Friday, July 25, 2014

NAMNA YA KUINGIA NA KUTOKA



                                            
                                                  JUMAPILI YA 17 YA MWAKA
  1. Fal 3: 5.7 -12
  1. Rum 8: 28 - 30
  1. Mt. 13: 44 - 52

“Ee Bwana…sijui inipasavyo kutoka wala kuingia…Basi umpe mtumishi wako moyo wa hekima” (1 Wafalme 3: 7-9). 
  
Maisha ni kuingia na kutoka. Ukiingia vizuri utatoka vizuri. Tunaingia shuleni na kutoka. Tunaingia sehemu za kazi na kutoka. Tunaingia Kanisani na kutoka. Tunaingia nyumbani na kutoka. Tunaingia hotelini na kutoka. Tunaingia kiwanjani na kutoka.Tunaingia dukani na kutoka. Tuingieje? Tutokeje? Kuna kitendawili kisemacho: aliingia kwenye nyama akatoka bila kula. Jibu ni kisu. Mwanafunzi akiingia shuleni kujifunza na kutoka bila ushindi ametoka kama kisu kwenye nyama.  Timu ya mpira ikiingia uwanjani na kutoka imefungwa bila kufunga ni kama kisu kuingia kwenye nyama na kutoka bila kula. Tunahitaji hekima kujua namna ya kuingia na kutoka. Suleimani au Solomoni alisali: “Ee Bwana…sijui inipasavyo kutoka wala kuingia…Basi umpe mtumishi wako moyo wa hekima” (1 Wafalme 3: 7-9).

Usiingie mikono mitupu. “Zenani” jina la watu wa kabila la Xhosa wa Afrika Kusini lina maana ya : “Umeleta nini?” Ni swali ambalo tunaulizwa. Kuna rafiki yangu alikuwa anafanya sherehe ya kuzaliwa. Aliniimbia nikifika mlangoni mwake nifungue mlango kwa miguu. Nikamuuliza kwa nini nifungue mlango kwa mguu akasema: “Ufungue kwa miguu kwa vile mikono itakuwa imebeba zawadi.” Hata tunapoingia nyumba ya Mungu tuingie tumebeba zawadi. Namna ya kuingia kanisani. Usiingie mikoni mitupu. Biblia yasema: “wala asitokee mtu mbele yangu mikono mitupu” (Kutoka 34:20).  Hata mamajusi hawakwenda kumsujudia mtoto Yesu mikono mitupu bali waliingia pangoni na zawadi. 

Ingia kwa mtazamo chanya. Watu wenye mtazamo chanya wanapendwa na kuheshimiwa kuliko ambao kila mara wanalalamika na kuwa na mtazamo hasi. “Baadhi ya watu hulalamika kwa vile maua ya waridi yaana miiba: ninashukuru miiba ina maua ya waridi,” alisema Alphonse Karr, katika kitabu kiitwacho, A Tour Round My Garden. Huo ni mtazamo chanya. Kuna padre aliyeingia hotelini kwa mtazamo chanya. Aliagiza kikombe cha kahawa ingawa ulikuwa wakati wa chakula cha mchana. Ilikuwa ni siku ya kufunga. Kwa mshangao aliona kijana muumini katika Kanisa lake akiwa na mlima wa nyama choma kwenye sahani yake. Kijana alisema: “Naamni padre sikakukwaza.” Padre kwa mtazamo wake chanya alisema: “Nachukulia kuwa umesahau kuwa siku ya leo ni siku ya kufunga.” Kijana alijibu: “Nakumbuka bila mashaka yoyote kuwa leo ni siku ya kufunga.” Padre kwa mtazamo chanya akasema: “Utakuwa mgonjwa na daktari bila shaka amekwambia kutofunga.” Kijana akasema: “Hapana nina afya nzuri sana.” Padre aliinua macho yake mbinguni na kusema: “ Ee Mungu huyu kijana anatoa mfano mzuri kwa kizazi hiki. Anakubali makosa yake badala ya kusema uongo.” Padre alikuwa na mtazamo chanya.

Ingia kwa salamu. “Asubuhi njema! Mchana mwema! Usiku mwema! Hizi sio salamu tu. Hizi ni baraka zenye nguvu, zinazoanzisha mambo mazuri. Kwa hiyo kama ni asubuhi, mchana au usiku akikisha salamu unaisema vizuri,” alisema  Franco Santoro. Bwana Yesu alisema: “Mnapoingia nyumba isalimuni” (Mathayo 13: 12). Kuna mtu aliingia kwenye nyumba na kumsalimu mwenye msongo wa mawazo: Habari za leo. Aijibu. Sijui. Akamsalimu tena . Habari za leo. Yeye alijibu kama za juzi. Alikuwa na msongo wa mawazo. Kusalimu ni kutakia mtu amani.

Ingia kwa shukrani. “Ingieni malango mwake kwa shukrani” (Zab 100:4).

Toka kwa malengo. Jua unapokwenda. Kutoka kwa malengo kunahitaji hekima. “Kama haujui unapokwenda, labda utaishia mahali fulani pengine,” alisema Laurence J. Peter. Kuna mtu ambaye alikuwa kwenye matatu kondakta akamwomba alipe nauli akasema: “Nauli nitakupa ila najiuliza naenda wapi?” Hakutoka nyumbani kwa malengo. Thomas Carlyle alisema: “Mtu asiye na lengo ni kama meli bila usukani – mtu aliyepotea, mtu bure, kabwela.”
Toka kwa furaha. Nyota njema huonekana asubuhi. Anza siku yako kwa kuvaa vazi la furaha. Njia ya kuwa na furaha ni kuwafanya wengine kuwa na furaha. “Sambaza upendo kila mahali unapokwenda. Mtu yeyote asije kwako bila kutoka akiwa na furaha zaidi,” alisema mwenye heri Teresa wa Calcutta. Kama mfalme Sulemaini au Solomoni tuombe hekima ya kujua namna ya kutoka na namna ya kuingia.

Counter

You are visitor since April'08