Saturday, March 8, 2014

PAMOJA NA YESU HAKUNA KUSHINDWA PAMOJA NA SHETANI HAKUNA KUSHINDA


                               JUMAPILI YA 1 YA KWARESIMA MWAKA A
 

1. Mwanzo 2: 7-9, 3: 1-7
2. Warumi 5: 12-19
3. Mt. 4: 1-11

 

 UTANGULIZI

Ukiwa pamoja na Yesu hakuna kushindwa. Ukiwa pamoja na shetani hakuna kushinda. Shetani hana meno ya kuuma.  Lakini Shetani ni mjanja. Ni mwerevu. Ni mdanganyifu. Ni mwenye kuahadaa. Ni mwenye ghiliba. Ni mwenye hila. Ni muongo. Ni mwasi. Ni mwovu. Ni adui. Ni Baba wa uongo. Lakini UKWELI ni ngao dhidi ya uongo wa shetani. Ni baba wa njia za mkato ambazo zinageuka na kuwa njia ndefu. Ni vizuri kujua ukweli huu, “Shetani ana uwezo wa kupendekeza jambo baya lakini hakupewa uwezo wa kukulazimisha kulitenda” (Mt. Cyril wa Yerusalemu.” Shetani alipendekeza mambo mbalimbali kwa Yesu lakini hakushinda.

 
Hadithi: Kuna mtoto aliyekuwa anawatupia watu Kanisani mawe madogo sana – changarawe padre alipomwagalia yeye alisema, padre endelea na mahubiri yako mimi nakusaidia watu wasisinzie. Shetani anaweza kupendekeza uje Kanisani lakini anaweza kukwambia sinzia kidogo.

 
SHETANI YUPO

Shetani wa mtu ni mtu. Methali hiyo inatumiwa na watu kuonyesha kuwa shetani hayupo. Mbaya wa binadamu ni binadamu mwenziwe. Je shetani yupo? Jorge Kardinali Medina alijibu swali hilo tarehe 26 Januari 1999, “Yeyote anayesema shetani hayupo sio muumini tena.” Shetani yupo ingawa hatumuoni. Kuna vitu maishani ambavyo vipo ingawa hatuvioni. Mfano, microwave (wimbi maikro), ultravioletrays (miali isiyoonekana kwa jicho), upepo upo lakini hatuoni. Ingawa shetani yupo lakini ni mfungwa. Mt. Augustini anamlinganisha shetani kama mbwa aliyefungwa kwenye myororo anaweza kukuhumiza ikiwa utamkaribia. Lakini kuna ambao wanamuona shetani kila mahali. Wakisikia paka anato sauti isiyo ya kawaida wanasema, huyo ni shetani maana sauti hiyo siyo ya kawaida.

 

 

SHETANI NI MJANJA

Shetani ni mjanja. Ni mwerevu. Ni mdanganyifu. Ni mwenye kuahadaa. Ni mwenye ghiliba. Ni mwenye hila. Ni muongo. Ni mwasi. Ni mwovu. Ni adui. Ni Baba wa uongo. Ni baba wa njia za mkato ambazo zinageuka na kuwa njia ndefu. “Shetani ana uwezo wa kupendekeza jambo baya lakini hakupewa uwezo wa kukulazimisha kulitenda.” (Mt. Cyril wa Yerusalemu.”

 

Shetani ni mpenda giza. Lakini, JIBU LA GIZA NI MWANGA. Ukiwa na dhambi moyoni mwako unakuwa na giza. Shetani anapenda hilo giza. Ukiileta dhambi hiyo kwenye mwanga katika sakramenti ya kitubio unamfukuza shetani. Dhambi ni mali ya shetani. Ananusa palipo na dhambi na kuelekea huko. Ni kama kwenye chumba chako ukiwa na uchafu, mende watafurika huko maana una mali zao yaani uchafu.

 

UJANJA WA SHETANI

 

1.                                                                                                                              PENDEKEZA SHUGHULI NYINGI

 Shetani anaweza kukushawishi ili uwe na shughuli nyingi ili usishughulikie jambo lilo muhimu. Eva alikuwa msaidizi wa Adamu na Adamu msaidizi wa Eva katika raha na shida katika magonjwa na afya. Lakini Eva alipokuwa anajaribiwa na Adamu, Adamu alikuwa na shughuli nyingi hakuwa pamoja na Eva. Pengine shughuli nyingi zinaweza kuwa namna ya uvivu. Nina shughuli nyingi sitaenda Kanisani. Hapo kuna uvivu wa kwenda Kanisani.

