Saturday, December 31, 2016

TAZAMA NYUMA USHUKURU TAZAMA MBELE UFIKIRI


                            Sherehe ya Maria Mama wa Mungu
                                                  1 Januari 2017
1. Hes 6: 22-27
2. Gal 4: 4-7
3. Lk 2: 16-21

Furaha bila shukrani nini? Ipo wapi shukrani bila kumfikiria Mungu? Tunapomaliza mwaka wa 2016 tunafurahi. Furaha haikamiliki bila kumshukuru Mungu. Sababu ya kushukuru tunayo, tumemaliza mwaka salama. Nia ya kushukuru tunayo, penye nia pana njia. Uwezo wa kushukuru tunao. Tunaweza kusema au kuandika au kuashiria tunashukuru.  “Shukrani inazaliwa katika mioyo ambayo huchukua muda kuhesabu baraka za wakati uliopita,” alisema Charles E. Jefferson. Tulipoanza mwaka 2016 tulisikia maneno haya: “Bwana akubarikie na kukulinda; Bwana akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili; Bwana akuinulie uso wake, na kukupa amani” (Hesabu 6: 22-27). Liwalo na liwe ukweli ni kwamba umebarikiwa. Baraka ulizombewa umezipata. Tazama nyuma shukuru. Mungu anapokubariki ina maana anakufikiria. Mwaka mzima wa 2016 umefikiriwa na Mungu. Tunapofunga mwaka tutafakari maneno haya ya busara ya mtu fulani.
“Leo kwenye basi niliona msichana mzuri sana akiwa na nywele za dhahabu. Nilimwonea wivu-alionekana mzuri sana name nikafikiri ningekuwa mzuri kama yeye. Ghafla aliposimama kutelemka alikuwa na mguu mmoja na gongo la kutembelea aliponipita alitabasamu. Ee Mungu, nisamehe ninapolalamika. Nina miguu miwili – dunia ni yangu. Nilienda dukani kununua pipi. Kijana aliyekuwa anauza pipi alikuwa mchangamfu, nilizungumza naye aliniambia: ‘Ni vizuri kuzungumza na watu kama wewe, unaona mimi ni kipofu.’ Mungu nisamehe ninapolalamika; nina macho mawili – dunia ni yangu. Nilipotelemka chini kwenye mtaa niliona mtoto ana macho ya bluu. Alisimama na kutazama watoto wengine wakicheza. Ilionekana hakufahamu jambo la kufanya. Nilisimama na kumuuliza; ‘Kwa nini haungani na watoto wengine  kucheza?’ Alinitazama bila kusema neon. Nilitambua hauwezi kusikia. Ee Mungu, nisamehe ninapolalamika. Nina masikio mawili – dunia ni yangu. Pamoja na miguu ya kunipeleka kule ninakotaka kwenda, pamoja na mcho ya kuona kuchwa kwa kujua, pamoja na masikio ya kusikia lile ambalo nitalijua, ee Mungu nisamehe ninapolalamika. Nimebarikiwa dunia ni yangu kweli.”
Mshukuru Mungu  ameuvika taji mwaka 2016. Tunasoma hivi katika Zaburi: “Umeuvika mwaka taji ya mema yako; mapito yako yamejaa mafuta (Zaburi 65:12). Hata kuwepo kwa maadui katika maisha yako Mungu amekusaidia kuvaa taji. Wakati mwingine ili kufanikiwa katika maisha unahitaji maadui. Unahitaji watu watakaokuzomea ili umkimbilie Mungu.  Unahitaji watu watakaojaribu kukutia hofu ili uwe na ujasiri. Unahitaji watu watakaosema “HAPANA” ili ujifunze kujifanyia. Unahitaji watu watakaokutakatisha tamaa ili uweke matumaini yako yote kwa Mungu. Unahitaji watu watakaokufanya upoteze kazi yako ili uazishe biashara yako. Unahitaji watu watakaokuuza kama Yozefu ili uweze kwenda Misri  kuwa Waziri Mkuu katika nchi ya utumwa. Unahitaji Mwenye nyumba katili unapopangisha nyumba yako ili usipate faraja kwenye nyumba ya wengine uweze kujenga nyumba yako. Haya yanaitwa mapito. Uenda umepitia haya mwaka 2016. Hiyo ni vunja vunja ya Mungu ili aweze kukubariki. Mungu anavunja ili kubariki. Teke la adui mgongoni linakusogeza mbele.
Tazama mbele ufikiri. Papa Fransisko alisema kuna lugha tatu: ya kwanza fikiria vizuri, ya pili hisi vizuri, ya tatu tenda vizuri. Bikira Maria alifikiria vizuri. “Lakini Maria aliyaweka na kuyatafakari mambo hayo yote moyoni mwake” (Luka 2:19). Bikira Maria alifikiri vizuri, alihisi vizuri na kutenda vizuri. Tarehe moja Januari ni siku ya kuombea amani duniani. Hatuwezi kuwa na amani kama kufikiri kwetu si kuzuri. Kuwa na amani fikiria amani, hisi amani, na tenda yanayoleta amani. Kuna aina mbali mbali za kufikiri kadiri ya John Maxwell.  Kwanza ni kufikiria picha kubwa. Watu wanapimwa kwa makubwa wanayofikiria.  Alvin Toffer alisema, “Fikiria mambo makubwa wakati unafanya mambo madogo, ili mambo yote madogo yaelekee upande huo.” Pili ni kufikiria kwa kufokasi. Fokasi ni mahali miale ya nuru ikutanapo. Kuwa makini na lengo lako. Mambo ambayo si muhimu yanayokuondoa katika lengo lako usiyatilie maanani.  Kuwa na faili ya mambo muhimu mezani kwako yafuatilie kila siku. Tatu kufikiria kibunifu. Jiulize maswali haya: kwa nini jambo lifanyike namna hii tu? Nini chanzo cha tatizo hili? Ni masuala gani yanalizunguka tatizo hili? Hili linanikumbusha nini? Nini kinyume chake? Ni ishara gani au taswira gani inalielezea vizuri? Kwa nini ni muhimu? Nani anamtazamo tofauti katika hili? Jambo gani litatokea kama hatulitatui? Nne ni kufikiria kuhalisia. “Wajibu wa kwanza wa kiongozi ni kubainisha uhalisia,” alisema Max de Pree. Uhalisia unakupa msingi wa kujenga.  Tano ni kufikiria kimkakati. Watu wengi wanatumia muda mwingi wakipanga namna ya kufurahia kipindi cha mapumziko kuliko kupanga juu ya maisha yao. Sita ni kufikiria kwa kuangalia uwezekano.  “Hakuna jambo linaloaibisha kama kuona mtu anafanya jambo ambalo ulisema haliwezekani,” alisema Sam Ewing.  Saba fikiria kwa kutafakari. Tafakari uzoefu wako, uliyoyaona, njia ulizokosea. Kukosa njia ni kujua njia. Nane fikiria kwa kuhoji mawazo ya wengi, wengi wanachopendelea. “Ugumu haupo katika mawazo mapya bali kukwepa mawazo ya zamani.” Galileo aliposema dunia inazunguka jua alihoji kile wengi walichoamini kwamba jua linazunguka dunia. 
Hitimisho
Tumuige Bikira Maria Mama wa Mungu katika kufikiria kwa kutafakari. Yesu ni Mungu. Bikira Maria ni Mama wa Yesu. Hivyo Bikira Maria ni Mama wa Mungu (Theotokos). Mt. Maksimiliano Maria Kolbe alikuwa na haya ya kusema: "Wewe ni nani ee Maria Imakulata? Wewe ni nani ee Imakulata? Siwezi kuelewa maana yake nini kuwa kiumbe cha Mungu...Kuelewa maana yake nini kuwa mtoto wa Mungu ni nje ya uwezo wangu mwenyewe. Wewe ni nani ee Imakulata? Si kiumbe tu, si mtoto wa kulea tu, bali ni Mama wa Mungu, lakini si Mama mlezi tu, bali ni Mama halisi wa Mungu."
 

Saturday, November 5, 2016

KIFO SIO NUKTA NI ALAMA YA MKATO

                                 
                                                        JUMAPILI YA 32 YA MWAKA C
“Kwani Mungu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai, maana kwa sababu yake wote wanaishi” (Lk 20: 38).
1.  2 Makabayo 7: 1-2.9-14
2.  2 Thess 2: 16-3:5
3.  Lk 20: 27-38

