Saturday, June 28, 2014

MTAKATIFU ANAANGUKA MARA 99 NA KUINUKA MARA 100



                       
                                            SIKUKUU YA PETRO NA PAULO MITUME
1. Mate 12: 1-11
2. 2 Timotheo 4: 6-8, 17-18
3.  Mathayo 16: 13 -19

Hayati Nelson Mandela aliwahi kukiri hivi: “Mimi sio mtakatifu, isipokuwa kama unamfikiria mtakatifu kuwa ni mdhambi ambaye anajaribu kila mara.” Kuna aliyesema baada ya kuungama dhambi zake kwa Mungu kuwa kabla ya kuungama alikuwa ni mdhambi anayeikimbilia dhambi sasa ni mdhambi anayeikimbia dhambi. “Kanisa sio Jumuiya ya wakamilifu, bali Jumuiya ya wadhambi,” alisema Papa Benedict XV, Kiongozi wa ngazi ya juu ya Kanisa Katoliki aliyestaafu. Ukweli huu unasemwa kwa namna nyingine na Billy Graham mhubiri maarufu: “Sote ni wadhambi. Kila mtu unayekutana naye popote duniani ni mdhambi.”  Wadhambi sio watu wakuchukia. “Chukia dhambi, mpende mdhambi,” alisema Mahatma Gandhi.  Kumchukia mdhambi badala ya dhambi ni jambo linaloshangaza. Lucius Annaeus Seneca alisema: “Watu wengi wana hasira, na sio dhidi ya dhambi, bali dhidi ya mdhambi,”
Mchungaji alimwambia mwana Kwaya: “watu hamsini wameniambia kuwa haujui kuimba hivyo nakufukuza kutoka kwenye kwaya.” Naye mwana kwaya alimjibu mchungaji: “Watu zaidi ya hamsini wamesema haujui kuhubiri hivyo nawe ufukuzwe kanisani.” Kuhubiri ni kipaji au karama. Kuimba ni kipaji au karama. Kinachotufanya watakatifu si kipaji au karama bali fadhila. Je kuna ukarimu katika kutumia hivyo vipaji? Je kuna unyenyekevu katika kutumia hivyo vipaji? Je kuna imani katika kutumia hivyo vipaji? Kuna upendo katika kutumia hivyo vipaji? Je kuna ujasiri katika kutumia vipaji hivyo. Bikira Maria mama wa Yesu alimpendeza Mungu kwa ubikira wake, lakini alibeba mimba kwa unyenyekevu wake. Mtakatifu Petro Kiongozi wa kwanza wa Kanisa alikuwa na kipaji cha uongozi, kipaji cha kuandika lakini kilichomfanya mtakatifu ni: ujasiri, upendo, unyenyekevu na ukarimu. Mtume Paulo alikuwa na kipaji cha kuhubiri, kuandika lakini kinachomfanya mtakatifu ni imani. Alisema mwenyewe: “imani nimeitunza.” Hawa watakatifu walikuwa watu wachangamfu. Kununa si sifa nzuri kwa watakatifu mtakatifu: “Mungu anilinde na watakatifu walionuna,” Mtakatifu Tereza wa Avila.
Mchungaji Hudson Taylor alisema: “Watu maarufu wote wa Mungu walikuwa watu wadhaifu.” Lakini Mungu aliwabadili wakawa watakatifu. Kanisa Katoliki Katika kitabu cha Maombi wakati wa sikukuu ya Mitume Watakatifu Petro na Paulo tarehee 29 Juni, hukiri udhaifu wa mtume Petro :  Ndugu wapenzi, Mungu alionyesha nguvu ya neema yake alipomwita Petro, mvuvi dhaifu, awe mwamba ambao juu yake alijenga kanisa lake..." Petro baada ya kujitazama alimwambia Yesu, “Ondoka kwangu  mimi mdhambi.” (Luka 5:8) Nabii Isaya alijitazama, Basi, mimi nikasema, “Ole wangu! Mimi nimeangamia, maana, midomo yangu ni najisi, na watu ninaoishi nao ni najisi kama mimi.” (Isaya 6:5) Mtume Paulo alipojitazama, alisema, “Maana mimi ni mdogo kabisa miongoni mwa mitume, na wala sistahili kuitwa mtume, kwa sababu nililidhulumu kanisa la Mungu.” (1 Wakorintho 15:9). Tunaposoma maisha ya hawa wadhambi waliogeuka kuwa watakatifu tutafakari ukweli huu: Biblia haikuandikwa ili kutufanya wasomaji bali watakatifu.
Simoni Petro baada ya kumkiri Yesu kuwa ni Masiya na Mwana wa Mungu baadaye Yesu alipoweka wazi mpango wake na sera yake ya kutufia msalabani Petro alimkemea Yesu naye Petro alikemewa akiambiwa rudi nyuma yangu shetani. Simoni Petro alishinda mtihani wa nadharia lakini hapa mtihani wa vitendo ulimshinda. Kuwa Masiya kivitendo ni kuwafia wengine. Mfalme alikuwa na shida ya moyo. Walitaka kumbadilishia moyo na kumpa moyo wa mtu mwingine. Lakini hapakuwepo na mtu aliyepata ajali. Hivyo akaitisha mkutano. Akaomba watu kama kuna anayeweza kunisaidia yaani kuwa tayari kufa kwa ajili yangu atoe moyo wake. Watu wote wakaamusha mikono. Akasema sasa nimchague nani. Akurusha unyoya wa ndege na kusema ukimwangukia mmoja wenu huyo ndiye atanipa moyo. Kila ulipokuwa unamkaribia mtu anaupuliza kwa hewa ya mdomoni unazidi kupaa angani. Walimpenda kwa maneno na sio kwa matendo.

