Wednesday, April 8, 2015

UKIPANDA HURUMA UTAVUNA HURUMA



                                                   
                              MATENDO SABA YA KIROHO YA HURUMA
                                                      MWAKA B
 Jumapili ya Huruma ya Mungu
1. Matendo 2: 42 - 47
2. 1 Petro 1: 3-9
3. Yohane 20: 19 – 31
UTANGULIZI
Mojawapo ya neno muhimu sana katika lugha ya Kiswahili ni neno huruma. Huruma inashikilia mambo mengi yasiharibike: upendo, umoja, mshikamano, msamaha na  amani. “Ukitaka watu wengine wawe na furaha, huruma iweke katika matendo. Ukitaka kuwa na furaha huruma iweke katika matendo,” alisema  Dalai Lama.  Biblia yasema: “Heri walio na huruma, maana watahurumiwa” (Mathayo 5:7). Hii ni heri pekee ambapo unavuna ulichopanda. “Mwenye huruma ni yule aliye na huzuni moyoni; anahesabu mateso ya wengine kama mateso yake, na anahuzunishwa na maombolezo yao kama ya kwake,” alisema Remigius Baba wa Kanisa. Hapa haki na huruma vinaungana, kimojawapo kinapaswa kuchanganyikana na kingine; haki bila huruma ni ukatili; na huruma bila haki ni ziada kwa hiyo anatoka kwenye heri ya haki na kuiendea nyingine ya huruma. “Huruma sio katika kutoa sadaka tu, bali katika kila dhambi ya ndugu, tunapochukuliana mizigo alisema Baba wa Kanisa Jerome. “Mungu anafurahishwa sana na hisia zetu za kufadhili watu wote, atatoa huruma yake kwa walio na huruma tu,” alisema  Hilary. “Mwanzoni zawadi inaonekana kulingana na kilichotolewa; lakini kusema kweli ni zaidi sana; kwa vile huruma ya kibinadamu na huruma ya kimungu haviwezi kulinganishwa,” alisema Mtakatifu Yohane Chrysostom. Aliyenacho atapewa zaidi.
Watu katika uwanja wa kiuchumi wanazungumzia kununua hisa katika makampuni sisi tunazungumzia kununua hisa za huruma maana Mungu ni tajiri katika huruma (Dives in Misericordia) . “Lakini Mungu ni mwenye huruma nyingi. Alitupenda kwa mapendo yasiyopimika, hata, ingawa tulikuwa tumekufa kwa sababu ya dhambi, alitufanya hai pamoja na Kristo. Kwa neema ya Mungu nyinyi mmeokolewa.” (Waefeso 2: 4-5) Watu wote wanahitaji huruma masikini na matajiri. Huruma sio kwa matajiri tu kama methali ya Kiyahudi inavyotoa kejeli, “Mahakama ina huruma kubwa sana iwapo mshitakiwa ni tajiri sana.” Leo tunasherehekea Jumapili ya Huruma ya Mungu. Ibada ambayo imeenezwa na Mt. Faustina wa Poland baada ya kutokewa na Bwana wetu Yesu Kristu.

MAANA YA NENO HURUMA
Kadiri ya “Kamusi ya Maana na Matumizi,” huruma ni moyo wa imani. Ni moyo wa kupenda kumsaidia mwenye shida. Mfano, “Niliingiwa na huruma nikampa mwombaji fedha za kununulia chakula.” Kuelewa maana ya neno huruma tunaweza kutumia neno la Kilatini, “Misericordia.” Neno hili lina maneno mawili: cordia ambapo yanatoka maneno kama kadiolojia Kiingereza cardiology maana yake taaluma ya moyo; cardiac arrest maana yake shtuko la moyo; cardiac maana yake – a kuhusu moyo; cardiac musle maana yake msuli moyo. Neno “miseri” linamaanisha mateso na shida. Misercordia linaamanisha kuwa na moyo ambao huko tayari kuteseka kwa ajili ya wengine, kuwa na moyo ambao unateseka kwa ajili ya wenye shida. Moyo wa Yesu ni moyo wa namna hii. Huruma ni kiini cha kusamehe. Kuna matendo saba ya kiroho ya huruma.

