Saturday, May 10, 2014

UNAVYOFIKIRIA NDIVYO UTAKAVYOKUWA




                                  JUMAPILI YA 4 YA PASKA
                JUMAPILI YA MCHUNGAJI MWEMA NA KUOMBEA MIITO
                     “Vijana wenu wataona njozi” (Matendo ya Mitume 2:17

Mdo 2: 14a. 36-41
1 Pet 2: 20b-25
Yn 10: 1-10

Picha ina thamani zaidi ya maneno 1000. Bwana wetu Yesu Kristu alikuwa fundi wa kupiga picha akilini, wa kufundisha kwa kuleta picha. Picha ya mchungaji: Yesu ni mchungaji. Si mchungaji tu ni mchungaji mwema. Anatoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Yesu ni mlango. (Yohane 10:7). Wachungaji huko Uyahudi walilala mlangoni mwa pango walimo wanyama ili kuzuia wanyama kama kondoo wasitoke pangoni na kuzuia wanyama wakali wasiingie pangoni. Yesu ni lango kuelekea kwa Baba.
Mtume Petro naye alikuwa bingwa wa kupiga picha akilini na kutumia lugha ya picha. “Maana mlikuwa kama kondoo waliopotea, lakini sasa mmemrudia mchungaji na msimamizi wa roho zenu” (1 Petro 2:25). Tunaona picha ya mchungaji na msimamizi. Tumuuige Bwana Yesu Kristu na mtume Petro tuwe mafundi wa kupiga picha ya wito tunaoutamani.
Piga picha akilini unataka kuwa nani. Kupiga picha akilini ni namna ya kufikiria. “Namna yetu ya kufikiri inatengeneza matokeo mazuri au mabaya,” alisema  Stephen Richards.  Wito wowote unaoutamani lazima uupigie picha. Unatamani kuwa padre au mchungaji piga picha unahubiri, piga picha unaendesha ibada. Unataka kufunga ndoa, piga picha unavikwa pete, piga picha ya arusi. Unataka kuwa daktari, piga picha unatibu mgonjwa, piga picha umevalia kama daktari. Tunasoma hivi katika Biblia: “Vijana wenu wataona njozi” (Matendo ya Mitume 2:17). Ni vizuri vijana kuwa na njozi, kuwa na ndoto. Kuna kitendawili kisemacho: usiku mzima nimetazama filamu. Jibu ni ndoto. Vijana hawana budi kuota ndoto za mchana. Ni kupiga picha ya kile unachokitaka, na unachokitamani. Alfred A. Montapert alikuwa na haya ya kusema:  “Kufanya mambo makubwa lazima kwanza kuota ndoto, halafu piga picha, halafu panga…amini…tenda!” 
 Suala la kuota ndoto na kupiga picha si la vijana tu hata wazee. Tunasoma hivi katika Biblia: “Na Wazee wenu wataota ndoto” (Matendo ya Mitume 2:17). Nakubaliana na Jack Youngblood  aliyesema: “Napiga picha akilini ya mambo kabla ya kuyafanya. Ni kama kuwa na karakarana akilini.”  Kupiga picha akilini ni kuangalia ambavyo havipo na havionekani. Tunaaswa hivi: ““Tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana” (2 Wakorintho 4:18). Kardinali Polycarp Pengo wa Tanzania alipokuwa bado kijana mdogo alienda Kanisani kusali. Siku hiyo ilikuwa ni kumbukumbu ya Mtakatifu Polycarp Askofu na Shahidi. Baada ya kutoka Kanisani alimwambia mama yake kuwa anapenda naye kuwa Askofu na shahidi. Mama yake alimwambia kuwa hawezi kuwa Askofu kabla ya kuwa padre. Yeye alizidi kusisitiza kuwa Kanisani walisema Polycarp alikuwa Askofu hawajazungumzia suala la padre. Kilichotokea ni historia. Kijana huyo amekuwa Askofu na sasa ni Kardinali Polycarp Pengo. Huu ni ushahidi wa hoja ninayoijenga: unavyofikiria ndivyo utakavyokuwa. Nakubaliana na Robert Collier  aliyesema: “Tazama mambo kwa namna ambayo ungependa kuwa nayo badala ya jinsi yalivyo,” alisema.
  Ukiwa unaelekea mahali fulani ingawa haujafika unapiga picha kukoje. Ukiomba piga picha Mungu atakupatia. Ili kupiga picha unahitaji macho ya imani. Biblia ina mifano mingi kuhusu jambo hili. Walau tuuone mfano mmoja: Mungu akamleta nje Abramu, akasema: “Utazame mbinguni, uhesabu nyota, kama waweza kuzihesabu. Akamwambia: Ndivyo uzao wako utakavyokuwa. Abramu akamwamini Bwana” (Mwanzo 15: 5-6). Mungu alimtaka Abramu apige picha. Kuamini maana yake ni mtu kuweka matumaini kwa Mungu hata kama hakuna ushahidi kwamba Mungu atafanya kitu. Kwa macho Abramu hakuwa na mtoto. Kwa macho Abramu alikuwa amezeeka. Kwa macho Sarah alikuwa amezeeka. Kwa imani uzao wao utakuwa kama nyota.
Juu ya kisa cha Abramu Joel Osteen alikuwa na haya ya kusema: “ Mungu alijua kuwa Abrahamu alihitaji picha ya ahadi katika akili yake. Abarahamu na Sarah walikuwa wamezeeka na bila mtoto, katika maumbile, ilikuwa hali ambayo haiwezekani. Lakini kila mara Abrahamu alipotozama nyota, alikumbushwa ahadi ya Mungu. Alianza kuona ahadi kupitia macho ya imani. Huwezi kuzaa ndoto ambayo  kwanza hujaiwazia. Lazima huiwazie ndani mwako kupitia macho ya imani kabla ya kuitoa nje. Badili kile unachokiona, utabadili kile unachozalisha.”
Omba “kama” kwamba” Umepata
