Saturday, August 29, 2015

MOYONI UMEJAZA NINI?



                               

                                        Jumapili ya 22 ya Mwaka B

1. Kumb 4: 1-2, 6-8
2.  Yakobo 1: 17-18, 22, 27
3.  Mk 7: 1-8, 14-15, 21-23


“…Kwa maana kutoka ndani ya watu, kutoka mioyo yao, yanatoka mawazo mabaya; uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, choyo, ukorofi, hila, ufisadi, wivu, matusi, kiburi, upumbavu.Maovu hayo yote yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi” (Marko 7: 15-23)

Mungu anapompima mtu, anaweka utepe kuzunguka moyo wake na si kichwa chake. Mwalimu wa shule ya wanafunzi wadogo wa elimu dini waliokuwa wakikutana Jumapili alikuwa akiwaambia watoto wadogo juu ya taji la utukufu na zawadi huko mbinguni kwa watu wema. Mwishoni mwa somo aliwauliza wanafunzi wa shule ya awali, “Nani atapata taji kubwa?” Palikuwepo na kimya, mtoto mmoja akainua mkono, “Mwenye kichwa kikubwa.” Tofauti na jibu hili Mungu haangalii ukubwa wa kichwa bali ukubwa wa moyo: moyo wenye upendo, ukarimu, mawazo safi, unyenyekevu.  “Kila mtu anaweza kupenda ua la waridi; lakini inahitaji moyo mkubwa kupenda jani,” alisema Askofu Fulton Sheen. Kila mtu anaweza kupenda chumvi lakini inahitaji moyo mkubwa kumpenda muuza chumvi. Kila mtu anaweza kupenda kinywaji kilichomo kwenye glasi, lakini inahitaji moyo mkubwa kuipenda glasi. Kila mtu anaweza kuchukia dhambi lakini inahitaji moyo mkubwa kumpenda mdhambi.

Kama hakuna adui ndani, adui wa nje hawawezi kukudhuru. Ni methali ya Kiafrika. Mawazo mabaya ni adui wa ndani. Wakiwemo moyoni adui wa nje anaweza kukudhuru. Yesu alitaja maadui kumi na wawili ambao wanaweza kuwa moyoni: “…Kwa maana kutoka ndani ya watu, kutoka mioyo yao, yanatoka mawazo mabaya; uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, choyo, ukorofi, hila, ufisadi, wivu, matusi, kiburi, upumbavu.Maovu hayo yote yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi” (Marko 7: 15-23)

Mungu anatazama moyo na kuangalia moyoni. Tunapoimba Mungu hatazami midomo tu anatazama moyo. Tunapoimba Mungu hatazami kinanda tu anatazama moyo. Unapotoa sadaka Mungu hatazami pesa tu uliyotoa anatazama moyo. Kutoa ni moyo vidole huachia. Tunapomwabudu Mungu, Mungu anatazama moyo. Mtu anaposema nakupenda kwa moyo wote, hoja si kupenda kwa moyo wote hoja ni aina gani ya moyo. Watu wanapenda moyo unaojali. Watu hawajali unajua kiasi gani mpaka wanapojua unajali kiasi gani. Mioyo yetu ni kama sanduku tunatofautiana namna ya kujaza sanduku. Swali: moyoni umejaza nini? Wengine wanaweka mengi kwenye sanduku kama wanavyoweka mengi moyoni. Wengine wanaweka machache. Mwenyezi Mungu anaangalia moyoni:”…siangalii mambo kama wanavyoangalia binadamu wenye kufa. Binadamu huangalia uzuri wa nje, lakini mimi naangalia moyoni” ( 1 Samueli 16: 7). Tunapozungumza maneno ni maelezo ya wazo. Kila mara unapoongea unachokifikiria na kinachokuwa moyoni kinakuwa kwenye gwaride watu wanaona.





Maneno yako ni madirisha ya moyo wako. Lililo moyoni ulimi huiba. “Kinywa hutaja yanayofurika moyoni” (Mathayo 12: 34). Ukisema, “asante” shukrani imefurika moyoni. Ukisema, “nakupenda” upendo umefurika moyoni. “Mtu mwema hutoa mema katika hazina njema ya moyo wake, na mtu mwovu hutoa maovu katika hazina mbovu ya moyo wake; kwa maana kutoka kinywa chake hunena yafurikayo moyoni” (Luka 6: 45).

