Saturday, October 29, 2016

SHUKA CHINI



                                                               
                                                    Jumapili ya 31 ya Mwaka C
1. Hekima 11: 22-12:2
2. II Thes: 1: 11-2:2   
3. Lk 19: 1-10

UTANGULIZI
Zakayo ni “ngamia” aliyepitia tundu la sindano. Alikuwa na pesa kama serikali. Alikuwa na pesa kama njugu, lakini alipata wokovu. Alikuwa anacheka kwa nje lakini analia kwa ndani. Zakayo aliyepanda mkuyu alishuka chini. Kupanda mti ni kutoishi uhalisia. Hatuishi mtini. Ni kama umkute tajiri mkubwa duniani kama Bill Gate amepanda mti yuko anatafakari.  Zakayo alikaa kwenye mkuyu akitafakari mada aliyoipenda sana: PESA SABUNI YA ROHO. Zakayo alihesabu vichwa vya watu na kufikiria kama wangelipa kodi angepata cha juu kikubwa. Kuwa na nadharia bila matendo ni kukaa juu kwenye mkuyu. Kama tuna ndoto za kesho bila kuzifanyia kazi leo tunaambiwa kama Zakayo: Shuka toka juu. Wengine wanaopoolewa wanakuwa juu mtini wanafikiri kila siku itakuwa kama siku ya harusi. Shuka toka juu. Yale yanayosemwa siku ya HARUSI yanapitia sikio moja na kuingia sikio jingine. Kwao HARUSI ni sherehe ya ushindi. Ameshinda amempata Bwana huyo. Ameshinda amempata Bibi. Toka juu uje chini. Kuna maisha baada ya harusi. Cha msingi leo isipite bila kuitumia vizuri. Kuna wanaoandaa harusi na hawaandai ndoa hao wako kwenye mti wa mkuyu washuke chini.
 Kulitaja bure jina ni kukaa juu bila kujali uhalisia. Kuwa na mali bila Mungu ni kukaa kwenye mkuyu. Kutoona uzuri katika ubaya wako ni kukaa kwenye mkuyu. Yesu  alimwona Zakayo akaona si mwovu bali ni mkosefu. Aliona upande wa pili wa Zakayo uzuri wake. Zakayo alikuwa mfupi wa kimo. Hakuwa mfupi wa kila kitu. Wakati mwingine hatuoni vizuri watu tunafikiri ni wafupi wa kila kitu. Wengine ni warefu kipesa, warefu kiunyenyekevu, warefu wa kutoa fidia, warefu wa kusaidia maskini.  Kushuka chini ni kutambua uzuri katika ubaya wako.

KUSHUKA CHINI NI NGAMIA KUPITIA TUNDU LA SINDANO
Lakini kwa nini Zakayo? Yesu aliona juhudi za Zakayo za kutamani kumwona. Yesu aliona chanya za Zakayo. Mungu akisema nitakubariki hakuna atakayezuia. Yesu alimbariki Zakayo. Yesu ni jibu. Pengine hatuoni hilo. Tunamwona Zakayo akipitia kwenye tundu la sindano. Zakayo alikuwa tajiri. Wokovu unawajia matajiri pia. “Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri” (Luka 19:2). Zakayo alikuwa mfupi wa kimo lakini ufupi si ugonjwa. Baadaye alipotoa fidia mara nne ya alichochukua anakuwa mrefu kiroho.  Wokovu si kwa ajili ya maskini tu, wokovu ni kwa ajili ya matajiri pia. Mali bila Mungu ni kuishi kwenye mawingu, nadharia, ni kukaa kwenye mkuyu. Lazima kushuka chini. Kama umemsahau Mungu umejisahau. Mchungaji alikuwa anataniana na tajiri ambaye hakuonekana kanisani hata mara moja. Tajiri alimwambia mchungaji: “Jinsi ulivyo mtu wa Mungu ukienda motoni, nitashangaa sana.” Mchungaji  naye alimwambia tajiri: “Wewe usivyokanyaga Kanisani, ukienda mbinguni nitashangaa sana.”  Matajiri kama Zakayo wana uwezekano mkubwa kama maskini kupitia kwenye tundu la sindano. Mtumishi wa Mungu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema, “Watakatifu wengi wametoka katika makazi duni ya maskini, lakini hatuwezi kuendekeza makazi duni ya maskini ili kuwapata watakatifu.” Hatuwezi kuendekeza umaskini ili kuwapata watakatifu. Matajiri wakimtegemea Mungu wakawa na umaskini wa roho wanakuwa watakatifu

