Saturday, August 9, 2014

MAWIMBI KATIKA BAHARI YA MAISHA



                           
                                       Jumapili ya 19 ya Mwaka A
  1. 1 Wafalme 19:9, 11-13
  1. Warumi  9:1-5
  1. Mathayo 14:22-33

Kumbuka kuwa bahari shwari haitoi wanamaji stadi. Matatizo kama mawimbi yanaweza kukuimarisha. Hivyo usipoteze wakati wako kupambana na ukuta ukifikiri utageuka kuwa mlango! Kuwa na mtazamo hasi dhidi ya matatizo ni kama kupambana na ukuta. “Wavuvi wanajua kuwa bahari ni hatari na ina dhoruba ya kuogopesha, lakini hawajawahi kuona hatari hizi kama sababu tosha za kubaki kandokando ya bahari au ufukweni,” alisema Vincent van Goth. Wavuvi hujitosa kwenye maji marefu. Wavuvi ni mfano wa kuigwa tunapokumbana na mawimbi ya matatizo katika bahari ya maisha. Kuna mtu aliyemwambia mvuvi hivi: wewe hauogopi kwenda baharini kuvua samaki. Mjomba wako, kaka yako, babu yako wote walikufa maji kwa nini hauogopi? Mvuvi alijibu hivi: watu wengi hufa wakiwa vitandani lakini watu hawaachi kulala vitandani. “Kuna mambo ambayo unajifunza vizuri sana wakati kuna utulivu na mengine wakati kuna dhoruba,” alisema Willa Cather
Kwa Yesu kila mara mawingu hayakuwa bluu. Kuna wakati wingu lilikuwa jeusi likiashiria dhoruba ya matatizo. Alikataliwa na wasamaria katika kijiji cha Wasamaria. Kwa Ayubu mawingu hayakuwa kila mara ya bluu. Kuna wakati alifikiria kuwa kama hasingezaliwa. Katikati ya mawimbi ya matatizo Ayubu alizidi kuimarika. Ni kama jani la chai linapata nguvu ya kugeuza rangi ya maji likiwa kwenye maji moto. Ukiwa kwenye mawimbi ya matatizo kumbuka ukweli huu: Kwanza tuko salama kwenye mawimbi ya matatizo tukiwa na Mungu kuliko tukiwa pasipokuwa na mawimbi ya matatizo bila Mungu. Mungu anaweza kutuliza mawimbi au akayaacha mawimbi akamtuliza binadamu. Pili, maisha bila mawimbi ya matatizo na magumu yatafanya uwezekano wa mazuri kuwa ni ziro. Tatu, joto likizidi kutanuka kunazidi. Matatizo makubwa yanaweza kukufanya uwe mkubwa. Kuna methali isemayo: anayesema sijawahi kuliona jambo hili huwa si mkubwa kiumri. Nne ukiomba mvua inyeshe kuwa tayari kukanyaga matope. Tano jua kuwa mawimbi ya matatizo yanakujia ili kukuimarisha na wala sio kukudhoofisha.
                                                IMANI HABA
“Ewe mwenye imani haba mbona uliona shaka” (Mathayo 14:31)
Maisha ni kigeugeu. Mambo yalimgeuka mtume Petro. Petro alikuwa ni mtu aliyefanya maamuzi ya ghafla na ya haraka. Hakufikiri sana kabla ya kutenda. Jambo hili pengine ni busara ulikilinganisha na mtu ambaye anafikiri sana mwishowe hatendi lolote. Katika nafsi ya Petro kuna mchanganyiko wa mambo. Anatamani kuwa na Yesu. Pia anatamani kuonesha kuwa anaweza kutenda analolitenda Yesu: kutembea juu ya maji. Kuna upendo na majivuno kama ilivyo kwa kila mmoja wetu. Petro ana ujasiri na woga. Anaanza vizuri, anaona dhoruba na kuogopa. Anakosa imani.

