Saturday, March 15, 2014

USIJISAHAU, USIMSAHAU, USIWASAHAU




                                                 Jumapili ya 2 ya Kwaresima

1. Mwanzo 12: 1-4
2.  2 Timotheo 1: 8-10
3.  Mathayo 17: 1-9

 USIJISAHAU
Kama umemsahau Mungu umejisahau.” Ni methali ya Kiswahili. Wakati Yesu alipogeuka sura katika mlima Tabor Mtume Petro  alijisahahu katika masuala mawili. Kwanza alijisahau yeye na wenzake  katika suala la kusali. “Petro na wenzake walikuwa wameshikwa na usingizi, lakini walipoamka, waliona utukufu wake na wale watu wawili wakisimama naye” (Luka 9: 32).  Kuacha kusali ni kujisahau. Mtoto mmoja aliyeitwa John alikuwa anajiandaa  kusali sala za jioni alipomuuliza mama yake, “Ni lini unanishauri niache kusali kama baba alivyoacha kusali?”Mama alimweleza mtoto wake kuwa sala haina mambo ya likizo, haina kustaafu. Sala haina kuhairisha.
Pili alijisahau katika suala la kujenga vibanda. Petro alimwambia Yesu, “Mwalimu, ni vizuri kwetu kukaa hapa; tutajenga vibanda vitatu, kimoja chako, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya.” (Mathayo 17: 4). Juu ya mtume Petro Caro Kardinali Maria Martini alikuwa na haya ya kusema. “Tilia maanani kutojipendelea kwake: vibanda ni kwa ajili ya Yesu, Musa na Eliya, wakati  mitume wanaweza kukaa nje ambako ni wazi.” Ingawa mtume Petro akujipendelea hakujipenda au alijisahau.  Marcus Tullius Cicero aliwahi kusema: “Sijawahi kusikia mtu ambaye ni mzee sana akisahau alipozika pesa yake! Wazee hukumbuka wanachokipenda: tarehe za kesi za madai, na majina ya wanaowadai na wadaiwa.” Kama tunakumbuka tunachopenda tusiwasahau watu wengine hatuna budi kuwapenda.
Mfanyabiashara anaweza kujisahau. Anatafuta pesa lakini hawezi kula vizuri au kulala mahali pazuri. Huko ni kujisahau. Mvuvi anaweza kujisahau. Wakati anauza samaki anakula chakula bila kitoweo. Fundi seremala wakati anatengeneza milango mizuri kwa ajili ya watu wengine unakuta mlango wake una matundu makubwa ya kupitisha kichwa. Mfinyanzi hulia kwenye kipande cha chungu. Ni methali ya Tanzania. Anayetengeneza vyungu vya kupikia yeye anatumia kipande cha chungu kilichovunjika. Fundi cherehani wakati anashonona mitindo mipya unakuta yeye anavaa nguo zilizochanika. Ni kujisahau. Daktari wakati anahimiza watu wengine wamalize dozi yeye akiugua anashindwa kumaliza dozi. Ni kujisahau. Unaweza kukuta mtu anauza baisikeli wakati yeye hana baisikeli. Ni kujisahau. Mwalimu anayefundisha somo la kuwekeza yeye hawekezi hata kidogo kuwekeza. Mwalimu anafundisha somo la Mipango Mikakati wakati yeye hana hata diari. Ni kujisahau. Mlinzi anaweza kujisahau. Unaweza ukagundua wizi umetokea mahali fulani lakini aliyesaidia kufanikisha zoezi hilo la kuhujumu ni mlinzi. Mwindaji anakuwa muwindwa. Kuna methali ya wahaya isemayo: Wanaolinda vibuyu vya pombe ndio wanaovivunja. Mwanampotevu alijisahau kuwa Baba yake ni Tajiri alikuwa tayari kujishibisha kwa r chakula cha nguruwe. Usijisahau wewe ni Mwana wa Mungu. Umeumbwa kwa mfano na sura ya Mwenyezi Mungu.


