Friday, March 21, 2014

HAUJAKATALIWA


                                                           

 

  1. Kut 17: 3-7
  1. Rum 5: 1-2.5-8
  1. Yn 4: 5-42

 

“Kuzomewa kunasikika sana kuliko kushangiliwa,” alisema Lance Armstrong.  Kama wewe umezomewa, umesemwa, umekataliwa na watu kumbuka Mungu wetu ni Mungu wa fursa nyingine, nafasi nyingine, Mungu hajakukataa.  “Nachukulia kukataliwa kama mtu anayepiga vuvuzera masikioni mwangu kuniamsha ili kuendelea na safari badala ya kurudi nyuma,” alisema Sylivester Stallone. Katika maisha tunkumbana na visa vya kukataliwa. Ombi la kazi kukataliwa. Ombi la kuongezewa mshahara kukataliwa. Ombi la uchumba kukataliwa. Hoja zako kwenye mkutano kukataliwa. Maoni yako kukataliwa. Lakini Mungu hajakukataa.

Katika Biblia tunasoma: “Mara hapo wafuasi wake walirudi na wakashangaa kumkuta anasema na mwanamke” (Yohane 4: 27). Mwanamke huyu alikuwa Msamaria. Alienda kuchota maji saa sita mchana kwenye Kisima cha Yakobo. Alijitahidi kukwepa wanawake wengine. Historia yake ilikuwa mbaya. Alikwepa majungu. Alikwepa kuyoshewa kidole. Alikwepa watu. Alikuwa na wanaume watano kabla na aliyekuwa naye wakati huo hakuwa mme wake. Wafuasi wa Yesu walishangaa kumkuta anaongea na mwanamke wa aina hii. Licha ya kukataliwa na wasamaria ni kama alikuwa amekataliwa na wafuasi wa Yesu. Kisa hiki kinatupa mafundisho yafuatayo.

Saa ambayo haumtafuti Yesu. Yeye anakutafuta. “Nilikubali wanikaribie watu wasioniuliza kitu, wanipate wale wasionitafuta” (Isaya 65:1). Yesu alimtafuta mwanamke huyu kumpa habari njema ya wakovu. Ni kama mchungaji mwema anayeacha kondoo tisini na tisa na kwenda kumtafuta kondoo aliyepotea. Yesu alimpata Zacchaeus na sio Zacchaeus aliyempata Yesu. Yesu alimtafuta Saulo (Paulo). Sio Paulo aliyemtafuta Yesu. Wakati tunapomtafuta Mungu naye anatutafuta.

Katika ubaya wako kuna uzuri. Mwanamke huyu Msamaria aliacha mtungi wake na kwenda kuwaita watu wamuone Yesu. Wamuone yule aliyemwambia aliyotenda. Wamuone Masiya. Mkwepaji watu anakuwa mtangazaji na habari njema. Kuna hadithi juu ya mitungi miwili ya kutekea maji. Muuza maji alikuwa anabeba mitungi hiyo miwili. Mmoja ulikuwa mtungi usio na ufa. Mtungi wa pili ulikuwa na nyufa tatu. Kila mara maji katika mtungi wenye nyufa yalimwagika. Mchota maji alilipwa pesa kidogo sababu hiyo. Mtungi wenye nyufa kila mara ulisononeka na kuwa na huzuni ukimwambia mteka maji kuwa unamfanya kupata kiasi kidogo cha fedha unamwaga maji njiani. Mteka maji aliuwaambia mtungi. Usijidharau. Sijakukataa. Tazama nyuma kila unapomwaga maji, unamwagilia maua ya bwana wangu na yanafanya sehemu hii ipendeze. Katika ubaya wa mtungi huu palikuwepo na uzuri. Yesu aligundua nyufa kwenye moyo, dhamira ya mwanamke Msamaria kisiwani.

Ukibadilika Mungu anakurudishia heshima ya kusikilizwa. Kadiri Bwana Yesu alivyongea na mwanamke mwanamke huyo alibadilika katika kumtabua Yesu ni nani. Kwanza alimuita wewe, baadaye Myahudi, baadaye Bwana au Sir, baadaye nabii na hatimaye Masiya. Kubadilika huku kunaakisi na kubadilika kimtazamo. Mwanamke huyo alipokimbia kutoa habari kwa watu aliowakwepa tunaambiwa: “Katika mji ule Wasamaria wengi walimsadiki kwa sababu ya neno la mwanamke yule aliyeshuhudia” (Yohane 4:39). Wasamaria walianza kuamini neno la mwanamke huyo. Kama unasimama kuongea watu wanasema wewe kaa chini au msimpe kipaza sauti. Heshima yako Mungu anaweza kuirudisha. Jambo la msingi ni kubadilika na kuacha ubaya.

Kukataliwa ni changamoto. “Watu wema wanapokufikiria kuwa wewe ni mtu mbaya, unakuwa na moyo wa kusaidia watu wabaya. Unawaelewa,” alisema Criss Jami. Usijidharau kwa vile watu wengine wamekudharau. Wewe sio bidhaa mbovu. Wewe si takataka. Wewe ni mpakwa mafuta kwa vile ulibatizwa. Inashangaza buibui anavyotengeneza utando wa kukamata wadudu lakini yeye hakamatwi. Inasemekana mwili wake unatoa mafuta ambayo hutiririka miguuni na kulainisha anapopita. Yeyote aliyebatizwa ana upako wa Roho Mtakatifu, ule uwezo wa kukwepa maovu. Lakini shida hatutumii uwezo huo. Ni kama stima au umeme. Watu wengi wanatumia stima au umeme kuona tu. Lakini unaweza kutumiwa kunyoshea nguo, kupikia, viwandani, kwenye runinga, simu, video kutaja matumizi machache.

Haujakataliwa. Mungu anakujua kwa jina. “Nitafanya na hilo neno uliloniomba, kwa maana umepata upendeleo wangu, na kwamba nakujua kwa jina lako” (Kutoka 33:17). Mungu anakupenda kama kwamba ni wewe peke yake duniani. Ukikataliwa kumbuka wewe si wa kwanza kukataliwa. Yesu alikataliwa na watu wa kijijini kwake. “Hakuna nabii mwenye kukubaliwa mjini mwake” (Luka 4:24).

ULICHOPATA KWA IMANI KITAPOTEA UKIKUFURU: Kutajwa kwa shamba na kisima cha Yakobo (Yn 4: 6) kunafunua ukweli huo. “Njiani alifika mji wa Samaria uitwao Sikari, karibu na Shamba ambalo Yakobo alimpa mwanawe Yozefu. Pale palikuwa na kisima cha Yakobo.” (Yn 4: 5-6). Kisima cha Yakobo kilikuwa karibu na Mlima Gerizimu. Yohana anataja mahali hapo penye Kisima, “kukumbusha mababu walichopata kwa imani kwa Mungu, wayahudi walikipoteza kwa kukufuru kwao,” alisema Baba wa Kanisa Theophyl. Ukiomba kupata kazi usikufuru. KAZI NI MBAYA UKIWA NAYO.

 

Counter

You are visitor since April'08