Sababu kubwa ya kupotea kwa imani ya Petro ni kuwa macho yake, mawazo yake, moyo wake alivielekeza kwenye dhoruba badala ya Kristu. Alipomtazama Yesu Kristu imani ilipatikana akalia kwa sauti, “ Bwana, niokoe !” ( Mt 14; 30). Licha ya Petro kuwa na imani haba Yesu alimuokoa. “ Hapo, Yesu akanyosha mkono wake, akamshika … wakapanda mashuani, na upepo ukakoma”. ( Mt 14: 31-32). Nasi tunapambana na matatizo. Matatizo ya siku hizi ni kama: umasikini, makazi yasiyofaa, ukosefu wa kazi, magonjwa yasiyo na tiba, ukosefu wa riziki, uzinifu, uzazi kwa namna isiyo halali, ukatili na vita, ukabila- damu inakuwa nzito kuliko maji ya ubatizo. Wakati tunazama kwenye lindi la maji ya matatizo tumuombe Yesu atuokoe.

Katika kilele cha dhoruba Yesu alijitokeza. Katika kilele cha hatari, katika upeo wa wasiwasi Yesu alijitokeza. Anakuja wakati ambapo hategemewi kabisa. Mitume walifikiri ni mzuka wakauotea mbali. Yesu ni Mkombozi wakubariki. Ni Mkombozi tunayeweza kumkimbilia. Alifanya kile ambacho binadamu hawezi kufanya. Alitembea juu ya maji. Vile ambavyo hatuwezi kufanya tumuachie yeye. Wakati tunapozama kwenye bahari ya matatizo tulie kwa sauti: “Bwana utuokoe !”
Shibisha imani yako na mashaka yako utayakondesha. Imani ikiongezeka mashaka yanapungua na kinyume chake ni kweli. “Imani si kujaribu kuamini jambo bila ya kuzingatia ushahidi: imani ni kujaribu kufanya jambo bila kuzingatia matokeo,” alisema Sherwood Eddy.
“Wanashinda wale wanaoamini wanaweza,” alisema Virgil. Ni katika mtazamo huo Erasmus alisema, “Amini kuwa unacho na unakuwa nacho.” Swali kubwa hapa si kuwa una imani au hauna imani. Jambo la msingi ni imani katika nini na imani katika nani. Ili kufanikiwa na kushinda unahitaji kuwa na imani katika Mungu na kujiamini hata ikiwa imani ndogo au haba inatosha kukuondolea vikwazo, vihunzi na vizingiti. Tunasoma hivi katika biblia, mitume wakamwambia Bwana, Tuongezee imani. Bwana akasema, Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng’oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii” (Luka 17: 5-6).
Kifungu cha Biblia hicho kinabainisha ukweli huu, imani kidogo yaweza kufanya mambo makubwa. Ni ukweli unaoendana na ujumbe wa methali ya Kiswahili, Kidogo kidogo kamba ukatika. Nguvu ya mbegu haitegemei ukubwa au udogo wake inategemea uhai uliofichwa katika mbegu hiyo. Kuna nguvu ambayo imefichwa ndani mwako. Kama ni hivyo unahitaji kujiamini kuwa utaweza kufanikiwa katika maisha. Kwa imani na kujiamini ndege imevumbuliwa. Kwa imani na kujiamini simu za mkononi zimegunduliwa. Kwa imani na kujiamini utalaamu wa kutengeneza runinga umefunuliwa.
Mitume walipoomba kuongezewa imani, Yesu hakusema nimewaongezea imani. Hakuahidi kuwaongezea imani. Ni kama aliwaambia anza na mlicho nacho, kidogo huvuta kikubwa, kidogo huzaa kikubwa, laini huzaa ngumu. Walikuwa kama mfanyabiashara asemaye nina pesa kidogo sana ngoja iwe nyingi ndipo nianze kufanya biashara. Je, itaongezekaje bila kuzalisha, kuuza na kununua? Walikuwa kama mkulima asemaye nina mbegu lakini hazitoshi nitalima nikiwa na mbegu za kutosha. Anza na ulicho nacho. Hawezi kusema sina pesa yote ya kujenga na kumalizia nyumba. Anza kujenga na pesa uliyo nayo. Ili kuwa na zaidi anza na ulicho nacho. Aliyenacho ataongezewa ndivyo  Bwana Yesu alivyofundisha.
