Saturday, December 31, 2016

TAZAMA NYUMA USHUKURU TAZAMA MBELE UFIKIRI


                            Sherehe ya Maria Mama wa Mungu
                                                  1 Januari 2017
1. Hes 6: 22-27
2. Gal 4: 4-7
3. Lk 2: 16-21

Furaha bila shukrani nini? Ipo wapi shukrani bila kumfikiria Mungu? Tunapomaliza mwaka wa 2016 tunafurahi. Furaha haikamiliki bila kumshukuru Mungu. Sababu ya kushukuru tunayo, tumemaliza mwaka salama. Nia ya kushukuru tunayo, penye nia pana njia. Uwezo wa kushukuru tunao. Tunaweza kusema au kuandika au kuashiria tunashukuru.  “Shukrani inazaliwa katika mioyo ambayo huchukua muda kuhesabu baraka za wakati uliopita,” alisema Charles E. Jefferson. Tulipoanza mwaka 2016 tulisikia maneno haya: “Bwana akubarikie na kukulinda; Bwana akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili; Bwana akuinulie uso wake, na kukupa amani” (Hesabu 6: 22-27). Liwalo na liwe ukweli ni kwamba umebarikiwa. Baraka ulizombewa umezipata. Tazama nyuma shukuru. Mungu anapokubariki ina maana anakufikiria. Mwaka mzima wa 2016 umefikiriwa na Mungu. Tunapofunga mwaka tutafakari maneno haya ya busara ya mtu fulani.
“Leo kwenye basi niliona msichana mzuri sana akiwa na nywele za dhahabu. Nilimwonea wivu-alionekana mzuri sana name nikafikiri ningekuwa mzuri kama yeye. Ghafla aliposimama kutelemka alikuwa na mguu mmoja na gongo la kutembelea aliponipita alitabasamu. Ee Mungu, nisamehe ninapolalamika. Nina miguu miwili – dunia ni yangu. Nilienda dukani kununua pipi. Kijana aliyekuwa anauza pipi alikuwa mchangamfu, nilizungumza naye aliniambia: ‘Ni vizuri kuzungumza na watu kama wewe, unaona mimi ni kipofu.’ Mungu nisamehe ninapolalamika; nina macho mawili – dunia ni yangu. Nilipotelemka chini kwenye mtaa niliona mtoto ana macho ya bluu. Alisimama na kutazama watoto wengine wakicheza. Ilionekana hakufahamu jambo la kufanya. Nilisimama na kumuuliza; ‘Kwa nini haungani na watoto wengine  kucheza?’ Alinitazama bila kusema neon. Nilitambua hauwezi kusikia. Ee Mungu, nisamehe ninapolalamika. Nina masikio mawili – dunia ni yangu. Pamoja na miguu ya kunipeleka kule ninakotaka kwenda, pamoja na mcho ya kuona kuchwa kwa kujua, pamoja na masikio ya kusikia lile ambalo nitalijua, ee Mungu nisamehe ninapolalamika. Nimebarikiwa dunia ni yangu kweli.”
Mshukuru Mungu  ameuvika taji mwaka 2016. Tunasoma hivi katika Zaburi: “Umeuvika mwaka taji ya mema yako; mapito yako yamejaa mafuta (Zaburi 65:12). Hata kuwepo kwa maadui katika maisha yako Mungu amekusaidia kuvaa taji. Wakati mwingine ili kufanikiwa katika maisha unahitaji maadui. Unahitaji watu watakaokuzomea ili umkimbilie Mungu.  Unahitaji watu watakaojaribu kukutia hofu ili uwe na ujasiri. Unahitaji watu watakaosema “HAPANA” ili ujifunze kujifanyia. Unahitaji watu watakaokutakatisha tamaa ili uweke matumaini yako yote kwa Mungu. Unahitaji watu watakaokufanya upoteze kazi yako ili uazishe biashara yako. Unahitaji watu watakaokuuza kama Yozefu ili uweze kwenda Misri  kuwa Waziri Mkuu katika nchi ya utumwa. Unahitaji Mwenye nyumba katili unapopangisha nyumba yako ili usipate faraja kwenye nyumba ya wengine uweze kujenga nyumba yako. Haya yanaitwa mapito. Uenda umepitia haya mwaka 2016. Hiyo ni vunja vunja ya Mungu ili aweze kukubariki. Mungu anavunja ili kubariki. Teke la adui mgongoni linakusogeza mbele.