Meli ikianza safari yake toka Kisumu hadi mwanza Tanzania wale walioko Kisumu wanasema meli imeenda. Wale walioko Tanzania wanaoiona kwa mbali wanasema meli imekuja. Mtu akiaga dunia tunasema “Ameenda.” Walioko mbinguni au toharani wanasema, “Amekuja.”  Hivyo kifo sio kituo bali ni koma. KWETU KIFO SIO UKUTA NI MLANGO. Kwetu kifo sio kizuizi bali ni daraja. Mbio za sakafuni huishia ukingoni. Mbio zetu haziishii ukutani bali tunapitia zinafika mlangoni na tunapita.
Hadithi ikiwa nzuri sana kwenye gazeti inakatizwa na chini yake yanaandikwa maneno itaendelea toleo lijalo. Mtu anapoaga dunia maisha yake yanaendelea toleo lijalo. Toleo Lijalo ni motoni, mbinguni au toharani. Kuna mshika kipenga aliyeaga dunia akaenda motoni. Huko alikuta uwanja mzuri sana na watu wamejipanga kucheza mpira alifurahi sana. Timu mbili ziliingia yeye akashika kipenga. Wachezaji wakasalimiana na kushika nafasi zao. Yeye mshika kipenga akauliza: “Mpira wapi?”. Aliambiwa huku ndio maana kunaitwa motoni. “The hell of it” ni kwamba hakuna mpira. Motoni ni kama una hamu ya chakula na hauwezi ukala. Kuna kitu kinakosekana.
MZAHAA JUU YA KIFO NA MAISHA BAADA YA KIFO: “Ukristo kwa kiini chake ni dini ya ufufuko. Dhana ya ufufuko iko kwenye kitovu chake. Ukiondoa ufufuko, ukristo unauharibu,” alisema John R. W. Stott.  Mungu wetu si Mungu wa wafu ni Mungu wa walio hai. Masadukayo kidini walikuwa mahafidhina na hawakupokea mafundisho yaliyokuwa nje ya vitabu vya kwanza vya Agano la Kale. Waliyakataa mafundisho juu ya ufufuko, malaika na pepo wabaya. Mara kwa mara Yesu alibishana nao. Kusema kweli kifo si nukta bali ni alama ya mkato maisha yanaendelea.  Kule mbinguni hapakuwepo kuoa au kueolewa. Tutaishi kama malaika. Tumefanywa kidogo chini ya malaika (Zaburi 8:6).
Masadukayo walifanya mzahaa juu ya kifo na maisha baada ya kifo. Walifikiri kifo ni mwisho wa safari. Walifikiri kifo ni kikomo. Walifikiri kifo ni kituo. Walijiuliza kama “Alichokiunganisha Mungu mwanadamu hasitenganishe.” Kwa nini sasa Mungu atenganishe mbinguni?” Walimuuliza swali Yesu lenye mtego. Walitazamana. Walikonyezana. Wakasema tumumweza. Walimuuliza kama mambo mazuri yatakuwa huko. Kuna wengine labda wanafanya mzaha kama huo. Wanauliza kama kuwa mbinguni ni sherehe nani watakuwa wanapika? Kuni hizo zitatoka msitu upi? Jiko litakuwa wapi? Ni aina gani ya pombe zitakuwa huko? Mafarisayo walikuwa kama chura ambaye alikuwa anabishana na kusema hakuna nchi kavu dunia yote ni maji. Ni kama watoto wawili mapacha waliokuwa kwenye tumbo la mama yake mmoja alipozaliwa mwingine alilia sana na kusema kaka yangu ameaga dunia. Wote wakakutana duniani.
MASADUKAYO WALIFIKIRIA MAMBO YA KARIBU
Tunafikiri mambo ya karibu. Sala zetu ni za mambo ya karibu na sio za mambo ya mbali sana. Watoto shuleni wanafikiria maksi. Pengie tunafikiria kesho. Mtu anaenda kufanya mkataba anafikiria atakavyomdanya mtu. Hafikirii kesho itakuwaje.

MUNGU WA IBRAHIMU NI MUNGU WAKO NA WA JAMAA YAKO ALIYEKUFA
Abrahamu anaitwa “Rafiki wa Mungu,” (Isaya 41:8), “Mtumishi wa Mungu” (Zaburi 105:6) Mungu alimbadili Abrahamu anaweza kukubadili wewe. Abramu alimdanganya Farao na kusema Sarai si mke wake (Mwanzo 11: 10 – 20) Sasa  Mungu wetu ni Mungu wa Ibrahimu. Isaka alidanganya hakusema kuwa Rebeka ni mke wake maana alikuwa mzuri sana. (Mwanzo 26: 6-10) Yakobo aliiba haki ya Esau (Mwanzo 27: 1 – 29). Walikuwa wameoa wanawake wazuri sana. Mungu aligeuza maisha yao anaweza kugeuza maisha yako. Na Mungu akaitwa Mungu wa Kamau, Mungu wa Onyango, Mungu wa Kilonzo, Mungu wa Mutua, Mungu wa Anna. Ibrahimu alikuwa baba wa imani.
 MAISHA BAADA YA MAISHA
Katika tamaduni za kiafrika mtu akiwa anaomboleza anamwambia marehemu amsalimie jamaa zake walioaga dunia. Anasema: Nisalimie babu yangu, nisalimie nyanya yangu. Nisalimie mjomba wangu. Nisalimie mama mdogo. Mfano wa majina: immortality of name: mjukuu anapewa jina la babu. Mtoto wa kike anapewa jina la nyanya yake. Tunataka jina la mtu liendelee kutajwa. Immortality of fame: Tunataka sifa ya mtu iishi milele. Tunajenga sanamu za ukumbusho. Kuna immortality of influence: Jina la baba linawapa watoto ushawishi. Immortality of power: Tunataka mamlaka yaendelee kwa kuanzisha mashirika ya kutoa msaada. Nyerere Foundation. Aliyeanzisha zawadi ya Nobel Prize.
KIFO SIO NUKTA NI ALAMA YA MKATO
Kifo kipo katika miguu tunatembea nacho. Ndivyo isemavyo methali moja ya kiafrika.  Sio tu kwamba tunatembea nacho katika miguu tu pengine tunasafiri nacho katika vyombo vya majini, angani na barabarani.  Hadithi inapokuwa tamu kwenye gazeti au runinga hukatizwa na chini yake maneno “Itaendelea Toleo Lijalo,” huandikwa. Maisha ya marehemu waliokufa  ni hadithi ambayo itaendelea toleo lijalo. Toleo lijalo ni huko mbinguni,  toharani au motoni. 
Katika adhimisho la misa huwa tunasali: “Tunasikitika kwa sababu tunajua kwamba lazima tutakufa, lakini tunatulizwa kwa kuwa alituhaidia uzima wa milele. Ee Bwana, uzima wa waamini wako hauondolewi ila unageuzwa tu. Nayo makao ya hapa duniani yakishabomolewa, tunapata makao ya milele mbinguni.”  Sayansi inatwambia kuwa hakuna kitu chochote katika maumbile, hata chembe ndogo inaweza kupotea kabisa kabisa. Maumbile hayajui kutokuwepo, yanachokijua ni mabadiliko. Ukweli huu wa kisayansi unahimarisha imani yetu katika kuendelea kuishi katika maisha ambayo yamegeuzwa. Kusema kweli kifo ni kudondoka kwa ua ili tunda liweze kukomaa. Kuna maisha baada ya kifo. Kuna maisha baada ya maisha. Katika somo la kwanza saba wako mbinguni na saba wa kufikirika wa Injili wako mbinguni. Katika somo la kwanza tunasoma hivi: “Karibu na kukata roho, akasema, “Ewe mpotovu, unatuondoa uzima wa sasa, lakini Mfalme wa ulimwengu atatufufua sisi, tunaokufa kwa ajili ya amri zake, naye atatupatia tena maisha ya uzima wa milele” (2 Wamakabayo 7: 9).
NAMNA GANI?
 Ingawa kifo huja mara moja tu kwa kila mtu, swali linabaki ni kifo cha namna gani ? Baadhi ya wakristu husali na kumuomba Mungu wafe kifo chema. Sala yao huwa hivi, “Na kifo cha ghafla na kisichotazamiwa, utuopoe, Ee Bwana.”  Masadukayo walisumbuliwa na swali la namna gani baada ya ufufuko mpaka walitambulikana hivi: “ndio watu wanaokana ufufuko wa wafu” (Lk 20: 27). Masadukayo walikuwa ni tabaka la kikabila kati ya Wayahudi wa Palestina wakiwemo kati yao familia za kikuhani, wamiliki wa ardhi na wafanyabiashara matajiri – ambao bila shaka walikuwa wazaliwa wa watawala wa kihasmonea. Jina lao linatokana na jina la Zadoki kuhani mkuu wa mfalme Daudi (2 Sam 19: 12) na walihesabiwa katika kundi lao makuhani wengi sana katika Israeli. Wao walishikilia kwa nguvu mafundisho ya Torati na kuyaacha kando mafundisho  makuu yasiyokuwamo humo. Matokeo yake walikataa ufufuko na uwepo wa malaika.  Katika masuala ya imani namna gani tunamwachia Mungu.
Juu ya namna gani ya kwanza  hakuna anayemjua mjumbe wa kifo atakuja lini. Ni busara kila tufanyalo katika maisha tujiulize, “Halafu?” Kama hadithi ya vijana wawili. Kijana mmoja alimuuliza mwingine. “Utafanya nini ukikua?” “Nitachukua somo la biashara.” “Halafu?” “Nitatafuta kazi.” “Halafu?” “Nitapata fedha nyingi kama mshahara.” “Halafu?” “Nitatafuta msichana nioe” “Halafu?” “Nitakuwa na watoto.” “Halafu?” “Nitawalea watoto” “Halafu?” “Nitakuwa babu?” “Halafu?” “Labda nitafanywa chifu.” “Halafu?” “Nitatawala watu.” “Halafu?” “Nitazeeka.” “Halafu?” ““Halafu?”, halafu, halafu, halafu usiulize zaidi ya hapo.” “Bila shaka uwe unafikiria kuwa siku moja utakufa.” Lakini tumaini linabaki kuwa kifo sio nukta, sio kikomo, bali ni alama ya mkato hadithi ya maisha inaendelea.
KWA NINI?
Masadukayo walijishughulisha na namna gani walipomuuliza swali Yesu la mtego. “Atakuwa mke wa nani?” Yesu alijishughulisha na “kwa nini?” Badala ya masadukayo kuleta mtanziko halisi, wanajaribu kuonesha upuuzi wa mahubiri ya Yesu juu ya ufufuko wa miili. Yesu analiondoa swali kutoka kwenye uwanja wa kuchekesha na kulifanya kauli nzito kuhusu ufufuko na kupaa kwake mwenyewe mbinguni na vile vile hatima ya ubinadamu na ukamilisho wa historia ya binadamu. Jibu la kwa nini ya Yesu kwanza Mungu wetu ni Mungu wa walio hai: “Kwani Mungu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai, maana kwa sababu yake wote wanaishi” (Lk 20: 38).
Pili dini ya kikristo ni dini ya ufufuko. Ukiondoa ufufuko unafuta dini ya kikristu. Kutokana na Pasaka wakristo inabidi wawe watu wa matumaini, watu wa ukweli, watu wa amani, na watu wa kutenda mema. “Kama hakuna ufufuo wa wafu, basi, Kristo naye hakufufuka na kama Kristo hakufufuka, basi mahubiri yetu hayana maana na imani yetu haina maana…Lakini ukweli ni kwamba Kristo amefufuliwa kutoka wafu.” (1 Wakorintho 15: 13-20).
Kifo Kiwe Zawadi
Kuna methali ya Ujerumani isemayo hastahili kuishi anayeishi kwa ajili yake tu. Binadamu wengi wako tayari kufia imani, kufia mtu, kufia dini, kufia shirika na kufia familia. Hawaishi kwa ajili yao nafsi zao tu. Ukiwafia wengine, unakifanya kifo kiwe zawadi kwa wengine. Ipo misingi ya kumfanya mtu amfie mwingine au alifie shirika, kampuni, au dini. Yesu aliifia dunia Yesu alifia watu kama Kayafa alivyotabiri ili waneemeke, waokoke. “Huyo Kayafa ndiye aliyekuwa amewashauri Wayahudi kwamba ni afadhali mtu mmoja afe kwa ajili ya watu.” (Yohane 18: 14). Yesu alikufa kwa ajili ya watu. Jambo la kujiuliza ni unafia nini? Kutokana na neno kufa tuna neno kufia yaani kupigana kwa namna zote ili kutetea kitu au jambo fulani. “Ni baraka kufia jambo fulani, sababu unaweza kwa urahisi kufia bure,” alisema Andrew Young. Kuwafia wengine hakuhitaji kujipendelea. Mtu anayejipendelea hafikiri kama kuna wengine duniani anajiona kitinda mimba duniani. Unapowafia wengine unafanya kifo chako zawadi kwa kizazi kijacho au watu wengine.

