Monday, December 24, 2012

KRISMASI NI KRISTU KWANZA



                                    MISA YA USIKU
1. Isa 9: 2-7
2. Tit. 2: 11-14
3. Lk 2: 1-14

UTANGULIZI
Yesu anapoingia vivuli vinatoweka. Alizaliwa usiku ili kufukuza giza. Ili afukuze giza tumpe nafasi. Krismasi ni Kristu Kwanza.
MAHUBIRI YENYEWE
Krismasi ni zaidi ya mti wa Krismasi. Krismasi ni zaidi ya kadi za Krismasi. Krismasi ni zaidi ya likizo. Krismasi ni zaidi ya kubadilishana zawadi. Krismaisi ni zaidi ya kula vizuri na kunywa sana . Krismasi ni zaidi ya kuuuza na kununua. Krismasi ni zaidi ya kununua nguo mpya. Kuna mwanaume mmoja alikuwa anakoa sana Kanisani siku ya Krismasi. Tulipomaliza adhimisho la Misa nilimuuliza mke wake, “Mbona mmeo alikuwa anakoa sana Kanisani.” Nilijibiwa na huyo mama, “Yeye ni kawaida yake siku ya Krismasi akinunua suti mpya.”  Tunapokimbizana kusherehekea Krismasi tujiulize, nini chanzo cha haya yote? Krismasi ni Kristu kwanza. Krismasi ni sherehe ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa Yesu Kristu kama wakristo wanavyoamini. “Krismasi ni Kristu, Kristu wa haki na upendo, wa uhuru na amani,” alisema Francis J. Spellman. Tukumbuke kuwa Yesu Kristo mwana wa Maria alipozaliwa alikosa nafasi katika nyumba ya wageni. Je, atabanana katika moyo wako na wageni wengine? Je atakosa nafasi katika moyo wako. Kama kwako Krismasi ni Kristu kwanza hatakosa nafasi katika moyo wako kama alivyokosa nafasi katika nyumba ya wageni.
 Tunasoma hivi katika Biblia: “Walipokuwa wakikaa huko, siku zake za kuzaa zilitimia, (Maria) akamzaa mwanawe, mzaliwa wa kwanza. Akamzungushia vitambaa, akamlaza horini, kwa maana walikosa kupata nafasi katika nyumba ya wageni” (Luka 2:7). Hakukuwa na chumba katika Nyumba ya wageni. Nyumba ya wageni ni hoteli. Inamaanisha ni sehemu yoyote ambayo msafiri aliweza kukirimiwa. Hakukuwa na chumba kwa ajili ya Yesu katika Bethlehemu ikiwa ndiyo ishara ya kukataliwa Yerusalemu. Kushughulikia likizo ya Krismasi tukamsahau Yesu ni kumyima nafasi moyoni ambao ni kama nyumba ya wageni.
 Tukiitazama Krismasi kwa miwani ya kubadilishana zawadi, “Krismasi imejikita katika kubadilishana zawadi: zawadi ya Mungu kwa binadamu-Mtoto wake; na zawadi ya binadamu kwa Mungu pale tunapojitoa kwa Mungu kwanza,” alisema Vance Havner. Krismasi ni zawadi toka kwa Mungu ambayo mtu hawezi kuifanya iwe yake binafsi bila kumshirikisha mwingine. Mshirikishe mwingine habari njema za Yesu Kristu.
 Tukitazama Krismasi kwa miwani ya mti wa Krismasi, ni zaidi ya mti wa Krismasi. “Yeye asiye na Krismasi moyoni mwake hawezi kuikuta chini ya mti,” alisema Roy L. Smith. Chini ya miti nyingi ya Krismasi tarehe 25 Desemba patakuwepo na zawadi nyingi. Katika mti wa Kalvari msalabani palikuwepo na zawadi moja lakini inazijumlisha zawadi zote- zawadi ya Mungu kwetu ya mwana wake wa pekee Yesu Kristu. Tunapochukua zawadi toka mtini wa Krismasi tukumbuke zawadi kubwa Yesu Kristu katika mti wa msalaba. Krismasi ni Kristu kwanza.
 Tukiitazama Krismasi kwa miwani ya upendo, “Kuna upendo wakati wa Krismasi kwa sababu Krismasi ilitokana na upendo. Moyo huu wa upendo na kumtukuza Mungu ubaki ukiwaka,” alisema Joseph Emms Seagram (1841 - 1919) mwingereza raia wa Canada  na mwanasiasa. Natamani moyo huu wa Krismasi tungeutia katika chupa za marashi na kutumia marashi haya kila siku. Kila siku ifanye Krismasi katika familia yako kwa kuwapulizia watu marashi ya maneno ya upendo. Namna hii Krismasi itakuwa ni Kristu Kwanza kwa vile tunaweka katika matendo upendo wake. Kuna mpiga picha siku ya Krismasi ambaye wakati anapiga picha alikuwa karibu sana na mishumaa inayowaka shati lake lilichomwa na moto. Watu walizima moto huo. Mchungaji mmoja alianzia katika tukio hilo kuhubiri. Akisema, “Kuna mmoja wetu ambaye amewaka moto kwa ajili ya Kristu.” Nasi tuwake moto kwa ajili ya Kristu si katika kuchoma nguo bali tuwake moto wa mapendo.  Yesu alikuja kuishi pamoja nasi ili baadaye tuweze kuishi naye mbinguni. Hivyo, tumtangulize tunapoadhimisha Sherehe ya Krismasi.
                                                                  
