Friday, July 25, 2014

NAMNA YA KUINGIA NA KUTOKA



                                            
                                                  JUMAPILI YA 17 YA MWAKA
  1. Fal 3: 5.7 -12
  1. Rum 8: 28 - 30
  1. Mt. 13: 44 - 52

“Ee Bwana…sijui inipasavyo kutoka wala kuingia…Basi umpe mtumishi wako moyo wa hekima” (1 Wafalme 3: 7-9). 
  
Maisha ni kuingia na kutoka. Ukiingia vizuri utatoka vizuri. Tunaingia shuleni na kutoka. Tunaingia sehemu za kazi na kutoka. Tunaingia Kanisani na kutoka. Tunaingia nyumbani na kutoka. Tunaingia hotelini na kutoka. Tunaingia kiwanjani na kutoka.Tunaingia dukani na kutoka. Tuingieje? Tutokeje? Kuna kitendawili kisemacho: aliingia kwenye nyama akatoka bila kula. Jibu ni kisu. Mwanafunzi akiingia shuleni kujifunza na kutoka bila ushindi ametoka kama kisu kwenye nyama.  Timu ya mpira ikiingia uwanjani na kutoka imefungwa bila kufunga ni kama kisu kuingia kwenye nyama na kutoka bila kula. Tunahitaji hekima kujua namna ya kuingia na kutoka. Suleimani au Solomoni alisali: “Ee Bwana…sijui inipasavyo kutoka wala kuingia…Basi umpe mtumishi wako moyo wa hekima” (1 Wafalme 3: 7-9).

Usiingie mikono mitupu. “Zenani” jina la watu wa kabila la Xhosa wa Afrika Kusini lina maana ya : “Umeleta nini?” Ni swali ambalo tunaulizwa. Kuna rafiki yangu alikuwa anafanya sherehe ya kuzaliwa. Aliniimbia nikifika mlangoni mwake nifungue mlango kwa miguu. Nikamuuliza kwa nini nifungue mlango kwa mguu akasema: “Ufungue kwa miguu kwa vile mikono itakuwa imebeba zawadi.” Hata tunapoingia nyumba ya Mungu tuingie tumebeba zawadi. Namna ya kuingia kanisani. Usiingie mikoni mitupu. Biblia yasema: “wala asitokee mtu mbele yangu mikono mitupu” (Kutoka 34:20).  Hata mamajusi hawakwenda kumsujudia mtoto Yesu mikono mitupu bali waliingia pangoni na zawadi. 

Ingia kwa mtazamo chanya. Watu wenye mtazamo chanya wanapendwa na kuheshimiwa kuliko ambao kila mara wanalalamika na kuwa na mtazamo hasi. “Baadhi ya watu hulalamika kwa vile maua ya waridi yaana miiba: ninashukuru miiba ina maua ya waridi,” alisema Alphonse Karr, katika kitabu kiitwacho, A Tour Round My Garden. Huo ni mtazamo chanya. Kuna padre aliyeingia hotelini kwa mtazamo chanya. Aliagiza kikombe cha kahawa ingawa ulikuwa wakati wa chakula cha mchana. Ilikuwa ni siku ya kufunga. Kwa mshangao aliona kijana muumini katika Kanisa lake akiwa na mlima wa nyama choma kwenye sahani yake. Kijana alisema: “Naamni padre sikakukwaza.” Padre kwa mtazamo wake chanya alisema: “Nachukulia kuwa umesahau kuwa siku ya leo ni siku ya kufunga.” Kijana alijibu: “Nakumbuka bila mashaka yoyote kuwa leo ni siku ya kufunga.” Padre kwa mtazamo chanya akasema: “Utakuwa mgonjwa na daktari bila shaka amekwambia kutofunga.” Kijana akasema: “Hapana nina afya nzuri sana.” Padre aliinua macho yake mbinguni na kusema: “ Ee Mungu huyu kijana anatoa mfano mzuri kwa kizazi hiki. Anakubali makosa yake badala ya kusema uongo.” Padre alikuwa na mtazamo chanya.

Ingia kwa salamu. “Asubuhi njema! Mchana mwema! Usiku mwema! Hizi sio salamu tu. Hizi ni baraka zenye nguvu, zinazoanzisha mambo mazuri. Kwa hiyo kama ni asubuhi, mchana au usiku akikisha salamu unaisema vizuri,” alisema  Franco Santoro. Bwana Yesu alisema: “Mnapoingia nyumba isalimuni” (Mathayo 13: 12). Kuna mtu aliingia kwenye nyumba na kumsalimu mwenye msongo wa mawazo: Habari za leo. Aijibu. Sijui. Akamsalimu tena . Habari za leo. Yeye alijibu kama za juzi. Alikuwa na msongo wa mawazo. Kusalimu ni kutakia mtu amani.

Ingia kwa shukrani. “Ingieni malango mwake kwa shukrani” (Zab 100:4).