 

2.                                                                                                                              KUTIA MASHAKA

 

Shaka ni wasiwasi. Ni babahiko. Ni tuhuma. Ni hangaiko. KUTIA MASHAKA ni mbinu anayotumia shetani. Shetani kwa mbinu hii anakubabahisha. Anakuletea wasiwasi, tuhuma na mahangaiko. Anakuweka katika njia panda. Anakuweka katikati ya mambo mawili. Unaanza kujiuliza, “Niteme! Nikitema natema utamu. Nimeze! Nikimeza nameza moto.” Shetani anawaletea mashaka wanaojua ukweli wa mambo.  Shetani alimletea mashaka Eva si kwamba alikuwa hajui ukweli wa mambo: “Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, msile matunda ya miti yote ya bustani?” Neno “ati,” linadokeza mashaka.

 

Shetani alimletea Yesu  mashaka, “Ikiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe nikate,” ikiwa ndiwe mwana wa Mungu jitupe chini.”  Neno “ikiwa,” linadokeza mashaka. Padre alijibu simu, “Leta Katoni sita za whisky, nyumbani kwangu.” Padre alielewa sauti hiyo kuwa ni ya Mkristu wake. Alimjibu, “Mimi ni paroko wako.” Alitegemea Mkristu huyo aombe msamaha, badala yake Mkristu huyo alijibu, “Unafanya nini kwenye stoo ya pombe.”  

 

Shetani anaweza kukuletea mashaka wakati wa msiba na matatizo. Kama Mungu anakupenda kweli, kwanini amemchukua mke wako? Kama Mungu anakupenda kweli kwanini amemchukua mme wako? Kama Mungu anakupenda kwa nini umepatwa na maradhi ambayo yanakufanya usitoke kitandani kutwa kucha?

 

3.                                                                                                                              KUONDOA HOFU

Kuondoa hofu ni mbinu ambayo shetani hutumia kuondoa mbegu iliyopandwa moyoni. Watu hukimbia kumkwepa nyoka na nyoka hukimbia kukwepa watu.” Hiyo ni methali ya Yoruba. Inatufunulia juu ya woga na hofu. Shetani alimuondolea hofu Eva. “Nyoka akamwambia mwanamke, ‘Hakika hamtakufa.” (Mwanzo 3:4)  Shetani alipomjaribu Yesu alitaka kumwondolea hofu, “Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, ‘Atakuagiza malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.” (Mathayo 4: 6) Shetani alimuondolea hofu kwa kutumia Biblia. Shetani anaweza kukuondolea hofu kwa kutumia Biblia vibaya. Kuna watu wanaofanya ulevi kuwa halali kwa kutumia maneno ya Paulo kwa Timotheo, “Usinywe maji tu, bali unywe divai kidogo kwa ajili ya tumbo lako, kwani unaugua mara kwa mara.” (1 Timotheo 5: 23) Mtume Paulo wa Tarsus hapingi kunywa divai bali anapendekeza kiasi katika neno kidogo. Anapinga ulevi. Lakini kifungu hiki kinaweza kutumiwa vibaya kuendekeza tabia ya ulevi.

 

Shetani anaweza kukuondolea hofu na ukasikia sauti kwenye moyo wako inakwambia, “Ukiiba hautakamatwa.” Lakini za mwizi ni arobaini. Unaweza kusikia sauti inakwambia moyoni, “Kumtazama mwanamke kwa kumtamani sio shida.” Lakini safari ndefu huanza kwa hatua moja. Yesu alisema, “...atakayemtazama mwanamke kwa kumtamani, amekwisha zini naye moyoni mwake.” (Mathayo 5: 28) Shida sio kutazama. Shida ni mawazo unayojenga baada ya kutazama. Maana makosa huanza kwanza na kuwaza baadaye ni kutekeleza. Kuna mtu aliyemwambia mwenzake, “Nilipomuona mwanamke huyo nilitenda dhambi za mawazo.” Rafiki yake akauliza, “Kwani uliyafurahia mawazo hayo.” Mtu huyo akajibu, “Sikuyafurahia bali yalinifurahisha.” Mawazo ya kutenda kinyume na matakwa ya Mungu kama yanakufurahisha ina maana unayafurahia na hapo ni mwanzo wa kupiga mbizi katika bahari ya ubaya na uovu.  Askofu Cyril (315-387) aliyekuwa Askofu wa Yerusalemu mwaka 349 alikuwa na haya ya kusema, “Shetani ana uwezo wa kupendekeza jambo baya lakini hakupewa uwezo wa kukulazimisha kulitenda.”  Shetani akipendekeza uue hakulazimishi kuua. Shetani akipendekeza uibe hakulazimishi uibe. Shetani akipendekeza useme uongo hakulazimishi kusema uongo. Lakini ujue kuwa ukiwa pamoja na Yesu hakuna kushindwa. Ukiwa pamoja na shetani hakuna kushinda.