1. KUFUNDISHA WASIOJUA
Yesu Alimfundisha Mtume Thoma
Hasiyejua ana shida. Ukimfundisha unatatua shida. Mtume Thoma aitwaye Didymus “Pacha,” alikuwa hajui kweli juu ya ufufuko wa Yesu na haamini. Yesu alipowatokea wanafunzi wake alimwambia Thoma, “Lete kidole chako hapa uitazame mikono yangu; lete mkono wako ukautie ubavuni mwangu. Usiwe na mashaka, ila amini.” (Yohane 20: 27) Yesu alimfundisha Thoma aitwaye Didymus kwa kutumia USHAHIDI. Thomas alielewa, akasema, “Bwana wangu na Mungu wangu.” (Yohane20: 28) Aliamini katika ubinadamu wa Yesu Kristu na Umungu wa Yesu Kristu. Katika Kanisa Katoliki ni Msimamizi wa Wanasayansi wanaofanya utafiti. Katika Litania ya Moyo Mtakatifu wa Yesu tunasali, “Moyo wa Yesu, zinamokaa hazina za hekima na elimu,” “Utuhurumie.” Alimpa elimu juu ya ufufuko wake Thomas. Hilo ni tendo la huruma. “Kutokujua kutokujua kwako ni ugonjwa wa kutokujua,” alisema A.A. Alcott. Hao wanahitaji kufundishwa.
Umuhimu wa Kufundisha
Tunapata changamoto la kuwafundisha wasiojua. Kuna methali ya Kichina isemayo, “Nipe samaki nitakula siku moja. Nifundishe kuvua nitakula maisha yangu yote.” Kufundisha mtu namna ya kupata chakula ni zaidi ya kumpa chakula ambacho atakula siku moja. Ni tendo la kubwa la huruma. Atakula chakula siku zote za maisha yake. Kwa walimu kuwa na huruma kwa mwanafunzi wako “A,” na “B,” siku moja mmoja wao atarudi chuoni hapo kuwa profesa. Kuwa na huruma kwa mwanafunzi wako, “C,” siku moja atarudi hapo na kuwajengea mahabara ya mamilioni.

Mtu ambaye hajui jambo fulani ni mbumbumbu. Kuna ambao wanajua kuwa hawajui hao ni wanyenyekevu hao ni wazuri kwa kufundishwa. Kuna wajuaji hao ni wenye majivuno. wanajifanya kuwa wanajua kila kitu. Hao wanahitaji kufundishwa kwanza umuhimu wa unyenyekevu. Kuna ambao wanajua kuwa hawajui lakini wana woga. Watie moyo wawe na moyo mkuu wasiogope. Mfano Mwalimu Denis Mapunda alimuuliza mwanafunzi aitwaye Aristides Swala, “Nani aliandika Biblia?” Mwanafunzi mwenye hofu alijibu, “Sio mimi mwalimu!” Kuna msemo wa Amerika husemao, “Kitu chenye bei kubwa sana hapa duniani ni ujinga.” Ukisaidia kumfundisha mjinga unatoa msaada mkubwa sana.

Tufundishe Neno la Mungu
Ni vizuri tuwafundishe wenzetu ambao hawajui neno la Mungu yaani Biblia. “Maandiko yote matakatifu yameandikwa kwa uongozi wa Mungu, na yanafaa katika kufunidishia ukweli, kuonya, kusahihisha makosa, na kuwaongoza watu waishi maisha adili, ili mtu anayemtumikia Mungu awe mkamilifu, na tayari kabisa kufanya kila kazi njema.” (2 Timotheo 3: 16-17) Mwanamke kijana alipojifungua mtoto wake wa kwanza alitaka kutangaza habari njema juu ya kujifungua kwake mtoto kwa rafiki yake. Alituma ujumbe wa simu ya mkono. “Isaya 9:6” Rafiki yake hakuwa na mazoea ya kusoma biblia. Hivyo baada ya kupata ujumbe huo alimwambia mmbe wake Tereza amejifungua mvulana ana uzito wa ratili 9 na aunsi 6. Lakini kwani wamemuita Isaya?” Hakujua kuwa maneno ya Isaya 9:6 “ Maana mtoto amezaliwa kwa ajili yetu, tumepewa mtoto wa kiume.” Mtu wa namna hii anahitaji kufundishwa neno la Mungu.

Tufundishe Kumjua Mungu
Hasiyekujua hakuthamini. “Watu wangu wameangamia kwa kutonijua, maana wewe kuhani umekataa mafundisho.” (Hosea 4: 6) Hatuna budi kuwafundisha watu kumjua Mungu. Katika Katekismu ya Kanisa Katoliki tumefundishwa kuwa, “Mungu alituumba ili tumjue, tumpende ili baadaye tuishi naye milele yote.”