Ng’ombe licha ya kuwa na miguu minne huanguka. Ni methali ya wanandi. Kama mambo ni hivyo itakuwaje mtu mwenye miguu miwili. Methali hii inatufundisha kuwa binadamu hukosea. Lakini upo uwezekano wa kusahihisha makosa. Kuanguka chini si kushindwa. Kushindwa ni kutoamka toka chini, “Kwa maana mwenye haki huanguka mara saba akaondoka tena” (Mithali 24:16). Mtakatifu ni yule anayeanguka mara 99 na kuamka mara 100. Mwana mpotevu alianguka lakini aliamka toka chini, “Utukufu wetu wa juu haupo katika kutoanguka kamwe, bali kuamka ghyflukila tunapoanguka” (Oliver Goldsmith).

Lakini tuna adui anayefurahi tunapoanguka. Adui huyo ni shetani tusimfurahishe. “Usifurahie maafa yangu ewe adui yangu! Nikianguka, nitainuka tena; nikiwa gizani, Mwenyezi – Mungu ni mwanga wangu” (Mika 7: 8). Sio shetani anayecheka na kufurahi tunapoanguka hata adui zetu wengine ambao ni mawakala na mawikili wake. Hata watakatifu walikuwa na adui kama hao wakawashinda kwa kushirikiana na neema za Mungu kama tusomavyo katika misale ya waumini: “Watakatifu tunaowaheshimu leo walikuwa binadamu kama sisi, na pengine wapo tuliowaelewa. Wao walishinda adui za roho zetu kwa kutumaini neema za Mungu.”    
Binadamu huanguka. Hoja si kuanguka hoja ni kuinuka. Maneno haya yazame moyoni mwako. “Nikianguka nitainuka.” Unapoanguka, unapotenda dhambi unakuwa gizani. Lakini Mungu ni mwanga wako. Mwanga wa Mungu ni neema ya utakaso tunayopata tukitubu. Kumbuka hoja si namna unavyoanza hoja ni namna unavyomaliza. Mwanampotevu alianza vibaya akamalizia vizuri. Biblia yasema, “Mtu mwema huanguka mara nyingi lakini huinuka, lakini mtu mwovu huangamizwa na janga” (Methali 24:16).
Ni kweli mtakatifu ni yule anayeanguka mara 99 na kuinuka mara 100. Udhaifu wa Musa ulikuwa hasira. Lakini Mungu alimgeuza kuwa “mtu mpole kuliko wote duniani” (Hesabu 12:3). Udhaifu wa Ibrahimu ulikuwa ni woga. Mara mbili alidai mke wake alikuwa ni dada yake. Mungu alimgeuza jasiri na kumfanya baba wa imani. Daudi mzinzi alifanywa kuwa mtu aupendezaye myo wa Bwana. Yohane mwenye majivuno mmojawapo wa wana wa ngurumo akawa mtume wa upendo. Udhaifu wa Gidioni ilikuwa ni kutojiamini akawa mtu shujaa. Saulo muuaji aligeuzwa kuwa mtangazi Injili akawa Paulo. Simoni dhaifu akawa Petro mwamba. Nakubalina na maneno ya Mtakatifu Yohane Paulo II: “Sisi sio jumla ya udhaifu wetu na kushindwa kwetu. Ni jumla ya upendo wa baba kwetu na uwezo wetu wa kweli wa kuwa sura ya mwanawe.”
Kadili tumbili anavyopanda juu ndivyo makalio yanazidi kuonekana. Binadamu kadili anavyopanda katika ngazi vya vyeo vya jamii kasoro zake ndogo zinaonekana haraka. Mfalme Daudi naye aliingia katika kapu hilo hilo . Alitenda kosa na Bathsheba, baada ya kukemewa na nabii Nathani aliomba msamaha. Zaburi yote ya 51 katika Biblia ni Zaburi ya kuomba msamaha. “Nihurumie, Ee Mungu, kadiri ya fadhili zako; ufutilie mbali makosa yangu, kadiri ya wingi wa huruma yako” (Zaburi 51:1). Baada ya kutubu na kumgeukia Mungu na kuishi maisha mazuri aligeuka na kuwa  mtakatifu. Mifano hiyo ni ushahidi tosha kuwa mtakatifu ni mdhambi aliyeanguka lakini akainuka na kumgeukia Mungu. Lakini ukweli huo si tiketi ya kumkosea Mungu na kusema nitainuka. Haujui utakufa namna gani? Ajali huenda isikupe muda wa kumgeukia Mungu. Kumbe wakati uliokubalika ni sasa. Amua, inuka, achia.
