Saturday, October 15, 2016

SALI MPAKA UNASALI

                                                        
                                                      Jumapili ya 29 ya Mwaka C
1. Kut 17: 8-13
2. 2 Tim 3: 14-4:2
3. Lk 18: 1-8

                               SALI DAIMA NA KWA MOYO MPAKA USHINDE MAJARIBU
Katika kusali hatupaswi kusali kama watoto watundu na watukutu ambao hubonyeza kengele wafunguliwe mlango na baada ya hapo hukimbia kwenda kubonyeza kengele mlango mwingine. Sali mpaka unasali ni kusali mpaka mlango ufunguliwe. “Tatizo karibu la kila mtu anayesali ni kuwa anasema ‘Amina’ na kukimbia kabla Mungu hajawa na nafasi ya kujibu. Kumsikiliza  Mungu ni muhimu sana kuliko kumpa mawazo yetu,” alisema Frank Laubach. George Muller alipoulizwa juu ya kiasi cha muda anaoutumia kusali alijibu, “Masaa mengi kila siku. Lakini naishi katika moyo was ala. Nasali ninapotembea na ninapolala na ninapoamka. Na majibu kila mara yanakuja.”  Kabla ya kufanya shughuli yoyote Sali. Kwa vile shughuli haziishi utasali daima. "Haitoshi kuanza kusali, haitoshi kusali kwa jinsi inavyopaswa; haitoshi kuendelea kusali kwa muda; lakini lazima tusali kwa uvumilivu, kwa kuamini, mpaka tupate jibu,” alisema George Müller.
Katika Biblia kuna kisa cha mjane ambaye hakuacha kumwomba hakimu ampatie haki yake. Aliomba kwa matumaini ya kusikilizwa. Katika mji mmoja kulikuwa na hakimu asiyemcha Mungu wala kumjali mtu. Na katika mji huo kulikuwa na mama mjane, naye alimwendea tena na tena akisema, ‘Nipatie haki kwa adui yangu.’ Siku nyingi hakutaka, kisha akajiambia, ‘Ingawa simchi Mungu wala simjali mtu, kwa kuwa mjane huyu ananisumbua nitahakikisha amepata haki yake, ama sivyo ataendelea kuja hadi amenichosha.” Bwana akaendelea kusema, “Sikilizeni asemavyo hakimu mbaya. Na Mungu, je, hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku? Je, atakawia kuwasaidia?” Nawaambieni atawapa haki upesi (Luka 18: 1-8).  Mfano unajaribu kumlinganisha Mungu na hakimu mbaya. Kama hakimu mbaya anaweza baadaye kusikiliza kwa vile mjane alivumilia itakuwaje Mungu mwenye huruma. “Bwana wetu baada ya kuongea juu ya majaribu na hatari ambazo zilikuwa zinakuja anaogeza kwa haraka baadaye kidogo tiba yake ambayo ni sala ya daima na itolewayo kwa moyo,” alisema Baba wa Kanisa Theophyl.
SALI MPAKA IMANI ISHINDE
Juu ya maneno “Mwana wa mtu atakapokuja ataikuta imani duniani” Mtakatifu Augustini alikuwa na haya ya kusema: “Bwana wetu aliongeza maneno haya kuonesha kuwa imani  inaposhindwa, sala inakufa. Hivyo ili tusali lazima tuwe na imani na ili imani yetu isishindwe lazima tusali. Imani inamwaga sala na kule kumwaga moyo katika sala kunazaa uthabiti wa imani.”   