Tazama mbele ufikiri. Papa Fransisko alisema kuna lugha tatu: ya kwanza fikiria vizuri, ya pili hisi vizuri, ya tatu tenda vizuri. Bikira Maria alifikiria vizuri. “Lakini Maria aliyaweka na kuyatafakari mambo hayo yote moyoni mwake” (Luka 2:19). Bikira Maria alifikiri vizuri, alihisi vizuri na kutenda vizuri. Tarehe moja Januari ni siku ya kuombea amani duniani. Hatuwezi kuwa na amani kama kufikiri kwetu si kuzuri. Kuwa na amani fikiria amani, hisi amani, na tenda yanayoleta amani. Kuna aina mbali mbali za kufikiri kadiri ya John Maxwell.  Kwanza ni kufikiria picha kubwa. Watu wanapimwa kwa makubwa wanayofikiria.  Alvin Toffer alisema, “Fikiria mambo makubwa wakati unafanya mambo madogo, ili mambo yote madogo yaelekee upande huo.” Pili ni kufikiria kwa kufokasi. Fokasi ni mahali miale ya nuru ikutanapo. Kuwa makini na lengo lako. Mambo ambayo si muhimu yanayokuondoa katika lengo lako usiyatilie maanani.  Kuwa na faili ya mambo muhimu mezani kwako yafuatilie kila siku. Tatu kufikiria kibunifu. Jiulize maswali haya: kwa nini jambo lifanyike namna hii tu? Nini chanzo cha tatizo hili? Ni masuala gani yanalizunguka tatizo hili? Hili linanikumbusha nini? Nini kinyume chake? Ni ishara gani au taswira gani inalielezea vizuri? Kwa nini ni muhimu? Nani anamtazamo tofauti katika hili? Jambo gani litatokea kama hatulitatui? Nne ni kufikiria kuhalisia. “Wajibu wa kwanza wa kiongozi ni kubainisha uhalisia,” alisema Max de Pree. Uhalisia unakupa msingi wa kujenga.  Tano ni kufikiria kimkakati. Watu wengi wanatumia muda mwingi wakipanga namna ya kufurahia kipindi cha mapumziko kuliko kupanga juu ya maisha yao. Sita ni kufikiria kwa kuangalia uwezekano.  “Hakuna jambo linaloaibisha kama kuona mtu anafanya jambo ambalo ulisema haliwezekani,” alisema Sam Ewing.  Saba fikiria kwa kutafakari. Tafakari uzoefu wako, uliyoyaona, njia ulizokosea. Kukosa njia ni kujua njia. Nane fikiria kwa kuhoji mawazo ya wengi, wengi wanachopendelea. “Ugumu haupo katika mawazo mapya bali kukwepa mawazo ya zamani.” Galileo aliposema dunia inazunguka jua alihoji kile wengi walichoamini kwamba jua linazunguka dunia. 
Hitimisho
Tumuige Bikira Maria Mama wa Mungu katika kufikiria kwa kutafakari. Yesu ni Mungu. Bikira Maria ni Mama wa Yesu. Hivyo Bikira Maria ni Mama wa Mungu (Theotokos). Mt. Maksimiliano Maria Kolbe alikuwa na haya ya kusema: "Wewe ni nani ee Maria Imakulata? Wewe ni nani ee Imakulata? Siwezi kuelewa maana yake nini kuwa kiumbe cha Mungu...Kuelewa maana yake nini kuwa mtoto wa Mungu ni nje ya uwezo wangu mwenyewe. Wewe ni nani ee Imakulata? Si kiumbe tu, si mtoto wa kulea tu, bali ni Mama wa Mungu, lakini si Mama mlezi tu, bali ni Mama halisi wa Mungu."
 

Counter

You are visitor since April'08