Korintho ambao Mtume Paulo aliwaandikia barua walikuwa na tatizo la kubaguana.Kubaguana huku ni kama moto uliongezewa petroli ya maneno na majungu. Palikuwepo na kauli mbiu nne: Mimi ni wa Paulo, Mimi ni wa Apolo, Mimi ni wa Petro na Mimi ni wa Kristo. Waliwashabekia wahubiri mbalimbali lakini wote walikuwa wanamhubiri Kristu. Hatuna budi kuwa na kauli mbiu moja: Mimi ni wa Kristo. Naweza kusema: Umtafute Kristu: umpate Kristu:umpende Kristu. Kinachotakiwa ni kuwa na moyo wa umoja. “Usijali maneno ya watu wakisema kwamba una moyo wa umoja. Wanataka nini? Uwe Chombo cha kuvunjika vipandevipande mara tu kinaposhikwa?” Alihoji Josemaria Escriva (1902-1975) wa Hispania.

Mfano wa msumari unaonesha umuhimu wa umoja. Msumari usipokazwa sana au ulegeapo na kutoka ulipotiwa. Sehemu kubwa pia ulegea ama magurudumu ya mtambo huathirika au kuvunjika. Kazi hucheleweshwa. Pengine mtambo mzima huingiwa na ubovu. Josemaria Escriva alisema, “Usisahu kwamba umoja ndio alama ya uzima: kupotea umoja kuna maana ya kuoza, ishara dhahiri ya kuwa maiti.”

Jambo lingine la kuzingatia ni katika kuleta umoja ni kuvumiliana. Kuna hadithi ya wayahudi inayomhusu mzee wa miaka themanini aliyekutana na Abrahamu. Abrahamu alikuwa amekaa karibu na mlango wa nyumba yake. Mgeni huyo alimuomba Abrahamu akae kwake walau siku moja. Abrahamu alimuuliza mzee huyo, je wewe ni mtu anayeamini? Mzee huyo alijibu, naamini na kuabudu jua. Abrahamu alimfukuza na kusema kuwa hauwezi kulala hapa na kumuita mbwa mchafu. Usiku alipolala Abrahamu Mungu alimtokea katika ndoto na kumwambia: Abrahamu haukuweza kumvumilia mzee huyo walau kwa usiku mmoja. Mimi nimemvumilia miaka themanini. Katika dunia hii watu wana imani tofauti. Kinachohitajiwa ni kupendana, kuvumiliana na kueleweshana polepole bila kuleta mfarakano maana sisi ni wanadamu yaani watoto wa Adamu. Mungu ni Baba yetu sote. Biblia yasema, “Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wanchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao” (Matendo 17: 16).

Mwanga wa umoja una nguvu unaweza kuangaza, taifa zima na dunia nzima na kufukuza giza la kutoelewana na utengano.Tukumbuke kuwa kidole kimoja hakivunji chawa. Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu. Kitaifa umoja ni uhai, utengano ni kifo. “Bwana aliweka wengine sabini na wawili, aliowatuma wawili wawili wamtangulie katika miji na vijiji vyote alivyotaka kuvitembelea mwenyewe” (Luka 10:1).

 “Peke yetu tutafanya machache, pamoja tutafanya mengi,” alisema Helen Keller. Nguvu kubwa ya uongozi wowote ni umoja, na hatari kubwa kwa uongozi wowote ni utengano. Katika kuungana uongozi unasimama, katika kutengana uongozi unaanguka. Uongozi unahitaji moyo wa ushirikiano. Yesu kama kiongozi wa kuigwa hakufanya kazi peke yake. Tunasoma hivi katika Biblia, “Bwana aliweka wengine sabini na wawili, aliowatuma wawili wawili wamtangulie katika miji na vijiji vyote alivyotaka kuvitembelea mwenyewe” (Luka 10:1). Kifungu hiki cha Biblia kinabainisha ukweli kuwa macho mawili huona vizuri kuliko moja. Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.

 

Viongozi wazuri lazima washirikiane katika kugawana baraka na kugawana lawama, kugawana mema na kugawana shutuma. Anayefunga gori ni mmoja lakini timu yote husherekea. Wachezaji wote wanagawana furaha ya ushindi. Hivyo hivyo timu ikishindwa wachezaji wote wanagawana majonzi ya kushindwa. Ushirikiano katika mambo muhimu ni jambo muhimu. Yesu aliwataka wafuasi wake wasiwakatishe tamaa wale ambao walikuwa wanafanya miujiza kwa jina lake ingawa hawakuwa katika kundi moja. Kumbuka maneno ya Marko mwinjili katika Biblia, “Mwalimu, tulimuona mtu akiwafukuza pepo wabaya kwa jina lako, hata baada ya kuwa haandamani nasi, hivyo tukamkataza. Msimkataze, Yesu akanena, kwani hakuna anayeweza kutenda miujiza kwa jina langu akarudi kunisema vibaya. Kwa sababu asiye mpinzani wenu yu upande wenu.”

 

Yale yanayotuunganisha kama ndugu na binadamu ni ya muhimu kuliko yale yanayotutenganisha. Kuwa na lengo moja kama kuboresha maisha ya watu ni jambo ambalo halina budi liunganishe viongozi. Kwamba viongozi wanamhudumia mtu yule yule ni jambo la kuwaunganisha viongozi. Yesu alishirikiana na watu wa aina yote. Alishirikiana na matajiri waliomwazima mwanapunda. Alishirikiana na maskini wengine aliwatibu kama wakoma kumi. Alishirikiana na wenye dhambi kama Zaccheus na alishirikiana na watu wasio kuwa na hila kama Nathanaeli. Uongozi wake ulijumuisha wavuvi kama Simoni Petro na watoza ushuru kama Mathayo.

 

Vidole siku moja vilikuwa na ugomvi. Kidole gumba kilisema mimi ni bora sana, bila mimi hauwezi kushika kalamu, pili ni mnene na mfupi. Kidole cha shahada nacho kilianza kujisifu na kusema, mimi ni bora sana, bila mimi mzazi hawezi kuonya. Bila mimi walimu hawawezi kufundisha na kuonya. Kidole cha kati kilisema, tujipange mstari nani mrefu zaidi. Mimi ni bora. Kidole cha pete kilinyamazisha vidole vingine na kusema, mimi ni bora. Bila mimi maaskofu pete zao hawataziweka wapi? Bila mimi Bwana na Bibi arusi pete zao wataziweka wapi? Kidole cha mwisho kadogo kikasema, sisi vidole vidogi viwili ni bora. Mtu akiwa anasali na viganja viko kifuani sisi tunakuwa tumekaribia altare. Vidole kwa kawaida vinafanikiwa vinapounagana na si pale vinaposhindwa kushirikiana. 

Counter

You are visitor since April'08