Saturday, August 2, 2014

SHUKRANI INATANGULIA MUUJIZA



                                     
                                             JUMAPILI YA 18 YA MWAKA A
1. Isaya 55: 1-3    
2.  Warumi 8: 35, 37 -39
3. Mathayo 14: 13-21

“…alitazama juu mbinguni (Mathayo 14:19)” . “ Alimshukuru Mungu (Yohane 6:11).”

Toa shukrani kwa jambo dogo na utapata makubwa,” ni methali ya kabila la Hausa Nigeria.  Asiyeshukuru hupewa mara moja.” Ni methali ya wahaya. Kusema kweli tukishukuru katika kila jambo Mungu atatufanyia miujiza. Shukuru kabla ya kula. Shukuru kabla ya kusafiri. Shukuru kabla ya kufanya mtihani. Shukuru kabla ya kutafuta mchumba. Shukuru kabla ya kutafuta kazi. Shukuru kabla ya kuanza kazi. Shukuru kabla ya kwenda Hospitalini. Na baadaye shukuru, yaani baada ya kula, baada ya kutoka Hospitalini kutaja machache. “shukrani kila mara hutangulia muujiza,” alisema Ann Voskamp. Kukumbuka kusema “asante” kunaongeza miujiza katika maisha yetu. Maneno mawili haya “asante sana,” ni maneno ya kimiujiza. “Shukrani ni utajiri. Malalamishi ni umaskini,” alisema Doris Day. Anton Dvorak, mwanamuziki mashuhuri wa Czeche alizoea kuandika kwenye ukurasa wa mwisho wa kila mswaada wake maneno haya: “Namshukuru Mungu! Nimeridhika na kazi hii!
Bwana wetu Yesu Kristu alipofanya muujiza wa kulisha watu zaidi ya elfu tano alipopewa samaki wawili na mikate mitano alitazama juu mbinguni (Mathayo 14:19). Alimshukuru Mungu (Yohane 6:11). Muujiza huu aliufanyia jangwani. Shukrani ilitangulia muujiza. Mtakatifu Yohane Chyrisostom alikuwa na haya ya kusema: “Wayahudi katika kuelezea muujiza walikuwa na msemo: ‘Je, aweza kutupa chakula jangwani’ (Zaburi 78: 19). Kwa sababu hii aliwaongoza kwenda jangwani, ili muujiza usiwe na chembe yoyote ya kudhaniwa vibaya na mtu asifikiri kuwa chakula kimeletwa toka mji wa karibu. Lakini hata kama mahali ni jangwa ni yeye anayelisha dunia; ingawa saa ilikuwa imepita yeye hayuko chini ya masaa. Ingawa Bwana mbele ya mitume aliponya wagonjwa, mitume hawakuwa wakamilifu kiasi cha kuweza kutambua ambacho angeweza kufanya kuhusu chakula. Wao walisema, ‘uwaage watu ili waende vijijini wakajinunulie chakula” (Mathayo 14: 15).
Kuna hadithi ya Wayahudi juu ya nani wa kushukuru. Omba omba wawili walizoea kuomba misaada kwa mfalme kando kando ya barabara kwenye jiji kubwa. Walizoea kwenda kwenye ikulu ya mfalme, ambaye alihakikisha wanapewa msaada. Mojawapo wa omba omba alimshukuru mfalme kwa ukarimu wake, lakini mwingine alimshukuru Mungu kwa kumpa mfalme nguvu na njia za kusaidia watu wake. Hilo lilimhuhumiza mfalme alimwambia omba omba huyo: “Kwa nini ninapokuonesha ukarimu unamshukuru Mungu na sio mimi.” Maskini alimjibu: “Kama Mungu hasingekuwa mkarimu kwako, usingekuwa na chochote cha kunipa.” Mfalme aliamua kumpa omba omba huyu fundisho. Alimwamuru mpishi wake kutengeneza mikate miwili na kuficha kwenye mkate mmoja madini yenye thamani sana na kuhakikisha maskini aliyekuwa anamshukuru mfalme na sio Mungu anapata mkate huo wenye madini. Mpishi alifanya hivyo.
