Saturday, May 24, 2014

MWISHO WA MATUMAINI NA MATUMAINI YASIYO NA MWISHO



                
                                                             JUMAPILI YA 6 YA PASKA
1. Mdo 8: 5-8, 14 -17
2. 1 Pet 3: 15-18
3. Yn 14: 15-21

“Mwe tayari sikuzote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu” (1 Pet 3: 15).
Kuna aliyekuwa anagonga jiwe kwa nyundo ili alivunje vipande vipande. Aligonga mara mia moja jiwe halikunjika akakata tamaa. Mwenzake waliyekuwa wanafanya kazi hiyo pamoja alikuja na kugonga jiwe mara moja liwe lilivunjika. Iliitajika mara ya mia na moja jiwe livunjike lakini mgongaji wa kwanza alikata tamaa. Kukata tamaa ni mwisho wa matumaini. Mtume Petro anatutaka tuikie wito huu: “Mwe tayari sikuzote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu” (1 Pet 3: 15). Tumaini lililo ndani yetu ni hili: Maisha pamoja na Yesu ni matumaini yasiyo na mwisho, bila yeye, ni mwisho usio na matumaini. Tumaini letu ni hili:  “Sitawaacha ninyi yatima” (Yn 14: 15-21). Matumaini hayamuui yeyote.” Hii ni methali ya Kongo. Ingawa matumaini hayaliwi kama chakula hatuwezi kuishi bila matumaini. “Matumaini ni nguzo ya dunia.” Ndivyo isemavyo methali ya Kiafrika. Matumaini ni kumpokea Roho Mtakatifu. “nao wakampokea Roho Mtakatifu” (Mdo 8: 17). Kukata tamaa ni kumkataa Roho Mtakatifu.

