Saturday, February 25, 2017

KUMBUKA KUKUMBUKA


 
                                                          Jumapili ya 8 ya Mwaka A
1.     Isa 49: 14-15
1 Kor 4:1-5
Mt. 6: 24-34
 
Je, mwanamke aweza kumsahau mtoto wake, aweza kumsahau mzao wa tumbo lake asimhurumie? Hata kama yeye angemsahau lakini mimi sitakusahau wewe hata kidogo” (Isaya 49: 15-15).  Sifa mojawapo ya Mwenyezi Mungu ni kukumbuka. Tumuige katika hilo. Kumbuka kukumbuka. Kuna aliyesema, “Kila mara kumbuka kusahau mambo yaliyokuhuzunisha lakini usisahau kamwe mambo yaliyokufurahisha. Kila mara kumbuka kusahau marafiki waliokusaliti lakini usisahau marafiki waliobaki nawe. Kila mara kumbuka kusahau matatizo yaliyopita lakini usisahau kukumbuka baraka zinazokujia kila siku.” Sisi kama binadamu tuna changamoto ya kusahau.
Visa hivi hapa vinabainisha ukweli huu. Kuna mtoto mdogo ni kama machoni alikuwa anatuma ujumbe: Ukimwona mama yangu kwenye “facebook” tafadhali mkumbushe bado niko kwenye beseni la kuogea. Mama alimsahau mtoto. Kuna baba mmoja ambaye alikuwa anampeleka shule kwa gari mtoto wake aliyekuwa amesinzia. Akasahau akaenda naye kazini. Akasahau kuwa yupo kiti cha nyuma akatoka na kufunga gari. Vyoo vyote vilikuwa vimefungwa. Alipotoka ofisini wazo lake lilikuwa kupitia shuleni kumchukua mtoto. Alipofungua mlango wa nyuma wa gari kuweka kompyuta yake ndogo alikuta mtoto ameishaaga dunia. Mwenyezi ni tofauti na wazazi hao. Tumuige Mungu katika kukumbuka.
Tunasoma katika Biblia, “Je, mwanamke aweza kumsahau mtoto wake, aweza kumsahau mzao wa tumbo lake asimhurumie? Hata kama yeye angemsahau lakini mimi sitakusahau wewe hata kidogo” (Isaya 49: 15-15). Kuna majina ya watu yanayosisitiza kuwa Mungu anakumbuka. Zahari maana yake Mungu amekumbuka. Zakaria maana yake Yehova amekumbuka au kukumbukwa na Mungu. Sakeri (Jina la Kiebrania) kukumbukwa na Mungu. Alazia maana yake Bwana amekumbuka.
Kwanza kukumbuka ni kuhuisha yaliyopita (anamnesis). Bwana Yesu alisema, “Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi.” Alitaka tuhuishe tendo lake la kujitoa sadaka. Ni kuweka jana katika leo. Ni kuitia nguvu leo. Watu hukumbuka siku za kufunga ndoa, kufunga nadhiri, siku za kuzaliwa, siku ya kupata uhuru, siku ya mashujaa. Wakati wa kuaga mwili wa marehemu wengine huuisha maisha yao na marehemu au huisha misiba yao nao hulia sana.  
Pili, ni kufukua kumbukumbu zilizopotea (Zakar kwa kiebrania). Ni kufufua yaliyozikwa zamani. Tuna methali isemayo bichi huamsha lililokauka.  Daudi alifufua ya zamani na kusema, “Mama yangu alinichukua mimba hatiani” (Zaburi 51: 7). Tatu ni kufikiri au kutafakari (Zakar). Katika mtazamo huu Ayubu alisema, “Mimi mwenyewe nikifikiri hali yangu, naona bumbuazi natetemeka mwili wangu wote” (Ayubu 21:6). Nne kukumbuka ni kutaja (zakar). Tano ni kwendea mtu maalumu (mimnéskó). Kupoteza uwezo wa kukumbuka kuna matokeo mabaya.
Kwanza, ukipoteza uwezo wa kukumbuka unapoteza uwezo wa kushukuru. Kushukuru ni kukumbuka. Ukikumbuka utashukuru. Siku ya Kushukuru ilikuwa imekaribia wanafunzi wa darasa la awali –Kindergarten au chekechea waliambiwa kuchora picha ya kitu ambacho katika maisha yao kimewasaidia na hivyo wanamshukuru Mungu kwa kitu hicho. Baadhi ya wanafunzi walichora nyumba, wengine walichora gari, ndege, chakula, kinyango. Mtoto mmoja alichora mkono. Wanafunzi walianza kujiuliza ni mkono wa nani...mkono wa Mungu? Mkono wa Polisi? Mkono wa mkulima? Hakuna aliyeweza. Wakati wa mapumziko mwalimu alimwendea mwanafunzi huyo na kumuuliza. Mkono huu ni wa nani? Mwanafunzi wa darasa la awali alijibu, “Ni mkono wako mwalimu.” Mwalimu alitokwa na machozi alivyokumbuka alivyokuwa anamsaidia mwanafunzi huyo kuvuka barabara akimshika mkono kwa vile alikuwa ni mlemavu wa mguu. Pia Alimshika mkono kumsaidia kuandika a, e, i, o, u. Ni kwa namna hiyo Mungu anatushika mkono tufungue mlango wa kutoka kwenye majaribu.
Pili, ukipoteza uwezo wa kukumbuka unapoteza uwezo wa kuthamini. Ukikumbuka utathamini. Tatu, ukipoteza uwezo wa kukumbuka, unapoteza uwezo wa kupenda. Ukikumbuka utapenda.
Tutakase kumbukumbu za mabaya. “Ni vizuri zaidi kusahau na kutabasamu kuliko kukumbuka na kuhuzunika,” alisema Christine Rosetti. Namna ya kutakasa kumbukumbu mbaya ni matukio yaliyopita kuyapa maana. Kosa la Adamu na Eva la kula tunda limeitwa na Kanisa Katoliki-Kosa lenye heri lililomleta mkombozi.
ROHO MTAKATIFU NI MKUMBUSHAJI: “Kila dokezo tunalopokea la kukumbuka ni kwa neema ya Roho Mtakatifu,” alisema Mt. Augustino wa Hippo.  Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia” (Yohane 14:26)
Katika masuala ya imani Roho Mtakatifu anatukumbusha yale ambayo Yesu alisema. Katika masuala ya majaribu ya kutenda mabaya, tunakumbuka aya fulani kwenye Biblia, amri ya Mungu, ushauri mzuri wa rafiki, fundisho la Kanisa, methali inayoonya, msemo unaokataza tendo baya, inakuja picha ya Yesu, picha ya hukumu ya mwisho. Hayo mambo yanapita akilini mwetu. Ni kazi ya Roho Mtakatifu.
 

