Saturday, May 17, 2014

KUULIZA SI UJINGA



                                                
                                                  JUMAPILI YA TANO YA PASKA
Mtume wa Yesu Thomasi alimuuliza Yesu: “Bwana, hata uendako hatujui; basi, twaijuaje njia?” (Yohane 14: 5).
Anayeuliza njia hatakosa njia. Ni methali ya Kiswahili. Kuuliza ni msingi wa kujua. Kuuliza ni msingi wa hekima. “Ufunguo wa kwanza wa hekima ni kuuliza kwa uangalifu na mara nyingi …kwa kuwa na mashaka unauliza na kwa kuuliza unafikia ukweli,” alisema Peter Abelard mwanafalsafa wa Kifaransa (1079 – 1142). Kuna mtoto aliyemuuliza maswali mengi baba yake kama: Baba lami inatengenezwa na nini? Baba kwa nini Mungu ameficha madini mbali sana? Baba kiberiti kinatengenezwaje? Baba mimi nilitoka wapi na namna gani? Baba yake akamwambia mtoto mimi ningewasumbua wazazi wangu kwa maswali mengi kama haya ingekuwaje? Mtoto akamjibu: “Ungepata majibu ya kunijibu.”  “Mtoto anaweza kuuliza maswali elfu moja ambayo mtu mwenye busara sana hawezi kujibu,” alisema Jacob Abbott. Nakubaliana na Charles Proteus Steinmetz aliyesema: “Hakuna mtu yeyote anageuka mpumbavu isipokuwa akiacha kuuliza maswali.” Huyu alikuwa mwamerika mwenye asili ya Kijerumani (1865 – 1923).
Mtume wa Yesu Thomasi alimuuliza Yesu: “Bwana, hata uendako hatujui; basi, twaijuaje njia?” (Yohane 14: 5). “Kuuliza si upumbavu ni tamaa ya kusikiliza yote vizuri kabisa.” Ni methali ya Kilozi. Mtume Thomasi Msimamizi wa Watafiti alikuwa na tamaa ya kusikiliza vizuri. Yesu alimjibu: Mimi ni Njia Ukweli na Uzima.  Wahaya wa Tanzania wana methali isemayo: Kuulizia njia wakati umekanyaga kwenye njia hiyo. Thomasi alipoulizia njia alikuwa kwenye njia ya Yesu. Wanafunzi wa Yesu walijulikana kama Wanafunzi wa Njia. Yesu alisema kuwa yeye ni Njia. Swali la Mtume Thomasi lilikuwa swali la msingi. Methali ya Kiswahili inasema yote: Usiende bila kuuliza. Mtume Thomasi alijua kama isemavyo methali ya Uganda: Kuuliza ni kujua. “Ukitaka jibu lenye hekima, lazima kuuliza swali lenye maana,” alisema Johann von Goethe. Thomasi aliuliza swali lenye maana na alipata jibu lenye hekima.
Wayahudi ni watu waliongolea sana njia. Katika Biblia tunasoma maneno kama haya: Njia za Mungu si njia zetu. “Patakuwepo na barabara kuu, nayo itaitwa njia takatifu: wasio safi hawataruhusiwa pale” (Isaya 35:8). Njia inaweza kumaniisha falsafa au mtazamo mfano Njia za Mungu si njia zetu. Falsafa ya Yesu ni Ijumaa Kuu kwanza Jumapili ya Paska baadaye au dhiki kwanza faraja baadaye. Yesu yeye ni njia kwa maana hii. Fikiria huko nchi ya ugenini. Unaulizia njia. Mtu anakwambia. Chukua barabara ndogo upande wa kulia utakayokutana nayo. Ukifika kwenye makutano ya barabara panda kushoto. Nenda moja kwa moja. Utaona Kanisa upande wa kulia. Pita hapo. Usitoke barabara hiyo. Hesabu barabara ndogo nne upande wa kushoto. Barabara ya tano ndipo penyewe upande wa kulia kwake. Lakini fikiria huyo mtu uliyemuuliza anakwambia nitakupeleka mimi mwenyewe. Yesu hakutoa ushauri na maelekezo. Anatuongoza yeye mwenyewe. Hatumwambii tu juu ya njia yeye mwenyewe ni njia.
“Jambo muhimu ni kutoacha kuuliza,” alisema Albert Einstein. Mitume hawakuacha kumuuliza Yesu. Baada ya Thomasi kuuliza swali hilo Philipo naye aliuuliza: “Bwana, utuoneshe Baba, yatutosha.” Philipo alitaka kumuona Mungu kwa macho ya akili yaani kumwelewa. Mazoea ambayo huleta dharau labda yalimfanya kuuliza swali la namna hiyo. Matendo ya Yesu yalikuwa ya kimungu kama: kutembea juu ya maji, kufufua wafu, kukemea upepo na ukamtii, kuponya wagonjwa kwa neno tu, na kusamehe dhambi. Kama tunataka kumjua Mungu hatuhitaji kuifikiria njia yetu kwa mzunguko au kutumia muda mwingi katika utafiti wa pekee. Tunachohitaji kufanya ni kumwangalia Kristo, kuona alichokifanya, kusikiliza kile alichofundisha, kuangalia alivyotenda, kuangalia jinsi alivyopenda, kuangalia ni nani aliyempendelea, nani alishirikiana naye na kwa sababu gani, nani na pamoja na nani alikula chakula chake, ni nani aliyemkaripia au kumtetea, kwa sababu yeye ni sura ya kibinadamu ya Mungu. Kuna aliyesema hivi: “Mungu atajibu maswali yetu yote kwa njia moja na njia moja tu – kwa kuitaja, kutuonesha zaidi kuhusu Mwana Wake.” Mwana wake ni Yesu.