Barua kutoka moyoni inawezwa kusomwa usoni. Ni methali ya Kiswahili. Uso wa mtu unaonesha kilichomo moyoni. Katika lugha ya kawaida tunatambua umuhimu wa moyo. Kuna mifano michache: Ana moyo mwepesi: ana huruma nyingi na mwepesi wa kumsamehe mtu aliyemkosea. Fulani ana moyo wa simba: ni shujaa; mjasiri mkubwa; haogopi kufanya jambo. Kipendacho moyo ni dawa (methali). Ana moyo mweupe: hana hila au nia mbaya. Suala la kupatana ni suala la moyo: “Moyo wa binadamu umeumba kupatanisha yanayokinzana,” alisema David Hume. Naye Harbert Hoover alikuwa na mawazo hayo aliposema: “Amani haifikiwi kwenye meza ya baraza au kwa mikataba, bali kwenye mioyo ya watu.”  Ni moyo unaopenda. “Moyo wa kupenda hausemeki.” Ni methali ya Kiswahili. Jicho halisau moyo ulichoona. Ni methali ya Kiafrika. Yote yakishasemwa wito ni moyoni jazeni mawazo mazuri.

MAWAZO YA UKARIMU, SADAKA NA HISANI: Moyo wa binadamu haupimwi kwa ukubwa wa pochi bali kwa ukubwa wa moyo wenyewe. Tunazungumzia moyo usiofungwa, ulio wazi. “Gereza baya sana litakuwa moyo uliofungwa,” alisema Mt. Yohane Paulo II.  Moyo uliojaa uchoyo ni moyo uliofungwa. Kilijochaa hufurika. Moyo ukijaa ukarimu, ukarimu utafurika. Moyo ukijaa mawazo ya sadaka, sadaka itafurika. Moyo ukijaa mawazo ya hisani, hisani itafurika. “Kuna tofauti kubwa sana kati ya zawadi na sadaka. Sadaka ni zawadi kujumlisha na upendo na kujumlisha na hulka ya mtoaji. Zawadi hutoka kwenye pochi; sadaka hutoka moyoni,” alisema Askofu Fulton Sheen. Kuna mtoto wa mitaani aliyekutana na Padre akamuuliza, “Padre gari lako ulinunua kwa shilingi ngapi?” Padre alijibu, “Sijui.” Mtoto akasema, “Unaendesha gari haujui bei yake.” Padre alimwelewesha mtoto, “Gari hili nilipewa na kaka yangu.” Mtoto alisema, “Ningekuwa na moyo kama kaka yako ningekununulia gari.” Hakusema, “Ningekuwa na ndugu kama huyo akaninunulia gari.” Mambo yote yanategemea moyo.Mtoto huyu wa mitaani alikuwa na moyo wa ukarimu. Kuna mtu aliyeenda kwa tajiri kuomba elfu tatu. Tajiri akampa elfu hamsini. Yule aliyeomba elfu tatu akashangaa na kusema, “Bwana Mkubwa, Chifu, Bosi! Mimi nimeomba elfu tatu wewe mbona umenipa hamsini.” Bwana huyo akasema, “Elfu tatu zinakutosha wewe kuomba lakini hazinitoshi mimi kutoa.”