Kama unawafia wengine ukitoka haja kubwa kiache choo katika hali ya usafi maana wewe si wa mwisho kukitumia, wewe si kitinda mimba. Ukimaliza kidato cha nne usiharibu dawati au viti vya kukalia maana wewe si wa mwisho au kitinda mimba. Ukiviacha katika hali nzuri unawafia wengine. Fikiria kizazi kijacho. Kifie kizazi kijacho. Usimalize raslimali za dunia maana wewe si kitinda mimba duniani. Jitoe kwa ajili ya wengine. “Unatoa kidogo unapotoa kutoka katika mali yako, lakini unatoa zaidi unapojitoa wewe mwenyewe,” alisema Kahlil Gibran.
 Kuna methali isemayo, “kifo kinafuta kila kitu isipokuwa ukweli.” Kifo hakifuti ukweli wa maneno yetu na matendo yetu. Wakati wa kufani maneno yetu yawajenge tunaowaacha nyuma. Kuna mchungaji ambaye alikuwa anafanyiwa jubileo ya miaka 40 katika uchungaji. Alikuwa mgonjwa sana. Aliombwa kusema neno. Mwanzoni alikataa.Baada ya kuombwa kuzungumza alisema, “Afya ni mali.” Aliketi chini. Wakristu waliomba ufafanuzi. Aliamka na kusema. “Afya ni mali. Afya yangu si nzuri. Ni mbaya sana. Nyinyi mmechangia afya yangu kuwa mbaya.” Mchungaji huyo hakumwingiza Mungu katika ugonjwa wake. Kama Ayubu angetulia katika Mungu, “Bwana ametoa Bwana ametwaa jina lake litukuzwe.” Baada ya miezi miwili aliaga dunia. Kifo chake kiliwaacha waliopaswa kumpa huduma wakisutwa na dhamiri. Kifo chake hakikuwa zawadi kwa wengine. Kufa ni lazima, kama biblia isemavyo, “Kwa kila kitu kuna majira, na wakati kwa kila jambo duniani:…kuna…wakati wa kufa” (Mhubiri 3: 2), swali unakufa je? Yesu akiwa kufani aliwasamehe watesi wake. Kifo chake kilikuwa ni zawadi kwa watesi, walipata zawadi ya msamaha.
Juu ya kufanya vifo vyetu viwe zawadi, Henri J.M.Nouwen alikuwa na haya ya kusema, “Namna gani tunafanya vifo vyetu zawadi kwa wengine? Mara nyingi maisha ya watu yanaharibiwa, yanadhuriwa au kuwa na majeraha maisha yao yote kwa vifo vya jamaa au marafiki zao. Lazima tufanye tuwezalo ili kukwepa ili.Tunapokuwa kufani tunalowaambia wale ambao wako karibu nasi, iwe kwa kusema au kuandika ni muhimu. Tunapowashukuru, kuwaomba msamaha kwa makosa yetu na kuwasamehe kwa ya kwao na kuwaonesha nia ya kutaka waendelee na maisha yao bila kusutwa na dhamiri lakini wakikumbuka neema za maisha yetu basi vifo vyetu vinakuwa zawadi kweli.”

 Hasara kubwa si kifo bali  kinachokufa ndani mwetu. “Kifo si hasara kubwa sana katika maisha yetu. Hasara kubwa sana ni kile kinachokufa ndani mwetu wakati tunaishi,” alisema Normani Cousins mtunga insha na mwariri wa  Amerika (1912 – 1990). Wakati tunaishi kuna mambo ambayo yanaweza kufa kama shauku, moyo wa kutoa, moyo wa kujitoa, uchaji kwa Mungu, utii, usafi wa moyo. Vikifa ni hasara kubwa. 

Saturday, October 29, 2016

SHUKA CHINI



                                                               
                                                    Jumapili ya 31 ya Mwaka C
1. Hekima 11: 22-12:2
2. II Thes: 1: 11-2:2   
3. Lk 19: 1-10

UTANGULIZI
Zakayo ni “ngamia” aliyepitia tundu la sindano. Alikuwa na pesa kama serikali. Alikuwa na pesa kama njugu, lakini alipata wokovu. Alikuwa anacheka kwa nje lakini analia kwa ndani. Zakayo aliyepanda mkuyu alishuka chini. Kupanda mti ni kutoishi uhalisia. Hatuishi mtini. Ni kama umkute tajiri mkubwa duniani kama Bill Gate amepanda mti yuko anatafakari.  Zakayo alikaa kwenye mkuyu akitafakari mada aliyoipenda sana: PESA SABUNI YA ROHO. Zakayo alihesabu vichwa vya watu na kufikiria kama wangelipa kodi angepata cha juu kikubwa. Kuwa na nadharia bila matendo ni kukaa juu kwenye mkuyu. Kama tuna ndoto za kesho bila kuzifanyia kazi leo tunaambiwa kama Zakayo: Shuka toka juu. Wengine wanaopoolewa wanakuwa juu mtini wanafikiri kila siku itakuwa kama siku ya harusi. Shuka toka juu. Yale yanayosemwa siku ya HARUSI yanapitia sikio moja na kuingia sikio jingine. Kwao HARUSI ni sherehe ya ushindi. Ameshinda amempata Bwana huyo. Ameshinda amempata Bibi. Toka juu uje chini. Kuna maisha baada ya harusi. Cha msingi leo isipite bila kuitumia vizuri. Kuna wanaoandaa harusi na hawaandai ndoa hao wako kwenye mti wa mkuyu washuke chini.
 Kulitaja bure jina ni kukaa juu bila kujali uhalisia. Kuwa na mali bila Mungu ni kukaa kwenye mkuyu. Kutoona uzuri katika ubaya wako ni kukaa kwenye mkuyu. Yesu  alimwona Zakayo akaona si mwovu bali ni mkosefu. Aliona upande wa pili wa Zakayo uzuri wake. Zakayo alikuwa mfupi wa kimo. Hakuwa mfupi wa kila kitu. Wakati mwingine hatuoni vizuri watu tunafikiri ni wafupi wa kila kitu. Wengine ni warefu kipesa, warefu kiunyenyekevu, warefu wa kutoa fidia, warefu wa kusaidia maskini.  Kushuka chini ni kutambua uzuri katika ubaya wako.

KUSHUKA CHINI NI NGAMIA KUPITIA TUNDU LA SINDANO
Lakini kwa nini Zakayo? Yesu aliona juhudi za Zakayo za kutamani kumwona. Yesu aliona chanya za Zakayo. Mungu akisema nitakubariki hakuna atakayezuia. Yesu alimbariki Zakayo. Yesu ni jibu. Pengine hatuoni hilo. Tunamwona Zakayo akipitia kwenye tundu la sindano. Zakayo alikuwa tajiri. Wokovu unawajia matajiri pia. “Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri” (Luka 19:2). Zakayo alikuwa mfupi wa kimo lakini ufupi si ugonjwa. Baadaye alipotoa fidia mara nne ya alichochukua anakuwa mrefu kiroho.  Wokovu si kwa ajili ya maskini tu, wokovu ni kwa ajili ya matajiri pia. Mali bila Mungu ni kuishi kwenye mawingu, nadharia, ni kukaa kwenye mkuyu. Lazima kushuka chini. Kama umemsahau Mungu umejisahau. Mchungaji alikuwa anataniana na tajiri ambaye hakuonekana kanisani hata mara moja. Tajiri alimwambia mchungaji: “Jinsi ulivyo mtu wa Mungu ukienda motoni, nitashangaa sana.” Mchungaji  naye alimwambia tajiri: “Wewe usivyokanyaga Kanisani, ukienda mbinguni nitashangaa sana.”  Matajiri kama Zakayo wana uwezekano mkubwa kama maskini kupitia kwenye tundu la sindano. Mtumishi wa Mungu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema, “Watakatifu wengi wametoka katika makazi duni ya maskini, lakini hatuwezi kuendekeza makazi duni ya maskini ili kuwapata watakatifu.” Hatuwezi kuendekeza umaskini ili kuwapata watakatifu. Matajiri wakimtegemea Mungu wakawa na umaskini wa roho wanakuwa watakatifu

KUSHUKA CHINI NI KUTOLITAJA BURE JINA
Zakayo ni neno la Kebr linamaanisha “msafi.” Zakayo alilitaja bure jina lake lenye maana ya msafi. “Pale palikuwa na mtu, jina lake Zakayo” (Luka 19:2). Zakayo alikejeliwa kwa kuitwa msafi. Alikuwa na pesa chafu. Hakuwa msafi. Alitakasa pesa. Alitengwa na jamii kwa vile alikuwa mtu wa kitu kidogo, alichukua cha juu, alikula mlungura. Yesu alitaka jina lake liwe na uhalisia wa mambo: msafi awe na matendo safi, mawazo safi na maneno safi.  Mtoto kumuita baba yake “baba” lakini hamheshimu ni kulitaja bure jina. Kutaja neno “Kanisa” lakini husali wala kutoa sadaka ni kulitaja bure neno “Kanisa.” Shuka chini.

