Thursday, April 17, 2014

MATENDO SABA YA YESU ALHAMISI KUU




“Kila tendo la Neno aliyetwaa mwili ni fundisho kwetu,” alisema Mt. Augostino. Alhamisi Kuu ya Kwanza Yesu alifanya matendo saba katika kuwaosha miguu mitume wake. Matendo saba hayo ni somo la kujifunza. Bwana Yesu na mitume wake walikuwa katika chumba cha Karamu ya mwisho kinachoitwa Cenaculum. Hiki kilikuwa ni chumba cha kulia chakula cha jioni (cena) kilichokuwa orofani katika nyumba. Kwa kawaida matendo makuu yanayokumbukwa Siku ya Alhamisi Kuu ni kuwekwa Sakramenti ya Ekaristi, Daraja Takatifu na amri ya Bwana ya Mapendo ya kidugu. Lakini kuna utajiri mwingine uliojificha katika matendo saba ya kuwaosha miguu mitume kama tunavyosoma katika Injili ya Yohane: “…aliinuka kutoka mezani, akaweka kanzu  yake kando, akatwaa kitambaa cha kitani, akajizungushia kiuononi. Kisha akatia maji katika chombo, akaanza kuiosha miguu ya wafuasi na kuifuta kwa kitambaa alichojizungushia” (Yohane 13: 3-5).

ALIINUKA KUTOKA MEZANI

Mazuri huachwa kwa ajili ya mazuri zaidi. Ni fundisho la kwanza tunalolipata katika tendo la kwanza la Yesu Alhamisi Kuu ya Kwanza. Bwana Yesu na wafuasi wake walikuwa hawajamaliza mlo wa jioni. Aliacha mazuri mezani. Fundisho alilotaka kulitoa lilikuwa zuri zaidi. Fundisho kuhusu ukuu wa huduma. Ilikuwa ni fursa nyingine ya kumtafakarisha Yuda Iskarioti ajue kuwa tunda la huduma ni amani na pia hasilipe wema kwa ubaya. Lakini yote kwa Yuda Iskarioti ilikuwa kama kupiga ngoma ikiwa imezamishwa majini. Ukweli unabaki kuwa mazuri yanaachwa kwa ajili ya mazuri zaidi. Kama unaweza kumsaidia mtu muda wa kupumzika baada ya chakula sio muhimu kiasi cha kutotoa huduma muhimu kwa wenye shida. John Wesley alisema: “Fanya mazuri yote kadiri uwezevyo, kwa vitendea kazi vyote uwezavyo, kwa njia zote uwezavyo, mahali pote uwezavyo, kwa watu wote uwezavyo, kwa kiasi uwezacho.” Mazuri huachwa kwa ajili ya mazuri zaidi. Kuna methali ya Tanzania isemayo: Jambo linalomfanya mwanamwali alie huwa halipo kwa mme wake bali nyumbani anakotoka. Inabidi kuwaacha wazazi na kuambatana na mme wake. Anaacha mazuri kwa ajili ya mazuri zaidi. Anawaacha wazazi ili naye awe mzazi awe na familia yake.

Pili kuinuka kwa Yesu toka mezani ni muhitasari  wa umwilisho wake. Alitoka mbinguni na kuacha mazuri ambayo sikio halijawahi kusikia. Aliacha mazuri ambayo jicho halijawahi kuona. Neno alitwaa mwili. Tunaalikwa tuinuke. Maneno yetu yageuke kuwa matendo. Yachukue mwili. Yasibaki maneno tu.

Tatu kadiri ya rejeo chini ya ukurasa katika Biblia ya Kiafrika, kuinuka kwa Yesu  kutoka mezani ni dokezo la ufufuko. Kuinuka ni fursa ya kuvuta watu kwake. Alisema: “nitakapoinuliwa nitawavuta watu wengi kwangu.”