USIMSAHAU
Yesu usimsahau. Mto ambao usahau chanzo chake utakauka. Ni methali ya Yoruba. Yesu ni chanzo chako usimsahu. Kuna aliyesema: “Tukikutana na ukanisahau, haujapoteza chochote. Ukikutana na Yesu Kristo na ukamsahau, umepoteza kila kitu.” Mateso, shida, visitufanye tumsahau Yesu wa utukufu.  Mtume Yohane mmoja wa watatu aliandika: “Nasi tumeona utukufu wake” (Yohane 1: 14). Petro aliandika: “tulikuwa mashahidi wenyewe tulioona kwa macho yetu utukufu wake” (2 Petro 1: 16). Hii ni kumbukumbu ya kugeuka sura. Mitume kabla ya kuimarishwa na Roho Mtakatifu na kabla ya ufufuko walisahau Yesu wa utukufu, Yesu wa kugeuka sura. Petro alimfuata kwa mbali. Petro alimkana Yesu. Yohane akikumbuka vizuri Yesu wa utukufu alikuwa amesimama chini ya msalaba. Yakobo alikimbia. Usimsahau Yesu wa kugeuka sura. Katika Misale ya Waumini Chapa ya kumi ya mwaka 2008 katika kituo cha kumi na tano tunasali hivi: “Twakushukuru, ee Yesu, kwa mateso yako, lakini twakushukuru hasa kwa ufufuko wako, kwa kuwa huo ndio unaotupa hakika ya kuwa hatukuzaliwa kwa ajili ya mateso na maumivu, bali kwa ajili ya heri ya milele.” Katika maneno haya tunajifunza kuwa mateso hayana kauli ya mwisho. “Tuishi maisha yetu kama kwamba Kristo anakuja mchana huu,” alisema Jimmy Carter.
Mtakatifu Thomas Aquinas aliweka wazi lengo la Yesu kugeuka sura: “Wewe uligeuka sura mlimani, na kadiri walivyoweza, wafuasi wako walitafakari utukufu wako ee Kristo Mungu ili watakapokuona umesulubiwa waelewe kwamba mateso yako yalikuwa ya hiari, na watangaze duniani kwamba Wewe ni kweli mng’aro wa Baba.” Hapa tunajifunza kuwa Ijumaa Kuu inatangulia Jumapili ya Paska. Hapa tunajifunza kuwa mtaka cha uvunguni sharti ainame. “Imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi” (Matendo ya Mitume 14:22).
Katika hadithi za Aesop kuna hadithi ya mbwa aliyeona sura yake ikiakisiwa kwenye dimbwi la maji chini ya miguu yake. Ingawa alikuwa ameshikilia mfupa, aliona wivu kuona mbwa kwenye dimbwi la maji akiwa na mfupa mdomoni. Alifungua kinywa chake ili kumbwekea mbwa mwingine na kuweza kumnyanganya mfupa. Utukufu kama wa Yesu wa kudumu ndio tunautafuta. Usiache utukufu huu na kukimbilia mambo yanayopita. Usiache mtego ambao umekamata ukaenda kuchungulia mtego uliotegwa.
USIWASAHAU
Watu wengine usiwasahau. Kusahau ni sawa na kutupa. Ni methali ya Kiafrika. Usiwatupe wenzako. Ukisikia mtu anasema amewatupa ndugu zake. Ina maana amewasahau. Petro alimwambia Yesu, “Mwalimu, ni vizuri kwetu kukaa hapa; tutajenga vibanda vitatu, kimoja chako, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya.” (Mathayo 17: 4). Mt. Petro alisahau kuna watu wanawangoja chini ya Mlima.  Alisahau kuwa kuna mitume wenzake.  Yesu Kristu alitaka kuwaonesha kidogo utukufu ambao ni matokeo ya kubeba msalaba.  Ijumaa Kuu kwanza, Jumapili ya Paska baadaye.  Kula kutamu, kulima mavune.  "Mavune" maana yake " machofu".  Utukufu huu ilibidi Mt. Petro arudi chini ya mlima na wenzake waufanyie kazi.  Ukiona vyaelea vyaundwa. 