Walipotoka kwa mfalme, njiani maskini aliyekuwa anamshukuru mfalme badala ya Mungu aligundua kuwa mkate wake ni mzito isivyo kawaida; kwake ilimaanisha uliokwa vibaya. Hivyo alimwomba mwenzake wabadilishane mikate. Walifanya hivyo na baada ya hapo kila mmoja akashika njia yake. Yule maskini ambaye kila mara alimshukuru Mungu alipoanza kula mkate alikuta madini yenye thamani sana kwenye mkate na alimshukuru Mungu kuwa sasa hataenda tena ikulu na kuomba msaada toka kwa mfalme.
Baada ya muda mfalme aligundua kuwa mmoja wa omba omba haji tena ikulu kuomba. Alimuuliza mpishi wake kama hakukosea katika kuwapa mikate ile na kuchanganya. Alikuwa na uhakika kuwa hakuchanganya hiyo mikate. Mfalme alimuuliza maskini ambaye aliendelea kuja kwake: “Ule mkate wangu usio wa kawaida uliopewa kipindi fulani uliuweka wapi?” Maskini alikiri kwa kusema kiukweli: “Mkate wangu ulikuwa mzito, hivyo nilifikiri uliokwa vibaya. Hivyo nilibadilishana na mwenzangu.” Mfalme alielewa kwa nini ombaomba mwingine alimshukuru Mungu. Tukumbuke kuwa utajiri wote na mali zote hutoka kwa Mungu. Mungu pekee anaweza kumfanya mtu maskini awe tajiri na tajiri awe maskini – bila kujali watu hata wafalme wanafikiria nini.”
Kumshukuru Mungu ni utangulizi wa muujiza. Muujiza katika hadithi ya wayahudi ni somo tosha juu ya kumshukuru Mungu. “Unapoamka asubuhi toa shukrani kwa ajili ya mwanga wa asubuhi, kwa ajili ya uhai wako na nguvu. Toa shukrani kwa ajili ya chakula chako na furaha ya kuishi. Kama hauoni sababu ya kushukuru, kosa liko kwako,” alisema Tecumseh (1768-1813). Wamebarikiwa wale ambao wanaweza kutoa bila kukumbuka na wale ambao wanaweza kupokea bila kusahau. Kutosahau kunamaanisha kuwa na shukrani.
Pale ulipoweka nukta Mungu anaweka alama ya mkato mambo mazuri yanakuja. Yeye akiamua kuweka nukta usiweke alama ya kushangaa.  Filipo aliweka nukta kwenye masuala ya kulisha wanaume elfu tano. Filipo mfuasi wa Yesu aliona kuna tatizo raslimali kidogo zisioweza kutosha kulisha wanaume elfu tano wanaojua kula chakula. “Filipo akamjibu, “Mikate ya dinari mia mbili haiwatoshi, ili kila mmoja apate kidogo tu.” (Yohane 6: 7). Yesu anatwaa utajiri kutoka kwenye ufukara wa mtoto mwenye samaki wawili na mikate mitano . Anabadili  kidogo kinakuwa kikubwa. “Kuongezwa kwa mikate kunasimuliwa kikamilifu katika Injili zote nne. Muujiza huo una uhusiano wa moja kwa moja na Ekaristi.” Mfululizo wa vitenzi: Akaitwaa…akaibariki, akaimega, akawapa unadokeza Ekaristi. Kidogo unachoweka mikononi mwa Yesu atakibariki kiwe kingi. Neno kula katika Biblia limetumika mara elfu. Katika masimulizi ya Injili mara nyingi tunamuona Yesu anaenda kula au anatoka kula. Tunajifunza kuwa njaa ni tatizo. Ni tatizo la kiuchumi. Ni tatizo la kijamii. Ni tatizo la kidini pia. Linahitaji pia suluhisho la kidini. Lisilowezekana linawezekana.