KUSHUKA CHINI NI KUTAMBUA UZURI KATIKA UBAYA WAKO
Anayetembea dhiraa moja kumkaribia Mungu, Mungu anatembea mbili kumkaribia. Ni methali ya Wayahudi. Dhiraa ni kipimo cha mkono mmoja au nusu yadi. Unamtafuta Mungu na Mungu anakutafuta. Mungu anaitafuta mbegu ya uzuri na wema iliyopandwa ndani mwako. Mbegu hiyo ni kitambulisho. Mungu anakutafuta licha ya kasoro zako, kama methali ya Wahaya isemavyo: akupendaye hukupenda na uchafu wako. Sababu kubwa ni ipi? Jibu ni ingawa kuna ubaya katika uzuri lakini kuna uzuri katika ubaya wako.
Masimulizi juu ya Zakayo yanabainisha ukweli huo. Tunasoma hivi. “Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri (Luka 19: 2). Jina Zakayo maana yake asiye na kosa, asiye na hatia, mwadilifu. Alikuwa na jina zuri, ingawa alidharauliwa kwa sababu ya vitendo vya kupokea rushwa au kutoza kitu kidogo. Katika ubaya wake kuna jina lake ambalo ni zuri. Jina la Zakayo lilihusishwa na pesa, Zakayo – mkopeshaji, Zakayo – mla rushwa, Zakayo – mtu wa kitu kidogo, Zakayo – Mtu anayetaka chakula ya watoto, Zakayo mwizi na Zakayo fisadi. Yesu alimuita Mwana wa Abrahamu. Yesu alimuita jina zuri “mwana wa Abrahamu.” Alikuwa mwana wa Abrahamu kiimani. Kama unaitwa Malaya Yesu anakuita “Mwana wa Abrahamu.” “Kama unaitwa pumbavu,” Yesu anakuita “Mwana wa Abrahamu.”  Kuna methali ya Tanzania isemayo, jina baya humwaribia mwenye hilo jina. Kinyume chake ni kweli jina zuri humwokoa mwenye hilo jina. Jina Zakayo lina maana nzuri yaani mwadilifu.
Msitari wa tatu unasema hivi, “Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo” (Luka 19:4). Zakayo alikuwa mfupi wa kimo kimwili na kiroho alikuwa mfupi sababu alikuwa anataka kitu kidogo. Jambo zuri katika ufupi wa kiroho ni kwamba Zakayo alikuwa na tamaa ya kumwona Yesu. Yesu ni mtu muhimu. Tunahesabu kalenda kutoka mwaka Yesu alipozaliwa. Yeye ni kitovu cha historia ya dunia. Watu wanaoenda makanisani ni kwa vile wana tamaa ya kumwona Yesu. Ingawa Zakayo alikuwa mtu mbaya mla rushwa lakini katika ubaya wake palikuwepo na uzuri:tamaa ya kumwona Yesu. Mbegu ya wokovu ilianza kuchipuka ndani mwake kwa vile alitaka kumwona Yesu. Mambo yaliyomzuia kumuona Yesu sio tu wingi wa watu bali wingi wa makosa yake. Kama una makosa tubu na kumgeukia Mungu ili umuone Yesu kwa macho ya imani.
Katika msitari wa nne tunasoma hivi: “Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile” (Luka 19:4). Uzuri katika ubaya wa Zakayo ni unyenyekevu. Mheshimiwa Zakayo kwa kupanda mti ili kumwona Yesu anaonesha unyenyekevu unaohitajiwa ili kumwona Yesu. Alipanda mti. Ni jambo la kushangaza ukiniona mimi padre Kamugisha nimepanda mti ili kumwona kiongozi fulani anayepita. Ili ni tendo ambalo hufanywa na watoto. Naye Yesu alimwambia kama mtoto anavyoambiwa:shuka. 
KUSHUKA CHINI NI KUTAMBUA KUWA YESU ANAKUJUA KWA JINA
 Tunasoma hivi, “Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako” (Luka 19:5). Yesu anakujua kwa jina. Alimuita Zakayo kwa jina. “Zakayo shuka upesi.”  Hapo ulipo Yesu anakuona na anakujua kwa jina. Anajua na namba yako ya simu. Yesu hajui tu namba yako ya simu anajua na ujumbe unaoandika na unaotumiwa. Anajua neno la siri lakufungulia kompyuta yako.
KUSHUKA CHINI NI KUTOKUSITASITA KATIKA MASUALA YA WOKOVU
 Kusema nitafanya jambo zuri kesho ni kuwa kwenye mkuyu. Shuka chini. Usiyahirishe ya leo mpaka kesho. Hata kama kuna milima ya vipingamizi. Maji hupita kati ya milima na wewe pia pita kati ya milima. “Kwa muda wa miaka 33 iliyopita, kila asubuhi nimejitazama kwenye kioo nakujiuliza: ‘Kama leo ingekuwa siku ya mwisho ya maisha yangu, ningetaka kufanya ambalo niko karibu kufanya?’ Kila mara jibu langu ambapo limekuwa hapana katika siku nyingi kwenye mstari, najua kuwa lazima nibadili kitu fulani,” alisema Steve Jobs aliyezaliwa mwaka 1955 na kuaga dunia mwaka 2011 mwanzilishi wa kampuni ya Apple. Je, kila unalolifanya leo unajiuliza swali alilojiuliza Steve Jobs. Kusitasita na kuhairisha ni maadui wa kutumia fursa za leo.
 Kuna mtu ambaye alisema: “Kusitasita ni chanzo cha matatizo yangu yote. Hata hivyo sijui vizuri maana ya neno kusitasita kesho nitatazama maana yake kwenye kamusi.” Mtu huyu bado alikuwa na tatizo la kusitasita. Tuna mtu wa kuigwa katika Biblia aliyeitumia vizuri siku iitwayo leo naye ni Zakayo. Yeye alikuwa mfupi wa kimo lakini hakuwa mfupi wa tamaa ya kumwona Yesu, hakuwa mfupi kifedha, hakuwa mfupi kiunyenyekevu maana alipanda mti aweze kumwona Yesu ingawa yeye alikuwa mtu tajiri sana. Alipanda mti wa mkuyu ili aweze kumwona Yesu. Biblia yasema: “Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako” (Luka 19:5). Zakayo alishuka haraka akamkaribisha Yesu kwa furaha. Fursa hiyo aliitumia vizuri. Wakati wa kusulubiwa Yesu ulikuwa karibu na Yesu hakupitia njia hiyo tena. Zakayo angekosa kumkaribisha Yesu angepoteza nafasi adimu. Pia Yesu alimwambia: “Leo wokovu umefika katika nyumba hii” (Luka 19:9). Katika masimulizi haya neno leo limetumika mara mbili. Liwezekanolo leo lisingoje kesho.
“Fursa za leo zinafuta kushindwa kwa jana,” alisema Gene Brown. Zakayo ambaye alikuwa mtoza ushuru aliyekuwa pia tapeli na fisadi alipokutana na Yesu alisema: “Sikiliza Bwana! Mimi nitawapa maskini nusu ya mali yangu, na kama nimenyanganya mtu yeyote kitu, nitamrudhia mara nne (Luka 19: 8). Fursa aliyoipata Zakayo ilifuta makosa mabaya ya jana kwa vile alikuwa tayari kutoa fidia ya asilimia 400. Huwezi kurudi nyuma na kuanza mwanzo mpya lakini leo unaweza kuanza mwisho mpya. Hoja si namna unavyoanza hoja ni namna unavyomaliza. Itumie vizuri leo. Shakaspeare aliandika katika kitabu chake chake kiitwacho Julius Caesar: “Kuna kupwa na kujaa katika maisha ya watu, fursa hiyo inapotumiwa wakati wa mafuriko inakuelekeza kwenye bahati; isipotumiwa safari zote katika bahari ya maisha zinaishia kwenye maji mafupi na matatizo chungu nzima.” Maisha ni fursa itumie. Maisha ni wimbo uimbe. Maisha ni kengele igonge. Maisha ni barabara ipitie. Maisha ni mti upande.
Yesu alimwambia Zakayo: “Leo wokovu umefika katika nyumba hii” (Luka 19:9). Yesu alisema maneno haya kumfariji Zakayo aliyesemwa sana na watu na si kuwajibu wasengenyaji. Leo inaweza kuwa Jumapili ambayo inaitwa siku ya Bwana. Hii ni siku ya imani. Hii ni siku ya wokovu. Unaitumiaje siku ya Jumapi?