Petro hakulielewa bado neno hilo alipotamani kuishi na Kristo mlimani. Amekuwekea hayo, Petro, baada ya kifo chako lakini sasa yeye mwenyewe anakuambia: shuka kuangaika duniani, ukatumikie duniani, ukadharauliwe, ukasulubiwe duniani.Uzima umeshuka ili kuuawa:Njia imeshuka ili isikie uchovu wa duniani; chemichemi imeshuka ili kupata kiu;nawe wakataa kuteseka? (Mt. Augustino Sermo 78,6: PL38,492-493;Lk9:33). Cha bure hakipatikani. Mtaka cha uvunguni sharti ainame.
Kuwakumbuka watu wengine ni jambo muhimu. Mwizi msalabani alitaka kukumbukwa (Luka  23:42).  Wahaya wana msemo husemao, "Maji yakichemka hayasahau ubaridi."  Tusisahau makundi ya watu chini ya mlima, wenye shida, wenye matatizo.  Kuna mgonjwa wa kutembelea chini ya mlima, kuna wafu wa kuzika chini ya mlima, kuna mfungwa wa kutembelea chini ya mlima, kuna aliyeuchi ni wa kuvisha chini ya mlima.
Mtoa ahadi asiwasahau wale aliowapa ahadi. Nasi katika maisha tusiwasahau wengine.  Ahadi tunazofanya wakati wa matatizo na karaha, wakati wa matezo na masumbufu tunazisahau wakati wa raha, wakati wa utulivu.  Kukopa harusi, kulipa matanga.  Daktari alimwambia mgonjwa, “utapona lakini unaumwa sana”.  Mgonjwa alimjibu, “Tafadhali, Daktari fanya kila unaloweza kuakikisha ninapona.  Nikipona nitatoa milioni thelathini kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali mpya.”  Miezi michache baadaye mgonjwa huyo alipokuwa amepona kabisa daktari alimkumbusha ahadi yake: “Ulisema ukipona utatoa msaada wa milioni thelathini?”  Mgonjwa aliyepona alishangaa, “Kama nilisema hivyo, nilikuwa mgonjwa kweli.”   Mgonjwa aliyepona alimsahau daktari.
Mwalimu usiwasahau wanafunzi ni wateja wako wanakutegemea uwape elimu. Wanafunzi wanahitaji msaada toka kwa walimu kutokana na visa vifuatavyo: Mwalimu wakati wanaandikisha wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza. Mwalimu alimwambia mwanafunzi: “ Nitajie majina ya baba yako na mama yako. Mwanafunzi alijibu.” Majina yao ni Dadi na Mami.”  Katika kisa kingine mwalimu alimuuliza mwanafunzi: “Taja vitu viwili ambavyo havikuwepo miaka mia moja iliyopita.” Mwanafunzi alijibu: “Ni mimi na wewe.” Lakini binadamu si kitu. Mwalimu alimuuliza mwanafunzi: “Mama mdogo kwa Kiingereza anaitwaje?” Mtoto alijibu: “Anaitwa – minimum.” Na mama mkubwa anaitwaje?” mwalimu aliendelea kuuliza licha ya mwanafunzi kukosea. Mwanafunzi alijibu anaitwa maximu.” Mwanafunzi alikosea. Wanafunzi wanahitaji kusaidiwa.
Mwanasiasia usiwasahau wapiga kura wapo chini ya mlima wanakungoja.  Daktari, nesi, mganga, muuguzi usiwasahau wagonjwa. Wagonjwa wana hofu zao wengine hawaelewi. Kuna mtu mmoja alikuwa anatoka Hospitalini analia. Karibu na lango palikuwa na mgonjwa anaingia akauliza kwa nini unalia. Mgonjwa akasema wamekata kidole changu wakati wanatoa damu ili kuipima. Mgonjwa mwingine wa kiume akashtuka na kusema: “Mimi itakuwaje maana naenda wapime mkojo.” Mchungaji usiwasahau kondoo wako. Wakristu msiwasahau wachungaji.  Mtawala usiwasahau wale unaowatawala. Mzazi usiwasahau watoto wako. “Kuku mwenye vifaranga hamezi mnyoo.” Ni methali ya kisukuma. Watoto msiwasahau wazazi wenu. “Hujui kama unawapenda wazazi wako mpaka hapo wanapokufa.” Ni methali ya Namibia.