KUSHUKA CHINI NI KUTOLITAJA BURE JINA
Zakayo ni neno la Kebr linamaanisha “msafi.” Zakayo alilitaja bure jina lake lenye maana ya msafi. “Pale palikuwa na mtu, jina lake Zakayo” (Luka 19:2). Zakayo alikejeliwa kwa kuitwa msafi. Alikuwa na pesa chafu. Hakuwa msafi. Alitakasa pesa. Alitengwa na jamii kwa vile alikuwa mtu wa kitu kidogo, alichukua cha juu, alikula mlungura. Yesu alitaka jina lake liwe na uhalisia wa mambo: msafi awe na matendo safi, mawazo safi na maneno safi.  Mtoto kumuita baba yake “baba” lakini hamheshimu ni kulitaja bure jina. Kutaja neno “Kanisa” lakini husali wala kutoa sadaka ni kulitaja bure neno “Kanisa.” Shuka chini.

KUSHUKA CHINI NI KUTAMBUA UZURI KATIKA UBAYA WAKO
Anayetembea dhiraa moja kumkaribia Mungu, Mungu anatembea mbili kumkaribia. Ni methali ya Wayahudi. Dhiraa ni kipimo cha mkono mmoja au nusu yadi. Unamtafuta Mungu na Mungu anakutafuta. Mungu anaitafuta mbegu ya uzuri na wema iliyopandwa ndani mwako. Mbegu hiyo ni kitambulisho. Mungu anakutafuta licha ya kasoro zako, kama methali ya Wahaya isemavyo: akupendaye hukupenda na uchafu wako. Sababu kubwa ni ipi? Jibu ni ingawa kuna ubaya katika uzuri lakini kuna uzuri katika ubaya wako.
Masimulizi juu ya Zakayo yanabainisha ukweli huo. Tunasoma hivi. “Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri (Luka 19: 2). Jina Zakayo maana yake asiye na kosa, asiye na hatia, mwadilifu. Alikuwa na jina zuri, ingawa alidharauliwa kwa sababu ya vitendo vya kupokea rushwa au kutoza kitu kidogo. Katika ubaya wake kuna jina lake ambalo ni zuri. Jina la Zakayo lilihusishwa na pesa, Zakayo – mkopeshaji, Zakayo – mla rushwa, Zakayo – mtu wa kitu kidogo, Zakayo – Mtu anayetaka chakula ya watoto, Zakayo mwizi na Zakayo fisadi. Yesu alimuita Mwana wa Abrahamu. Yesu alimuita jina zuri “mwana wa Abrahamu.” Alikuwa mwana wa Abrahamu kiimani. Kama unaitwa Malaya Yesu anakuita “Mwana wa Abrahamu.” “Kama unaitwa pumbavu,” Yesu anakuita “Mwana wa Abrahamu.”  Kuna methali ya Tanzania isemayo, jina baya humwaribia mwenye hilo jina. Kinyume chake ni kweli jina zuri humwokoa mwenye hilo jina. Jina Zakayo lina maana nzuri yaani mwadilifu.
Msitari wa tatu unasema hivi, “Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo” (Luka 19:4). Zakayo alikuwa mfupi wa kimo kimwili na kiroho alikuwa mfupi sababu alikuwa anataka kitu kidogo. Jambo zuri katika ufupi wa kiroho ni kwamba Zakayo alikuwa na tamaa ya kumwona Yesu. Yesu ni mtu muhimu. Tunahesabu kalenda kutoka mwaka Yesu alipozaliwa. Yeye ni kitovu cha historia ya dunia. Watu wanaoenda makanisani ni kwa vile wana tamaa ya kumwona Yesu. Ingawa Zakayo alikuwa mtu mbaya mla rushwa lakini katika ubaya wake palikuwepo na uzuri:tamaa ya kumwona Yesu. Mbegu ya wokovu ilianza kuchipuka ndani mwake kwa vile alitaka kumwona Yesu. Mambo yaliyomzuia kumuona Yesu sio tu wingi wa watu bali wingi wa makosa yake. Kama una makosa tubu na kumgeukia Mungu ili umuone Yesu kwa macho ya imani.
Katika msitari wa nne tunasoma hivi: “Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile” (Luka 19:4). Uzuri katika ubaya wa Zakayo ni unyenyekevu. Mheshimiwa Zakayo kwa kupanda mti ili kumwona Yesu anaonesha unyenyekevu unaohitajiwa ili kumwona Yesu. Alipanda mti. Ni jambo la kushangaza ukiniona mimi padre Kamugisha nimepanda mti ili kumwona kiongozi fulani anayepita. Ili ni tendo ambalo hufanywa na watoto. Naye Yesu alimwambia kama mtoto anavyoambiwa:shuka. 
KUSHUKA CHINI NI KUTAMBUA KUWA YESU ANAKUJUA KWA JINA