Ni katika kuuliza mambo mengi yamevumbuliwa. “Katika mambo yote, biashara na shughuli binafsi, ni jambo lenye tija kwa sasa na baadaye kutundika alama kubwa ya kuuliza kwenye mambo ambayo umeyachukulia kuwa ni ya kweli,” alisema Bertrand Russell. Kuuliza si ujinga ni kutaka kujua. “Lugha ilivumbuliwa ili kuuliza maswali. Majibu yanaweza kuwa minongono au ishara, lakini maswali lazima yaulizwe kwa sauti. Ubinadamu ulikomaa pale ambapo mtu aliuliza swali la kwanza. Kudumaa kijamii hakutokani na kukosekana kwa majibu bali kutukuwepo na msukumo wa kuuliza maswali,” alisema Eric Hoffer.Ukweli unabaki. Kuuliza si ujinga.
MASWALI NI NUSU YA MAJIBU
 “Anayeuliza mengi, atajifunza mengi, na kubaki na mengi,” alisema Francis Bacon (1561 – 1626) mwanafalsafa wa Uingereza. Methali ya Kiswahili inayapa uzito maneno ya mwanafalsafa huyo: Kuuliza si ujinga. Kuuliza swali hakumaanishi mwulizaji ni mjinga bali huonyesha kuwa angetaka kujielimisha au kujifahamisha. Ukiuliza maswali unajua mengi. Baba alimwambia mtoto wake wa miaka mitano. Wewe ni mtoto wa ajabu katika kuuliza maswali mengi. Sijui ingekuwaje kama mimi ningeuuliza maswali mengi nikiwa mtoto. Mtoto akamjibu: ungepata majibu ya kujibu baadhi ya maswali yangu. Maswali yanaweza kukusaidia kumpima mtu anayeuliza. Ni katika msingi huu Voltaire (1694 – 1778) mwandishi wa Kifaransa na mwanahistoria alisema: “Wahukumu watu kwa maswali yao, badala ya majibu yao.” Kadiri ya mwandishi huyu unaweza kugundua mjinga. “Atakuwa ni mjinga sana kwa vile anajibu kila swali analoulizwa,” alisema Voltaire.
Yesu akiwa na umri wa miaka kumi na miwili alikuwa na ufahamu wa kushangaza. Ufahamu huo ulionekana katika kuwauliza walimu wa sheria maswali. Tunasoma hivi: “Ikawa baada ya siku tatu, walimkuta hekaluni, ameketi kati ya walimu akiwasikiliza na kuwauliza maswali; nao wote waliomsikia walistaajabia ufahamu wake na majibu yake” (Luka 2:46).  Bila shaka Bwana Yesu aliuliza maswali sahihi kupata majibu sahihi. Ni kweli “ufundi na sayansi ya kuuliza maswali ni chanzo cha ujuzi  wote,” kama alivyosemaThomas Berger. Lazima katika maisha hujioji maswali mbalimbali juu ya maendeleo yako kama: Je una mtazamo chanya au hasi? Je unashindwa kupanga au unapanga kushindwa? Je umetoka wapi? Uko wapi? Unakwenda wapi? Pilipili usiyokula kwa nini inakuwasha? Je unatembea barabara kuu ya wito wako au uko kwenye mchepuko au vichochoroni? Kwa nini uliumbwa? Yaliyopita si ndwele kwa nini unaishi katika wakati uliopita? Je ya wengine sebuleni ya kwako moyoni?
Zig Ziglar aliyekuwa na ufundi mkubwa wa kutia watu moyo aliweka katika maandishi maswali kama haya: “Je unajiandalia ya kesho au unaingoja kesho? Je unajua zaidi kuhusu kazi yako, familia yako, na kuhusu wewe leo kuliko ilivyokuwa jana? Ni habari gani mpya au ufundi gani mpya umejifunza? Je unaiacha kesho itokee tu, au unachukua hatua kesho iwe unavyotaka iwe? Je unaacha jana ikufundishe au ikushinde? Je unajua kuwa mtu mwingine ana maoni mengine na yanaweza kuwa sahihi?” Alihitimisha kwa kusema: “Maswali ni majibu kweli, na ukiuliza ya kutosha nay a kweli, utaishia kwa mtu wa furaha zaidi, mwenye afya zaidi..” Ingawa anayaona maswali ni majibu, mimi nayaona maswali ni nusu ya majibu. Ni kama barua ilivyo nusu ya kuonana. Kuelewa swali ni kama nusu ya jibu. Kuuliza swali sahihi unaweza kupata jibu sahihi. Uwe kama  Anne Rice aliyesema: “Kila mara ninatazama kila mara ninauliza maswali.”  Kuuliza swali sahihi ni jambo la msingi. “Mwanasayansi sio mtu anayetoa majibu sahihi, bali ni yule anauliza maswali sahihi,” alisema Claude Lévi-Strauss. Alikazia umuhimu wa kuuliza maswali sahihi.
Sio kila swali linakuwa na matokeo mazuri. Inategemea ni swali la namna gani.  Mwanamke fulani alimwambia mme wake: haunipendi tena, maana unapoona ninalia hauniulizi kwa nini ninalia. Samahani sana maswali haya yamenifanya nitoe pesa nyingi katika kuyajibu.




Counter

You are visitor since April'08