Saturday, October 15, 2016

SALI MPAKA UNASALI

                                                        
                                                      Jumapili ya 29 ya Mwaka C
1. Kut 17: 8-13
2. 2 Tim 3: 14-4:2
3. Lk 18: 1-8

                               SALI DAIMA NA KWA MOYO MPAKA USHINDE MAJARIBU
Katika kusali hatupaswi kusali kama watoto watundu na watukutu ambao hubonyeza kengele wafunguliwe mlango na baada ya hapo hukimbia kwenda kubonyeza kengele mlango mwingine. Sali mpaka unasali ni kusali mpaka mlango ufunguliwe. “Tatizo karibu la kila mtu anayesali ni kuwa anasema ‘Amina’ na kukimbia kabla Mungu hajawa na nafasi ya kujibu. Kumsikiliza  Mungu ni muhimu sana kuliko kumpa mawazo yetu,” alisema Frank Laubach. George Muller alipoulizwa juu ya kiasi cha muda anaoutumia kusali alijibu, “Masaa mengi kila siku. Lakini naishi katika moyo was ala. Nasali ninapotembea na ninapolala na ninapoamka. Na majibu kila mara yanakuja.”  Kabla ya kufanya shughuli yoyote Sali. Kwa vile shughuli haziishi utasali daima. "Haitoshi kuanza kusali, haitoshi kusali kwa jinsi inavyopaswa; haitoshi kuendelea kusali kwa muda; lakini lazima tusali kwa uvumilivu, kwa kuamini, mpaka tupate jibu,” alisema George Müller.
Katika Biblia kuna kisa cha mjane ambaye hakuacha kumwomba hakimu ampatie haki yake. Aliomba kwa matumaini ya kusikilizwa. Katika mji mmoja kulikuwa na hakimu asiyemcha Mungu wala kumjali mtu. Na katika mji huo kulikuwa na mama mjane, naye alimwendea tena na tena akisema, ‘Nipatie haki kwa adui yangu.’ Siku nyingi hakutaka, kisha akajiambia, ‘Ingawa simchi Mungu wala simjali mtu, kwa kuwa mjane huyu ananisumbua nitahakikisha amepata haki yake, ama sivyo ataendelea kuja hadi amenichosha.” Bwana akaendelea kusema, “Sikilizeni asemavyo hakimu mbaya. Na Mungu, je, hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku? Je, atakawia kuwasaidia?” Nawaambieni atawapa haki upesi (Luka 18: 1-8).  Mfano unajaribu kumlinganisha Mungu na hakimu mbaya. Kama hakimu mbaya anaweza baadaye kusikiliza kwa vile mjane alivumilia itakuwaje Mungu mwenye huruma. “Bwana wetu baada ya kuongea juu ya majaribu na hatari ambazo zilikuwa zinakuja anaogeza kwa haraka baadaye kidogo tiba yake ambayo ni sala ya daima na itolewayo kwa moyo,” alisema Baba wa Kanisa Theophyl.
SALI MPAKA IMANI ISHINDE
Juu ya maneno “Mwana wa mtu atakapokuja ataikuta imani duniani” Mtakatifu Augustini alikuwa na haya ya kusema: “Bwana wetu aliongeza maneno haya kuonesha kuwa imani  inaposhindwa, sala inakufa. Hivyo ili tusali lazima tuwe na imani na ili imani yetu isishindwe lazima tusali. Imani inamwaga sala na kule kumwaga moyo katika sala kunazaa uthabiti wa imani.”   Kuna baba ambaye alielezea kisa hiki kuwa wakati wa wanafamilia kusali kila mwanafamilia ilibidi kumwombea mtu mmoja. Mtoto wake wa kiume alimwomba Mungu amsaidie rafiki yake kuwa mtu mwema shuleni alikuwa mbaya. Juma lililofuata walipokutana kwa ajili ya sala za familia baba huyo alimuuliza mtoto wake kama atamwombea rafiki yake Eddie tena. “Hapana, nilimuombea Eddie juma lililopita  nab ado ni mbaya.” Kijana huyu alikosa uvumilivu wa mwanamke mjane. Katika somo la kwanza tunaambiwa hivi: “Ikawa, Musa alipoinua mikono yake, Israeli ilishinda. Alipoiacha mikono kushuka, Amaleki ilishinda kwa kuwa mikono ya Musa ilichoka, walitwaa jiwe, wakaliweka chini yake. Akaketi juu yake, Haruni na Huri wakaitegemeza mikono yake, mmoja upande huu, na mwingine upande huo. Na hivi mikono ya Musa haikulegea tena mpaka jua lilipokuchwa. Yoshua akamshinda Amaleki na watu wake kwa makali ya upanga” (Kutoka 17: 11-13).Hapa tunaiona nguvu ya Mungu inayoleta ushindi.
SALI PAPO HAPO SALI SASA
Kusali mpaka unasali ni kusali papo hapo, hakuna kungoja kidogo, hakuna goja kwanza, sio kungoja siku ya pili“Yeye aliyekuokoa amekuonesha ambalo angetaka wewe ufanye. Angetaka uwe mtu wa papo hapo katika sala,” alisema Mtakatifu Yohane Chyrisostom. Ishara ya radi kupiga ikijionesha Sali papo hapo. Ukipata taarifa za msiba muombee marehemu papo hapo. Ukimwambia mtu nitakuombea muombee papo hapo usije ukasahau. Ukiwa na wazo linalokuondoa kwenye sala lifanye liwe sala papo hapo. Mtakatifu Bernard alikuwa amepanda farasi siku moja na huku anasali. Alikutana na maskini omba omba akaanza kuzungumza naye. Maskini alimuuliza Bernard alichokuwa anafanya juu ya farasi wakati anasafiri, na Bernard alisema kuwa alikuwa anasali. “Lakini mara nyingi huwa na mambo yanayonitoa kwenye sala,” alisema Bernard. “Ee, sawa, huwa sina mambo yanayonitoa kwenye sala,” maskini alisema. “Hilo jambo zuri, nitakupa farasi huyu kama unaweza kusema sala ya ‘Baba Yetu’ bila hata mara moja kuwa na mawazo mengine.” “ Ee hilo ni jambo rahisi,” alisema maskini na kuanza kusali, “Baba Yetu uliye mbinguni; jina lako litukuzwe…” Maskini alinyamaza. “Niambie, kiti cha kukalia kitakuwa pamoja na farasi?”
SALI KWA KUTAFAKARI BARAKA UNAZOZIOMBA
Yeye aliyekuokoa amekuonesha ambalo angetaka wewe ufanye. Angetaka uwe mtu wa papo hapo katika sala, angetaka utafakari moyoni baraka unazoziomba, Angetaka uombe na kupokea kile ambacho wema Wake unataka kutoa. Hakatai kutoa baraka zake kwa wale wanaosali,” alisema Mtakatifu Yohane Chyrisostom.
SALI KWA KUSHIRIKIANA NA NEEMA YA MUNGU
Katika jarida la Your Life (Maisha Yako) kuna hadithi juu ya wasichana wawili ambao walikuwa katika hatari ya kuchelewa shuleni. Mmoja alisema, “Tusimame na tusali ili Mungu atusaidie tuweze kufika huko mapema.” Mwingine alisema: “Hapana, tukimbie kwa nguvu zetu zote, na tusali wakati tukikimbia.” Kwa kusali wakati unakimbia unashirikiana na neema ya Mungu.



SALI KAMA KWAMBA KILA KITU KINAMTEGEMEA MUNGU
Baadhi ya watu husema sala na watu wengine husali. Kusali mpaka unasali sio kusema sala. Kusali mpaka unasali ni kuwa na moyo wako kuwa katika sala. “Katika sala ni vizuri zaidi kuwa na moyo bila maneno kuliko kuwa na maneno bila moyo,” alisema John Bunyan. Kusali mpaka unasali ni kumsifu Mungu yeye havimbi kichwa kwa masifu yetu. “Usiogope kumsifu Mungu sana; tofauti na binadamu yeye havimbi kichwa kamwe,” alisema Paul Dibble. Kusali mpaka unasali ni kumshukuru Mungu. George Herbert alisali, “Wewe ambaye umenipa mambo mengi sana, nipe jambo moja zaidi – moyo wenye shukrani.” Sala siyo kumtumia Mungu. Ukifanya hivyo hujasali mpaka umesali. Usipoamini unachokiomba kwamba utakipata hujasali mpaka umesali. “Sala zetu zitajibiwa tutakapoamini katika tunachokiomba,” alisema John Iverson.  Unaposali kwa imani unasali mpaka unasali. “Sala zetu zinasikika mbinguni zikiwiana kwa kiasi kikubwa sana na imani yetu. Imani ndogo itakupatia huruma kubwa , lakini imani kubwa itakupa huruma kubwa zaidi,” alisema Mchungaji Charles H. Spurgeon.
Tunasoma hivi katika Biblia: “Lakini hampati kitu kwa sababu hamwombi. Mnaomba, lakini hampewi kitu kwa sababu mnaomba vibaya, yaani kwa nia ya kushibisha tamaa zenu” (Yakobo 4: 2-3). Mungu anajibu ombi ambalo litamtukuza zaidi. Kuna Wakristo ambao waliishi kama sehemu moja. Wa kwanza alikuwa mkulima na wa pili alikuwa mvuvi. Hapakuwepo na mvua kwa muda wa wiki kadhaa. Mkulima siku moja alienda kanisani kuomba. Aliomba Mungu  afanye mvua inyeshe. Lakini hapakuwepo na mvua. Jirani yake naye alienda kuomba mvua isinyeshe kwa vile alikwa anampeleka rafiki yake kuvua samaki . Mvua haikunyesha siku hiyo. Mungu alisikiliza maombi yote mawili. Lakini alijibu lile ambalo aliona linampa sifa zaidi. Kama ombi lako halimpi Mungu sifa hujasali mpaka umesali.
Mungu anawatumia watu kujibu sala. Licha ya ukweli  mtegemee Mungu  hata kama watu wanachelewa kukupa kile Mungu alichopitisha kwao. Mtoto mdogo alikuwa anasali sala zake za usiku pamoja na mama yake: “Bwana, mbariki mama, mbariki baba na Mungu naomba unipe baisikeli mpya!!!” Mama yake alimwambia, “Mbona unasema kwa sauti ya juu sana maneno ya mwisho, Mungu sio kiziwi.” Mtoto alisema, “Lakini babu aliyeko chumba jirani masikio yake hayasikii vizuri.” Mt. Augustini alisema, “Sali kama kwamba kila kitu kinamtegemea Mungu.” Jiweke mikononi mwa Mungu asilimia 100.
Omba vitu vikubwa toka kwa Mungu. Kumuomba vitu vidogo ni kama kukutana na Bill Gates wa Marekani ukamwomba shilingi elfu mbili, wakati umekutana na bilionea, mwenye pesa kama serikali.
Omba mapenzi ya Mungu yafanyike. “Lengo letu la sala lazima liwe mapenzi ya Mungu, na si mapenzi yetu,” alisema D. Laurence Scupoli katika kitabu chake, The Spiritual Combat (1843). Kuna aliyesema, “Mungu hakupi unachotaka, anakupa unachostahili.” Usimwambie Mungu sikiliza kwa kuwa mtumishi wako anaongea, bali ongea kwa kuwa mtumishi wako anasikiliza. Hapo unasali mpaka unasali.
Ujue kuwa vita ni vya Mungu. “Msiogope, wala kufadhaishwa na umati huu mkubwa, maana hivi si vita vyenu bali vita vya Mungu” (2 Mambo ya Nyakati 20:15). Ukiwa na Mungu wewe ni umati.
FANYA KAZI KAMA KWAMBA KILA KITU KINAKUTEGEMEA WEWE