Imani ni ufunguo wa mafanikio. Na sifa ya mtu anayefanikiwa ni kuwa ana imani. Imani kamili ndiyo kumtegemea Mungu na kumtumaini na kumtii. Tukiwa na imani kwa Mungu twaweza kusema, “Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa” (Waebrania 13:6). Hatuna budi kuwa na imani na uwezo Mungu aliotujalia yaani kujiamini. Kuna hadithi juu ya wakristu ambao walimuomba mchungaji wakati wa ibada wa Jumapili iliyokuwa inafuata waombe kupata mvua baada ya mvua kutonyesha kwa kipindi cha muda mrefu. Walishangaa siku hiyo ya maombi ya Jumapili mchungaji aliposema hayuko tayari kuomba kupata mvua maana watu hawaonyeshi imani kwa vile hawakwenda na miavuli ya kujikinga mvua. Imani lazima ionekane katika matendo. Ni Mungu nisaidie na wewe unaweka juhudi na maarifa. Henry Ford alisema, “Kama unaamini unaweza kufanya jambo fulani au hauamini kama unaweza kufanya jambo fulani, uko sawa.” Usipoamini kwamba jambo fulani linaweza kufanyika halitafanyika. Ukiamini litafanyika. Imani inafukuza mashaka kama mwanga hufukuzavyo giza. Mashaka yakibisha hodi mlangoni mwako itume imani ijibu mashaka. Sala yetu iwe kama ya kijana mmoja kwenye Biblia, “Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu” (Marko 9: 24).
Yesu anaweza kunyamazisha mawimbi ya matatizo. Tunasoma hivi katika Biblia: “Ikatokea dhoruba kubwa na mawimbi yakapiga chombo, hata kikaanza kujaa maji. Naye Yesu alilala usingizi shetrini juu ya matandiko. Wakamwamsha na wakamwambia, “Mwalimu, huhangaiki tukiangamia? Akaamka, akaukemea upepo, akaiamuru bahari, “Nyamaza! Tulia!” Upepo ukakoma, kukawa shwari kabisa (Marko 4: 37-39). Tuwe pamoja na Yesu  alale kwetu tunaposafiri katika bahari ya maisha. Bahari, kama yalivyo maisha yote si lazima ituchachafye. Mambo yanaweza kuelea na kwenda kwa raha; ikiwa yanatugeukia basi Yesu hatakosa kutusaidia kwani tunaye karibu. “Yesu alinyamazisha bahari si kwa kutumia fimbo kama Musa, si kwa kutumia sala kama Elisha alipokuwa Jordan, na wala si kwa sanduku la agano kama Joshua, mwana wa Nun kwa sababu hizi wafuasi wake walifikiri kuwa Yesu ni Mungu kweli, lakini wakati alikuwa amelala walifikiri yeye ni binadamu tu,” alisema Theophil.