MAMBO YA KUKATISHA TAMAA
Mazingira: Nyika Tupu
“Palikuwa na nyasi nyingi mahali  pale”  (Yohane 6: 10). Katika Injili ya Marko tunapata maelezo haya: “Mahali hapa ni pa ukiwa (Nyika tupu)” (Marko 6:35). Mahali pa ukiwa kuna njaa. Penye nyika tupu kuna njaa. Palipo na njaa ya upendo ni nyika tupu. Ofisini ukiwa na njaa ya upendo ni nyika tupu. Kwenye familia ukiwa na njaa ya upendo ni nyika tupu. Lakini katika maisha kuna ambao wanaona nyika tupu bila kuona raslimali zilizopo. Kuna Kampuni ya kutengeneza viatu iliyotuma watu wawili kwenda visiwani kuona uwezekano wa kuanzisha biashara ya kuuza vitua huko. Mmoja alipoona watu hawana viatu wanatembea peku peku, akatuma ujumbe kuwa ziandaliwe konteina tano huku watu wanahitaji viatu. Mwingine akatuma ujumbe kwenye makao makuu ya kampuni ya viatu kuwa visiwani watu wana utamaduni wa kutovaa viatu kwa hiyo wasiandae mzigo wowote wa kutuma visiwani.
Kupita kwa Wakati
“Mahali hapa ni ukiwa na saa imepita” (Mathayo 14: 15). Wakati ulikuwa umekwenda. Labda kuna jambo ulitegemea kupata muda unaona umepita. Ulitegemea kupata mme lakini saa imepita. Ulitegemea kupata kipato kizuri lakini saa imepita. Ulitegemea kwenda chuoni  lakini saa imepita. Kumbuka maneno haya: “Mawazo yangu si mawazo yenu” (Isaya  55: 8). Wakati wa Zechariah na  Elizabeth kuzaa ulikuwa umepita lakini Mungu akawafanyia muujiza wakampata mtoto Yohane Mbatizaji. Kupita kwa muda pengine ni suala la mtazamo. Kijana anapokalia stovu yenye moto dakika moja ni kama saa moja. Lakini msichana mrembo anapokaa karibu naye saa moja ni kama dakika.
Ukubwa wa Tatizo
“Yesu alipoinua macho na kuona umati mkubwa wa watu wanamjia, alimwambia Filipo, tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula?” (Yohane 6: 5). Watu walikuwa wengi wanaume wapata elfu tano bila kuhesabu watoto na wanawake. Watu walikuwa wengi. Tatizo lilikuwa kubwa. Mungu wetu ni mkubwa kuliko matatizo yetu. Ukiwa na tatizo usimwambie Mungu nina tatizo kubwa bali liambie tatizo Mungu wangu ni mkubwa. Unapopata tatizo kubwa kama Goliathi, unajibu vipi? Ni kubwa si rahisi kushambuliwa. Jibu kama Daudi. Ni mnene sana, siwezi nikalenga nikakosa. “Daudi akasema, Bwana aliyeniokoa na makucha ya samba, na makucha ya dubu, ataniokoa na mkono wa mfilisti huyu” ( 1 Sam 17:37).
Uchache wa Raslimali
“Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, “Yupo mtoto aliye na mikate mitano ya shayiri na samaki wawili; lakini hii ni nini kwa watu wengi kama hawa?” (Yohane 6: 8). Mtu anaweza kusema hili haliwezekani kwa vile raslimali ni chache. Licha ya uchache wa raslimali Yesu alifanya muhujiza. Katika somo la kwanza tunaona uchache wa raslimali mikate ya shayiri ishirini (2 Wafalme 4: 42). Lakini Elisha akasisitiza, “Uwape watu, ili wale, kwa kuwa Bwana asema hivi: Watakula na kusaza.” (2 Wafalme 4: 42).
