Saturday, July 19, 2014

MPE MUDA NA JIPE MUDA



                                       JUMAPILI YA 16 YA MWAKA A


1. Hek 12: 13. 16-19
2. Rum 8: 26-27
3. Mt 13: 24 -43

ACHENI VIKUE PAMOJA MPAKA WAKATI WA MAVUNO.” (MT 13: 30)


Kuna hadithi juu ya mzee mwenye miaka sabini  aliyemtembelea Abrahamu, akiomba hifadhi ya usiku mmoja. Mtu huyo alikataa kushiriki kwenye sala za kuomuomna Mungu mmoja. Abrahamu alimuuliza anaabudu Mungu yupi. Mzee huyo alisema anaabudu “moto.” Abrahamu alimwambia hawezi kumpokea mtu wa namna hiyo nyumbani kwake. Akamfukuza. Usiku Mungu alimtokea kwenye ndoto na kumwambia: “Abrahamu mtu huyu nimemvumilia kwa kipindi cha miaka sabini. Wewe huwezi kumvumilia hata usiku mmoja.” Mungu wetu anatupa muda ili tubadilike. “Lakini wewe, mtawala wa nguvu, unahukumu kwa upole, na kutuongoza kwa huruma nyingi; maana uwezo unao wa kutenda utakalo wakati wowote” (Hekima ya Sulemani 12: 18). “Yeye huvumilia, maana hapendi mtu yeyote apotee” (KKK Na 2822; 2 Pet 3:9; Mt 18:14).  Nyuma ya pazia ya kubadilika kuna subira. “Watu wote husifia subira, ingawa ni wachache wako tayari kuiweka katika matendo,” alisema Thomas a Kempis. “Kipande kikubwa cha barabara ya kwenda mbinguni kinapitiwa kwa spidi ya maili thelathini kwa saa,” alisema Evelyn Underhill. Taratibu ndio mwendo. “Subira ni mzizi na mlinzi wa fadhila zote,” alisema Papa Mtakatifu Gregory I.

Chini kwenye kitako cha subira kuna mbingu. Ni methali ya Kanuri. Kitakachopoa hakikuchomi. Ni methali ya Wahaya wa Tanzania. Roma haikujengwa siku moja. Tabia nzuri haijengwi siku moja. Kuna maneno yalikutwa yameandikwa kwenye ukuta wa Mnara wa London na wafungwa: “Sio taabu zinoua bali kukosa subira tunapozikabili taabu.” Hayo yalikuwa maneno ya wafungwa. Magereza ni nyumba za watakatifu watarajiwa iwapo watabadilika. “Subira ni kifyonza mshtuko kikubwa sana kati ya vifyonza mshtuko vyote. Jambo pekee ambalo unaweza kupata kwa kufanya mambo kwa haraka sana ni matatizo,” alisema Henri Fournier Alain.   Kwa kawaida tunataka ushauri umbadilishe mlevi baada ya saa moja. Tunataka mahubiri yawabadili watu wakitoka Kanisani. Tunataka kufumba na kufumbia mtu mbaya ageuke kuwa mzuri baada ya kupewa onyo au taadhari. Tunataka hotuba ya kisiasa ilete matokeo ya papo kwa papo. Tunahitaji kuwapa watu muda wa kubadilika. Tunahitaji kujipa muda wa kubadilika.

“Ufunguo wa kila kitu ni subira. Unapata kifaranga kwa kuangua yai na si kwa kuvunja yai,” alisema Arnold H. Glasow. “Tabia nzuri haijengwi ndani ya wiki moja au mwezi moja. Inajengwa kidogo kidogo, siku kwa siku. Juhudi za muda mrefu zenye subira zinahitajika kujenga tabia nzuri,” alisema mwanafalsafa Heraclitus. Katika Hadithi za Aesop kuna hadithi juu ya subira na uvumilivu.   