Toka kwa malengo. Jua unapokwenda. Kutoka kwa malengo kunahitaji hekima. “Kama haujui unapokwenda, labda utaishia mahali fulani pengine,” alisema Laurence J. Peter. Kuna mtu ambaye alikuwa kwenye matatu kondakta akamwomba alipe nauli akasema: “Nauli nitakupa ila najiuliza naenda wapi?” Hakutoka nyumbani kwa malengo. Thomas Carlyle alisema: “Mtu asiye na lengo ni kama meli bila usukani – mtu aliyepotea, mtu bure, kabwela.”
Toka kwa furaha. Nyota njema huonekana asubuhi. Anza siku yako kwa kuvaa vazi la furaha. Njia ya kuwa na furaha ni kuwafanya wengine kuwa na furaha. “Sambaza upendo kila mahali unapokwenda. Mtu yeyote asije kwako bila kutoka akiwa na furaha zaidi,” alisema mwenye heri Teresa wa Calcutta. Kama mfalme Sulemaini au Solomoni tuombe hekima ya kujua namna ya kutoka na namna ya kuingia.

Saturday, July 19, 2014

MPE MUDA NA JIPE MUDA



                                       JUMAPILI YA 16 YA MWAKA A


1. Hek 12: 13. 16-19
2. Rum 8: 26-27
3. Mt 13: 24 -43

ACHENI VIKUE PAMOJA MPAKA WAKATI WA MAVUNO.” (MT 13: 30)


Kuna hadithi juu ya mzee mwenye miaka sabini  aliyemtembelea Abrahamu, akiomba hifadhi ya usiku mmoja. Mtu huyo alikataa kushiriki kwenye sala za kuomuomna Mungu mmoja. Abrahamu alimuuliza anaabudu Mungu yupi. Mzee huyo alisema anaabudu “moto.” Abrahamu alimwambia hawezi kumpokea mtu wa namna hiyo nyumbani kwake. Akamfukuza. Usiku Mungu alimtokea kwenye ndoto na kumwambia: “Abrahamu mtu huyu nimemvumilia kwa kipindi cha miaka sabini. Wewe huwezi kumvumilia hata usiku mmoja.” Mungu wetu anatupa muda ili tubadilike. “Lakini wewe, mtawala wa nguvu, unahukumu kwa upole, na kutuongoza kwa huruma nyingi; maana uwezo unao wa kutenda utakalo wakati wowote” (Hekima ya Sulemani 12: 18). “Yeye huvumilia, maana hapendi mtu yeyote apotee” (KKK Na 2822; 2 Pet 3:9; Mt 18:14).  Nyuma ya pazia ya kubadilika kuna subira. “Watu wote husifia subira, ingawa ni wachache wako tayari kuiweka katika matendo,” alisema Thomas a Kempis. “Kipande kikubwa cha barabara ya kwenda mbinguni kinapitiwa kwa spidi ya maili thelathini kwa saa,” alisema Evelyn Underhill. Taratibu ndio mwendo. “Subira ni mzizi na mlinzi wa fadhila zote,” alisema Papa Mtakatifu Gregory I.

Chini kwenye kitako cha subira kuna mbingu. Ni methali ya Kanuri. Kitakachopoa hakikuchomi. Ni methali ya Wahaya wa Tanzania. Roma haikujengwa siku moja. Tabia nzuri haijengwi siku moja. Kuna maneno yalikutwa yameandikwa kwenye ukuta wa Mnara wa London na wafungwa: “Sio taabu zinoua bali kukosa subira tunapozikabili taabu.” Hayo yalikuwa maneno ya wafungwa. Magereza ni nyumba za watakatifu watarajiwa iwapo watabadilika. “Subira ni kifyonza mshtuko kikubwa sana kati ya vifyonza mshtuko vyote. Jambo pekee ambalo unaweza kupata kwa kufanya mambo kwa haraka sana ni matatizo,” alisema Henri Fournier Alain.   Kwa kawaida tunataka ushauri umbadilishe mlevi baada ya saa moja. Tunataka mahubiri yawabadili watu wakitoka Kanisani. Tunataka kufumba na kufumbia mtu mbaya ageuke kuwa mzuri baada ya kupewa onyo au taadhari. Tunataka hotuba ya kisiasa ilete matokeo ya papo kwa papo. Tunahitaji kuwapa watu muda wa kubadilika. Tunahitaji kujipa muda wa kubadilika.

“Ufunguo wa kila kitu ni subira. Unapata kifaranga kwa kuangua yai na si kwa kuvunja yai,” alisema Arnold H. Glasow. “Tabia nzuri haijengwi ndani ya wiki moja au mwezi moja. Inajengwa kidogo kidogo, siku kwa siku. Juhudi za muda mrefu zenye subira zinahitajika kujenga tabia nzuri,” alisema mwanafalsafa Heraclitus. Katika Hadithi za Aesop kuna hadithi juu ya subira na uvumilivu.   