Dunia ni bahari yenye mawimbi inahitaji wanamaji stadi. Duniani kuna mengi sawasawa na bahari. Kuna papa na nyangumi tena wale wa hatari. Lakini ukweli unabaki: Bahari shwari haitoi wana maji stadi. Bahari iliyotulia haiwezi kuwatoa wanamaji hodari. Kuna methali ya Kiswahili isemayo: Bahari haishi zinge. Zinge ni machafuko ya mara kwa mara (mabadiliko ya ghafla). Bahari daima imo katika mabadiliko wala haitabiriki. Maisha kama vile bahari yamejawa na mema na maovu na yanapotujia sharti tuwe tayari kuyakabili. Huko Mkoa wa Kagera nchini Tanzania kuna mashindano ya kupatia mwaka mpya jina. Mshindi huwa anapewa zawadi. Kuna mwaka ulioitwa kwa lugha ya Ruhaya “Galaziwa enzii” maana yake: “Ataogelea mwanamaji stadi”. Nchi ilikuwa katika matatizo makubwa ya kiuchumi baada ya vita kati ya Tanzania na Uganda miaka ya 1978 na 1979. Matatizo hayo ni kama mawimbi kwenye bahari. Kuvuka mwaka huo kulilinganishwa na kuvuka bahari na ni mwanamaji stadi alitegemewa kuvuka. Mfano huo unaipa nguvu falsafa hii: DUNIA NI BAHARI inahitaji wanamaji stadi.
Watoto wasipopata malezi mazuri familia inakuwa ni mtumbwi unaoyumbishwa na mawimbi. Watoto wanahitaji kueleweshwa. Mfano kuna mtoto aliyefungua chumba cha wazazi wake bila kubisha hodi. Baba akupenda jambo hilo. Akamwambia. “Kila unapotaka kufungua mlango wowote ule, lazima ubishe mlango kwa kusema, hodi hapa!” Siku moja baba huyo alimtuma mtoto akalete soda toka friji au jokufu . Baada ya kumgonja dakika kumi mtoto bila kurudi. Baba alienda kutazama kulikoni. Akamkuta mtoto anabisha kwenye mlango wa friji akisema. “Hodi hapa! Hodi hapa!” Biblia inasema, “NAYE YESU AKAENDELEA KUKUA KATIKA HEKIMA NA KIMO; AKAZIDI KUPENDWA NA MUNGU NA WATU” (LUKA 2: 52). Muombee mtoto wako azidi kukua katika hekima, azidi kupendwa na Mungu na watu.
Tunapozungumzia bahari kuwa na picha ya vurugu, machafuko, ghasia, fujo. Ni picha hiyo tunasoma kitabu cha Mwanzo: “Hapo mwanzo, Mungu aliumba mbingu na dunia. Dunia ilikuwa bila umbo na tupu. Giza lilikuwa limefunika vilindi vya maji na roho ya Mungu ilikuwa ikitanda juu ya maji” (Mwanzo 1:1-2). Tunapozungumzia bahari kuwa na picha ya maharamia wa kisomalia wanaoteka meli baharini. Kuwa na picha ya meli ya maharamia. Tunapozungumza mambo ya maji kuwa na picha ya Kisiwa cha Migingo na vita vya maneno vinazunguka kisiwa hicho. Kuwa na picha ya kuzama kwa meli ya RMS Titanic. Usiku wa tarehe 14 Aprili 1912 meli hiyo ilikuwa ikitokea Uingereza na kuelekea jiji la New York ilipogonga mwamba wa barafu ilizama baadaye baada ya masaa 2 na dakika arobaini na tano usiku wa kuamkia tarehe 15 Aprili 1912. Watu walioaga dunia ni 1, 517. Waliokoka ni watu 706. Jumla ya watu walikuwa ni 2,223. Huko Tanzania mwaka 1996 meli ya MV BUKOBA ilizama katika ziwa Victoria watu zaidi ya 700 waliaga dunia.
