JUMAPILI YA 1 YA KWARESIMA MWAKA A
1. Mwanzo 2: 7-9, 3: 1-7
|
2. Warumi 5: 12-19
|
3. Mt. 4: 1-11
|
UTANGULIZI
Ukiwa pamoja na Yesu hakuna kushindwa. Ukiwa pamoja na
shetani hakuna kushinda. Shetani hana meno ya kuuma. Lakini Shetani ni
mjanja. Ni mwerevu. Ni mdanganyifu. Ni mwenye kuahadaa. Ni mwenye ghiliba. Ni
mwenye hila. Ni muongo. Ni mwasi. Ni mwovu. Ni adui. Ni Baba wa uongo. Lakini
UKWELI ni ngao dhidi ya uongo wa shetani. Ni baba wa njia za mkato ambazo
zinageuka na kuwa njia ndefu. Ni vizuri kujua ukweli huu, “Shetani ana uwezo wa kupendekeza jambo baya lakini hakupewa uwezo wa
kukulazimisha kulitenda” (Mt.
Cyril wa Yerusalemu.” Shetani
alipendekeza mambo mbalimbali kwa Yesu lakini hakushinda.
Hadithi: Kuna mtoto aliyekuwa anawatupia watu Kanisani mawe
madogo sana – changarawe padre alipomwagalia yeye alisema, padre endelea na
mahubiri yako mimi nakusaidia watu wasisinzie. Shetani anaweza kupendekeza uje
Kanisani lakini anaweza kukwambia sinzia kidogo.
SHETANI YUPO
Shetani wa mtu ni mtu.
Methali hiyo inatumiwa na watu kuonyesha kuwa shetani hayupo. Mbaya wa binadamu
ni binadamu mwenziwe. Je shetani yupo? Jorge Kardinali Medina alijibu swali hilo tarehe 26 Januari
1999, “Yeyote anayesema shetani hayupo sio muumini tena.” Shetani yupo ingawa
hatumuoni. Kuna vitu maishani ambavyo vipo ingawa hatuvioni. Mfano, microwave
(wimbi maikro), ultravioletrays (miali isiyoonekana kwa jicho), upepo upo
lakini hatuoni. Ingawa shetani yupo lakini ni mfungwa. Mt.
Augustini anamlinganisha shetani kama mbwa aliyefungwa kwenye myororo anaweza kukuhumiza
ikiwa utamkaribia. Lakini kuna ambao wanamuona shetani kila mahali. Wakisikia
paka anato sauti isiyo ya kawaida wanasema, huyo ni shetani maana sauti hiyo
siyo ya kawaida.
SHETANI NI MJANJA
Shetani ni
mjanja. Ni mwerevu. Ni mdanganyifu. Ni mwenye kuahadaa. Ni mwenye ghiliba. Ni
mwenye hila. Ni muongo. Ni mwasi. Ni mwovu. Ni adui. Ni Baba wa uongo. Ni baba
wa njia za mkato ambazo zinageuka na kuwa njia ndefu. “Shetani ana uwezo wa kupendekeza jambo baya lakini hakupewa uwezo wa
kukulazimisha kulitenda.” (Mt.
Cyril wa Yerusalemu.”
Shetani ni
mpenda giza.
Lakini, JIBU LA GIZA NI MWANGA. Ukiwa na dhambi moyoni
mwako unakuwa na giza.
Shetani anapenda hilo giza. Ukiileta dhambi hiyo kwenye mwanga
katika sakramenti ya kitubio unamfukuza shetani. Dhambi ni mali ya shetani. Ananusa palipo na
dhambi na kuelekea huko. Ni kama kwenye chumba chako ukiwa na uchafu, mende
watafurika huko maana una mali
zao yaani uchafu.
UJANJA
WA SHETANI
1.
PENDEKEZA SHUGHULI NYINGI
Shetani anaweza kukushawishi ili uwe na shughuli nyingi ili
usishughulikie jambo lilo muhimu. Eva alikuwa msaidizi wa Adamu na Adamu
msaidizi wa Eva katika raha na shida katika magonjwa na afya. Lakini Eva
alipokuwa anajaribiwa na Adamu, Adamu alikuwa na shughuli nyingi hakuwa pamoja
na Eva. Pengine shughuli nyingi zinaweza kuwa namna ya uvivu. Nina shughuli
nyingi sitaenda Kanisani. Hapo kuna uvivu wa kwenda Kanisani.
2.