Kunguru akiwa nusu mfu kwa sababu ya kiu, aliliona gudulia au jagi la maji ambalo wakati fulani lilikuwa limejaa maji; kunguru alivyotia mdomo wake uliochongoka na mgumu kwenye jagi aligundua palikuwepo na maji kidogo yaliyobaki na hakuweza kuyafikia. Alijajaribu na kujaribu lakini haikuwezekana, mwishowe alikata tama. Baadaye alipata wazo. Alichukua changarawe na kuidondosha kwenye jagi. Alichukua changarawe nyingine na kuidondosha kwenye jagi. Alichukua changarawe nyingine na kuidondosha kwenye jagi. Alichukua changarawe nyingine na kuidondosha kwenye jagi. Alichukua changarawe nyingine na kuidondosha kwenye jagi. Alichukua changarawe nyingine na kuidondosha kwenye jagi. Alichukua changarawe nyingine na kuidondosha kwenye jagi. Alichukua changarawe nyingine na kuidondosha kwenye jagi. Alichukua changarawe nyingine na kuidondosha kwenye jagi. Hatimaye aliona maji yanakaribia mdomo wake. Alichukua changarawe nyingine chache na kuzidondosha kwenye jagi aliweza kunywa maji na kumaliza kiu yake. Ukweli tunaojifunza katika hadithi ni: uvumilivu una malipo. Ni ukweli huo huo tunaojifunza katika methali zifuatazo: tone tone ujaza ndoo. Polepole ndio mwendo. Mwenye subira mwishowe hupata (Igbo); Mwanamke mwenye subira ana utajiri wote uliopo duniani (Jabo); Atembeaye polepole hufika mbali (Luyia); Ukikuta mto umefurika subiri (Kiswahili); Subira ikificha kitu, hasira haitatafuta na kupata (Mamprussi); Usiwe mkosa subira unapouliza mpaka unakuwa na hasira wakati wa kusikiliza unapowadia (Misri ya zamani)

Katika Biblia kuna mfano wa magugu katikati ya ngano. “Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyependa mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu? Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Wataumwa wakamwambia, Badi, wataka twende tukayakusanye? Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue pamoja hata wakati wa mavuno” (Mathayo 13: 24-30).

Maneno haya ni muhimu: acheni vikue pamoja hata wakati wa mavuno. Watu wanasukumwa kuwagawanya binadamu katika makundi mawili wema na waovu, marafiki na maadui. Matokeo mabaya ya ubaguzi na mgawanyo wa namna hii ni kushindwa kuvumiliana na hamu ya kutatua kwa haraka na kwa fujo mivutano inayotokana nayo. Kama Mungu alivyo mtulivu na mvumilivu kwa watu wote, basi sisi nasi tuchukue msimamo wa namna hiyo hiyo. Mitume ambao wengi walikuwa wavuvi walifikiri wanajua mambo ya magugu na ngano. Walizoea kuosha nyavu, kuvua samaki na kuuza samaki. Na kama waliuliza Bwana hauwezi kuangamiza waovu kama tunavyoangamiza samaki waliooza? Hauwezi kutumia mbinu za wavuvi katika kilimo.

JIPE MUDA WA KUBADILIKA
Msitari kati ya dhambi na fadhila, wema na ubaya ni mwembamba. Msitari kati ya uongo na ukweli, magugu na ngano, baraka na laana, ni mwembamba. Mawili mawili yanaingiliana. Yameshikamana. Mdhambi wa leo anaweza kuwa mtakatifu wa kesho.

Kuna hadithi juu ya Wema na Uovu. Siku moja Wema na Uovu walikutana ufukweni mwa bahari. Waliambizana. “Tuvue nguo zetu na tuogelee baharini.” Baada ya kuogelea kwa muda baharini Uovu ulitoka haraka majini na kuja ufukweni na kuvaa nguo za Wema na kwenda zake. Baadaye Wema ulitoka majini na kuja ufukweni na kugundua kuwa nguo zake zimechukuliwa na Uovu. Wema ukiona aibu kwenda uchi ulivaa nguo za Uovu. Hadi leo Wema na Uovu wanatembea na mavazi ya uigizaji.

Baraka inaweza kuwa na sura ya balaa. “Baraka zetu zinazoeonekana mara nyingi zinajitokeza kwetu katika sura ya maumivu, upotezaji na kukatishwa tamaa; lakini tuwe na subira na muda mfupi tutaziona katika sura zake sahihi,” alisema Joseph Addison. Kama mambo ni hivyo jipe muda wa kubadilika. Iliripotiwa kuwa nyumba yake huko Washington imeungua moto, Thomas Hart Benton aliacha kikao cha baraza na kufika kwenye eneo la tukio la maafa. Akitazama mabaki alisema, “Inarahisisiha kuaga dunia. Kuna machache ya kuacha.” Alijipa muda na kukabili maafa kwa utulivu badala ya hasira. Usikate tamaa. “Mwenye haki ya kukata tamaa ni yule tu ambaye dhambi zake ni kubwa kama huruma ya Mungu,” alisema Mtakatifu Augustino wa Hippo (354 – 430). Kwa kawaida dhambi zetu ni ndogo zikilinganishwa na huruma ya Mungu.

MPE MUDA MWENZAKO
Mpe muda mwenzako. Tembo hakui siku moja (Methali ya kigio). Urefu haulakishwi (Methali ya Ndebele). Baba wa Kanisa Jerome alikuwa na haya ya kusema: “Kuna nafasi ya kutubu, tunaonywa kuwa tusimgoe ndugu yetu kwa haraka, kwa vile leo aliye na mafundisho potofu leo, kesho anaweza kukua katika hekima na kuanza kutetea ukweli, Bwana aliongeza maneno haya, msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo.”  Katika msingi huu, mpe Mungu muda afanye mabadiliko ndani mwako. Mpe mke wako muda. Wape watoto wako muda wakue katika hekima na umbo.