MATUMAINI NI MTAZAMO CHANYA
Watu wanapokwambia, “Kata tamaa,”  matumaini yanasema, “jaribu tena.” Watu wanapokwambia, “nusu glasi haikujaa,”  matumaini yanasema, “nusu glasi imejaa.” Watu wanapokwambia, “matatizo ni mengi,”  matumaini yanasema, “yana mwisho” Watu wanapokwambia, “mlango wa kazi umefungwa,”  matumaini yanasema, “Mungu anafungua mlango mwingine.” Siku moja nilikutana na msichana niliyesoma naye Chuo Kikuu. Alikuwa na mimba. Aliniambia Mungu amemfungulia mlango, dirisha na madirisha madogo. Niliuliza namna gani aliniambia kuwa baada ya kumaliza masomo chuo kikuu alipata kazi. Pili alimpata mme bora. Tatu alikuwa na mimba. Mungu wetu si kuwa anaweza kukufungulia mlango tu bali anaweza kukufungulia milango na madirisha. Endelea kuvumilia na endelea kuamini ukitafuta suluhisho la shida. Endelea kutumaini.
MATUMAINI NI SILAHA
Shetani alitumia mateso, misiba, balaa, na mikosi kumkatisha Ayubu tamaa. Lakini ayubu hakukata tamaa. “Hapo Shetani akaondoka mbele ya Mwenyezi Mungu, akamtesa Ayubu...Mkewe akamwambia, ‘Bado tu ungali ukishikilia unyofu wako? Mtukane Mungu, ufe? Ayubu akamjibu mkewe, “...Tukipokea mema kutoka kwa Mungu, kwa nini tukatae kutoka pia mabaya kutoka kwake?” (Ayubu 2: 7-10). Ayubu alitumia silaha ya matumaini kwa Mungu katika mapambano yake na shetani. Matumaini yamebeba uvumilivu. Mvumilivu hula mbivu. Kupata pancha sio mwisho wa safari.  Matumaini yamebeba subira. Subira yavuta heri.
YESU NI SHUJAA WA MATUMAINI
Maisha pamoja na Yesu ni matumaini yasiyo na mwisho, bila yeye, ni mwisho usio na matumaini. Yesu alipokuwa msalabani alivumilia sababu alikuwa na matumaini katika ufufuko na katika ushindi. Makuhani wakuu, waandishi, na wazee walimcheka wakisema, “Aliwaokoa wengine, kujiokoa mwenyewe hawezi. Kama ni mfalme wa Israeli, basi ashuke sasa msalabani, nasi tutamsadiki” (Mathayo 27: 42). Yesu hakushuka toka msalabani. Ni kama unamwambia askari atoke uwanja wa vita ili umwamini kuwa ni askari. Ni kama unamwambia mwanandoa atoke kwenye ndoa ili umwamini kuwa ameolewa. Ni kama unamwambia mwanafunzi aache shule ili umwamini kuwa yeye ni mwanafunzi. Yesu hakushuka toka msalabani alivumilia. Matunda yake ni kwamba kwa uvumilivu wake alituonyesha njia.Hakuna Jumapili ya Paska bila Ijumaa Kuu. Alitukumboa. Fikiria stampu kwenye barua. Manufaa yake yapo katika uwezo wake wa kubaki kwenye bahasha mpaka bahasha imfikie mlengwa. Huo ni mfano wa nguvu ya uvumilivu wa kulishughulia jambo kwa muda mrefu bila kuliacha.
MATUMAINI NI HITAJI LA BINADAMU
Matumaini yetu yawe kama nywele na kucha. Haijalishi unazikata mara ngapi haziachi kuota. Hata ukiwa kwenye matatizo kuwa na matumaini. Matatizo ni giza la kukusaidia kuona nyota.   Katika giza la matatizo uwe na matumaini. Ukitembea  usiku wenye giza unaona nyota. Katika mtazamo huo Stephanie Meyer  alisema: “Napenda usiku. Bila giza tusingeona nyota.”  Katika matatizo unahitaji kuwa na matumaini. Usikatishwe tamaa na giza la maneno ya kukukatisha tamaa. Baba wa Uchimbaji mafuta Edwin L. Drake aliambiwa mwaka 1859: “Unataka kuchimba mafuta? Unamaanisha kuchimba ardhi ukitafuta mafuta utakuwa umerukwa na akili!” Kilichofuata ni historia bwana huyo hakusikiliza maneno ya kukatisha tamaa. Katika yote unahitaji matumaini. Ni kweli alivyosema Louise Phillipe: “Giza linapokuwa giza nene, nyota inaangaza sana.”
Biblia yasema: “Kabila lililotembea gizani limeona nuru kuu” (Isaya 9:2). Katika kutembea gizani unaweza kuona nyota. Wana wa Israel waliogandamizwa na kuteswa katika giza la mateso waliona nuru kuu. “Nyakati za balaa mbaya sana na machafuko zimekuwa nyakati za uzalishaji kwa watu wanaofikiri sana. Chuma kisichokuwa na uchafu kinatolewa penye joto jingi sana. Radi inayoangaza sana inatokana na wingu na dhoruba jeusi sana,” alisema Charles Caleb Colton.  Kumbe matatizo ni giza la kusaidia kuona nyota. Vitu vingi vimevumbuliwa kutokana na matatizo. Waisraeli katika matatizo makubwa ya ukame wamegundua kilimo cha umwagiaji kwenye shina la mche tu. Wanazalisha matunda na kuuza nchi za nje nchi yenye ukame. Katika matatizo ya giza umeme umevumbuliwa. Tulizoea kusema barua nu nusu ya kuonana. Katika matatizo ya kutoonana sasa kumevumbuliwa namna ya kuonana kupitia Skype. Sio vizuri kuwa na matatizo ukabweteka. Pengine si vizuri sana kuongejea giza ili uone mwanga. Methali ya Kifaransa inasema: “Yeye anayengojea kuvaa viatu vya marehemu anaweza kutembea pekupeku kwa muda mrefu.
