“asiyepokea msalaba wake akanitafuta, hafai
kwangu.”(Mathayo 10:38)
“Msalaba unamaanisha
hakuna maangamizi ya meli baharini bila matumaini; hakuna giza bila mapambazuko;
hakuna dhoruba bila bandari,” alisema Papa Mt.Yohane Paulo II. “Kwa kuchukua msalaba, haimaanishi kitu kingine
chochote zaidi ya kwamba tunapaswa kupokea na kuteseka kwa sababu ya maumivu, mambo yanayopingana, mateso na kujikatalia
tunavyopitia,” alisema Mtakatifu Francis wa Sales. Inabidi tubebe misalaba yetu
badala ya kuiongelea tu. Tarehe 25 Oktoba 1970 Papa Paul VI aliwatangaza watakatifu mashahidi40 wa Kiingereza.
Alexander Briant alijitengenezea kimsalaba kidogo wakati wa kufungwa kwake jela
na siku ya kuuwawa kwake alikishikilia mikononi mwake wakati wa hukumu ya kifo
inatolewa.Walimyanganya kimsalaba chake, lakini alimwambia jaji: “Unaweza
kukichukua toka mikononi mwangu na si
kutoka moyoni mwangu.” Msalaba juu ya Golgotha hauwezi
kukubadilisha wewe kama si haukusimikwa moyoni mwako.
Msalaba
ni mzigo lakini unabebeka kwa vile ni mzigo mwepesi. “Ukiubeba msalaba ipasvyo,
msalaba utakubeba,” alisema Thomas à Kempis. Watoto ni misalaba lakini
wanabebeka. Mzazi akiwabeba vyema nao baadaye watoto watambeba, akiisha zeeka
hana nguvu watamtunza kama aliwaandalia vizuri maisha ya kesho. Kuna mtoto wa
miaka kumi na miwili alikuwa amembeba mdogo wake wa mwaka mmoja. Alipoulizwa na
jirani kama ni mzito. Mtoto alijibu, “Si mzito kwa vile ni ndugu yangu.” Siku
moja rafiki wa baba aliyekuwa na watoto wanne alimuuliza, “Kwa nini unawapenda
watoto wako?” Baba huyo alifikiria kwa dakika
na kupata jibu moja ambalo angelitumia, “Kwa sababu ni wangu.” Watoto wanapendwa na wanapendeka. Wanabebeka
kwa vile wanapendwa. Nao watoto wanawajibu kama isemavyo, ukibebwa bebeka.
Yesu
alisema, “Mtu akitaka kuwa mfuasi wangu, ajikane mwenyewe, lazima ajitwike
msalaba wake kila siku, anifuate” (Luka 9: 23). “Msalaba unabebwa kwa namna mbili: mwili kwa kujinyima na moyo
unapoguswa na huruma” alisema Mtakatifu Gregori. Mzazi anajinyima mambo
mazuri ya mwili kama kujipamba, mafuta, chakula kizuri, sehemu nzuri ya kukaa
ili mtoto wake asome shule kwa namna hiyo anaubeba msalaba. Mzazi akifikiria
maisha ya mbele anawaonea watoto wake huruma aubeba msalaba. Mungu hakupi msalaba wa kubeba unaozidi uwezo
wako. “Msalaba Mungu anaokutumia ameutathimini kwa macho yake yanayojua yote,
ameuelewa kwa akili yake ya kimungu, ameujaribu na haki yake yenye hekima, umeupa
joto kwa mikono yake ya upendo, ameupima kwa mikono yake kujua kuwa haupitilizi
ukubwa hata kwa inchi moja na haupitilizi uzito hata kwa ratili moja, “ alisema
Mtakatifu Francis de Sales. Wajibu ni msalaba lakini unabebeka: wajibu wako kwa
umma, kwa familia, kwa Mungu na kwako wewe ni msalaba lakini unabebeka.
Msalaba
unabebwa kila siku. Lakini si kila siku
ni kila saa. “Na sisi, kwa nini tumo hatarini kila saa? Siku kwa siku nipo
taabani” (1 Wakorintho 15:30-31). Inavyoonekana ni jambo gumu kufa kila siku
kuliko kufa mara moja. Ina maana kila mara unatoa sadaka ya kitu fulani iwe
hata muda wako kwa ajili ya wengine. Mfanyakazi ofisini anabeba msalaba wake wa
kazi kila saa. Anaporudi nyumbani kama ana wazazi wa kuwatimizia aja zao
anafanya hivyo, kama ana mwenzi wa ndoa anamjali, kama ana watoto anasikiliza
shida zao. Ni kila siku karibu ni kila saa kuubeba msalaba.
Sala:
Ee Bwana wetu Yesu Kristo nisaidie ili hamasa na nguvu zangu
vitoke kwenye kujikatalia na msalaba. Amina.