VIRUTUBISHO VYA KUTATUA MATATIZO
 Kama Kwamba Umepata
Yesu  akawaambia, Waketisheni  Watu” (Yohane 6: 10).  Yesu aliwataka watu wakae mkao wa kula chakula “kama kwamba” chakula kimeishapatikana. Muujiza wa kuongeza mikate ulikuwa haujafanyika lakini Yesu alitenda kama kwamba. Kuna wakristu katika parokia moja hapa Tanzania walimuomba padre Jumapili iliyokuwa inafuatia iwe siku ya kuomba kupata mvua. Wakristu hao walishangazwa na padre aliposema hayuko tayari kufanya maombi ya kuomba mvua kwa vile wakristu hawakwenda na miavuli ya kujikinga na mvua. Suala la kuwa na miavuli linadokeza maana ya “kama kwamba.” Yesu aliwambia wakoma kumi waende wajioneshe kwa makuhani kama kwamba wamepona. Bikira Maria aliwaambia watumishi: lolote atakalowambieni fanyeni “kama kwamba” Yesu amekubali.
Piga picha ya kile unachokitaka. Bila shaka Bwana Yesu Kristu alipiga picha ya muujiza, picha ya ongezeko la samali wawili na mikate mitatu.  Suala la kupiga picha ni muhimu ili ufanikiwe. “Akamleta (Abramu) nje akasema:Utazame mbinguni, uhesabu nyota, kama waweza kuzihesabu.Akamwambia: Ndivyo uzao wako utakavyokuwa” (Mwanzo 15:5). Mungu alisisitiza umuhimu wa kupiga picha.
Shukuru Usikufuru
“Yesu akaitwaa mikate, akashukuru” (Yohane 6: 11). Shukrani inabadili “hakitoshi” kuwa “kinatosha.” Shukrani inabadili kidogo kuwa kikubwa. Kushukuru ni kuomba tena.
Mshirikishe Yesu
Mipango bila kumshirikisha Yesu haina mafanikio ya kimihujiza. Filipo mwanahesabu hakumweka Yesu katika hesabu zake. Alisema dinari mia mbili kugawa kwa wanaume elfu tano haitoshi. Angesema dinari mia mbili  kujumlisha na Yesu na kugawa kwa wanaume elfu tano watoto na wanawake inatosha. Katika mipango yako mshirikishe Yesu. Katika hesabu zako mshirikishe Yesu.
Kidogo Kivute Kikubwa
Mungu wetu ni Mungu anayehitaji mchango wako. Mchango wa samaki wawili na mikate mitano ni kidogo kilichovuta kikubwa. Mungu anahitaji upige hatua ya kwanza. Katika hadithi za Kiyahudi ambazo hazikuandikwa katika Biblia kuna hadithi isemayo: Musa alipopiga maji yake na fimbo katika Bahari Nyekundu maji hayakugawanyika wana wa Israeli wapiti bali mtu wa kwanza ulitangulia na kuingia majini ndipo maji yakagawanyika. Piga hatua ya kwanza.
Tafakari maneno ya Mtakatifu Josemaria Escriva: “Omnia possibilia sunt credenti – yote yawezekana kwake yule anayesadiki. Hayo ni maneno ya Kristu. Vipi wewe huwezi kumwambia kama walivyosema mitume: adauge nobis fidem - utuongezee imani.” Nelson Mandela aliyekuwa mstari wa mbele kuleta uhuru wa walio wengi Afrika Kusini jambo ambalo lilionekana kama ndoto, alisema, “Kwa kawaida jambo linaweza kuonekana haliwezekani mpaka linapofanyika.” Ndani ya neno kisichowezekana kuna neno wezekana. Ndani ya neno lisilowezekana kuna neno wezekana.

                                                

Counter

You are visitor since April'08