 TUFANYE NINI ILI KUKABILIANA NA MAWIMBI YA MATATIZO KATIKA BAHARI
Yesu alikuwa na sehemu tatu za kutafuta usalama, sehemu tatu za kupumzika: kwenye mtumbwi, mlimani na jangwani. Alipokuwa amezungukwa na watu wengi sana na alipohitaji kupumzika alienda sehemu mojawapo. Tunahitaji kupumzika na Yesu. Lakini zaidi ya hayo tunahitaji yafuatayo:
1. KABILI MAWIMBI KWA UTULIVU BILA HOFU
Tukiona mawimbi tunakuwa na hofu, pengine hofu kubwa inatuingia ghafla. Hakuna kufikiri sawa sawa. Tunahangaika, tunakuwa na wasiwasi kama wafuasi wa Yesu kwenye mtumbwi. Watu wana namna mbalimbali za kujiliwaza. Siku moja baba mmoja kijana alikuwa anamsukuma mtoto wake ambaye alikuwa akilia kwenye kigari cha watoto. Aliendelea kusema, “Tulia Donald. Nyamaza sasa, Donald. Mambo yatakuwa shwari, Donald.” Mwanamke aliyekuwa akipita alimwambia baba huyo, “Unajua namna ya kumbembeleza mtoto ambaye analia kwa utulivu na pole pole.” Mwanamke huyo aliinama kwenye kigari na kuanza kusema “Unasumbuliwa na nini Donald.” Baba yake aliingilia kati haraka, “Hapana, hapana yeye ni Henry! Mimi ni Donald.!” Mama huyo akauliza, “Mbona ulikuwa ukimbembeleza aache kulia ukimwita Donald!” “ Nilikuwa ninajibembeleza mimi mwenye moyoni ninalia kama mtoto huyu!”
KABILI MAWIMBI YA MAWAZO MABAYA
KABILI MAWIMBI YA MAHUSIANO MABAYA
KABILI MAWIMBI YA KUSHINDWA
KABILI MAWIMBI YA MATARAJIO KUVUNJIKA
2. YESU NI JIBU: MWAMBIE AKUSHIKE MKONO
“Yesu alinyamazisha bahari si kwa kutumia fimbo kama Musa, si kwa kutumia sala kama Elisha alipokuwa Jordan, na wala si kwa sanduku la agano kama Joshua, mwana wa Nun kwa sababu hizi wafuasi wake walifikiri kuwa Yesu ni Mungu kweli, lakini wakati alikuwa amelala walifikiri yeye ni binadamu tu,” alisema Theophil.
3. MATATIZO MAKUBWA YANAHITAJI IMANI KUBWA
Nyakati za kujaribiwa imani ni nykati za kuimarisha imani. “Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali; ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto” (1 Pet 1: 6-7).
4. JUA KUWA YANA MWISHO
Mateso, shida, matatizo yana mwisho. Mateso hayana kauli ya mwisho. Furaha ina kauli ya mwisho. Katika kitabu cha Ufunuo tunasoma hivi: “Kisha, nikaona mbingu mpya na dunia mpya. Mbingu ile ya kwanza na dunia ile ya kwanza vilikuwa vimetoweka, nayo bahari pia haikuwako tena” (Ufunuo 21: 1). Bahari haikuwako tena. Mawimbi ya matatizo hayakuwako tena.
5. JIANDALIE SIKU MBAYA
“Umkumbuke Muumba wako siku za ujana wako kabla hazijaja siku mbaya wala haijakaribia miaka utakaposema: ‘Sina furaha katika vitu hivyo” (Mhubiri 12:1). Sasa ndio wakati wa kujenga msingi katika Mungu. Sasa ndio wakati wa kuanza ukurasa mpya na sura mpya. Sasa ndio wakati wa kujiwekea bonga pointi mbinguni. “Kwa hiyo, kila mtu anayesikia maneno yangu na kuyazingatia, anafanana na mtu mwenye busara, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba. Mvua zikavuma na kuipiga nyumba hiyo. Lakini haikuanguka kwa sababu ilikuwa imejengwa juu ya mwamba” (Mathayo 7: 24-25).
6. KWEPA PICHA HASI FIKIRIA PICHA KUBWA NA PICHA CHANYA
Kwepa picha hasi ya mambo: kwa nini mimi tu nataabika, Mungu ananiadhibu. “ Maisha yangu yamekwisha kwa machozi; naam, miaka yangu kwa kulalamika. Nguvu zangu zimeniishia kwa kutaabika; hata mifupa yangu imekauka” (Zaburi 31: 10).
  






Counter

You are visitor since April'08