Friday, April 22, 2016

UPENDO HAUFICHIKI, UPENDO UNAONEKANA



                                 
                                                     Jumapili ya 5 ya Paska
1.       Mdo 14: 21-27
2.       Ufu 21: 1-5a
3.       Yn 13: 31-33a.34-35
“Waliwaimarisha wafuasi roho na kuwatia moyo “ (Mdo 14: 22)
Hivyo watu wote watawatambua kuwa wafuasi wangu, mkipendana” (Yohane 13:34-35).
MUHTASARI
·         Upendo unaonekana katika ukaribu wa mioyo
·         Upendo unaonekana katika matendo na vipaumbele
·         Upendo unaonekana katika maneno ya kutia moyo
·         Upendo unaonekana katika kumbukumbu
·         Upendo unaonekana katika mahusiano
·         Upendo unaonekana katika zawadi au kutoa
·         Upendo unaonekana katika kusikiliza

Upendo unaonekana katika ukaribu wa mioyo. Palipo na upendo mioyo imekaribiana. Mioyo imeshibana. Wanaopendana ni wataalamu wa moyo. “Mtu yeyote anaweza kuwa mtaalamu wa moyo. Sharti pekee ni kumpenda mtu fulani,” alisema Angie Papadakis. Moyo wa Mtume Paulo na moyo wa Barnaba ilikuwa imekaribiana. Walipendana. Walishibana. Walikuwa wataalamu wa moyo. Jambo hilo linaonekana. Kuna methali ya Tanzania isemayo, nyumba hupakana lakini mioyo haipakani. Upendo unaonekana jinsi tunavyozungumza. Kwamba mioyo inapakana ni jambo linaloonekana kwa namna tunavyozungumza. Profesa alikuwa anatoa mafundisho juu ya haya hii: “Jibu pole hutuliza ghadhabu, bali neno kuhumiza huchochea hasira” (Mithali 15: 1). Profesa aliwauliza wanafunzi kwa nini tukiwa na hasira huwa tunapiga kelele au tunapaza sauti? Kwa nini watu wanapigiana kelele wanapokuwa na mfadhaiko? Mwanafunzi mmoja alijibu, ni kwa sababu tunapoteza utulivu wetu. “Lakini kwa nini upige kelele wakati mtu unayemwambia yupo karibu nawe?” aliuliza profesa. Wanafunzi walitoa majibu mbali mbali lakini hakuna jibu lililomridhisha profesa. Hatimaye alieleza hivi, “Watu wanapokasirikiana kuna umbali mrefu kati ya mioyo yao kisaikolojia. Ili kupunguza umbali wanapigiana kelele ili waweze kusikia. Jambo gani linatokea kama watu wanapendana? Hawapigiani kelele wanaongea kwa upole wananong’ezana, wanakaribiana palipo na upendo. Hatimaye hawahitaji hata kunong’onezana wanatazama. Ikitokea siku ukampigia kelele unayempenda   jua kuwa unaweka umbali kati yako na wewe. Jibu pole hutuliza hasira.
  
