2017 Julai 16 Jumapili ya 15
“Mpanzi
alikweda kupanda mbegu” (mathayo 13:3)
Alexander Maclaren aliandika: “Mfano wa
mpanzi, ni wa kihistoria na wa kinabii. Unaeleza uzoefu halisi wa Kristo, na unabashiri
juu ya watumishi wake.” Mafanikio au kushindwa, uzuri au ubaya, mpanzi Yesu
Kristo au Mungu wetu, usikate tamaa. Yesu akiwa amejaa neema anaonesha jitihada za kusonga mbele kila mara,
bila kuwa na mawazo ya kukata tamaa. Changamoto kwetu, tunapaswa kuwa kama Baba
yetu wa mbinguni Mpanzi Mkuu. Lazima tuungane nae tuanze kupanda mbengu za injili
zaidi na pasipo kubagua. “Unaposikia maneno, mpanzi alitoka akaenda kupanda
mbegu, usifikirie kwamba ni marudio.
Mpanzi anatoka mara nyingi kwa
malengo mbalimbali; kama kulima, kung’oa
magugu, kutoa miiba au kazi nyingine yoyote, lakini mtu huyo alienda moja kwa
mojakupanda. Ni jambo lilitokea kwa mbegu? Robo tatu ziliharibika, na robo moja
ilibakia; lakini siyo zote kwa namna ile, lakini kwa utofauti fulani, na
alivyopanda nyingine zilianguka njiani” (Mt. Yohane Krisostomu)
Shetani
anatumia mbinu ifuatazo kunyakua kilichopandwa moyoni yaani neno la Mungu. Shetani anatumia mbinu ya kutoona. Mwenye
macho haambiwi tazama. Yaani mtu akiwa na haja na kitu ni juu yake
kukishughulikia. Hauwezi kungoja kuletewa mambo mazuri. “Penye miti hakuna
wajenzi.” Ndivyo isemavyo methali ya Kiswahili. Ni kama watu hawaoni hiyo miti.
Kuna vitu ambavyo vinaweza kumfanya mtu hasione. Mazoea huleta dharau, lakini
mazoea huleta upofu. Tunaambiwa, “Kutazama mtatazama, lakini hamtaona.” (Mathayo
13: 14) Chuki bila sababu au maamuzi mbele yaweza kumfanya mtu hasione mfano
Nathanaeli. “Naye Nathanaeli akamwuliza Filipo, “Je, kitu chema chaweza kutoka
Nazareti?” (Yohane 1: 46) Ukabila unaweza kumfanya mtu asione zuri kutoka
kabila fulani. Ubaguzi wa rangi unaweza kumfanya mtu hasione jambo zuri kutoka
watu wa rangi tofauti na yake, ingawa damu yao wote ni nyekundu.
Mbinu nyingene ya shetani ya kuondoa mbegu iliyopandwa
moyoni ni kuleta shaka au mashaka. Shetani aliwaletea Adamu na Eva mashaka
katika sura ya nyoka kama tunavyosoma katika Biblia. “Basi nyoka
akamwambia huyo mwanamke, “Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, msile matunda ya
miti yote ya bustani?” (Mwanzo 3: 1) Shetani alimletea Yesu mashaka,
“Ikiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe nikate.” (Mathayo 4:
3) Maneno ati, eti na ikiwa ni maneno ya kuonyesha au kueleza shaka au
wasiwasi juu ya jambo. Mashaka
utengeneza milima ambayo imani inaweza kuhamisha. Sala ya mtu mwenye mashaka
iko hivi, “Ee Mungu – kama yupo Mungu kweli okoa roho yangu kama nina roho
kweli.Amina.”
Kuondoa hofu ni mbinu ambayo shetani hutumia kuondoa mbegu
iliyopandwa moyoni. Watu hukimbia kumkwepa nyoka na nyoka hukimbia kukwepa
watu.” Hiyo ni methali ya Yoruba. Inatufunulia juu ya woga na hofu. Shetani
alimuondolea hofu Eva. “Nyoka akamwambia mwanamke, ‘Hakika hamtakufa.” (Mwanzo
3:4) Shetani alipomjaribu Yesu alitaka kumwondolea hofu, “Ukiwa ndiwe
Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, ‘Atakuagiza malaika zake; Na
mikononi mwao watakuchukua; usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.” (Mathayo 4:
6) Shetani alimuondolea hofu kwa kutumia Biblia. Shetani anaweza kukuondolea
hofu kwa kutumia Biblia vibaya. Kuna watu wanaofanya ulevi kuwa halali kwa
kutumia maneno ya Paulo kwa Timotheo, “Usinywe maji tu, bali unywe divai kidogo
kwa ajili ya tumbo lako, kwani unaugua mara kwa mara.” (1 Timotheo 5: 23) Mtume
Paulo wa Tarsus hapingi kunywa divai bali anapendekeza kiasi katika neno
kidogo. Anapinga ulevi. Lakini kifungu hiki kinaweza kutumiwa vibaya kuendekeza
tabia ya ulevi.
Sala: Mpendwa Yesu, ulipanda Neno la Mungu kwa
mapendo, uvumilivu, juhudi na bila kuchoka, nisaidie kukuiga wewe uliye mpanzi
wa Neno la Mungu. Amina.