Mwanandoa usimsahau mwenzi wako wa ndoa. Kula umbakizie.  Mkumbuke. Usitake kwenda mbinguni peke yako. Ilikuwa ni wakati wa roho kuingia mbinguni. Watu waligawanywa kulingana na hali zao za maisha; hivyo, watu wa ndoa, watawa, mapadre, na watu wasio na miiito hiyo ya ndoa, utawa na upadre walikusanywa pamoja. Lango la mbinguni lilikuwa na mlango kwa kila hali ya maisha. Watu wa ndoa kwa mfano, walipaswa kuingia kupitia mlango wa kwanza. Hata hivyo mwanamume mmoja ambaye ndoa yake iliishatenguliwa kwenye mahakama ya serikali, zamu yake ya kuingia ilipowadia, alikuta kwamba mlango haufunguki tena.  “ Malaika”, alimwita mlinda mlango, “Nimejaribu kufungua huuu mlango kwa ufunguo wangu, lakini haufunguki”. “Mke wako yuko wapi ?” Malaika aliuliza. “Nilimpa talaka.” “Basi inabidi umtafute.” “Lakini sijui aliko!” alijibu mwanaume. “Heri ungelijua”, alisema malaika. “Lango la mbinguni kwa watu wa ndoa laweza kufunguliwa tu kwa funguo mbili’. “Lakini mke wangu ana nini la zaidi?” aliuliza kwa uchungu. “Bwana”, malaika akajibu, “ufunguo mwingine wa mlango anao yeye. Unahitaji ufunguo wake ili mpate kuingia pamoja”. (Angalisho Katika Kanisa Katoliki hakuna talaka. Panaweza kuwepo kutengana kwa muda. Au ndoa kubatilishwa kwa maana ya kutangazwa ndoa haikuwepo ni null and void)
Wakopaji msiwasahau waliowakopa. Isiwe kukopa arusi kulipa matanga. Tulio hai tuwakumbuke marehemu. Tuwaombee tusiwasahau.
HITIMISHO
Kumbuka kukumbuka. Kugeuka sura ni tukio linaloimarisha imani. “Tukio hili liliimarisha imani ya Mitume hao watatu kwa Bwana wetu Yesu. Bwana alijua kwamba imani yao itajaribiwa vikali sana baadaye watakapomwona bustanini katika mahangaiko makubwa, na hasa atakapokuwa anateswa na kuuawa msalabani. Kwetu sisi, hii ni nafasi ya kuiamsha upya imani yetu kwa Kristu Bwana wetu Msulubiwa na Mfufuka, ambaye heri yake tunatumaini kuishiriki baadaye. Kulitafakari fumbo hili kutujalie picha fulani ya heri hiyo ijayo.” (John Kabeya, Maisha ya Watakatifu, uk. 270). Yesu ni mfariji mateso tunayopitia. Unaweza kumweleza mtoto sababu za  kundugwa sindano nesi anapokuja kumdunga sindano anakimbia kumwendea mama yake. Kufarijiwa hakuhitaji sababu bali kujua kuna mfariji. 
Kuwa na utamaduni wa kupiga picha. Piga picha ya utukufu wa Kristo. Katika somo la kwanza tunaona utamaduni wa kupiga picha Mungu akamleta nje Abramu, akasema: “Utazame mbinguni, uhesabu nyota, kama waweza kuzihesabu. Akamwambia: Ndivyo uzao wako utakavyokuwa. Abramu akamwamini Bwana” (Mwanzo 15: 5-6).  Unapoomba kitu piga picha yake akilini.
Usimsahau Mungu katika kila kitu, hata kabla na baada ya kula. Kuna kijana alimwambia mwenzake mbona haukusali kabla ya kula. Mwenzake akamjibu hakuna haja mama anapika chakula kizuri sana. Kusahau kusali ni kujisahau na kumsahau Mungu. Toa huduma nzuri ulipo. Mhudumu katika hoteli moja alimwambia mteja. “Wewe na ni mara yako ya kwanza kuja hapa.” Mteja aliuliza: “Unajuaje?” Mhudumu alijibu: “Hapa mteja anayekula chakula harudi tena.” Huenda sababu mteja haudumiwi vizuri.

Counter

You are visitor since April'08