KUTIA MASHAKA
Shaka ni
wasiwasi. Ni babahiko. Ni tuhuma. Ni hangaiko. KUTIA MASHAKA ni mbinu
anayotumia shetani. Shetani kwa mbinu hii anakubabahisha. Anakuletea wasiwasi,
tuhuma na mahangaiko. Anakuweka katika njia panda. Anakuweka katikati ya mambo
mawili. Unaanza kujiuliza, “Niteme! Nikitema natema utamu. Nimeze! Nikimeza
nameza moto.” Shetani anawaletea mashaka wanaojua ukweli wa mambo. Shetani alimletea mashaka Eva si kwamba
alikuwa hajui ukweli wa mambo: “Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, msile
matunda ya miti yote ya bustani?” Neno “ati,” linadokeza mashaka.
Shetani
alimletea Yesu mashaka, “Ikiwa ndiwe
Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe nikate,” ikiwa ndiwe mwana wa Mungu
jitupe chini.” Neno “ikiwa,” linadokeza
mashaka. Padre alijibu simu, “Leta Katoni
sita za whisky, nyumbani kwangu.” Padre alielewa sauti hiyo kuwa ni ya Mkristu
wake. Alimjibu, “Mimi ni paroko wako.” Alitegemea Mkristu huyo aombe msamaha,
badala yake Mkristu huyo alijibu, “Unafanya nini kwenye stoo ya pombe.”
Shetani anaweza
kukuletea mashaka wakati wa msiba na matatizo. Kama Mungu anakupenda kweli,
kwanini amemchukua mke wako? Kama Mungu anakupenda kweli kwanini amemchukua mme
wako? Kama Mungu anakupenda kwa nini umepatwa na maradhi ambayo yanakufanya
usitoke kitandani kutwa kucha?
3.
KUONDOA HOFU
Kuondoa hofu ni mbinu ambayo shetani hutumia
kuondoa mbegu iliyopandwa moyoni. Watu hukimbia kumkwepa nyoka na nyoka
hukimbia kukwepa watu.” Hiyo ni methali ya Yoruba. Inatufunulia juu ya woga na
hofu. Shetani alimuondolea hofu Eva. “Nyoka akamwambia mwanamke, ‘Hakika
hamtakufa.” (Mwanzo 3:4) Shetani alipomjaribu Yesu alitaka kumwondolea
hofu, “Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa,
‘Atakuagiza malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; usije ukajikwaa mguu
wako katika jiwe.” (Mathayo 4: 6) Shetani alimuondolea hofu kwa kutumia Biblia.
Shetani anaweza kukuondolea hofu kwa kutumia Biblia vibaya. Kuna watu
wanaofanya ulevi kuwa halali kwa kutumia maneno ya Paulo kwa Timotheo, “Usinywe
maji tu, bali unywe divai kidogo kwa ajili ya tumbo lako, kwani unaugua mara
kwa mara.” (1 Timotheo 5: 23) Mtume Paulo wa Tarsus hapingi kunywa divai bali anapendekeza
kiasi katika neno kidogo. Anapinga ulevi. Lakini kifungu hiki kinaweza kutumiwa
vibaya kuendekeza tabia ya ulevi.
Shetani anaweza kukuondolea hofu na ukasikia
sauti kwenye moyo wako inakwambia, “Ukiiba hautakamatwa.” Lakini za mwizi ni
arobaini. Unaweza kusikia sauti inakwambia moyoni, “Kumtazama mwanamke kwa
kumtamani sio shida.” Lakini safari ndefu huanza kwa hatua moja. Yesu alisema,
“...atakayemtazama mwanamke kwa kumtamani, amekwisha zini naye moyoni mwake.”
(Mathayo 5: 28) Shida sio kutazama. Shida ni mawazo unayojenga baada ya
kutazama. Maana makosa huanza kwanza na kuwaza baadaye ni kutekeleza. Kuna mtu
aliyemwambia mwenzake, “Nilipomuona mwanamke huyo nilitenda dhambi za mawazo.”
Rafiki yake akauliza, “Kwani uliyafurahia mawazo hayo.” Mtu huyo akajibu,
“Sikuyafurahia bali yalinifurahisha.” Mawazo ya kutenda kinyume na matakwa ya
Mungu kama yanakufurahisha ina maana
unayafurahia na hapo ni mwanzo wa kupiga mbizi katika bahari ya ubaya na uovu.
Askofu Cyril (315-387) aliyekuwa Askofu wa Yerusalemu mwaka 349 alikuwa
na haya ya kusema, “Shetani ana uwezo wa kupendekeza jambo baya lakini hakupewa
uwezo wa kukulazimisha kulitenda.” Shetani akipendekeza uue hakulazimishi
kuua. Shetani akipendekeza uibe hakulazimishi uibe. Shetani akipendekeza useme
uongo hakulazimishi kusema uongo. Lakini ujue kuwa ukiwa pamoja na Yesu hakuna
kushindwa. Ukiwa pamoja na shetani hakuna kushinda.
4.