Yesu  akawaambia, Waketisheni  Watu” (Yohane 6: 10).  Yesu aliwataka watu wakae mkao wa kula chakula “kama kwamba” chakula kimeishapatikana. Muujiza wa kuongeza mikate ulikuwa haujafanyika lakini Yesu alitenda kama kwamba. Kuna wakristu katika parokia moja hapa Tanzania walimuomba padre Jumapili iliyokuwa inafuatia iwe siku ya kuomba kupata mvua. Wakristu hao walishangazwa na padre aliposema hayuko tayari kufanya maombi ya kuomba mvua kwa vile wakristu hawakwenda na miavuli ya kujikinga na mvua. Suala la kuwa na miavuli linadokeza maana ya “kama kwamba.” Yesu aliwambia wakoma kumi waende wajioneshe kwa makuhani kama kwamba wamepona. Bikira Maria aliwaambia watumishi: lolote atakalowambieni fanyeni “kama kwamba” Yesu amekubali.
Piga picha ya kile unachokitaka. Bila shaka Bwana Yesu Kristu alipiga picha ya muujiza, picha ya ongezeko la samali wawili na mikate mitatu.  Suala la kupiga picha ni muhimu ili ufanikiwe. “Akamleta (Abramu) nje akasema:Utazame mbinguni, uhesabu nyota, kama waweza kuzihesabu.Akamwambia: Ndivyo uzao wako utakavyokuwa” (Mwanzo 15:5). Mungu alisisitiza umuhimu wa kupiga picha.
 Linda vizuri mawazo yako, mawazo yako yanasikika Mbinguni. Ukifikiria kuwa tajiri, na mwaminifu, mawazo hayo yanasikika mbinguni. Ukifikiria kuwa maskini na myonge, mawazo hayo yanasikika mbinguni. Ukifikiria kuwa mtakatifu au kutenda dhambi, mawazo hayo yanasikika mbinguni. Mtu anayefanikiwa maishani ni mshindi. Mtu ambaye anashindwa maishani ni mshinde. Mshindi anasema ni jambo gumu lakini linawezekana. Mshinde anasema, linawezekana lakini ni jambo gumu sana . Mshindi anaona jibu kwa kila swali. Mshinde anaona swali katika kila jibu. Mshindi ni sehemu ya jibu. Mshinde ni sehemu ya tatizo. Mshindi anaona jambo zuri katika kila shida. Mshinde anaona shida katika kila jambo zuri. Marehemu Edward Cole alipokuwa meneja wa Kampuni General Motors aliulizwa swali, “Jambo gani linakufanya uwe tofauti na watu wengine – kwa nini umefanikiwa kuliko maelfu ya watu na kupata kazi ya juu sana katika General Motors?”  Bwana Edward Cole alifikiri kwa muda na kujibu, “Napenda matatizo!” Katika matatizo aliona jibu. Uwe na ndoto kubwa hata kama kuna matatizo kama Yozefu wa Agano la Kale. “Usiku mmoja, Yozefu aliota ndoto, lakini alipowasimulia ndugu zake, wao wakazidi kumchukia” (Mwanzo 37: 5). Ukiwa na ndoto kubwa utachukiwa lakini usikate tamaa. Yozefu alifanikiwa. Kwa Mungu hakuna lisilowezekana. Ulivyo sasa ni matokeo ya mawazo na fikira zako. Juhudi ukijumlisha na ndoto kubwa ukajumlisha na Mungu ni sawasawa na mafanikio.  Mafanikio yako ya kesho yanategemea jambo unalolifikiria leo. Nakubaliana na James Allen aliyesema, “Leo upo pale ambapo mawazo yako yamekuleta; kesho utakuwa pale ambapo mawazo yako yatakupeleka.”
Usitazame pale tu ulipo tazama na pale unapoweza kuwa. Usitazame chini ulipo tazama na juu unapoweza kuwa. Usifikirie jinsi ulivyo, fikiria unavyoweza kuwa. Yesu alimwambia Simoni mwana wa Yohane, “Wewe ni Simoni mwana wa Yohane. Sasa utaitwa Kefa” (Yohane 1: 42). Kefa ni Petro, yaani Mwamba.  Yesu alimtia moyo Simoni awe na picha ya mwamba. Alimtia moyo afikirie kuwa yeye ni mwamba. “Watu wana namna ya kuweza kubadilika wakawa unavyowatia moyo wawe na sivyo unavyowasumbua wawe,” alisema  Scudder N. Parker.
Mtu anavyofikiria katika akili yake anakuwa hivyo, na anavyochagua anakuwa hivyo” (Methali 23: 7). Zig ziglar alisema, “picha unayochora katika akili yako, akili yako itaifanyia kazi ili kuifanikisha. Unapobadili picha zako unabadili na utendaji.”  Kila kitu ambacho unaongeza na kufungia kwa maneno haya “mimi ni ....” Utageuka kuwa hivyo. Jibariki kwa maneno haya: Mimi ni mwema. Mimi ni mwaminifu. Mimi ni tajiri. Mimi ni mvumilivu. Mimi ni mchapakazi. Mimi ni mcha mungu. Mimi ni mwamba. Mimi ni mzuri. Mimi ni mwenye busara. Mimi ni mwenye heshima. Mimi ni mpole. Mimi ni mtoto wa Muungu.Mimi ni kisura, Mungu haumbi takataka. Mungu haumbi mtumba.
Mtu ni watu. Watu wanatujenga au wanatubomoa. Picha tuliyonayo, tunavyojiona uenda imetoka kwa watu wengine, imetoka kwako, imetoka kwa neno la Mungu, imetoka kwa wazazi, imetoka kwa shetani. Lakini Yesu ana picha yake, Yesu anaona uwezekano, yanayowezakana, unayoweza kufanya. Mwanamke alikuwa anamuuliza mme wake, “Sijui huko mbinguni patakuwepo na nguo za gharama sana za wanawake?” Mme wake akajibu, “ Unataka kuniambia tukiwa mbinguni nitaangaika kutafuta pesa za kukununulia nguo.” Mwanamke akamjibu, “Usiwe na wasiwasi, usiogope, wewe hautakuwa huko.” Maneno kama hayo hayamuinui mwanaume.