Kunguru akiwa nusu mfu kwa sababu ya kiu, aliliona gudulia au jagi la maji ambalo wakati fulani lilikuwa limejaa maji; kunguru alivyotia mdomo wake uliochongoka na mgumu kwenye jagi aligundua palikuwepo na maji kidogo yaliyobaki na hakuweza kuyafikia. Alijajaribu na kujaribu lakini haikuwezekana, mwishowe alikata tama. Baadaye alipata wazo. Alichukua changarawe na kuidondosha kwenye jagi. Alichukua changarawe nyingine na kuidondosha kwenye jagi. Alichukua changarawe nyingine na kuidondosha kwenye jagi. Alichukua changarawe nyingine na kuidondosha kwenye jagi. Alichukua changarawe nyingine na kuidondosha kwenye jagi. Alichukua changarawe nyingine na kuidondosha kwenye jagi. Alichukua changarawe nyingine na kuidondosha kwenye jagi. Alichukua changarawe nyingine na kuidondosha kwenye jagi. Alichukua changarawe nyingine na kuidondosha kwenye jagi. Hatimaye aliona maji yanakaribia mdomo wake. Alichukua changarawe nyingine chache na kuzidondosha kwenye jagi aliweza kunywa maji na kumaliza kiu yake. Ukweli tunaojifunza katika hadithi ni: uvumilivu una malipo. Ni ukweli huo huo tunaojifunza katika methali zifuatazo: tone tone ujaza ndoo. Polepole ndio mwendo. Mwenye subira mwishowe hupata (Igbo); Mwanamke mwenye subira ana utajiri wote uliopo duniani (Jabo); Atembeaye polepole hufika mbali (Luyia); Ukikuta mto umefurika subiri (Kiswahili); Subira ikificha kitu, hasira haitatafuta na kupata (Mamprussi); Usiwe mkosa subira unapouliza mpaka unakuwa na hasira wakati wa kusikiliza unapowadia (Misri ya zamani)

Katika Biblia kuna mfano wa magugu katikati ya ngano. “Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyependa mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu? Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Wataumwa wakamwambia, Badi, wataka twende tukayakusanye? Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue pamoja hata wakati wa mavuno” (Mathayo 13: 24-30).

Maneno haya ni muhimu: acheni vikue pamoja hata wakati wa mavuno. Watu wanasukumwa kuwagawanya binadamu katika makundi mawili wema na waovu, marafiki na maadui. Matokeo mabaya ya ubaguzi na mgawanyo wa namna hii ni kushindwa kuvumiliana na hamu ya kutatua kwa haraka na kwa fujo mivutano inayotokana nayo. Kama Mungu alivyo mtulivu na mvumilivu kwa watu wote, basi sisi nasi tuchukue msimamo wa namna hiyo hiyo. Mitume ambao wengi walikuwa wavuvi walifikiri wanajua mambo ya magugu na ngano. Walizoea kuosha nyavu, kuvua samaki na kuuza samaki. Na kama waliuliza Bwana hauwezi kuangamiza waovu kama tunavyoangamiza samaki waliooza? Hauwezi kutumia mbinu za wavuvi katika kilimo.

JIPE MUDA WA KUBADILIKA
Msitari kati ya dhambi na fadhila, wema na ubaya ni mwembamba. Msitari kati ya uongo na ukweli, magugu na ngano, baraka na laana, ni mwembamba. Mawili mawili yanaingiliana. Yameshikamana. Mdhambi wa leo anaweza kuwa mtakatifu wa kesho.

Kuna hadithi juu ya Wema na Uovu. Siku moja Wema na Uovu walikutana ufukweni mwa bahari. Waliambizana. “Tuvue nguo zetu na tuogelee baharini.” Baada ya kuogelea kwa muda baharini Uovu ulitoka haraka majini na kuja ufukweni na kuvaa nguo za Wema na kwenda zake. Baadaye Wema ulitoka majini na kuja ufukweni na kugundua kuwa nguo zake zimechukuliwa na Uovu. Wema ukiona aibu kwenda uchi ulivaa nguo za Uovu. Hadi leo Wema na Uovu wanatembea na mavazi ya uigizaji.