Kuna baba ambaye alielezea kisa hiki kuwa wakati wa wanafamilia kusali kila mwanafamilia ilibidi kumwombea mtu mmoja. Mtoto wake wa kiume alimwomba Mungu amsaidie rafiki yake kuwa mtu mwema shuleni alikuwa mbaya. Juma lililofuata walipokutana kwa ajili ya sala za familia baba huyo alimuuliza mtoto wake kama atamwombea rafiki yake Eddie tena. “Hapana, nilimuombea Eddie juma lililopita  nab ado ni mbaya.” Kijana huyu alikosa uvumilivu wa mwanamke mjane. Katika somo la kwanza tunaambiwa hivi: “Ikawa, Musa alipoinua mikono yake, Israeli ilishinda. Alipoiacha mikono kushuka, Amaleki ilishinda kwa kuwa mikono ya Musa ilichoka, walitwaa jiwe, wakaliweka chini yake. Akaketi juu yake, Haruni na Huri wakaitegemeza mikono yake, mmoja upande huu, na mwingine upande huo. Na hivi mikono ya Musa haikulegea tena mpaka jua lilipokuchwa. Yoshua akamshinda Amaleki na watu wake kwa makali ya upanga” (Kutoka 17: 11-13).Hapa tunaiona nguvu ya Mungu inayoleta ushindi.
SALI PAPO HAPO SALI SASA
Kusali mpaka unasali ni kusali papo hapo, hakuna kungoja kidogo, hakuna goja kwanza, sio kungoja siku ya pili“Yeye aliyekuokoa amekuonesha ambalo angetaka wewe ufanye. Angetaka uwe mtu wa papo hapo katika sala,” alisema Mtakatifu Yohane Chyrisostom. Ishara ya radi kupiga ikijionesha Sali papo hapo. Ukipata taarifa za msiba muombee marehemu papo hapo. Ukimwambia mtu nitakuombea muombee papo hapo usije ukasahau. Ukiwa na wazo linalokuondoa kwenye sala lifanye liwe sala papo hapo. Mtakatifu Bernard alikuwa amepanda farasi siku moja na huku anasali. Alikutana na maskini omba omba akaanza kuzungumza naye. Maskini alimuuliza Bernard alichokuwa anafanya juu ya farasi wakati anasafiri, na Bernard alisema kuwa alikuwa anasali. “Lakini mara nyingi huwa na mambo yanayonitoa kwenye sala,” alisema Bernard. “Ee, sawa, huwa sina mambo yanayonitoa kwenye sala,” maskini alisema. “Hilo jambo zuri, nitakupa farasi huyu kama unaweza kusema sala ya ‘Baba Yetu’ bila hata mara moja kuwa na mawazo mengine.” “ Ee hilo ni jambo rahisi,” alisema maskini na kuanza kusali, “Baba Yetu uliye mbinguni; jina lako litukuzwe…” Maskini alinyamaza. “Niambie, kiti cha kukalia kitakuwa pamoja na farasi?”
SALI KWA KUTAFAKARI BARAKA UNAZOZIOMBA
Yeye aliyekuokoa amekuonesha ambalo angetaka wewe ufanye. Angetaka uwe mtu wa papo hapo katika sala, angetaka utafakari moyoni baraka unazoziomba, Angetaka uombe na kupokea kile ambacho wema Wake unataka kutoa. Hakatai kutoa baraka zake kwa wale wanaosali,” alisema Mtakatifu Yohane Chyrisostom.
SALI KWA KUSHIRIKIANA NA NEEMA YA MUNGU
Katika jarida la Your Life (Maisha Yako) kuna hadithi juu ya wasichana wawili ambao walikuwa katika hatari ya kuchelewa shuleni. Mmoja alisema, “Tusimame na tusali ili Mungu atusaidie tuweze kufika huko mapema.” Mwingine alisema: “Hapana, tukimbie kwa nguvu zetu zote, na tusali wakati tukikimbia.” Kwa kusali wakati unakimbia unashirikiana na neema ya Mungu.