Mt. Augustini alisema, “Fanya kazi kama kwamba kila kitu kinakutegemea wewe.” Hapo unakuwa umesali mpaka umesali. Mungu anahitaji mchango wako. “Bali sisi tulimwomba dua Mungu wetu…tena tukaweka walinzi mchana na usiku” (Nehemia 4:9). Waliweka walinzi kama kwamba kila kitu kiliwategemea wao. Lakini walimwomba dua Mungu kama kwamba kila kitu kinamtegema Mungu. Sali kwa kushirikiana na neema ya Mungu. Katika jarida la Your Life (Maisha Yako) kuna hadithi juu ya wasichana wawili ambao walikuwa katika hatari ya kuchelewa shuleni. Mmoja alisema, “Tusimame na tusali ili Mungu atusaidie tuweze kufika huko mapema.” Mwingine alisema: “Hapana, tukimbie kwa nguvu zetu zote, na tusali wakati tukikimbia.” Kwa kusali wakati unakimbia unashirikiana na neema ya Mungu. 

Saturday, September 24, 2016

KUTOFANYA LOLOTE NI KOSA

                                            
                                                 Jumapili ya 26 ya Mwaka C
1.       Amo 6: 1a. 4-7
2. 1 Tim 6: 11-16
3.  Lk 16: 19-31

Kuna hadithi ya mtu ambaye aliaga dunia. Huko mbinguni mtume Petro aliangalia kwenye kitabu kikubwa na kusema, sikuona jina lako. Na kama jina lako halionekani utakwenda motoni. Mtu huyo akamjibu Petro, “Kwa nini niende motoni sikufanya lolote.” Petro akasema kwa vile ukufanya lolote, utaenda motoni. Tuogope kosa la kutofanya lolote kama tunavyoogopa ukoma. Mt. Ambrose alikuwa na haya ya kusema: “Si kila aina zote za umaskini ni takatifu, na si kila aina zote za utajiri ni uhalifu.” Umaskini wa roho ni utakatifu. Lazaro alikuwa maskini wa roho. Alichukuliwa mbinguni kwa vile alimtegemea Mungu. Tajiri Dives alifanya kosa la kutofanya lolote. Hakuwa mkarimu. Alikosa mbingu kwa kukosa kuwa mkarimu. Si kila utajiri ni uhalifu. Tajiri Dives hakuwa fisadi.
MAKOSA YA TAJIRI DIVES
Jicho Lisiloona Maskini
Tajiri anayesimuliwa katika injili ya leo tunaweza kumuita Dives neno la kilatini lenye maana ya tajiri. Dives hakumwona Lazaro ingawa alikuwa mlangoni pake. Labda angemwona angemwondoa kwa nguvu. Lipi kosa la Dives? Hakumfukuza Lazaro. Hakumdhuru Lazaro. Hakumwamuru atoke mlangoni. Hakumzuia kula vipande vilivyoanguka kutoka mezani. Kosa lake ni kuwa hakumwona Lazaro. Lile lililompeleka motoni si lile alilolifanya bali lile alilokosa kufanya alikosa kumsaidia masikini Lazaro.
Mwaka 1950 Albert Schweitzer alitajwa kuwa ni “Mtu wa karne.” Mwaka 1952 alitunukiwa nishani ya Amani ya Nobel. Akiwa na umri wa miaka 30, Schweitzer aliamua kuacha kazi ya kucheza kinanda ili awe daktari. Hatimaye alijenga Hospitali Afrika na kuajiri wafanyakazi. Schweitzer alisema hadithi juu ya Lazaro na tajiri iliathiri uamuzi wake wa kuwa daktari mmisionari. Kimantiki aliona kuwa ndugu yake wa kiafrika alikuwa ni Lazaro na yeye alikuwa ni tajiri. “Ningefurahiaje watu kunishangilia wakati Lazaro anateseka na maumivu,” alibainisha Albert Schweitzer aliyekuwa na macho yanayoona masikini. Huyu ni tajiri aliyekuwa na macho yanayoona masikini.
Kosa la Kutofanya Lolote
Tajiri katika Injili ya Luka (16:19-31) hashitakiwi kwa makosa mengine isipokuwa kosa la kutofanya lolote. Mtakatifu Yohane Chrysostom alikuwa na haya ya kusema juu ya kuteswa kwa tajiri motoni: “Aliteswa si kwa sababu alikuwa tajiri bali kwa sababu hakuwa na huruma.” Tajiri ambaye katika mapokeo ya Kanisa Katoliki anaitwa Dives alijiona yeye peke yake hakumwona Lazaro ingawa alikuwa mlangoni pake. Dives alijifungia katika Dives. Hakutoa. Hakuwa mkarimu. “Heri kutoa kuliko kupokea” (Matendo 20: 35). Tajiri Dives angepata heri kwa kutoa kwa maskini Lazaro. Akitoa maoni juu ya mfano huu Mt. Ambrose alizoea kusema: “Unapotoa chochote kwa maskini humpi yule kitu kilicho chako, bali unamrudishia tu kilicho chake, kwani  mali za ulimwengu huu ni mali ya wote, si ya matajiri tu.”
Kosa la Kuvaa Nguo za Gharama Sana
“Palikuwa na mtu tajiri aliyezoea kuvaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi” (Luka 16: 19).   Rangi ya zambarau ilikuwa ni rangi ya vazi la kifalme. Mtakatifu Gregory akitoa maoni juu ya mfano huu alikuwa na haya ya kusema: “Kama kuvaa nguo za zambarau na kitani safi lisingekuwa kosa, neno la Mungu lisengeelezea kwa uangalifu kamwe jambo hili. Hakuna anayetafuta nguo za gharama sana isipokuwa kwa sababu ya majivuno ili aonekane ni mweheshimiwa kuliko wengine;  hakuna anayetamani kuvaa nguo kama hizo isipokuwa kwa sababu kuonwa na wengine.”  Ukawaida ni fadhila ya kukumbatia maishani. Tajiri Dives hakuwa na fadhila hii ya ukawaida.
Changamoto Maishani
Si lazima ujiulize, “je niko tajiri?” bali jiulize “nani anakaa mlangoni pangu akiomba?” Si lazima yule anayeomba mkate. Kuna anayeomba msamaha. Kuna anayeomba neno la upendo. Kuna anayeomba shukrani, labda amepigwa teke kama methali ya kiswahili isemavyo “shukrani ya punda ni teke.” Kuna anayeomba maneno “pole na kazi.” Kuna anayeomba salamu. Ukweli unabaki tuko matajiri wa kutoa haya.
Kuwa na muda nao ni utajiri, “muda ni mali .” Tuwe na jicho linaloona wenye kuhitaji msaada wowote hata wa kisaikolojia. Ni vizuri kutoa tukiwa hai badala ya kungoja kutoa kwa njia ya  wosia. Hadithi ifuatayo inaeleza lile ambalo nataka kutoa kwa njia ya lugha ya picha. Siku moja nguruwe alilalamika mbele ya ng’ombe kuwa: “Licha ya kuwapa binadamu nyama nzuri, bado jina langu wanalitumia kutukana watu wengine wakisema ‘muone mdomo kama nguruwe’ au ‘wewe mchafu kama nguruwe.” Ngombe alimpa angalisho nguruwe, “ Lakini wewe nguruwe unatoa baada ya kufa. Mimi ninawapa watu maziwa nikiwa badohai.” Tutoe tukiwa bado hai.
Kutoa ni moyo vidole huachia. Hesabu ya kutoa kuwasaidia masikini ina mantiki yake ya kuwa tunazidisha kwa kutoa. Ni kweli kutoa kwaleta heri kama alivyosema mwandishi wa kitabu cha matendo ya mitume. Hata harufu nzuri hubaki kwenye mikono ya mtu anayetoa ua la waridi.
Kuna namna tatu za kutoa kama alivyobainisha Robert Rodenmayer: kutoa kwa kinyongo, kutoa kwa sababu ni wajibu, kutoa kwa kushukuru. Anyetoa kwa kinyongo husema, “Nachukia kutoa.” Mtu wa namna hii utoa kidogo, kwa sababu zawadi bila mtoaji si chochote. Anayetoa kama wajibu husema, “Ninapaswa kutoa.” Mtu wa namna hii anatoa zaidi, lakini hamna wimbo katika zawadi yake. Anayetoa kwa kushukuru husema, “Napenda kutoa.” Mtu huyu anatoa kila kitu na anaionesha dunia sura ya Mungu.”
Masikini kamwe wasifananishwe na kisogo kama kisemavyo kitendawili, “Kipo lakini hukioni.” Jibu la kitendawili hiki ni kisogo. Masikini wapo tuwaone, tuwasaidie. Mtakatifu Basil Mkuu (330-379) alituasa hivi: “Wakataa kutoa fedha kwa sababu eti, fedha zako hazitoshi kwa mahitaji yako mwenyewe; lakini huku ulimi wako ukiomba radhi, mkono wako unakuhukumu, kwa maana ile pete ya kidoleni mwako yadhihirisha uongo wako. Nguo zilizo za ziada zingewatosha maskini wangapi? Nawe wathubutu kumwondoa mtu maskini bila kumpa chochote?”