MPE MUNGU MUDA
“Hatuna budi kumgonja Mungu, kwa muda mrefu, kwa upole, katika upepo na unyevunyevu, katika ngurumo na radi, katika baridi na giza. Subiri, na atakuja. Haji kamwe kwa wale siosubiri,” alisema Frederick W. Faber.  Stanley alipoanza safari za uvumbuzi mwaka 1871 alikutana na Livingstone, kwa muda wa miezi kadhaa alikaa naye, lakini Livingstone hakumwambia Stanley mambo ya kiroho. Miezi yote hiyo Stanley alitazama kwa makini tabia ya Livingstone ambayo ilikuwa ya kushangaza akizingatia pia subira yake. Hakuelewa huruma aliyokuwa nayo Livingstone kwa waafrika. Kwa ajili ya Kristu na Injili yake mmisionari huyu alikuwa mwenye subira, asiyechoka, mwenye shauku, akitumika na kutumiwa na Bwana wake. Stanley aliandika: “Nilipoona subira isiyochoka, ari isiyokatizwa, wana wa Afrika waliopewa mwanga, niligeuka na kuwa Mkristu upandeni mwake, ingawa hakusema neno lolote kuhusu ukristo.”  Mungu alimgeuza Stanley polepole. Kazi ya kutakasa na kugeuza ni ya Roho Mtakatifu. “Lakini Roho anasaidia udhaifu wetu. Hatujui jinsi inavyotubidi kuomba. Roho mwenyewe anatuombea sisi kwa maombi yasiyosemeka. Lakini Mungu achunguzaye mioyo ajua nia ya Roho anayewaombea watakatifu kwa Mungu” (Warumi 8: 26-27).


FADHILA INASIMAMA KATIKATI
Subira ni fadhila ya kusimama katikakati. Kukosa subira ni jambo baya sana. Haraka haraka haina baraka. Na kuzidisha subira ni jambo baya sana. Mvumilivu hula mbivu akivumilia sana anakula mbovu. Subira kupita kiasi hutengeneza njia ya matatizo (Methali ya Kikuyu). Fadhila ya subira inasimama katikati ya kukosa subira na kusubiri kupitiliza. Methali ya wahaya inasema yote: Wamemsifu kuwa ni mkimbiaji mzuri akapitiliza kwao.



Saturday, July 12, 2014

MOYO WAKO UKOJE?

                                                          
                                                          JUMAPILI YA 15 MWAKA A

1. Isaya 55: 10-11
2.Warumi 8: 18-23
3. Mathayo 13: 1-23  (Mt 13: 1-9)

Ni moyo unaompelekea mtu mbinguni au motoni.” Ni methali ya Kiafrika.  Mungu hatazami sura ya nje anatazama yaliyomo moyoni. Mwenyezi Mungu alimkataa Eliabu hasiwe mfalme wa Israeli kwa vile Mungu hatazami sura ya nje, hatafuti warembo wa sura bali warembo wa moyo. Tunasoma katika Biblia, “Usiangalie sura yake na urefu wa kimo chake. Mimi nimemkataa kwani siangalii mambo kama wanavyoangalia binadamu wenye kufa. Binadamu huangalia uzuri wa nje, lakini mimi naangalia moyoni” ( 1 Samueli 16: 7). Katika Injili ya leo tunapewa aina nne za mioyo.

1.       MOYO WENYE TRAFIKI
Moyo wenye trafiki ni kama wapita njia ni wengi, magari ni mengi, baisikeli ni nyingi, boda boda ni nyingi. Katika Injili ya Mathayo tunaambiwa: “Mpanzi alikwenda kupanda mbegu. Katika kupanda, mbegu nyingine zilianguka kando ya njia. Wakaja ndege wa angani wakazidonoa” (Mathayo 13: 4). Moyo wetu ni kama njia. Kuna trafiki. Hoja si kuwepo kwa trafiki hoja ni namna ya kukabili trafiki. Trafiki isikuhumize kichwa. Mfano kwenye maisha ya ndoa ni kama msongamano wa magari ambapo hauchi nafasi kubwa ukiacha nafasi kubwa sana mwenye daladala anaingia. Ni bumper to bumper. Katika trafiki hiyo uenda kuna marafiki. Biblia yasema: “Msidanganyike! Urafiki mbaya huharibu tabia njema” (1 Wakorintho 15: 33).  Ni katika mtazamo huo inasemwa niambie rafiki yako nitakwambia tabia yako.  Kuna urafiki ambao unaunganishwa na jambo baya ukitoa jambo hilo baya hakuna urafiki. Wengine wanaunganishwa na ulevi, ukitoa ulevi hakuna urafiki. Wengine wanaunganishwa na umbeya, ukitoa umbeya hakuna urafiki. Urafiki wa kweli lazima uunganishwe na jambo zuri au na tabia nzuri.
Kuna watu wawili waliokuwa wanamjadili tajiri aliyefilisika. Mmoja akasema, “Tangia afilisike, nusu ya rafiki wake hawamtembeli tena, hawamjulii hali tena.” Mwingine akauliza habari juu ya nusu ya rafiki wake wengine. Mwenzake akamjibu: “Hawajui kama amefilisika.” Biblia yasema: “Kuna rafiki aliye mwenzi wa mezani, wala hatadumu karibu nawe siku ya taabu yako (Yoshua bin Sira 6:10). Rafiki katika taabu huyo ni rafiki wa kweli. Tusipokubali trafiki ituathiri mioyo itakuwa udongo mzuri. Simoni Petro alipotaka Bwana wetu Yesu Kristu aondokane na mpango wa kutukomboa Bwana Yesu alisema: “Ondoka kwangu” shetani.