Katika matatizo makubwa tunaweza kutambua uwepo wa Mwenyezi Mungu. Tunaweza kumwona Mungu. Biblia yasema: “Usifurahi juu yangu, ewe adui yangu, maana nikianguka, nitasimama tena, nikikaa katika giza, Bwana ni mwangaza wangu” (Mika 7:8). Katika giza utamwona Bwana mwangaza wako. Matatizo uliyonayo ni mwaliko wa kuwa na matumaini. Geuza hasi iwe chanya. Badili sumu iwe dawa. Badili jangwa liwe msitu. Badili mlima uwe tambarare. Penye giza washa mshumaa. Penye chuki panda upendo. Katika mto usiopitika jenga daraja.
Matumaini yawe mtaji wako na raslimali yako kwamba inawezekana.  Matumaini yatakuletea furaha katika giza la matatizo. “Kwa tumaini,mkifurahi katika dhiki, mkisubiri” (Warumi 12:12). Matumaini yetu yaendane na hali halisi yasionekane kama kichekesho. Kuna mpagaji aliyeulizwa: “Lini utalipa malimbikizo ya kodi ya chumba?” Alijibu: “Muda mfupi baada ya kupokea cheki  ambayo mchapishaji wa kitabu changu atanipa nitakulipa. Hii itategemea kama atakubali  kuchapisha kitabu hicho ambacho napanga kuandika nitakapapata jambo la kuandika juu yake na wazo fulani.” Ndoto zifanyiwe kazi. Kama una ndoto ya kujenga ghorofa angani anza kujenga msingi kuanzia chini. “Si kwamba mambo ni magumu ndio maana hatuthubutu, ni kwa sababu hatuthubutu ndiyo maana mambo ni magumu,” alisema mwanafalsafa Seneca.
“Namna tunavyoona tatizo ni tatizo,” alisema Stephen R. Covey. Unaweza kuona tatizo ni giza tu. Namna hiyo ya kuona ni tatizo. Lakini unaweza kuona tatizo kama giza la kukusaidia kuona nyota. Kumbe tatizo si tatizo. Tatizo ni namna tunavyoliona tatizo. Nchi zilizoendelea zimekabiliana na matatizo makubwa kwa mtazamo ambao si tatizo. Tunaweza kusema matatizo makubwa maendeleo “makubwa”. Mateso mengi na neema nyingi. Kumbuka kuwa penye matatizo kuna neema. Penye hasi kuna chanya. Penye kivuli kuna mwanga. Painapo ndipo painukapo.
USIKATE TAMAA PANCHA SIO MWISHO WA SAFARI
La kuvunda halina ubani. Maji yakimwagika hayazoeleki. Ni methali za kukatisha tamaa. Methali hizi zina maana  kuwa jambo likiharibika haliwezi kurekebishwa. Harufu mbaya ya uozo wa tabia haizuiwi. Kwa shetani la kuvunda halina ubani. Kwa Mungu la kuvunda lina ubani. Kwa shetani maji yakimwagika hayazoeleki, kwa Mungu maji yakimwagika yanazoeleka. “Hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu.” (Luka 1: 37) Mbinu ya nne ambayo shetani huitumia kuwafanya watu washindwe kutenda mazuri wengine wajiue ni kukata tamaa.
Shetani alitumia mbinu hii ya kukata tamaa kwa Yuda Iskarioti ambaye alimuuza Yesu baadaye Yuda Iskarioti alijiua. Tunasoma hivi katika Biblia, “Shetani akamwingia Yuda aitwaye Iskarioti...akaenda, akajadiliana na makuhani wakuu na walinzi wa hekalu kuhusu atakavyomsaliti Yesu kwao.” (Luka 22: 2-4) Maandiko haya yanasema Shetani alimuingia Yuda. Shetani alitumia mbinu yake ya kukata tamaa. “Yuda...alipoona kwamba wamekwisha mhukumu Yesu...akazitupa zile pesa hekaluni, akatoka nje, akaenda akajinyonga.” (Mathayo 27: 3-5) Yuda Iskarioti aliona kuwa mipango yake imeharibika alikata tamaa. Tatizo la dhambi ni kuwa mtu anaweza kuchukia hata zile pesa ambazo hakupata kwa njia ya halali. Yuda alichukia zile pesa. Kama Yuda Iskarioti angeomba msamaha tungekuwa na historia nyingine labda ya Mtakatifu Yuda Iskarioti Msimamizi wa Benki, Msimamizi wa watunza pesa  na Msimamizi wa Taasisi za Pesa. Alikata tamaa na kukosa matumaini ya kusamehewa.
Kuna methali ya wamaasai isemayo, “matumaini sio sawa na kukuta tamaa.” Mtu ambaye amekata tamaa hamlilii Mungu. Yuda hakumlilia Mungu. Mtu aliyekata tamaa hatafuti na haombi msamaha. Maisha yakikosa malengo yanakosa na maana. Namna hiyo sababu ya kuishi inaweza kuponyoka toka mikononi mwa mtu. Matumaini ni kinyume cha kukata tamaa.

Counter

You are visitor since April'08