Baraka inaweza kuwa na sura ya balaa. “Baraka zetu zinazoeonekana mara nyingi zinajitokeza kwetu katika sura ya maumivu, upotezaji na kukatishwa tamaa; lakini tuwe na subira na muda mfupi tutaziona katika sura zake sahihi,” alisema Joseph Addison. Kama mambo ni hivyo jipe muda wa kubadilika. Iliripotiwa kuwa nyumba yake huko Washington imeungua moto, Thomas Hart Benton aliacha kikao cha baraza na kufika kwenye eneo la tukio la maafa. Akitazama mabaki alisema, “Inarahisisiha kuaga dunia. Kuna machache ya kuacha.” Alijipa muda na kukabili maafa kwa utulivu badala ya hasira. Usikate tamaa. “Mwenye haki ya kukata tamaa ni yule tu ambaye dhambi zake ni kubwa kama huruma ya Mungu,” alisema Mtakatifu Augustino wa Hippo (354 – 430). Kwa kawaida dhambi zetu ni ndogo zikilinganishwa na huruma ya Mungu.

MPE MUDA MWENZAKO
Mpe muda mwenzako. Tembo hakui siku moja (Methali ya kigio). Urefu haulakishwi (Methali ya Ndebele). Baba wa Kanisa Jerome alikuwa na haya ya kusema: “Kuna nafasi ya kutubu, tunaonywa kuwa tusimgoe ndugu yetu kwa haraka, kwa vile leo aliye na mafundisho potofu leo, kesho anaweza kukua katika hekima na kuanza kutetea ukweli, Bwana aliongeza maneno haya, msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo.”  Katika msingi huu, mpe Mungu muda afanye mabadiliko ndani mwako. Mpe mke wako muda. Wape watoto wako muda wakue katika hekima na umbo.


MPE MUNGU MUDA
“Hatuna budi kumgonja Mungu, kwa muda mrefu, kwa upole, katika upepo na unyevunyevu, katika ngurumo na radi, katika baridi na giza. Subiri, na atakuja. Haji kamwe kwa wale siosubiri,” alisema Frederick W. Faber.  Stanley alipoanza safari za uvumbuzi mwaka 1871 alikutana na Livingstone, kwa muda wa miezi kadhaa alikaa naye, lakini Livingstone hakumwambia Stanley mambo ya kiroho. Miezi yote hiyo Stanley alitazama kwa makini tabia ya Livingstone ambayo ilikuwa ya kushangaza akizingatia pia subira yake. Hakuelewa huruma aliyokuwa nayo Livingstone kwa waafrika. Kwa ajili ya Kristu na Injili yake mmisionari huyu alikuwa mwenye subira, asiyechoka, mwenye shauku, akitumika na kutumiwa na Bwana wake. Stanley aliandika: “Nilipoona subira isiyochoka, ari isiyokatizwa, wana wa Afrika waliopewa mwanga, niligeuka na kuwa Mkristu upandeni mwake, ingawa hakusema neno lolote kuhusu ukristo.”  Mungu alimgeuza Stanley polepole. Kazi ya kutakasa na kugeuza ni ya Roho Mtakatifu. “Lakini Roho anasaidia udhaifu wetu. Hatujui jinsi inavyotubidi kuomba. Roho mwenyewe anatuombea sisi kwa maombi yasiyosemeka. Lakini Mungu achunguzaye mioyo ajua nia ya Roho anayewaombea watakatifu kwa Mungu” (Warumi 8: 26-27).


FADHILA INASIMAMA KATIKATI
Subira ni fadhila ya kusimama katikakati. Kukosa subira ni jambo baya sana. Haraka haraka haina baraka. Na kuzidisha subira ni jambo baya sana. Mvumilivu hula mbivu akivumilia sana anakula mbovu. Subira kupita kiasi hutengeneza njia ya matatizo (Methali ya Kikuyu). Fadhila ya subira inasimama katikati ya kukosa subira na kusubiri kupitiliza. Methali ya wahaya inasema yote: Wamemsifu kuwa ni mkimbiaji mzuri akapitiliza kwao.



Counter

You are visitor since April'08