2.       MOYO  WENYE MIAMBA AU MOYO MWAMBA
“Mbegu imeanguka kwenye mwamba” (Mathayo 13: 20). Mwamba haupenyeki. Ni moyo sugu. Dhamiiri imekufa. Mtu hayuko tayari kusamehe. Moyo unaweza kuwa mwamba kutoka na mabaya mtu aliyotendewa bila kusamehe. Mzee Joe alikuwa kufani kwenye kitanda cha mahuti. Kwa muda wa miaka mingi alikuwa hapatani na Bill, ambaye zamani alikuwa mmoja wa marafiki zake. Akitaka kunyosha mambo yake kabla ya kuaga dunia alimtuma Bill waongee na kumaliza mambo. Bill alipofika, Joe alimwambia kuwa anaogopa kwenda mbinguni akiwa na kinyongo naye. Kwa kusita na kwa kujikaza Joe aliomba msamaha kwa mambo aliyoyasema na kuyatenda. Alimwaakikishia Bill kuwa amemsamehe kwa makosa yote aliyomtendea. Mambo yote yalionekana kwenda vizuri mpaka hapo Bill alipojiandaa kuondoka. Alipokuwa anatoka chumbani, Joe alimuita, “Lakini kumbuka, nikipona, haya yote niliyosema hayana maana wala uzito.”
Yesu alisisitiza sana hitaji la kuwasamehe wengine kama tunavyosoma katika Biblia “Kisha Petro akamwendea Yesu, akamwuliza, ‘Je, ndugu yangu akinikosea, nimsamehe mara ngapi? Mara saba?’ Yesu akamjibu, ‘Sisemi mara saba tu, bali sabini mara saba.’” (Mathayo 18:21” Kusamehe mara sabini na saba kunamaanisha kusamehe kila mtu kila mara. Usipofanye hivyo moyo wako unakuwa mwamba.  Usiposamehe unafanya moyo wako uwe mwamba usiopenyeka.

“Jicho kwa jicho” mtazamo huo  utawaacha watu wengi wakiwa vipofu. “Jino kwa jino” mtazamo huo utawaacha watu wengi wakiwa vibogoyo. Kisasi kilicho bora ni kusahau. Ndivyo isemavyo methali ya Kiswahili. Lakini kisasi kilicho bora zaidi ni kusamehe.  Na pia kisasi kilichobora zaidi ni kutokuwa kama yule aliyekufanyia jambo baya ili pasiwepo watu wabaya wawili, yeye aliyekufanyia ubaya na wewe unayeshindwa kujibu ubaya kwa wema. Nelson Mandela alikuwa na haya ya kusema juu ya kusamehe waliomtendea vibaya: “Nilivyotembea kutoka mlangoni nakuelekea lango ambalo likuwa natokea na kwenda kwenye uhuru wangu, nilijua kuwa kama nisingeacha ukali wangu na chuki nyuma yangu, ningeendelea kuwa gerezani.” Kusamehe ni kumfungua mfungwa utagundua mfungwa ni wewe. Kabla ya kusamehe unakuwa kwenye gereza la chuki na kulipiza kisasi. Kumbuka chuki umchoma anayeitunza. “Msamaha ni manukato ambayo ua huacha kwenye kisigino kilicholikanyaga,” alisema Mark Twain. Kutosamehe ni kurudi nyuma. Nakubaliana na Libba Bray aliyesema: “Hatuwezi kurudi nyuma. Tunaweza tu kwenda mbele.”  MSAMAHA NI BREKI HAKUNA HAJA YA KUGONGA.
Mungu sio Adui wa Adui Zako
Martin  Niemoller alitoka katika gereza la Hitler akisema, “Ilininchukua muda mrefu kujifunza kuwa Mungu sio adui wa adui zangu. Na sio adui  wa maadui zake.” Kama unapenda watu wakupende nawe uwapende. Injili ya leo inatutaka tuwapende adui zetu: “Mmesikia kwamba imenenwa, ‘umpende jirani yako, na umchukie adui yako.’ Mimi lakini nawaambieni, wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowadhulumu…” (Mathayo 5:43-44).  Adui mpende. Ni methali ya Kiswahili. Usimchukie hasidi au adui yako. Adui zetu yafaa kuwachukulia makosa yao watutendeavyo. Huenda wakatubu na kuacha uovu wao. Tunaaswa na methali ya Kiswahili, Adui aangukapo mnyanyue. Ni methali nyingine ya Kiswahili kuhusu kumpenda adui na kumtendea mema. Ni ubinadamu kumsaidia adui yako akiwa na shida. “Tunapowachukia maadui wetu tunawapa uwezo juu yetu: uwezo juu ya usingizi wetu, hamu yetu ya chakula, shinikizo letu la damu, afya yetu na furaha yetu.” (Dale Carnegie) “Jinsi miti yote inavyojulikana kwa vivuli vyake, ndivyo hivyo watu wazuri wanajulikana kwa maadui wao.” (Methali ya Kichina).