Kuna mambo mawili tu mtu hawezi kuficha: kwamba amelewa na kwamba anapenda,” alisema Antiphanes. Lakini yapo mambo mengi ambayo hayafichiki, chuki haifichiki ikifichika ni kama kuficha moto kwenye karatasi. Kuna methali isemayo mapenzi ni kikohozi hayafichiki. Upendo unaonekana bila kujali kama mtu ana ulemavu au la. “Upendo ni lugha ambao kiziwi anaweza kusikia; Upendo ni wimbo ambao mlemavu anaweza kucheza; upendo ni mapambazuko ambayo kipofu anaweza kuona,” alisema Ramesh Umadkat. Palipo na upendo mwenye ulemavu atachangamka hata akiwa na mguu mmoja anaweza kudansi. “Upendo unaonekaje? Una mikono ya kuwasaidia wengine. Una miguu ya kuharakisha kuwaendea wahitaji. Una macho ya kuona shida na hitaji. Una masikio ya kusikia kushusha pumzi kwa majonzi na mateso ya watu. Hivyo ndivyo upendo unavyofanana,”alisema Mtakatifu Augustino wa Hippo Afrika ya Kaskazini.
Biblia inathibitisha kuwa upendo haufichiki, unaonekana. “Amri mpya nawapeni: mpendane. Kama mimi nilivyowapenda, nanyi pia mpendane. Hivyo watu wote watawatambua kuwa wafuasi wangu, mkipendana” (Yohane 13:34-35). Watakatifu wengi walikuwa na haya ya kusema juu ya haya hizo. “Yeyote kati yenu asiwe na hali ya kawaida tu kwa jirani yake isipokuwa muendelee kupendana ninyi kwa ninyi katika Yesu Kristo” (Mtakatifu Inyasi wa Antiokioa). Upendo unampambanua mkristo. “Mmoja lazima amwone Mungu katika kila mmoja” (Mtakatifu Katharina Laboure). “Ninakwambia mambo haya, kuwaburudisha ninyi, huku nikisali kwamba kwa kuwa wote tumeumbwa kwa dutu ile ile, ambayo ina mwanzo lakini haina mwisho, tuweze kupendana sisi kwa sisi kwa upendo mmoja. Kwa wale wote wanaojitambua wenyewe wanajua kuwa ni watu wadutu moja isiyokufa” (Mtakatifu Antoni wa Misri).

Upendo unaonekana katika matendo na vipaumbele. Vijijini au mijini wanaposema fulani anampenda fulani ni kwa sababu mapenzi yanaonekana. Asubuhi anamtembelea. Mchana anamtendembela. Jioni anamtembelea. Usiku anamtembelea. Watu wanaanza kusema maneno. Hivyo hivyo anayempenda Mungu ataonekana kila mara anaenda Kanisani kila siku. Atasali sala za asubuhi. Yaani atakutana na Mungu kabla ya kukutana na shetani. Atakutana na Mungu kabla ya kukutana na mazingira ya maisha. Atazungumza na Mungu kabla ya kuzungumza na watu wengi. Anaungana na Mungu kabla ya kuungana na watu wengine. Atasikiliza sauti ya Mungu kabla ya kusikiliza sauti za watu wengine. Atasikiliza habari kutoka mbinguni kabla ya kusikiliza habari kutoka BBC. Ataliita jina la Yesu kabla ya kuita majina mengine madogo. Kwa macho ya imani atamuona Yesu kabla ya kujiona kwenye kioo. Atafagia moyo wake kabla ya kufagia uwanja wake unaozunguka nyumba. Upendo kwa Mungu unaonekana. Yesu kwa vile alimpenda Mungu baba alisali asubuhi na mapema. “Asubuhi na mapema, kabla ya kupambazuka, aliamka, akaondoka, na kwenda mahali pa nyika alikosali” (Marko 1: 35).

Upendo unaonekana katika maneno ya kutia moyo. Lililo moyoni ulimi huiba. Moyoni pakiwepo upendo ulimi utaiba utaonekana katika maneno. Upendo wa Barnaba na mtume Paulo ulionekana katika matendo na maneno. Tunaambiwa. “Waliwaimarisha wafuasi roho na kuwatia moyo “ (Mdo 14: 22).  Jina Barnaba linamaanisha mwana wa kutia moyo. Unapotia moyo ni upendo unaonekana. Tuna mifano ya watu mbali mbali ambao wamesema maneno ya kutia moyo. “Hapajakuwepo kamwe usiku au tatizo ambalo limeweza kushinda mapambazuko au matumaini,” alisema Bern Williams. Hata pakiwepo usiku wa matatizo ya namna gani kutakucha. Matatizo hayapigi bao matumaini. Kuna aliyesema, “Mungu huwapeleka watu katika maji marefu si kwa ajili ya kuwazamisha majini bali kuwatakasa,” alisema John Aughey. Matatizo yanatakasa mawazo hasi, mawazo taka na mtazamo taka yanapotafakiriwa katika mtazamo chanya. Mtu fulani alisema, “Watu wasio sahihi wanapokuacha mambo sahihi yanaanza kutokea.” Maneno hayo yanatia matumaini kwa yule aliyeachwa na watu ambao wasio sahihi.