Saturday, February 4, 2017

USIJIFANYE MWANGA, KUWA MWANGA:



2017 Februari 5: Jumapili

“Ninyi ni mwanga wa ulimwengu” (Mathayo 5: 14)

 Katika hili, nyota wa zamani wa Uingereza katika runinga za Malcolm Muggeridge alisema “Siwezi sema ni kwa kiasi gani nimlipe mama Teresa. Alinionesha ukristo kwa matendo. Alinionesha upendo kwa vitendo. Alinionesha namna upendo wa mtu mmoja unavyoweza kuanzisha wimbi la upendo ambalo laweza kuenea dunia nzima”.Mama Teresa alikuwa ni mwanga wa ulimwengu ambaye aliangazaupendo kuliko kujifanya anapenda.Upendo wake haukuwa wa kujitangaza: ulikuwa ni moto wa altare.Ulitakiwa ukolezwe na upendo huo uendeleekuwaka; kwaiyo sala ilikuwa ni muhimu kwake. Mwanga unaotoka kwa Mungu, ni mali ya Mungu na unatakiwa kuangaza utukufu wake. Kamaupendo uking’aa lakini kwa mtu pekee  unaweza kuwa ni majivuno yaliyojaa kujionyesha;upendo wa Mungu ni heshima ya kweli. Katika tukio lolote tendo la utukufu wa Mungu ndiyo furaha kuu ya mwanadamu.