3.       MOYO WENYE MIIBA
Bwana Yesu Kristu alitoa tafsiri ya miiba: “Mbegu imeanguka kati ya miiba kwa mtu anayelisikia neno, lakini shughuli za dunia na ulaghai wa mali hulisonga neno” (Mathayo 13:22).  Miiba ni shughuli nyingi na ulaghai wa mali. Shughuli nyingi ni miiba katika kutekeleza neno la Mungu. Shetani anaweza kukushawishi ili uwe na shughuli nyingi ili usishughulikie jambo lilo muhimu. Eva alikuwa msaidizi wa Adamu na Adamu msaidizi wa Eva katika raha na shida katika magonjwa na afya. Lakini Eva alipokuwa anajaribiwa na Adamu, Adamu alikuwa na shughuli nyingi hakuwa pamoja na Eva. Pengine shughuli nyingi zinaweza kuwa namna ya uvivu. Nina shughuli nyingi sitaenda Kanisani. Hapo kuna uvivu wa kwenda Kanisani. Miiba hipo nje. Miamba hipo ndani.


4.       MOYO WENYE UDONGO WENYE RUTUBA
“Mbegu imeanguka katika udongo wenye rutuba kwa mtu anayelisikia neno na kulitunza moyoni. Akazaa na kutoa matunda, huyu mia, na huyu sitini, na mwingine thalathini” (Mathayo 13: 23). Hapa kuna udongo uliotayari kulimwa. Utayari ni jambo muhimu. Kuna hadithi ya Bwana aliyekuwa tajiri sana. Alipofika mbinguni alikaribisha kwenye nyumba ya nyasi. Alipinga sana. Aliambiwa hiyo ndiyo nyumba umeandaliwa. Aliuliza, “Hiyo mansion pale ni ya nani?” “Aliambiwa ni ya mpishi wako.”  “Inakuwaje ana nyumba nzuri sana kunizidi. Aliambiwa nyumba hapa zinajengwa kutokana na vifaa unavyotuma mbinguni. Wewe ulituma nyasi na miti.  Ukichukua glasi ya kuweka maji  ukakuta ni chafu ina mende waliokufa hauwezi kuweka maji. Ukitaka kunywa supu ukakuta bakuli ni chafu hauwezi kuweka supu yako. Mungu anataka kukupa neema lakini anajiuliza niweke wapi neema hizi? 

Saturday, July 5, 2014

SAFIRI NA MZIGO MWEPESI



                                                               
                                                             JUMAPILI YA 14 YA MWAKA A
1.       Zak 9: 9-10
Rum 8: 9.11-13
2.       Mt. 11: 25-30

“Mjitwike nira yangu na kujifunza kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu moyoni, nanyi mtazipatia roho zenu raha. Kwani nira yangu si nzito, na mzigo wangu ni rahisi kuuchukua” (Mathayo 11: 29 -30).   
Maisha ni safari na safari ni safari. Ni vizuri kusafiri na mzigo mwepesi. Ukitumia usafiri wa ndege lazima kufuata masharti ya uzito wa mzigo. Usizidishe kilo. Kama unaambiwa uwe na mzigo wa kilo ishirini ziwe kilo ishirini. “Hakuna ambaye anaangushwa na mzigo wa leo. Ni wakati mzigo wa kesho unapoongezwa kwenye mzigo wa leo ndipo uzito unaongezeka kuliko mtu anavyoweza kunyanyua. Usijitwike mizigo hivyo,” alisema George MacDonald. Katika mtazamo huu Bwana Yesu alipowafundisha wafuasi wake sala ya Baba Yetu alisema: “Utupe leo mkate wetu,” hatusemi utupe mkate wa kesho. Ni kujitwika mizigo ya kesho. Pia Bwana wetu Yesu Kristo alipendekeza kuchukua mzigo wake ambao ni mwepesi. “Mjitwike nira yangu na kujifunza kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu moyoni, nanyi mtazipatia roho zenu raha. Kwani nira yangu si nzito, na mzigo wangu ni rahisi kuuchukua” (Mathayo 11: 29 -30). Mzigo wa Yesu ni mzigo wa unyenyekevu. Huu ni mzigo mwepesi kuliko mzigo wa majivuno. Mzigo wa Yesu ni mzigo wa upendo. Huu ni mzigo mwepesi na rahisi kuliko chuki.
  “Nimeamua kujishughulisha na upendo. Chuki ni mzigo mzito sana haubebeki,” alisema  Martin Luther King, Jr. mpigania haki za binadamu. Anatwaambia kuwa upendo ni mzigo mwepesi. Amani ukilinganisha na vurugu ni mzigo mwepesi. Kuna mtu alimwambia jamaa mmoja: “Unasema wewe ni mpenda amani halafu unaenda na kumtupia tofali Casey?” Huyu mtu alijibu: “Casey alikuwa mtulivu baada ya kumtupia jiwe ujakosea mimi nimpenda amani.” Wanaofanyiwa ubaya wakiwa watulivu sio kwamba kuna amani ila wanataka kubeba mzigo mwepesi mzigo wa amani.
AMANI NI MZIGO MWEPESI
 Yesu aliwaambia mitume wake: “Kila nyumba mnayoingia, semeni kwanza, ‘Amani iwe na nyumba hii.” Amani haishurutushwi isipokuwa ni mapato ya kupokeana na kuelewana. “Ukitaka amani, ifanyie kazi haki,” alisema Papa Paulo VI aliyeliongoza Kanisa Katoliki mwaka 1963 hadi 1978. Bila haki hamna amani. Mambo yote mazuri yanazungumzia amani: Maendeleo, upendo, huruma, ukarimu, kujali, utu yote hayo yanaweza kuwa majina mapya ya amani. Kwa namna hii amani ni mzigo mwepesi.
Hellen Keller alikuwa mtoaji mada za kutia watu matumaini alikuwa kipofu na kiziwi. Aliulizwa: “Kama ungeombwa kuomba zawadi moja ungeomba zawadi ipi?” Walitegemea aombe zawadi ya kusikia au kuona. Kwa mshangao wa wengi alisema: “Ningeomba amani duniani.” Amani ni mzigo mwepesi kuliko kutoona au kutosikia kadiri ya mtazamo wa Hellen Keller. Tudumishe amani. Tufundishe amani. Tuombe amani. 

