SHEREHE YA UTATU MTAKATIFU
"Neema ya Bwana Yesu Kristo, na upendo wa Mungu Baba, na Ushirika wa Roho Mtakatifu viwe nanyi nyote” (2 Kor 13:13).
Mafiga mawili hayawezi kukiivisha chungu; lazima yawe matatu. Tutakapo kufanikiwa lazima tuwe tayari kushirikiana na wenzentu. Nafsi tatu za Utatu Mtakatifu zinashirikiana.
Jumapili ya leo wakatoliki kote duniani wanasherehekea Sherehe ya Utatu Mtakatifu. Inahusu imani kuwa Mungu ni mmoja katika nafsi tatu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Ni kama mafiga matatu. Wakatoliki hubatizwa kwa jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu (Mt 28: 19) na wala sio kwa majina ya Baba na Mwana na Roho Mtakatifu. Katika kufanikisha mambo kuna nguvu ya wingi au nguvu ya namba. Tunaona nguvu ya wingi katika uumbaji. “Mungu akasema: Tumfanye mtu kwa mfano wetu, afanane nasi” (Mwanzo 1:26). Ni Utatu Mtakatifu uliosema “tumfanye mtu,” katika kitabu cha Mwanzo. Ili kufanikiwa lazima kufikiria katika msingi wa “sisi.” Nafsi tatu zinafikiria katika msingi wa sisi. Nakubaliana na Ralph Chaplain Yusufu aliyesema: “Hauwezi ukawa na usalama, hata ukijaribu namna gani; kama haufikiri kwa msingi wa “sisi” badala ya mimi.” Lorii Myers alikuwa na mawazo hayo aliposema: “Sisi ni sawa na nguvu.”
Tunahitaji nguvu ya Utatu Mtakatifu tufanikiwe ambayo inaelezwa na mtume Paulo: “Neema ya Bwana Yesu Kristo, na upendo wa Mungu Baba, na Ushirika wa Roho Mtakatifu viwe nanyi nyote” (2 Kor 13:13).
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo: Bwana wetu Yesu Kristo anatoa neema hata kwa wahalifu.” Ukweli kuwa neema hutolewa hata kwa waalifu ni ukweli ambao tunauona msalabani. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo ilitolewa kwa mwizi Dismasi. Tunahitaji neema ili kufanikiwa. Neema ya Bwana Yesu inaonjeka. Ili kuonja neema ya Bwana wetu Yesu lazima kushirikiana nayo. Kuna ambaye alitaka kushinda bahati nasibu ya Kampuni ya Simu ya Tigo. Kila mara aliomba kushinda. Alisali kwa Bwana wetu Yesu Kristu. Usiku alitokewa katika ndoto. Yesu alimwambia: nataka ushinde lakini nunua vocha. Alitaka naye atoe mchango wake. Ni lazima kushirikiana na neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.
Upendo wa Mungu Baba: Kilichojaa hufurika. Ni methali ya Watanzania. Mungu Baba amejaa upendo na unafurika. Tunakiri upendo huu kwa sala ya shangwe “Abba! Baba! (Warumi 8:15. Upendo wa Mungu Baba unajieleza katika kumtuma Mwana wake wa Pekee. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amsadikiye asipotee, bali awe na uzima wa milele (Yn 3:16). Haya hii ni “Injili katika mfano mdogo.” Kutoa ni matokeo ya upendo. Unaweza kupenda bila kutoa. Lakini hauwezi kupenda bila kutoa.
Ushirika wa Roho Mtakatifu: Somo la pili lionaongelea ushirika huu: “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu” ( Warumi 8:16 ). Kama hewa ilivyo kwa mwili wa binadamu ndivyo Roho Mtakatifu alivyo katika maisha ya kiroho. Anatutia ujasiri. Roho Mtakatifu yupo nyuma ya pazia anafanya mambo. Anaunganisha pointi, matukio anapanga kalenda. Omba kuwa na ushirika naye. Tutumie mafiga haya matatu: Neema, Upendo na Ushirika. Tunahuitaji Utatu Mtakatifu. Tuuiige. Tujifunze kufanya mambo kwa pamoja. “Sala usafiri kwa haraka tunaposali pamoja.” Ni methali ya Kilatini
Sala: Ee Bwana wetu Yesu nisaidie niige Utatu Mtakatifu katika kushirikiana na wengine. Amina.