Martin Luther King Junior alisema, “Giza halifukuzi giza: mwanga tu unaweza kufanya hilo. Chuki haiwezi kufukuza chuki: upendo unaweza kufanya hilo.”  Upendo ni mwanga unaweza kufukuza giza la chuki. Upole ni mwanga unaweza kufukuza giza la hasira. Kuchapa kazi ni mwanga unaweza kufukuza giza la uvivu. Kuna mtu mmoja baada ya kuona anapata shida ya kusali kila wakati wa kulala kwa sababu ya urefu wa sala akaona aiandike sala yote nakuibandika ukutani, ikifika muda wa kulala anasema: Ee Mungu kama kawaida hapo ukutani,Amina! Huo ni uvivu. Wakristu walipewa sifa kubwa na Yesu alipowaita mwanga wa dunia. Lakini sifa hii inawaendea watu wote wanaotenda mema na kushinda ubaya kwa wema.
Buddha baada ya kuchunguza mshumaa alisema: “Maelfu ya mishumaa yanaweza kuwashwa na mshumaa mmoja, na umri wa mshumaa hautafupishwa. Furaha haipungui kwa kuwashirikisha wengine.” Hupotezi chochote kwa kuwasaidia wengine. “Mshumaa haupotezi chochote kwa kuwasha mishumaa mingine,” alichunguza hilo katika mishumaa James Keller. Joyce Meyer alisema hivi: “Biblia inasema kuwa Wakristo ni chumvi ya dunia na mwanga wa ulimwengu. Kazini, kwenye duka la vinywaji na hata kati ya marafiki wasio wastaarabu na wanafamilia, Watu wa Mungu wapo kuleta ladha katika hali mbaya.”
Mwanga unaonekana na unatusaidia kuona. Mfanyakazi lazima aonekane anafanya kazi. Kiongozi lazima akuone ili kupandishwa cheo. Mkristo lazima aonekane anakuwa mkristo jikoni, dukani, kiwandani, hotelini, uwanjani, sokoni, michezoni, bungeni, barabarani.

“Maneno yote yatakuwa hayafai kama hayatoki ndani – maneno ambayo hayatoi mwanga wa Kristo yanaongeza giza” (Mwenye heri Mama Teresa wa Calcutta). Kuwa mwanga wa dunia kunatudai kutumia maneno ambayo yanatoa mwanga wa Kristo.  Tunaweza kusema tusiende  mbele ya wanzetu na midomo mitupu.  Midomo ibebe maneno  yanayotia mwanga: maneno ya shukrani, maneno ya kutia moyo, maneno ya kuchangia hoja, maneno ya kusifu, maneno ya msamaha, maneno ya upendo hayo ni maneno ya kuleta mwanga. Tutafakari methali ya Poland, “Maneno yapimwe yasihesabiwe.” Yapimwe kama yanafaa au hayafai. Maneno yanayofaa yanaweza kutusafirisha kutoka kwenye matope hadi kwenye mwezi. Maneno yenye huruma ni mafupi lakini mwangwi wake unafika mbali. Matusi hayafai badala yake tumia maneno yenye huruma.
Sala: Ee Mungu naomba ulimi wangu utoe maneno yanayoleta mwanga, maisha yangu yawe mwanga wa kuwaangazia wengine, kazi zangu zikupe utukufu, watu waone wakutukuze. Amina.

Counter

You are visitor since April'08