UPENDO NI MZIGO MWEPESI
Yesu aliwatuma wafuasi wake sabini na wawili aliowatuma wawili wawili na kuwaambia “Msichukue mfuko wa fedha, wala mkoba, wala viatuu” (Luka 10: 4). Alitaka wasafiri na mzigo mwepesi. Kwanza wasisafiri na mzigo wa ubaguzi . Aliwatuma kwa watu wote. Namba sabini na mbili inawakilisha mataifa yote na watu wote. Kitabu cha mwanzo 10: 2-31 kinazungumzia namba kamili ya wazaliwa wa watoto wa Nuhu waliofanya idadi ya watu wa ulimwengu baada ya kutokea gharika na watu wote kufa hao ndio waliobaki. Injili haibinafishwi au kuhodhiwa na wachache. 
 Aliwatuma wawili wawili kutukumbusha amri kuu ya upendo yenye amri mbili:kumpenda Mungu na kumpenda jirani. Upendo huu ni mzigo mwepesi. “Chuki ni mzigo mzito wa kubeba, unaweza kumhumiza anayechukia kuliko anayechukiwa,” alisema Coretta Scott King.  Aliwatuma wawili wawili kuonesha umuhimu wa jumuiya. Ubinafsi na umimi ni mzigo mzito. Kuvaa uso wa usinikaribie. Ni kubeba mzigo mzito. Kuwa na mtazamo wa wengine watafanya ni kubeba mzigo mzito. Kuna mtoto alilalamikia kitanda walipokuwa wanalala anasema ni kigumu na kaka yake anachukua nusu. Mama akauliza kwa nini hasichukue nusu. Kijana akazidi kulalamika: “Anachukua nusu ya nusu kitanda.” Kusema kweli hiyo ni robo kumbe mtoto huyo alikuwa anachukua robo tatu na hajaridhika. Umimi au ubinafsi ni mzigo mzito. “Upendo hauisi mzigo, haufikiri tatizo, unajaribu lililo juu ya nguvu yake, hautoi sababu ya haiwezekani; unafikiria kuwa kila kitu ni kadiri ya sheria kwa ajili yake na yote yanawezekana,” alisema Thomas a Kempis.
Chuki bila sababu au maamuzi mbele kwa vile mtu ametoka kabila fulani au eneo fulani ni mzigo mzito. “Chuki bila sababu ni mzigo ambao unachanganya yaliyopita, na kutishia yajayo na kufanya yaliyopo yasifikike,” alisema Maya Angelou. Pia kuna methali ya Wayahudi isemayo: Maoni ambayo yana msingi wake katika chuki bila sababu yanaendelezwa na matumizi ya mabavu.
MAKOSA NI MZIGO MZITO
Makosa yetu ya zamani tusipoyaungama na kuyatubu  tukiyabeba tunabeba mizigo mizito. Mtunga zaburi alisema: “Kwani makosa yangu yamenifunika kichwa, kama mzigo mzito mno yamenilemea” (Zaburi 38: 5). Makosa ni mzigo. Yakobo alipotoa baraka na wosia alimwambia mtoto wake “Reuben, wewe ndiwe mzaliwa wangu wa kwanza, nguvu yangu, tunda la kwanza la uwezo wangu wa kuzaa, imekupasa kuwapita wengine kwa ukuu, kuwapita kwa nguvu; lakini ulifurika kama maji: wewe hutakuwa na ukuu. Kwa sababu ulikipanda kitanda cha baba yako, ulikichafua kitanda changu ulipokipanda” (Mwanzo 49: 3-4). Reuben alipoteza haki zake zote za mtoto wa kwanza kwa sababu ya dhambi yake ya kujamiana maharimu (Maharimu ni ndugu ambaye mtu hawezi kumwoa au kuolewa naye kwa sababu ya unasaba wao) Alikuwa na mambo mazuri matano na kosa moja. Kosa moja likawa uzito wa kumfanya kukosa ukuu au mafanikio makubwa.  Unapoungama makosa yako kwa Mungu unatua mzigo. Utakatifu ni mzigo mwepesi.  Mtunga zaburi anasema: “Umwekee Bwana mzigo wako, naye atakutegemeza” (Zaburi 55:23).
 “Mzigo wa kujifungia hauna uzito. Ni methali ya Kiswahili. Mtu anapojifungia mwenyewe mzigo hujaribu kwa kadiri ya uwezo au nguvu zake za kuubeba. Hawezi kamwe kujifungia mzigo mzito wa kumshinda. Jifungie mzigo wa upendo. Unapowafariji wengine unawabebea mzigo. “Hakuna anayejua uzito wa mzigo wa mwingine,” alisema George Herbert. “Mungu ameamrisha kuwa tujifunze kubebeana mzigo; kwa kuwa hakuna asiyenakosa, hakuna asiye na mzigo; hakuna anayejitosheleza,” alisema Thomas Kempis.
KISASI NI MZIGO MZITO
Katika msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristu tunaona mzigo mwepesi. Yeye aliwasamehe waliomkosea. Msamaha ni mzigo mwepesi. Katika msingi huu mtume Paulo alisema: “Mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu chochote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu” (Gal 6: 14-18). Kisasi ni mzigo mzito. Samehe kwa ajili ya afya yako. Miaka kadhaa iliyopita kampuni nyingi za kiamerika baada ya kupata ruhusa ya serikali zilizika takataka zilizokuwa zimajazwa kwenye mapipa ya vyuma. Walifunga mapipa yao vizuri sana na kuyazika. Baada ya muda mfupi mapipa hayo yalianza kuvuja na sumu hiyo ilionekana kwenye uso wa dunia na kusababisha uharibifu mkubwa sana. Walijaribu kuzika vitu vilivyokuwa na nguvu nyingi sana. Nasi mambo ni hivyo katika suala la kutosamehe. Lazima tusamehe ili sumu isitudhuru. Tunasoma hivi katika kitabu cha mithali: “Afichaye makosa yake hafanikiwi” (Mithali 28: 13). Msamaha ni mzigo mwepesi.
KUPOKEA HABARI NJEMA NI MZIGO MWEPESI
“Na mkiingia mjini wasiwapokee, nendeni nje katika barabara zake, mkaseme, “Hata mavumbi ya mji wenu yanayogandamana na miguu yetu tunawakung’utia” (Luka 10: 11). Ni kama laana. Lakini ukweli wa maisha. Ukinunua gari wanakuelezea matumizi yake. Kwamba baada ya kilometa kadhaa badilisha oil na belt usipofanya hivyo haupokei habari njema laana inakuwa kwa gari. Litaharibika haraka na hata kusababisha ajali. Kupokea habari njema ni mzigo mwepesi.
 TRAVEL LIGHT: LAY ASIDE EXTRA BAGGAGE