2. KUSHAURI WENYE MASHAKA
Kutoa ushauri ni tendo la huruma. Yesu anaitwa “Mshauri wa Ajabu” (Isaya 9:6). Bikira Maria Mama wa huruma anaitwa, “Mama wa Shauri Jema,” katika Litania ya Bikira Maria. Hatuna budi kuwaiga katika kutoa ushauri kwa wengine. Yesu alipowatokea wanafunzi wake alimwambia Thoma, “Lete kidole chako hapa uitazame mikono yangu; lete mkono wako ukautie ubavuni mwangu. Usiwe na mashaka, ila amini.” (Yohane 20: 27) Yesu alimshauri Mtume Thoma Mwenye Mashaka. Kutokana na masha ya mtume Thoma tuna nahau ya Kiingereza, “doubting Thomas,” mtu ambaye hukataa kuamini mpaka amepata ushahidi wa mambo. Ni mtu mwenye kushuku au mwenye mashaka.
Tobiti alimuasa Tobia kuomba ushauri: “Omba ushauri kwa watu wenye busara, wala usidharau kwa watu wenye busara, wala usidharau shauri lenye kufaa.” (Tobiti 4:18) Mtu mwenye mashaka au anayefanya jambo baya kuna upande wa mambo ambao hajaona mshauri. Mtu mmoja aitwaye Tendewa alimpa ushauri mlevi mmoja juu ya namna ya kuacha kunywa pombe. “Je unaweza kuniambia namna ya kufanya ili niache kunywa pombe?” Mlevi aliuliza. Tendewa alisema, “Ni rahisi kama kufungua mikono yako au viganja vyako.” Mlevi alidai kupata maelezo zaidi na kuahidi kutokunywa tena. Tendewa alimfafanulia, “Nitakuonyesha namna ya kufanya. Ukiwa na glasi yenye pombe kali fungua mikono yako au viganja vyako kabla ya kunywa. Na hautalewa tena.”

3. KUONYA WADHAMBI
Kuna methali ya kiafrika isemayo, “Nilisema,” anamzidi, “Nilinyamaza.” Anayeona uovu ukitendeka akaonya kwa kusema anamzidi yule anayeona uovu akakaa kimya. Mungu wetu ni Mungu mwenye huruma. Hakai kimya anaonya. “…niliwaonya vikali wazee wao nilipowatoa katika nchi ya Misri, na nimeendelea kuwaonya wanitii mpaka siku hii ya leo. Lakini wao hawakunitii, wala hawakunisikiliza.” (Yeremia 11:7-8)
Tuwe Tayari Kupokea Maonyo
“Ukiona bibi kizee anakimbia usiulize kuna nini na wewe kimbia.” Methali ya Jamaica. Kuna mambo mengi katika maisha yanayotuonya. Lazima tupokee maonyo. Bwana anatuasa,
Basi, ewe mtu, nimekuweka kuwa mlinzi wa Waisraeli. Utakaposikia neno kutoka kwangu utawapa onyo langu. Nikikwambia mtu mwovu: ‘Wewe mtu mwovu hakika utakufa; lakini wewe husemi chochote ili kumwonya yule mtu mwovu aachane na mwenendo wake; mtu huyo hakika atakufa kwa kosa lake; walakini nitakudai wewe kifo chake. Lakini ukimwonya mwovu aachane na mwenendo wake, naye haachani na mwenendo wake mbaya, yeye atakufa kwa kosa lake; lakini wewe utakuwa umeyaokoa maisha yako. (Ezekiel 33: 7-9)
4. KUVUMILIA MABAYA
Mvumilivu hula mbivu. “Tunamwamini Yesu ni wazi kwa sababu hakushuka toka msalabani” (General Booth). Alivumilia. Mtume Paulo anatuasa, “Mwe na msimamo uleule aliokuwanao Kristo Yesu” (Fil 2:5) Chenye mwanzo kina mwisho. Mateso, taabu vyote vina mwisho. Subira na saburi ni fadhila muhimu sana. Wafipa wana methali isemayo, “Mzigo uchukuao kichwani hukulemea siku moja tu.” Mvumilivu hula mbivu lakini akivumilia sana hula mbovu. Zinaiva na kuwa mbovu. Yesu alivumilia akiwa na mpango “B,” yaani wa kumtuma Roho Mtakatifu. Hatuna budi matatizo mengine kuyatafutia uvumbuzi yaliyo katika uwezo wetu na yale ambayo hayamo katika uwezo wetu tumwachie Mungu.