MAWAZO SAFI, NIA SAFI, NDOTO SAFI
Hakimu wakati anahukumu kesi juu ya wizi. Alimuuliza mwizi: Je huwa hauoni aibu kuweka mkono kwenye mfuko wa mtu ili umwibie. Mwizi huyo alijibu: “Huwa nakuwa na aibu nisipokuta kitu chchote.” Moyoni mwa mwizi huyo yalijaa mawazo mabaya, mawazo ya wizi. Hayo si mawazo safi. Familia moja ilikuwa na mazoea ya kuwakaribisha wageni wakati wa Kumbukumbu za Kuzaliwa za Wanafamilia. Baba alimuomba mtoto wake wa miaka mitatu kuongoza sala kabla ya kula. Mtoto alisita. Baba alisema sema ambavyo mama huwa anasema siku kama hii: Mtoto alifanya ishara ya msalaba na kusema, “Mama huwa anasema, “Kwa nini tumewaalika watu wengi chakula hakitoshi.” Unaweza kujua mawazo ya mama huyo. Wazo lolote ambalo linaleta mwanga lifikirie. Wazo lolote ambalo ni wazo taka achana nalo. Wazo lolote ambalo ni wazo mgando achana nalo. Wazo lolote ambalo ni wazo giza achana nalo. “Ndugu, yaliyo kweli, matukufu, adili, yaliyo matakatifu, ya kupendeza nay a sifa njema, yote yanayohusiana na ukamilifu, tena masifu, hayo yafikirieni hasa” (Wafilipi 4:8). Mawazo ya upendo ni mawazo safi. “Palipo na upendo, hakuna giza (Methali ya Burundi). Mawazo ya kusaidia wengine ni mawazo safi. “Lengo letu la kwanza katika maisha haya ni kuwasaidia wengine. Kama huwezi kuwasaidia wengine usiwahumize,” alisema Dalailama.

Heri walio na moyo safi, maana hao watamowona Mungu” (Mathayo 5: 8).“Tunateka nyara kila fikra ipate kushuka na kumtii Kristo” (2 Wakorintho 10:5). “Ni nani atakayependa katika mlima wa Bwana?” Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake? Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe, asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili, wala hakuapa kwa hila” (Zaburi 24 (23): 3-4).


MAWAZO YA UNYOFU, UAMINIFU NA UADILIFU
Kuna watu ambao hawawezi kusoma Biblia lakini wanaweza kusoma moyo wako. Kinachompendeza Mungu ni unyofu wa moyo. “Nawe wapendezwa na unyofu wa moyo; ndani ya moyo unanifundisha hekima” (Zaburi 51: 8). Mungu haangalii kwamba mtu amekujaribu na sketi fupi bali anaangali unyofu wako wa moyo. Mungu haangalii kwamba mtu aliacha pesa mezani zikakushawishi Mungu anaangalia unyofu wa moyo.

MAWAZO YA UCHESHI, UCHANGAMFU, FURAHA
“Moyo wenye furaha ni huduma nzuri sana tunayoweza kumpa Mungu,” alisema Marie Chaplain. “Moyo wenye furaha ni matokeo yasiyoepukika ya moyo unaowaka upendo,” alisema Mwenyeheri Mama Teresa wa Calcutta. Moyo unapodunda kwa ajili yaw engine unakuwa na furaha sana.