Neno masikini linaweza kuwa na maana nyingi. Masikini ni mtu yeyote mwenye haja dharura. Masikini ni mtu myonge hasiyekuwa na nguvu. Mtu ambaye yuko waya : ameishiwa na fedha. Mtu hasiyekuwa na mbele wala nyuma. Masiki ni mkata  na umasikini ni ukata. Maneno mengine ambayo yanaweza kutumika badala ya neno masikini ni fakiri, fukara, hohehahe na ombaomba.
Kwa hiyo masikini tunao wengi katika jamii zetu. Wanahitaji kusaidiwa. Marehemu Justin Kalikawe mwanamuziki katika wimbo wake “Bashekera Mbalibyezire” (Watu hucheka kwa sauti ya juu palipo vyakula tele) aliouimba katika lugha ya kabila la wahaya wa Tanzania alibainisha kuwa, “Kwenye msiba wa masikini wapo tu wanaukoo.” Kwenye msiba wa tajiri wanakutwa watu wengi ambao si wana ukoo. Alibainisha mwanamuziki huyo aliyeaga dunia katika asubuhi ya maisha yake.
Upendo kwa jirani unatutaka kuuchangamkia msiba hata wa masikini. Kabla ya kuzinyoshea vidole nchi tajiri na suala la kusaidia masikini lazima kwanza tujinyoshee wenyewe tusije tukagundua kuwa vidole vitatu vinatuelekea sisi wakati kidole gumba kinasema Mungu ni shahidi
Utakatifu wa Maskini
Mt. Ambrose alikuwa na haya ya kusema: “Si kila aina zote za umaskini ni takatifu, na si kila aina zote za utajiri ni uhalifu.” Maskini Lazaro hakupelekwa mbinguni kwa vile alikuwa na umaskini wa vitu alipelekwa mbinguni kwa sababu alikuwa na umaskini wa roho. Alimtegemea Mungu. Ukweli huu unabainishwa kutoka katika jina lake Lazaro maana yake: “Mungu ananisaidia.” Naye papa Yohane Paulo II alikuwa na haya ya kusema kwa wote wanaoteseka kama Lazaro:  “Wakati umefika kwa masikini Lazaro aweze kuketi kando ya yule tajiri ashiriki chakula kile kile badala ya kulazimishwa kula makombo yanayoanguka katoka mezani. Umasikini uliopita kiasi huzaa utumiaji nguvu, chuki na aibu.  Na njia ya kuung’olea mbali ni kufanya kazi ya kuleta haki, na hivyo kujenga amani.”
Lazaro Anafarijiwa
Kuna methali ya Yoruba isemayo, “Mtoto akijiingiza katika kulia mama atajiingiza katika kumfariji.” Tunapokuwa tunalia Mungu anatufariji. Tunapokuwa tunalia Bikira Maria Mfariji wa Wenye Uchungu anatufariji. Huko mbinguni kuna kutulizwa na kufarijiwa. Katika mfano wa Tajiri na Lazaro masikini tunaona Lazaro anatulizwa mbinguni. Kufarijiwa ni sifa ya mbinguni.   Tutafakari sifa hii ya mbinguni ya kufariji na kufarijiwa ambayo lazima ianzie duniani. Abrahamu alimwambia Dives aliyekuwa anateseka motoni, “Kumbuka mwanangu kwamba ulipokea mema yako katika maisha, naye Lazaro akapokea mabaya. Sasa lakini, yeye anatulizwa, nawe unateseka.” (Luka 16: 25) Kufarijiwa ni sifa ya maisha ya mbinguni. “Heri walio na huzuni, maana watafarijiwa.” (Mathayo 5: 4) Ni vizuri kufariji na kufarijiwa kuanzia duniani.
UKARIMU WA MBWA
Mbwa walimwonesha ukarimu Lazaro ambao Tajiri hakumwonesha. Walilamba vidonda vyake. Walimpa huduma ambayo wangejipa wao kama wangekuwa wamehumizwa. Mbwa akihumizwa hulamba vidonda vyake mwenyewe.
YESU KRISTO KAMA LAZARO
Mtakatifu Augustino alikuwa na haya ya kusema juu ya som la injili: “Hadithi hii inaweza kueleweka vinginevyo tukichukua Lazaro kumaanisha Bwana wetu; alilala kwenye mlango wa tajiri kwa  sababu alijishusha na kuwasikiliza wayahudi wenye majivuno katika kujishusha kwake katika ulimwilisho; akitamani kushibishwa na makombo yaliyoanguka kutoka meza ya tajiri hii ina maana alitafuta walau matendo madogo ya haki ambayo kwa majivuno yao wasingetumia katika meza yao (yaani mamlaka yao) matendo ya huruma ambayo yalikuwa madogo na bila nidhamu ya uvumilivu katika maisha ya kutenda mema ambayo wakati mwingine waliyatenda kwa bahati mbaya kama makombo mara nyingi yaangukavyo kutoka mezani. Vidonda ni mteso ya Bwana wetu mbwa waliovilamba ni watu wa mataifa, ambao wayahudi waliwaita najisi na licha ya hayo wakiwa na harufu nzuri ya ibada walilonja mateso ya Bwana wetu katika Sakramenti za Mwili na Damu yake duniani  kote.” 
HITIMISHO
Ushindwe wakati umejaribu. Ni methali ya Tanzania. Usipojaribu hautafanikiwa. Kutojaribu au kutofanya lolote ni zaidi ya kosa, ni dhambi. Kujaribu na kushindwa si uvivu. Ni methali ya Sierra Leone. Kuna ambaye alimuomba Mungu amsaidie kushinda bahati nasibu ya kampuni ya simu ya Safaricom. Kila siku mtu huyo alimuomba Mungu, lakini hakufanikiwa. Akiwa amelala aliota ndoto Mungu anamwambia kuwa yeye anataka ashinde lakini anamuomba anunue vocha (Credit card) aweke pesa kwenye simu. Mtu huyu alikuwa hafanyi lolote.

Si kwamba mambo ni magumu ndio maana hatuthubutu kufanya kitu. Ni kwa sababu hatuthubutu kufanya kitu ndio maana mambo ni magumu,” alisema mwanafalsafa wa Kirumi Seneca. Kutothubutu au kutojaribu ni kosa. Kwa kujaribu mara nyingi, tumbili hujifunza kuruka kutoka mtini. Methali hiyo ni busara ya mababu wetu.  “Binadamu hawezi kuvumbua bahari mpya kama hana ujasiri wa kupoteza kule kuona ufukwe,” alisema Andre Gide (1869-1951)mfaransa mwandishi na  mshindi wa zawadi ya Nobel katika fasihi mwaka 1947. Ili kuvumbua bahari mpya lazima uende mbali lazima ufanye kitu. “Mtu ambaye hajiweki katika hali ya hatari, hafanyi lolote, hana chochote, na si chochote na atakuwa si chochote. Anaweza kukwepa mateso na huzuni, lakini hawezi kujifunza na kuhisi na kubadilika na kukua na kupenda na kuishi,” alisema Leo F. Buscaglia (1924-1998). “guru” wa kiamerika mtetezi wa nguvu ya upendo. Kama kila mtu angejitahidi kufanya lolote zuri dunia ingekuwa mahali pazuri pa kukalika.  

Friday, July 29, 2016

HATUTULII TUTATULIA KATIKA MUNGU



            HATUTULII TUTATULIA KATIKA MUNGU
                
                                Jumapili ya 18 ya Mwaka C
                
1. Mhubiri  1:2; 2:21-23
Wokolosai 3:1-5, 9-11
Luka 12:13-21

UTANGULIZI
“Ee Bwana umetuumba kwa ajili yako hatutulii mpaka tutakapotulia katika wewe,” alisema Mtakatifu Augustini wa Hippo Afrika ya Kaskazini. Katika mali hatutulii tutatulia katika Mungu. Katika mapenzi hatutulii tutatulia katika Mungu.Katika mamlaka hatutulii tutatulia katika Mungu. Kuna anayesema nikipata gari nitakuwa nafuraha. Je ni kutokuwa na gari kunakuzuia usiwe na furaha.Kuna anayesema nikipanda cheo nitakuwa na furaha. Je, nikutopanda cheo kunakuzuia kutokuwa na furaha? Ni katika msingi huo Mhubiri anasema Ubatili. Mali bila Mungu ni ubatili. Mamlaka bila Mungu ni ubatili. Mapenzi bila Mungu ni ubatili. Furaha kamili tutaipata katika Mungu.