Upendo unaonekana katika kumbukumbu. Mchungaji Rick Warren katika kitabu chake, Maisha Yanayoongozwa na Malengo alikuwa na haya ya kusema, “Upendo huacha kumbukumbu. Jinsi unavyowatendea watu wengine, siyo utajiri au mafanikio yako ndicho kitu kinachodumu unachoweza kuacha duniani.” Kama Mama Theresa alivvyosema, “Sivyo unavyotenda, lakini kiasi gani cha upendo unaweka katika tendo hilo ndilo jambo la muhimu sana.”

Upendo unaonekana katika mahusiano. Mahusiano mazuri kati ya mtume Paulo na Barnaba ni ushahidi wa upendo. Mchungaji Rick Warren katika kitabu chake, Maisha Yanayoongozwa na Malengo alikuwa na haya ya kusema, “Nimekuwa kando ya kitanda cha watu wengi wanaokuwa katika kufa, wanaposimama pembezoni mwa umilele, na sijasikia yeyote akisema, ‘Nileteeni vyeti vyangu! Nataka kuviona mara moja tena. Nionyeshe zawadi zangu, medali zangu, ile saa ya dhahabu niliyopewa.’ Maisha yanapokoma duniani, watu hawajizungushii vitu. Tunachotaka kitunzunguke ni watu – watu tuwapendao na tulio na uhusiano nao. Katika mahusiano mtu hataki kumhumiza bila sababu anayempenda. Wakati wa ibada ya ndoa mchungaji aliuliza kama kuna mtu ana la kusema dhidi ya wanandoa watarajiwa. Kimya kikuu na mshangao vilitawala pale ambapo mwanamke  aliyekuwa amekaa kiti cha nyuma alienda mbele karibu na wanandoa amembeba mtoto. Bibi arusi alianguka na kuzirai. Mchungaji alimuuliza kama ana jambo lolote la kusema, “Hatusikii huko nyuma nimekuja mbele kusiliza vizuri wakiweka ahadi za ndoa.”

Upendo unaonekana katika zawadi au kutoa. Upendo unakufa unapouhodhi – unakua unapoutoa,” alisema Elbert Hubbard. Kuhodhi ni kukusanya mali au bidhaa na kuvirundika kwa matumizi binafsi. Katika kutoa tunawasaidia wengine. “Lengo letu kuu katika maisha haya ni kuwasaidia wengine. Na kama huwezi kuwasaidia, walau usiwaumize,” alisema Dalai Lama.
Upendo unaonekana katika kusikiliza. Weka hili katika kumbukumbu ya moyo wako: Hakuna mtu yeyote ambaye huwezi  kukosa kumpenda kama umesikiliza hadithi yake,” alisema Mary Lou Kownack. Ukimsikiliza utampenda. Mtume Paulo na Barnaba waliwatia watu moyo kwa sababu waliwasikiza. Tatizo kubwa siku hizi ni kutowasikiliza watu. “Barabara ya kuufikia moyo ni sikio,” alisema Voltaire. Unapomsikiliza mtu unagusa moyo wake. Kusikiliza ni kutoa huduma. “Kuwasikiliza wengine ni sehemu ya kwanza ya huduma ya kweli ya kikristo,” alisema Dietrich Bonhoeffer. Kusikiliza ni changamoto. “Yeye ambaye hamsikilizi tena ndugu yake muda mfupi atakuwa hamsikilizi Mungu,” alisema Dietrich Bonhoeffer.
  
Hitimisho
Upendo ni jambo la kujifunza. Kama watu wanajifunza kuchukia wanaweza kujifunza kupenda.”Hakuna mtu anayezaliwa akiwa anamchukia mtu mwingine kwa sababu ya rangi yake, historia yake, ama dini yake. Watu ni lazima wajifunze kuchukia, na kama wanaweza kujifunza kuchukia, wanaweza kufundishwa kupenda, kwa sababu upendo huja kiasili kwenye moyo wa binadamu kuliko chuki,” alisema Nelson Mandela (1918 – 2013).

Counter

You are visitor since April'08