 

 

4.                                                                                                                              TOA AHADI

Aliwapa ahadi Adamu na Eva, “Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.” Shetani alimpa ahadi Yesu, “Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake, akamwambia, “Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia.”

 

Ahadi ni deni. Ni kweli lakini Shetani hutoa ahadi hewa. Aliwapa ahadi Adamu na Eva, “Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.” Shetani alimpa ahadi Yesu, “Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake, akamwambia, “Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia.”

 

 “ Lakini nyinyi, watoto, ni wake Mungu na mmekwisha washinda hao manabii wa uongo; maana Roho aliye ndani yenu ana nguvu kuliko roho aliye ndani ya hao walio wa ulimwengu.” (1 Yohane 4:4)

 

 

Kutoa ahadi ya uongo ni kuhujumu ukweli. Ni kuhujumu sera ya Mungu sera ya ukweli. Tukumbuke kuwa DINI NI BIMA KATIKA DUNIA HII DHIDI YA MOTO WA MILELE AMBAPO SERA NZURI NI KUWA MKWELI.

 

 

5.                                                                                                                              VUTA KWINGINE

Shetani anaweza kukuvuta kwingine. Anakutoa kwenye barabara kuu. PITIA BARABARA KUU MCHEPUKO SI DILI. Yesu alianza kuwafundisha wanafunzi wake kwamba ni lazima Mwana wa Mtu apatwe na mateso mengi na kukataliwa na wazee na makuhani wakuu na waalimu wa sheria. Kwamba atauawa, na baada ya siku tatu atafufuka. Yesu aliwaambia jambo hilo waziwazi. Hapo, Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea. Lakini Yesu akageuka, akawatatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro akisema, ‘Ondoka mbele yangu Shetani! Mawazo yako si ya kimungu ila ni ya kibinadamu.” (Marko 8: 31 – 33) Hapana tuonaona nguvu ya HAPANA. Muite Yesu. “Naye Mungu aliye chanzo cha amani hatakawia kumponda Shetani chini ya miguu yenu.” (Warumi 16:20)

 

6.                                                                                                                              KUKATISHA TAMAA

Mtu aliyekata tamaa hamlii Mungu. Haombi. Yuda Iskarioti alikata tamaa. Hakuomba msamaha. Hakutoa machozi ya toba kama Petro. Shetani anapambana dhidi ya MATUMAINI.

 

7.                                                                                                                              KUNGOJA KESHO

Shetani anatumia mbinu ya kuhairisha mambo. Anaweza kukushawishi uende Kanisani lakini ikifikia suala la kutekeleza anakwambia ngoja kidogo.

 

 

8.                                                                                                                              FANYA BUBU

Mungu wetu sio kiziwi labda kama midomo yetu imekuwa bubu. Mbwa mwitu akitaka kumuua kondoo anamkaba koo kwenye shingo hasitoe sauti kumwita Bwana wake. Shetani akitaka kutumaliza anahakikisha hatutoi sauti. Anakuzuia kusali. Shetani aliwazuia Adamu na Eva wasimlilie Mungu na kuomba msaada wake. Wakati wa ubatizo Padre humgusa mtoto masikio na kinywa kwa kidole gumba, akisema: “Bwana Yesu aliyewafanya viziwi wasikie, na bubu waseme, akujalie uweze kusikia kwa masikio neno lake, na kuungama kwa mdomo imani ya kikristu, kwa sifa na utukufu wa Mungu Baba. Amina.” 

 

Adamu na Eva hawakuwa macho pia midomo yao ilifanywa bubu na shetani. Mtakatifu Petro anatuasa, “Mwe macho; kesheni! Maana adui yenu, Ibilisi, huzungukazunguka kama samba angurumaye akitafuta mawindo. Mwe imara katika imani na kumpinga.” (1 Petro 5:8-9) Kuwa imara katika imani kunahitaji kuinua mioyo juu na kumuomba Mungu atusaidie. Kwa kawaida mateso hutazama nyuma, wasiwasi huangalia pande zote, na imani hutazama juu. Katika taabu hatuna budi kufikiri kama Mtunga zaburi aliyesema, “Ee Bwana, nakuinulia nafsi yangu, ee Mungu wangu, nimetumaini wewe, nisiaibike, adui zangu wasifurahi kwa kunishinda.” (Zaburi 25:1). Mtunga zaburi anajua atazame upande upi-upande wa juu.

 

 

HITIMISHO

 Ushindi wa Yesu dhidi ya Shetani unatupa ukweli kuwa kushinda vishawishi kunawezekana. Yesu ni mwasisi wa ubinadamu mpya. Yesu ni mwasisi wa ushindi (Mwanzo 3:15).

Counter

You are visitor since April'08