KATIKA MALI HATUTULII
Kuna mtoto wa miaka saba alikuwa akitafuta michango ya kusaidia watoto wenye shida. Alipofika benki moja huko Tanzania. Meneja wa benki alimwambia kuwa ana sarafu ya shilingi mia mbili na noti ya shilingi mia tano. Achague kati ya sarafu ya mia mbili na noti ya shilingi mia tano. Mtoto huyo alimwambia meneja. “Nitachukua sarafu ya mia mbili lakini hili isipotee, nitaikunja kwenye noti hiyo ya shilingi mia tano.” Mtoto huyo alitaka kuchukua pesa yote. Hatutulii katika pesa. Katika Injili ya Luka 12: 16-20 tunapewa mfano wa mtu aliyemiliki mali lakini mali ilimmiliki. Alikuwa tajiri. Tumpe jina la Dives jina la kilatini maana yake  tajiri. Dives hakufikiria katika msingi wa methali isemayo, “Hakuna mifuko katika sanda.” Hakufikiria katika msingi wa msemo husemao, “sisi ni marehemu watarajiwa.” Mungu alimuita “mpumbavu.” Mpumbavu ni mtu mjinga, jua na zuzu. Biblia ina picha nyingi za mtu mpumbavu: “haifai kwa mpumbavu kuishi kwa anasa” (Methali 19: 10). Tajiri Dives aliishi kwa anasa. “Mpumbavu hudharau mafundisho ya baba yake” (Methali 15: 5). Tajiri Dives alidharau mafundisho ya Mungu Baba yake-Mpende Mungu kwa moyo wako wote, kwa akili zako zote na kwa nguvu zako zote. Hakumpa Mungu kipaumbele. “Mtoto mpumbavu ni huzuni kwa baba yake” (Methali 17: 25). Tajiri Dives alikuwa huzuni kwa Mungu –Baba yake.


Masimulizi hayo ni kama ifuatavyo, “Kulikuwa na tajiri mmoja ambaye shamba lake lilizaa mavuno mengi. Tajiri huyo akafikiri moyoni mwake: ‘Nitafanyaje nami sina mahali pa kuhifadhia mavuno yangu? Nitafanya hivi: nitabomoa ghala zangu na kujenga kubwa zaidi, nami nitahifadhi humo mavuno yangu yote na mali yangu. Hapo nitaweza kuiambia roho yangu: sasa unayo akiba ya matumizi kwa miaka na miaka. Ponda mali, kula, kunywa na kufurahi.” Lakini Mungu akamwambia: ‘Mpumbavu wewe; leo usiku roho yako itachukuliwa. Na vitu vile vyote ulivyojirundikia vitakuwa vya nani?” (Luka 12: 16-20).

Dives alipopata mavuno mengi alikuwa tayari tajiri kama serikali au mwenye pesa kama njugu. Hakuangalia uwezekano mwingine wa kutumia mali yake kama kuendeleza kazi ya Mungu, kusaidia maskini, kuacha zawadi ya watunzi, wateteaji amani. Alifikiria tumbo lake, usingizi wake, anasa zake. Hakumpa Mungu nafasi. Hakumpa jirani nafasi.


Tajiri Dives hakutulia katika mali. Hakumkaribisha Mungu katika maisha yake. Ni katika msingi huo Mhubiri anasema Ubatili. Mali bila Mungu ni ubatili. Mamlaka bila Mungu ni ubatili. Tayari alikuwa tajiri mkubwa sana alipopata mavuno yakutosha. Ebu tuchambue binadamu hasivyotulia katika mali. Mtu akijenga nyumba anajenga na ukuta lakini hatulii. Anaweka vipande vya chupa juu ya ukuta, lakini hatulii. Anaweka nyaya za umeme, lakini hatulii. Anajenga nyumba ndogo ya mlinzi, lakini hatulii. Anaweka kibao chenye maneno yasemayo, “Kuna Mbwa Mkali,” lakini hatulii hata kama mbwa huyo hana meno. Anaweka kibao chenye maneno, “Nyumba hii Inalindwa na Mitambo Maalum.” Lakini hatulii. Anaweka Kamera za kupiga picha lakini hatulii. Mtu mwingine ambaye ana imani katika uchawi anaweka mkia wa mjusi kama kusema, “Nyumba hii inalindwa na mkia wa mjusi.” Ni vizuri kuwa na ulinzi imara bila kuamini katika uchawi, lakini usimsahau Mungu. Mtunga Zaburi anatwaambia, “Mwenyezi-Mungu asipoijenga nyumba,waijengao wanajisumbua bure. Mwenyezi-Mungu asipoulinda mji, waulindao wanakesha bure” (Zaburi 127: 1). 


Tajiri Dives angefikiria kukiachia kizazi kijacho urithi. Lakini hakufanya hivyo. Kilikuwa ni kipindi cha masika yatokanayo na pepo za Monsuni katika Bahari ya Hindi, na mzee aliyekuwa amekula chumvi alikuwa akilima mashimo katika bustani yake. “ Unafanya nini ?” Jirani yake alimuuliza. “Ninapanda miti ya miembe” lilikuwa jibu. “ Unategemea utakula maembe toka katika miembe hiyo ?”“Hapana, sitaishi muda mrefu kwa ajili ya hilo. Lakini wengine watakula. Lakini maisha yangu yote nimekula maembe ambayo yamepandwa na watu wengine. Hii ndiyo njia ya kuonesha shukrani”.


Katika pesa hatutulii. Kuna mtu alienda kwa padre kumwomba padre afanye ibada ya kuzimzika mbwa wake. Padre akasema huwa tunafanya ibada kuzika binadamu na wala sio mbwa. Yule mtu akaondoka akiwa amehuzunika. Baada ya kutembea hatua kadhaa mbele aligeuka nyuma akamwambia huyo padre kama ungefanya ibada ya kumzika mbwa wangu ningekupa $ 1000. Padre huyo akasema, “Kwa nini ukuniambia kuwa mbwa wako ni mkatoliki ningemzika haraka.” Pesa ilimpofusha macho huyo padre hasijue mambo ya kiroho yanayohusu binadamu na wala sio mbwa.



KATIKA MAMLAKA HATUTULII
Napoleoni aliwahi kusema, “Nimejaribu kuvuta watu kwangu kwa kutumia mabavu lakini Yesu amewavuta kwake kwa kutumia upendo.” Watu walikuwa wakimshangilia Kaisari na kusema, “muungu, muungu, muungu.” Upandeni alikaa mtu aliyekuwa akimwambia, “Kumbuka wewe ni binadamu.” Tunapotafuta mamlaka tukumbuke sisi ni binadamu. Hatutulii katika mamlaka tutatulia katika Mungu.

Kuna hadithi juu ya mahali ilipofichwa furaha. Mungu alitaka kuficha furaha. Alijiambia, nikiificha nchi za kigeni watu watafika huko. Nikiificha kenye mamlaka watu watafuta mamlaka wayapate, nikiificha kwenye uzuri watu watajipodoa, nikiificha kwenye biashara watu watafanya biashara waipate, nikiificha kwenye mapenzi watu watafanya mapenzi waipate. Mungu akaificha ndani mwetu. Nenda katika moyo wako. Tunasafiri kwenda Ulaya lakini kuna mabao hawataki kusafiri kwenda katika mioyo kuona kuna nini? Kuna sauti ya Mungu katika moyo wako inayokwaambia kutenda mazuri na kuacha mabaya isikilize nawe utakuwa na furaha. Furaka kamili ni katika Mungu.



HATUTULII KATIKA MAISHA SISI NI MAREHEMU WATARAJIWA
“Utufundishe ufupi wa maisha yetu ili tuweze kuwa na hekima” (Zaburi 90:12). Tajiri anayezungumziwa katika Injili ya leo hakufikiria ufupi wa maisha yake. Vinginevyo angekuwa na hekima akumuacha Mungu aitwe Mungu na kumpa nafasi ya kwanza katika maisha yake. Hadithi inapokuwa tamu au nzuri katika gazeti hukatizwa na chini yake maneno “Itaendelea Toleo Lijalo” huandikwa. “Toleo Lijalo” kwa marehemu ni mbinguni au toharani au motoni. Tajiri aliyekuwa anapanga kufurahia mavuno yake aliambiwa ‘Mpumbavu wewe; leo usiku roho yako itachukuliwa.” Tajiri huyo hakujua kuwa alikuwa marehemu mtarajiwa. Tunasoma hivi katika kitabu cha Ayubu, “Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. Yeye huchanua kama vile ua, kisha hukatwa” (Ayubu 14: 1-2). Kuna kijana aliulizwa, “Baada ya kidato cha nne, nini kitafuata?” Alijibu, “Nitaendelea na masomo kidato cha tano na sita.” “Halafu?” “Nitajiunga na Chuo Kikuu.” Alijibu. “Halafu?” “Nitatafuta ajira?” Alijibu. “Halafu?” “Nitaanza kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.” Alijibu. “Halafu?” “Nitachumbia.” Alijibu. “Halafu?” “Nitafunga ndoa.” Alijibu. “Halafu?””Nitapata watoto.” Alijibu. “Halafu?” “Nitawapa elimu nzuri.” Alijibu. “Halafu?” “Nitastaafu.” Alijibu. “Halafu?” “Nitaanza kula pensheni.” Alijibu. “Halafu?” “Nitazeeka.” Alijibu. “Halafu?” “Halafu halafu…Mungu ataniita.” Alijibu kwa huzuni na kusitasita. “Ni mwanaume gani atakayeishi asione mauti?” (Zaburi 89:48). Niliwahi kuona maneno kwenye kaburi yameandikwa “Jinsi ulivyo ndivyo nilivyokuwa. Jinsi nilivyo ndivyo utakavyokuwa.” Kama ni hivyo tujitahidi kutulia katika Bwana.

Counter

You are visitor since April'08