SALI KAMA KWAMBA KILA KITU KINAMTEGEMEA MUNGU
Baadhi ya watu husema sala na watu wengine husali. Kusali mpaka unasali sio kusema sala. Kusali mpaka unasali ni kuwa na moyo wako kuwa katika sala. “Katika sala ni vizuri zaidi kuwa na moyo bila maneno kuliko kuwa na maneno bila moyo,” alisema John Bunyan. Kusali mpaka unasali ni kumsifu Mungu yeye havimbi kichwa kwa masifu yetu. “Usiogope kumsifu Mungu sana; tofauti na binadamu yeye havimbi kichwa kamwe,” alisema Paul Dibble. Kusali mpaka unasali ni kumshukuru Mungu. George Herbert alisali, “Wewe ambaye umenipa mambo mengi sana, nipe jambo moja zaidi – moyo wenye shukrani.” Sala siyo kumtumia Mungu. Ukifanya hivyo hujasali mpaka umesali. Usipoamini unachokiomba kwamba utakipata hujasali mpaka umesali. “Sala zetu zitajibiwa tutakapoamini katika tunachokiomba,” alisema John Iverson.  Unaposali kwa imani unasali mpaka unasali. “Sala zetu zinasikika mbinguni zikiwiana kwa kiasi kikubwa sana na imani yetu. Imani ndogo itakupatia huruma kubwa , lakini imani kubwa itakupa huruma kubwa zaidi,” alisema Mchungaji Charles H. Spurgeon.
Tunasoma hivi katika Biblia: “Lakini hampati kitu kwa sababu hamwombi. Mnaomba, lakini hampewi kitu kwa sababu mnaomba vibaya, yaani kwa nia ya kushibisha tamaa zenu” (Yakobo 4: 2-3). Mungu anajibu ombi ambalo litamtukuza zaidi. Kuna Wakristo ambao waliishi kama sehemu moja. Wa kwanza alikuwa mkulima na wa pili alikuwa mvuvi. Hapakuwepo na mvua kwa muda wa wiki kadhaa. Mkulima siku moja alienda kanisani kuomba. Aliomba Mungu  afanye mvua inyeshe. Lakini hapakuwepo na mvua. Jirani yake naye alienda kuomba mvua isinyeshe kwa vile alikwa anampeleka rafiki yake kuvua samaki . Mvua haikunyesha siku hiyo. Mungu alisikiliza maombi yote mawili. Lakini alijibu lile ambalo aliona linampa sifa zaidi. Kama ombi lako halimpi Mungu sifa hujasali mpaka umesali.
Mungu anawatumia watu kujibu sala. Licha ya ukweli  mtegemee Mungu  hata kama watu wanachelewa kukupa kile Mungu alichopitisha kwao. Mtoto mdogo alikuwa anasali sala zake za usiku pamoja na mama yake: “Bwana, mbariki mama, mbariki baba na Mungu naomba unipe baisikeli mpya!!!” Mama yake alimwambia, “Mbona unasema kwa sauti ya juu sana maneno ya mwisho, Mungu sio kiziwi.” Mtoto alisema, “Lakini babu aliyeko chumba jirani masikio yake hayasikii vizuri.” Mt. Augustini alisema, “Sali kama kwamba kila kitu kinamtegemea Mungu.” Jiweke mikononi mwa Mungu asilimia 100.
Omba vitu vikubwa toka kwa Mungu. Kumuomba vitu vidogo ni kama kukutana na Bill Gates wa Marekani ukamwomba shilingi elfu mbili, wakati umekutana na bilionea, mwenye pesa kama serikali.
Omba mapenzi ya Mungu yafanyike. “Lengo letu la sala lazima liwe mapenzi ya Mungu, na si mapenzi yetu,” alisema D. Laurence Scupoli katika kitabu chake, The Spiritual Combat (1843). Kuna aliyesema, “Mungu hakupi unachotaka, anakupa unachostahili.” Usimwambie Mungu sikiliza kwa kuwa mtumishi wako anaongea, bali ongea kwa kuwa mtumishi wako anasikiliza. Hapo unasali mpaka unasali.
Ujue kuwa vita ni vya Mungu. “Msiogope, wala kufadhaishwa na umati huu mkubwa, maana hivi si vita vyenu bali vita vya Mungu” (2 Mambo ya Nyakati 20:15). Ukiwa na Mungu wewe ni umati.
FANYA KAZI KAMA KWAMBA KILA KITU KINAKUTEGEMEA WEWE

Mt. Augustini alisema, “Fanya kazi kama kwamba kila kitu kinakutegemea wewe.” Hapo unakuwa umesali mpaka umesali. Mungu anahitaji mchango wako. “Bali sisi tulimwomba dua Mungu wetu…tena tukaweka walinzi mchana na usiku” (Nehemia 4:9). Waliweka walinzi kama kwamba kila kitu kiliwategemea wao. Lakini walimwomba dua Mungu kama kwamba kila kitu kinamtegema Mungu. Sali kwa kushirikiana na neema ya Mungu. Katika jarida la Your Life (Maisha Yako) kuna hadithi juu ya wasichana wawili ambao walikuwa katika hatari ya kuchelewa shuleni. Mmoja alisema, “Tusimame na tusali ili Mungu atusaidie tuweze kufika huko mapema.” Mwingine alisema: “Hapana, tukimbie kwa nguvu zetu zote, na tusali wakati tukikimbia.” Kwa kusali wakati unakimbia unashirikiana na neema ya Mungu. 

Counter

You are visitor since April'08