(Written in 2008 by Fr. Faustin Kamugisha)

 

A time to travel light is a time to lose. We are on a journey to heaven. As a matter of fact we are pilgrims. The less “baggage” we carry the more we can concentrate on essentials. Jesus told his disciples, “Take nothing for the journey.” The spirit of Christ is that we free ourselves of the superfluous, the unnecessary, and the piles of extra “things” that weigh us down physically and spiritually.  Excessive baggage can be a fear of criticism. A man was driving to town one morning with his wife. The weather was hot and the windows were rolled up. “Honey,” he said, “Please open the windows.” “Are you crazy? She exclaimed. “Do you want to let our neighbours driving in the next lane know our car isn’t air conditioner?” The man’s wife was afraid of being criticized.


 Excessive baggage can be an emotional baggage like anger. A boy once asked, “Dad, how do wars begin?” “Well, take the First World War,” said his father. “That got started when Germany invaded Belgium.” Immediately his wife interrupted him: “Tell the boy the truth. It began because somebody was murdered.” The husband drew himself up with n air of superiority and snapped back, “Are you answering the question, or am I?” Turning her back upon him in a huff, the wife walked out of the room and slammed the door as hard as she could. When the dishes stopped rattling in the cupboard, an uneasy silence followed, broken at length by the son when he said, “Daddy, you don’t have to tell me any more; I know now!” We all carry a lot of emotional baggage around with us.

We have to travel light: take nothing for the journey. We have to get rid of every weight and sin as the writer of the book of Hebrews advises us. “Therefore, since we are surrounded by so great a cloud of witnesses, let us strip off every weight and let lid ourselves of the sin that clings to us and persevere in running the race that lies before us while keeping our eyes fixed on Jesus, the leader and perfecter of faith. For the sake of the joy that lay before him he endured the cross, despising its shame, and has taken his seat at the right of the throne of God” (Hebrews 12: 1 – 2).  In the Christian life we have excessive baggage or discarding things. There may be habits, pleasure, self-indulgences, associations which hold us back. We must shed them off. 

In the Christian life we have a means. That means is steadfast endurance. This is a patience, which does not sit down and accepts things but the patience, which masters them. In the Christian life we have an example. That example is Jesus himself, for the sake of the joy that lay before him he endured the cross, despising its shame. 
We need to shed off buying addiction. There are people who are addicted to buying. Spending addiction can be a weight, which weighs us down spiritually and physically. The attitude of the spending addicts is that “I consume therefore I am.”  We do not imitate the high school boy who had twenty-six sweaters, most of which he never wore or the wife of one of the American ambassadors to England who had over one thousand pairs of shoes
There are people who are obsessive electronics equipment buyers, obsessive newspapers buyers, and obsessive bread buyers. There are people who think that if they have enough things to prove success the neighbours would think more of them. Many compulsive shoppers admit they do not love to shop, but rather love to buy. Shopping provides instant gratification. Parents travel light. Teachers travel light. Doctors travel light. Nurses travel light. Children travel light. Students travel light. Religious nuns travel light. Politicians travel light. Husbands travel light. Wives travel light.


Counter

You are visitor since April'08