5. KUSAMEHE MAKOSA BILA KUSITA
Kusamehe makosa ni tendo la huruma. Yesu alisisitiza sana hitaji la kuwasamehe wengine. “Kisha Petro akamwendea Yesu, akamwuliza, ‘Je, ndugu yangu akinikosea, nimsamehe mara ngapi? Mara saba?’ Yesu akamjibu, ‘Sisemi mara saba tu, bali sabini mara saba.’” (Mathayo 18:21” Kusamehe mara sabini na saba kunamaanisha kusamehe kila mtu kila mara. “Ni wazi kuwa sharti hili la kiukarimu la msamaha haliondoi masharti ambayo hayana upendeleo ya haki. Ikieleweka vizuri haki ina malengo ya msamaha. Hakuna mahali popote katika ujumbe wa Injili ambapo msamaha au huruma kama kiini chake humaanisha kujiigiiza katika kutenda maovu, kujiigiza katika kashfa, kutia wengine hasara au kutukana wengine. Katika hali yoyote ile kufanya malipizi kwa ajili ya maovu na kashfa, kufidia hasara na kufanya malipizi ya matukano ni masharti ya msamaha,” Alisema Papa Yohane Paulo wa Pili katika barua yake ya mwaka 1980 yenye kichwa cha habari, “Dives in Misericordia,” yaani “Tajiri katika Huruma.” (Namba 14)

6. KUFARIJI WANAOTESEKA
Mungu wetu ni mfariji. “Mungu hatufariji ili tufarijike tu bali tufanywe wafariji,” alisema hayo John Henry Jewett.
Kuwa na Ufundi wa Kufariji
Tunahitaji kuwa na ufundi wa maneno ya kufariji. Yesu aliwafariji mitume alipotokea kwao, aliwaambia, “Amani kwenu! Alipokwisha sema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi, hao wanafunzi wakafurahi mno kumwona Bwana.” (Yohane 20: 19-20) Yesu aliwaonyesha mikono. Kama mke wako anateseka kisaikolojia muoyeshe unavyompenda. Kama mme wako anateseka Kisaikolojia muonyeshe unavyompenda.
Fariji kwa Kulia na Wanaolia
Tufariji wanaoteseka. Mtume Paulo alituasa, “Furahi pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wenye kulia.” (Waroma 12: 15). Yesu alilia Lazaro alipokufa. Alilia na wanaolia.
Fariji kwa Kutumia Tiba ya Kuongea
Kuongea ni tiba. Kama una sononokeko na simanzi kuongea ni tiba. Kama una mfadhaiko kuongea ni tiba. Muulize mtu maswali ambayo hayambani mtu kutoa jibu la ndoa au hapana bali kuelezea. Kuna mitume wawili waliokuwa wanaenda Emmaus walikuwa wamekata tamaa. Yesu aliwauliza maswali mawili yanayohitaji majibu marefu ili waongee. Swali la Kwanza: “Mnazungumza nini huku mnatembea?” (Lk 24: 17). Swali la Pili: “Mambo gani?” (Lk 24: 19) Mitume hawa walikuwa wenye huzuni. Yesu aliwatia moyo waongee. Kuongea ni tiba na kutia mtu moyo aongee kunahitaji ufundi katika kuuliza maswali.

7. KUWAOMBEA WAZIMA NA WAFU
Kuwaombea Wazima
Kuwaombea wazima ni tendo la huruma. Yesu aliwaombea wanafaunzi wake:
“Baba Mtakatifu! Kwa nguvu ya jina lako ulionipa, tafadhali uwaweke salama ili wawe kitu kimoja kama sisi tulivyo mmoja.” (Yohane 17: 11)
Wazazi hawana budi kuwaombea watoto hao. Mtakatifu Monica alimuombea mtoto wake Augustini akabadilika na kuwa mtakatifu. Watoto hawana budi kuwaombea wazazi wao. Hatuna budi kuwaombea viongozi wetu. Unaweza kutumia Kanuni ya Vidole.
Kidole gumba kinasimama badala ya jamaa zako. Waombee. Kidole cha shahada kinasimama badala ya walimu na walezi. Waombee wazazi ambao ni walimu wa kwanza na waombee walimu wote. Kidole cha kati kinasimama badala ya viongozi wote wa kidini na wa serikali. Kidole cha pete kinasimama badala ya wale waliodhaifu kama wagonjwa waombee. Kidole cha kadogo kinasimama badala ya wewe. Jiombee.
Kuwaombea Wafu
Hadithi inapokuwa tamu katika gazeti hukatizwa na chini yake maneno “Itaendelea Toleo Lijalo” huandikwa. “Toleo lijalo” kwa marehemu waliolala ni mbinguni au toharani (Purgatorio) au motoni. Kama wako toharani hatuna budi kuwaombea. Tuna msingi ya kuwaombea wafu katika biblia: 2 Makabayo 12: 39-45; Mathayo 5: 25-26; Mathayo 12:32. Mtakatifu Monika kabla ya kifo chake alimwambia Mt. Augustino na kaka yake: “Muuzike mwili huu popote pale! Msijisumbue na chchote kwa ajili yake! Ninachowaombea ni kunikumbuka katika altare ya Bwana popote pale mtakapokuwa.” Tuwakumbuke marehemu katika altare ya Bwana.

Counter

You are visitor since April'08