 Tunasoma hivi, “Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako” (Luka 19:5). Yesu anakujua kwa jina. Alimuita Zakayo kwa jina. “Zakayo shuka upesi.”  Hapo ulipo Yesu anakuona na anakujua kwa jina. Anajua na namba yako ya simu. Yesu hajui tu namba yako ya simu anajua na ujumbe unaoandika na unaotumiwa. Anajua neno la siri lakufungulia kompyuta yako.
KUSHUKA CHINI NI KUTOKUSITASITA KATIKA MASUALA YA WOKOVU
 Kusema nitafanya jambo zuri kesho ni kuwa kwenye mkuyu. Shuka chini. Usiyahirishe ya leo mpaka kesho. Hata kama kuna milima ya vipingamizi. Maji hupita kati ya milima na wewe pia pita kati ya milima. “Kwa muda wa miaka 33 iliyopita, kila asubuhi nimejitazama kwenye kioo nakujiuliza: ‘Kama leo ingekuwa siku ya mwisho ya maisha yangu, ningetaka kufanya ambalo niko karibu kufanya?’ Kila mara jibu langu ambapo limekuwa hapana katika siku nyingi kwenye mstari, najua kuwa lazima nibadili kitu fulani,” alisema Steve Jobs aliyezaliwa mwaka 1955 na kuaga dunia mwaka 2011 mwanzilishi wa kampuni ya Apple. Je, kila unalolifanya leo unajiuliza swali alilojiuliza Steve Jobs. Kusitasita na kuhairisha ni maadui wa kutumia fursa za leo.
 Kuna mtu ambaye alisema: “Kusitasita ni chanzo cha matatizo yangu yote. Hata hivyo sijui vizuri maana ya neno kusitasita kesho nitatazama maana yake kwenye kamusi.” Mtu huyu bado alikuwa na tatizo la kusitasita. Tuna mtu wa kuigwa katika Biblia aliyeitumia vizuri siku iitwayo leo naye ni Zakayo. Yeye alikuwa mfupi wa kimo lakini hakuwa mfupi wa tamaa ya kumwona Yesu, hakuwa mfupi kifedha, hakuwa mfupi kiunyenyekevu maana alipanda mti aweze kumwona Yesu ingawa yeye alikuwa mtu tajiri sana. Alipanda mti wa mkuyu ili aweze kumwona Yesu. Biblia yasema: “Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako” (Luka 19:5). Zakayo alishuka haraka akamkaribisha Yesu kwa furaha. Fursa hiyo aliitumia vizuri. Wakati wa kusulubiwa Yesu ulikuwa karibu na Yesu hakupitia njia hiyo tena. Zakayo angekosa kumkaribisha Yesu angepoteza nafasi adimu. Pia Yesu alimwambia: “Leo wokovu umefika katika nyumba hii” (Luka 19:9). Katika masimulizi haya neno leo limetumika mara mbili. Liwezekanolo leo lisingoje kesho.
“Fursa za leo zinafuta kushindwa kwa jana,” alisema Gene Brown. Zakayo ambaye alikuwa mtoza ushuru aliyekuwa pia tapeli na fisadi alipokutana na Yesu alisema: “Sikiliza Bwana! Mimi nitawapa maskini nusu ya mali yangu, na kama nimenyanganya mtu yeyote kitu, nitamrudhia mara nne (Luka 19: 8). Fursa aliyoipata Zakayo ilifuta makosa mabaya ya jana kwa vile alikuwa tayari kutoa fidia ya asilimia 400. Huwezi kurudi nyuma na kuanza mwanzo mpya lakini leo unaweza kuanza mwisho mpya. Hoja si namna unavyoanza hoja ni namna unavyomaliza. Itumie vizuri leo. Shakaspeare aliandika katika kitabu chake chake kiitwacho Julius Caesar: “Kuna kupwa na kujaa katika maisha ya watu, fursa hiyo inapotumiwa wakati wa mafuriko inakuelekeza kwenye bahati; isipotumiwa safari zote katika bahari ya maisha zinaishia kwenye maji mafupi na matatizo chungu nzima.” Maisha ni fursa itumie. Maisha ni wimbo uimbe. Maisha ni kengele igonge. Maisha ni barabara ipitie. Maisha ni mti upande.
Yesu alimwambia Zakayo: “Leo wokovu umefika katika nyumba hii” (Luka 19:9). Yesu alisema maneno haya kumfariji Zakayo aliyesemwa sana na watu na si kuwajibu wasengenyaji. Leo inaweza kuwa Jumapili ambayo inaitwa siku ya Bwana. Hii ni siku ya imani. Hii ni siku ya wokovu. Unaitumiaje siku ya Jumapi?



Counter

You are visitor since April'08