MASIFU, PONGEZI, SHUKRANI, MAPENDO
“Ujaze moyo wako wingi wa mapendo na shukrani, unapowaza jinsi kila siku neema ya Mungu inavyokuokoa katika mitego unayotegewa njiani na adui,” alisema Mt. Josemaria Escriva. Kipimo cha mtu sio ukubwa wa imani yake bali ukubwa wa upendo wake. Msichana mmoja alikuwa amempenda kijana mmoja mtanashati na mchaMungu. Malengo yao ilikuwa waje kuoana baada ya muda. Kijana alijitoa sana kwa binti huyu hadi wenzake wakamuona mjinga, lakini ukweli ni kuwa alimpenda msichana Yule kwa dhati. Alimtafutia kazi alipomaliza chuo, alimshauri kuhusu mipango ya maisha na alikua akimuombea kila alipopata nafasi ya kuomba. Siku moja binti alikua anasherehekea siku yake ya kuzaliwa…hivyo akaalika marafiki zake, na watu wengine muhimu akiwemo mpenzi wake. Wageni wote walifika kwa wakati isipokuwa yule kijana alichelewa kidogo…Hivyo msichana akatumia muda ule ambao mpenzi wake hajafika kuwaeleza wageni namna yule kijana alivyokuwa wa muhimu kwake. Akamsifia sana, akasema atamvalisha pete ya uchumba karibuni, na akasema siku hiyo ya Siku ya Kuzaliwa kwake anategemea zawadi kubwa sana kutoka kwa huyo mpenzi wa nafsi yake. Baadaye kijana akaingia na kuketi kwenye meza ya wageni wahemishimiwa. Muda wa zawadi ulipofika watu wakamtunza binti zawadi mbalimbali na kijana akawa wa mwisho. Hivyo wageni wote wakawa na hamu ya kutaka kujua zawadi aliyoleta hasa baada ya Yule msichana kumsifia sana kijana akaamka na kutoa mfuko…kila mtu akataka kujua kilichokua ndani ya mfuko…mara kijana akafungua mfuko na kutoa mkate! Lahula! Watu wote wakastaajabu na kusema, “Mkate?” Lakini kabla hajasema lolote kuhusu ule mkate, Yule msichana akaanza kulia..akapandwa hasira kwa kuwa mpenzi wake amemuaibisha! Akiwa analia kwa kwikwi, akamshika shati na kumvua tai yake, akamwagia juisi, kasha akauchukua ule mkate na kuutupa! Maskini Yule kijana akaukimbilia ule mkate na kuuokota. Kisha akarudi mezani na kusema, “Mtoto nakushukuru kwa yote..Huenda umenidharau kwa kuwa nimekuletea zawadi  hii ndogo kwenye siku yako muhimu kama hii. Lakini kama ungetambua thamani ya zawadi hii, usingefanya haya.” Kisha akafungua ule mkate na kutoa vitu viwili alivyovificha ndani ya mkate…Kwanza akatoa ufunguo wa gari, ambalo alikuwa amemnunulia mpenzi wake na alitaka amkabidhi siku hiyo ya Kumbukumbu ya Kuzaliwa. Kisha akatoa pete ya uchumba na kusema “Nilimuomba Mungu anipe mwanamke atakayenipenda katika hali yoyote. Nilipanga leo nikuvalishe pete hii ili kuelekea ndoto yetu ya ndoa. Lakini kwa kuwa uliangalia nje, uliona mkate, badala ya pete hii ya thamani iliyokuwa ndani.Naamini mwanamke niliyemuomba kwa Mungu bado sijampata. Nashukuru kwa yote uliyonifanyia nimekusamehe, nawe naomba unisamehe kama nimekukwaza.” Kisha akachukua mkate wake, huyoo akaondoka. Msichana akaomba msamaha lakini alikuwa amechelewa. Fundisho usidharau kila mtu kwa kumtazama kwa nje. Mungu huangalia thamani ya kitu au mtu kwa ndani lakini wanadamu walio wengi huangalia nje. Wanaokudharau leo na kukuona mkate watagundua haukuwa mkate wa kawaida, kuna vingi vya thamani ndani mwako. Wote wanaokudharau leo, ipo siku watakusalimia kwa heshima.

Ujaze moyo wako masifu. Msichana huyo hakujaza moyo wake na masifu. “Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki, kusifu kunawapasa wanyofu wa  moyo, Mshukuruni Bwana kwa kinubi, kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa. Mwimbieni wimbo mpya, pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe” (Zaburi 33(32) 1: 1-3).


TUMUOMBE MUNGU ATUUMBIE MIOYO SAFI

Kuna mtu alikuwa anaulizia bei ya taulo. Mnunuzi: “ Taulo hiyo pale shilingi ngapi? Muuzaji: Laki mbili. Mnunuzi: Inasafisha hata dhambi! Muuzaji: kimya. Mnunuzi alishangaa bei ilikuwa juu. Taulo inaondoa maji haiondoi dhambi, inasafisha uchafu haisafishi makosa. Biblia inazungumzia hisopo inayosafisha. “Unisafishe kwa hisopo, nami nitakuwa safi; unioshe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji” (Zaburi 51: 9). Hisopo ni mmea mdogo wenye vitawi vingi unaofaa kwa kunyunyuzia katika madhehebu ya kutakasa (Hesabu 19:18; Law 14;4; Rev 1: 9). Wahaya walikuwa na mimea ya kutumia kutakasa katika ibada za kitamaduni: orweza na orugoshora. Ni kama mmea wa hisopo. Sala yetu iwe kama ya mfalme Daudi alipotembelewa na nabii Nathani baada ya kutenda dhambi na Bathsheba: “Uniumbie moyo safi, ee Mungu; ufanye upya roho thabiti ndani yangu” (Zaburi 51: 12).



Counter

You are visitor since April'08