AKAWEKA KANZU YAKE KANDO

Bwana wetu Yesu Kristu aliweka kando vazi la utukufu wake. Mtume Paulo anaweka wazi ukweli huu: “Muwe nao moyo aliokuwa nao Kristo Yesu, ambaye ijapokuwa alikuwa namna ya Mungu, hakuchukulia kwamba kuwa sawa na Mungun lilikuwa jambo la kushikamana nalo. Bali alijishusha mwenyewe” (Wafilipi 2: 6-7). Kumbuka vazi lake walilipigia kura. Bila shaka lilikuwa vazi zuri. Lilikuwa vazi la heshima. Aliliweka kando. Aliweka cheo chake kando. Ni mwaliko wa kuweka cheo kando na utukufu kando ili kutumikia.Palikuwepo na mwandishi mashuuri wa Kihindi aliyeitwa Suryakant Thripathi. Jina lake maarufu aliitwa Nirala kwa sababu maandishi yake yote yalikuwa na jina Nirala. Nirala alipenda sana kucheza na watoto. Siku moja alikuwa anacheza na watoto mitaani. Watu ambao walikuwa hawajawahi kumuona uso kwa uso walimtembelea. Walimuuliza Nirala mwenyewe bila kumjua: “Tafadhali unaweza kutuonesha nyumba ya Nirala. Tumekuja kumtembelea.” Nirala aliwaambia wangoje atawaonesha nyumba yake baadaye kidogo. Aliendelea kucheza na watoto na baada ya kumaliza aliwaambia kuwa yeye ndiye Nirala. Wageni walishangaa na kumuuliza: “Kwa nini ukutwambia mapema tulipokuuliza.” “Wakati huo sikuwa Nirala mwandishi,bali mcheza na watoto.” Unapocheza na watoto kuwa kama mtoto. Cheo chako kibadilike kulingana na mazingira. Tunasoma katika Biblia: “Kwa wanyonge nalikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu (1 Wakorintho 9:22). Kuna wimbo unasema: “Nimefufuka nab ado ningali pamoja nanyi..”

AKATWAA KITAMBAA CHA KITANI

Alitwaa umbo la mtumishi. Watumwa na watumishi huko Uyahudi enzi za Yesu walijulikana kama:  Watu wa Taulo.” Alichukua cheo cha mtumishi. Tendo hilo lilikuwa ni utabiri wa mateso na kifo chake. “Kabla ya kusulubiwa msalabani alivuliwa nguo Zake, na alipokufa aliwekwa kwenye nguo ya kitani,” alisema Mtakatifu Augustino. Tunaposhawishiwa kufikiria juu ya jina letu, shahada zetu, nafasi yetu, haki zetu, ubora wetu, hadhi yetu, ukuu wetu, mafanikio yetu, sifa zetu, fahari yetu, uwezo wetu tupige picha ya Bwana Yesu anachukua taulo. Katika taasisi na mashirika matatizo yanaweza kujitokeza kwa vile mtu fulani hakupewa nafasi yake. Watu wakubwa ukubwa wao unaweza kutotambuliwa vizuri. Lakini kuna ukubwa wa aina moja, ukubwa wa utumishi. Papa anaitwa “Mtumishi wa Watumishi.” Usijiulize watumishi wangapi wanakutumikia bali jiulize watumishi wangapi wanakutumukia. Ibn Batuta, Mwanafalsafa na mfanyabiashara wa Afrka Magharibi alisema: “Tukifa msitutafute katika makuburi yaliyopakwa chokaa na marumaru, bali mtutafute katika mioyo ya watu tuliowatumikia.”  

AKAJIZUNGISHIA KIUNONI

Bwana Yesu Kristo aliuzungushia Umungu wake taulo ya ubinadamu aliouchukua toka kwa Bikira Maria.  Kuzungusha taulo kiunoni kunadokeza utayari na wepesi wa kufanya kazi. Kumbuka bahati huwaendea walio tayari. Giuseppe Garibaldi  alisema: “Nipe mkono ulio tayari badala ya ulimi ulio tayari.” Yesu hakuwa tayari kwa maneno alikuwa tayari kwa matendo. Matendo yana kauli kuliko maneno. “Safari ya kwenda mbinguni ni kazi ngumu ambayo kila mmoja hana budi kujifunga mkanda ili aitekeleze, kwani kinyume na hapo ipo hatari ya kuishia mlangoni tu,” alisema Samweli Waiti Ndugwa. Jifunge mkanda utumikie.