TOA AHADI
Aliwapa ahadi
Adamu na Eva, “Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo,
mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu,
mkijua mema na mabaya.” Shetani alimpa ahadi Yesu, “Kisha Ibilisi akamchukua
mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake,
akamwambia, “Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia.”
Ahadi ni deni.
Ni kweli lakini Shetani hutoa ahadi hewa. Aliwapa ahadi Adamu na Eva, “Mungu
anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi
mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”
Shetani alimpa ahadi Yesu, “Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno,
akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake, akamwambia, “Haya yote
nitakupa, ukianguka kunisujudia.”
“ Lakini nyinyi, watoto, ni
wake Mungu na mmekwisha washinda hao manabii wa uongo; maana Roho aliye ndani
yenu ana nguvu kuliko roho aliye ndani ya hao walio wa ulimwengu.” (1 Yohane
4:4)
Kutoa ahadi ya
uongo ni kuhujumu ukweli. Ni kuhujumu sera ya Mungu sera ya ukweli. Tukumbuke
kuwa DINI NI BIMA KATIKA DUNIA HII DHIDI
YA MOTO WA
MILELE AMBAPO SERA NZURI NI KUWA MKWELI.
5.
VUTA KWINGINE
Shetani anaweza
kukuvuta kwingine. Anakutoa kwenye barabara kuu. PITIA BARABARA KUU MCHEPUKO SI
DILI. Yesu alianza kuwafundisha wanafunzi wake kwamba ni lazima Mwana wa Mtu
apatwe na mateso mengi na kukataliwa na wazee na makuhani wakuu na waalimu wa
sheria. Kwamba atauawa, na baada ya siku tatu atafufuka. Yesu aliwaambia jambo hilo waziwazi. Hapo,
Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea. Lakini Yesu akageuka, akawatatazama
wanafunzi wake, akamkemea Petro akisema, ‘Ondoka mbele yangu Shetani! Mawazo
yako si ya kimungu ila ni ya kibinadamu.” (Marko 8: 31 – 33) Hapana tuonaona
nguvu ya HAPANA. Muite Yesu. “Naye Mungu
aliye chanzo cha amani hatakawia kumponda Shetani chini ya miguu yenu.” (Warumi
16:20)
6.
KUKATISHA TAMAA
Mtu aliyekata tamaa hamlii Mungu. Haombi. Yuda Iskarioti alikata tamaa. Hakuomba msamaha. Hakutoa machozi ya
toba kama Petro. Shetani anapambana dhidi ya
MATUMAINI.
7.
KUNGOJA KESHO
Shetani anatumia
mbinu ya kuhairisha mambo. Anaweza kukushawishi uende Kanisani lakini ikifikia
suala la kutekeleza anakwambia ngoja kidogo.
8.
FANYA BUBU
Mungu wetu sio kiziwi labda kama
midomo yetu imekuwa bubu. Mbwa mwitu akitaka kumuua
kondoo anamkaba koo kwenye shingo hasitoe sauti kumwita Bwana wake. Shetani
akitaka kutumaliza anahakikisha hatutoi sauti. Anakuzuia kusali. Shetani
aliwazuia Adamu na Eva wasimlilie Mungu na kuomba msaada wake. Wakati wa
ubatizo Padre humgusa mtoto masikio na kinywa kwa kidole gumba, akisema: “Bwana
Yesu aliyewafanya viziwi wasikie, na bubu waseme, akujalie uweze kusikia kwa
masikio neno lake, na kuungama kwa mdomo imani ya kikristu, kwa sifa na utukufu
wa Mungu Baba. Amina.”
Adamu na Eva
hawakuwa macho pia midomo yao ilifanywa bubu na shetani. Mtakatifu Petro
anatuasa, “Mwe macho; kesheni! Maana
adui yenu, Ibilisi, huzungukazunguka kama
samba angurumaye akitafuta mawindo. Mwe imara katika imani na kumpinga.” (1
Petro 5:8-9) Kuwa imara katika imani kunahitaji kuinua mioyo juu na
kumuomba Mungu atusaidie. Kwa kawaida
mateso hutazama nyuma, wasiwasi huangalia pande zote, na imani hutazama juu.
Katika taabu hatuna budi kufikiri kama Mtunga zaburi aliyesema, “Ee Bwana,
nakuinulia nafsi yangu, ee Mungu wangu, nimetumaini wewe, nisiaibike, adui
zangu wasifurahi kwa kunishinda.” (Zaburi 25:1). Mtunga zaburi anajua atazame
upande upi-upande wa juu.
HITIMISHO
Ushindi wa Yesu dhidi ya Shetani unatupa
ukweli kuwa kushinda vishawishi kunawezekana. Yesu ni mwasisi wa ubinadamu
mpya. Yesu ni mwasisi wa ushindi (Mwanzo 3:15).