KRISMASI NI UPENDO KWA VITENDO
 “Krismasi…ni upendo kwa vitendo,” alisema Dale Evans Rogers (1912-2001) mchezaji cinema wa kike, mwimbaji na mtunzi wa nyimbo. Nakubaliana na maneno ya mtunzi huyo. Krismasi sio kisingizio cha watu kulewa, Krismasi sio kisingizio cha walinzi wanaolinda mali ya umma kutofanya kazi. Krismasi sio kisingizio cha watu kutapanya hovyo pesa na kukosa kubana matumizi. Krismasi si kisingizio cha baadhi ya wazazi kuwapokea watoto wa shule waliokuja likizo kwa shingo upande. Krismasi sio kisingizio cha kuchanganyikiwa. Krismasi ni wakati wa kufanya matendo ya upendo. Krismasi sio tu kipindi cha kufungua zawadi ni kipindi cha kuwafungia wengine zawadi. Krismasi ni upendo kwa vitendo. Krismasi ni sherehe ya kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristu. Alizaliwa kuokomboa ulimwengu. Ni jambo la upendo.
Kila mfuasi wa Kristu hata mwanasiasa anatakiwa siku ya Krismasi kufanya matendo ya upendo. Papa Benedict XVI Kiongozi wa juu kabisa katika Kanisa Katoliki katika kitabu chake, “Mungu ni Upendo,” aliandika, “ni lazima upendo uhuishe maisha yote ya walei, na kwa hiyo uhuishe pia kazi zao zote za siasa, ziwe pia kazi zao za ‘upendo kijamii.” Upendo pia utawale siasa. Siasa ikiwa kazi ya upendo kijamii Krismasi inakuwa ni upendo kwa vitendo. Hii ndiyo maana ya Krismasi. Mama Tereza wa Calcutta (1910-1997) mshindi wa zawadi ya Nobel 1979 alikuwa na mawazo kama haya aliposema: “Ni Krismasi kila unapomruhusu Mungu awapende wengine kupitia kwako…ndiyo, ni Krismasi kila siku unapompa tabasamu ndugu yako na kumpa mkono wa salamu.”
Juu ya kuzaliwa Yesu Kristu tunasoma hivi  katika Biblia: “Walipokuwa wakikaa huko, siku zake za kuzaa zilitimia, (Maria) akamzaa mwanawe, mzaliwa wa kwanza. Akamzungushia vitambaa, akamlaza horini, kwa maana walikosa kupata nafasi katika nyumba ya wageni” (Luka 2:7). Yesu alinyimwa nafasi katika nyumba ya wageni. Tunapokosa kutenda matendo ya upendo kwa vitendo tunamunyima  Yesu nafasi mioyoni mwetu siku ya Krismasi. “Krismasi ni kipindi cha kuwasha moto wa ukarimu ukumbini, na miale ya upendo moyoni,” Washington Irving. Bila kufanya hivyo ni kumunyima Yesu nafasi moyoni. Krismasi ni kipindi cha kuonesha ukarimu na kusamehe.
Krismasi si wakati wa watu kugombana na kutumia mabavu. Kufanya hivyo ni kumunyima Yesu Kristu nafasi mioyoni. Kuna insha iliyoandikwa na Mkurugenzi wa California Department of Mental Hygiene akionya: “Kipindi cha Krismasi kinajulikana kinasifika kwa msongo wa mawazo na matendo zaidi ya matumizi ya mabavu kuliko kipindi chochote cha mwaka.” Krismasi tofauti na ujumbe huo hakina budi kuwa kipindi cha kumwinua Yesu Kristu badala ya kuinua matumizi ya mabavu maana yeye alitetea amani. “Amani dunia itadumu, tutakapoiishi Krismasi kila siku,” alisema Helen Steiner Rice.
Hali ya hewa ya Krismasi haina budi kuwa ya upendo. Mtoto mmoja aliyepewa sanamu za kuchezea. Alilalamika kwa mama yake. Mimi naonyesha upendo kwa sanamu hizi lakini zenyewe hazionyeshi upendo. Yesu Kristu kwa kuzaliwa tuonyeshe upendo kwake. Kipimajoto cha upendo ni upendo kwa jirani zetu. Upendo kwa jirani lisiwe suala la Krismasi bali suala la maisha. Tusingoje Krismasi kupeana zawadi. Krismasi huwe utamaduni wa maisha. “Nitaiheshimu Krismasi moyoni mwangu, na kujaribu kuitunza mwaka mzima wote,” alisema Charles Dickens. Huwezi kupenda chumvi bila kupenda muuzaji wa chumvi. Huwezi kupenda Krismasi bila kumpenda Kristu. Benjamin Franklin alisema: “Watu wengi wanasheherekea siku ya Kuzaliwa Kristu! Wachache kweli, wanashika maagizo yake!” Ndugu msomaji nakutakia furaha ya Krismasi ambayo ni matumaini; roho ya Krismasi ambayo ni amani; moyo wa Krismasi ambao ni upendo kwa vitendo

Counter

You are visitor since April'08