 KISHA AKATIA MAJI KATIKA CHOMBO

“Kanisa lina maji na machozi, maji ya ubatizo na machozi ya kutubu,” alisema Mtakatifu Ambrose. Maji ni kimiminiko. Kutia maji chomboni kutukumbushe vimiminiko viwili: maji yatakasayo na machozi ya toba. Kadiri duniani panavyokuwepo na dhambi ndivyo tunavyohitaji kufanya toba. Mapdre ni vyombo vya kutakasa watu katika Sakramenti ya Upatanisho. Machozi ya toba yana nguvu: “Machozi kama ya Daudi huzima hata moto wa Jehanumu,” alisema Mtakatifu Chrysostomu. Sikitiko timilifu ni sifa ya toba ya kweli. “Lakini hata sasa, asema BWANA, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuomboleza” (Yoeli 2: 12). “ Kama ukiwa mbele ya mahakama ya kibinadamu baada ya hukumu kupitishwa, ukilia na kuomboleza, kwa kulia kwako hautabadili hukumu kamwe, lakini mbele ya baraza la kimungu utabadili hukumu kama kutoka ndani ya moyo wako utalia kwa ajili ya kupata huruma,” alisema Mtakatifu Chryosostomu.

 AKAANZA KUIOSHA MIGUU YA WAFUASI

Kuna aliyesema kuwa: “Kukaa majini si kutakata.” Yesu alipoosha miguu ya wafuasi wake si wote walitakatata. Nanyi mmekuwa safi lakini si nyote. Ni maneno ya Yesu. Yuda Iskarioti hakuwa safi. Alikuwa na mpango wa kumsaliti Yesu. Kukaa majini si kutakata. Samaki anakaa majini lakini ngozi yake si safi. Samaki anakaa majini lakini lazima kumuosha kabla ya kumla. Tunalazimika kutumia Sakramenti ya Upatanisho ili tupate neema ya utakaso. Kusali sala kunatupa neema ya msaada si neema ya utakaso. Tunahitaji neema hizo zote. Kuna methali ya Kidachi isemayo: “Rafiki akimuosha rafiki yake wote hutakata.” Ni vizuri marafiki wakasahishashana. “Kila mtu anapaswa kutunza kaburi la usawa wa kadiri ambalo ndanimo atazika makosa ya marafi wake. Tukumbuke kuwa: “Urafiki ni kama pesa, rahisi kuzipata kuliko kuzitunza,” alisema Samuel Butler. Yuda Iskarioti hakutunza urafiki wake na Yesu. Alimsaliti Yesu. Kutenda dhambi ni kumsaliti Yesu kwa vipande thelathini vya fedha.  Wanandoa hawana budi kusahihishana. Kuna methali ya Tanzania isemayo: “Viganja viwili ni kwa ajili ya kuoshana.”

NA KUIFUTA KWA KITAMBAA ALICHOJIZUNGUSHIA

 Yesu alitumia raslimali zake za kibinadamu kuwahudumia wengine. Tutumie raslimali tulizonazo kuwatumikia wengine. “Upendo una mikono kuwasaidia wengine. Upendo una miguu kuharakisha kuwasaidia masikini na wahitaji. Upendo una macho kuona mahangaiko na shida za wengine. Upendo una masikio kusikiliza kilio na sauti za huzuni za watu. Namna hiyo ndivyo upendo ulivyo,” alisema Mt. Augustino wa Hippo.

Huduma ni gharama ya ufuasi. Tulipe huduma hiyo. Upendo ni gharama ya ufuasi tulipe gharama hiyo. Yesu ametupa mfano wa unyenyekevu, mfano wa upendo, mfano wa huduma, mfano wa undugu na mfano wa utume.


Counter

You are visitor since April'08