Afadhali adui mzuri kuliko rafiki mbaya. Niambie rafiki yako nitakwambia tabia yako. Simoni Petro alikuwa na ndugu yake Andrea. Hawa hawakuwa tu ndugu bali walikuwa marafiki. Andrea alimleta Simoni Petro kwa Yesu. Andrea alimpa Simoni Petro picha nzuri. Kuna picha inayotoka kwa marafiki zetu. Wanavyotuona na sisi inatujengea picha tunavyojiona. Andrea alimuona Simon Petro kama mtu anayeweza kuwa mfuasi mzuri wa Yesu akamleta kwa Yesu. Katika maisha ungekuwa juu lakini marafiki zako wanapicha ya kukuweka chini. Ungekuwa mbali lakini picha kutoka kwa marafiki zako ni ya puani.  Picha ya Andrea ilikuwa ya juu.

Marafiki ambao hawakusaidii kuwa kama Yesu anavyotaka uwe, marafiki ambao hawakuinui wakiamua kukuacha waache waende: “WATU HAO WAMETOKEA KATI YETU LAKINI HAWAKUWA WA KWETU NA NDIYO MAANA WALITUACHA; KAMA WANGALIKUWA WA KWETU, WANGALIBAKI NASI. LAKINI WALIONDOKA, WAKAENDA ZAO, KUSUDI IONEKANE WAZI KWAMBA HAWAKUWA KAMWE WA KWETU” (I Yohane 2: 19).


Counter

You are visitor since April'08