Wenye afya hawamhitaji daktari bali wagonjwa. Yesu alikuja kuwaita wenye dhambi wapate kutubu.  Ukweli huu utufanye tutubu, tujute.  “Wafuate watakatifu, kwa sababu wale ambao uwafuata watakuwa watakatifu,” alisema Papa Mtakatifu Clement I. Orodha ya watakatifu ambao ni mifano ya kuigwa haifanyi kanisa liwe jumba la makumbusho la watakatifu bali ni mwaliko wa kuishi vizuri na kuwaiga. “Kanisa ni hospitali ya wadhambi  na sio nyumba ya makumbusho ya watakatifu,” alisema Pauline Phillips. Mwaliko wa kujitakatifuza ni mwaliko ambao unavuka ubinafsi. Mbinguni hauendi peke yako. “Jitakatifuze na utaitakatifuza jamii,” alisema Francis wa Assis. Leo Kanisa Katoliki linafanya Sikukuu ya Mitume Petro na Paulo. “Tunawaenzi, kuwaheshimu, na kuwapenda mitume zaidi ya watakatifu wengine, kwa sababu walimtumikia Mungu kwa uaminifu zaidi na kwa sababu walimpenda kwa ukamilifu zaidi,” alisema Mtakatifu Ignatius.  Yote yakishasemwa ukweli unabaki. Tukianguka tusimame.
Kama utakavyokumbuka Mtakatifu Paulo alikuwa ameshikilia nguo za Stefano akitazama alivyokuwa anapigwa mawe. Stefano aliwaombea wote na Paulo akiwemo wakati huo ni Saulo. Sala hizo zilikuwa na nguvu. Baadaye,  Saulo akawa Paulo. Muuaji akawa Mchungaji. Mwangamizaji akawa Muuokoaji. Adui wa Kanisa akawa rafiki wa Kanisa. Alitubu. Kila mdhambi ni mtakatifu mtarajiwa ambaye hajasimamishwa kwenye barabara iendayo Damascus. Kuna Askofu aliyetoa kichekesho kuwa Mitume Petro na Paulo walishindwa kuishi vizuri pamoja duniani Kanisa likawaunganisha pamoja katika Sikukuu ya Leo kwa vile wanaishi pamoja vizuri huko mbinguni. Tukumbuke hawa mababa ni nguzo za imani yetu. Tuwaige katika mazuri yao ambayo ni mengi kuliko kasoro zao. Kila mtu ni dhahabu inayohitaji kusafishwa. Kweli mtakatifu ni yule anayeaanguka mara 99 na kuinuka mara 100 tunamuita mtakatifu.

Saturday, June 21, 2014

SHUKURU USIKUFURU



                                              
SHEREHE YA MWILI NA DAMU TAKATIFU YA BWANA WETU YESU KRISTU
1. Kumb. 8: 2-3, 14-16
2. 1 Wakorintho 10: 16-17
3. Yn 6: 51 – 58

Ingawa tuna mioyo midogo lakini inaweza kubeba jambo kubwa nalo ni shukrani. “Tunapotoa kwa furaha na kupokea kwa shukrani, kila mtu anabarikiwa,” alisema Maya Angelou.  Kuna methali isemayo, “Hasiyeshukuru kwa jambo dago apewalo hatashukuru kwa jambo kubwa.” Leo hii wakatoliki sehemu zote duniani wanaandamana kusherehekea sherehe inayojulikana kama “Mwili na Damu ya Kristu.” Kwa jina lingine sherehe hii inajulikana kama “Sherehe ya Ekaristi Takatifu.” Neno “Ekaristi” linatokana na neno la Kigiriki ambalo linamaanisha shukrani. Ni sherehe inayohusu kumshukuru Mungu na utamaduni wa kushukuru. Kushukuru ni kitovu cha sherehe hii. Shukuru kwa kila jambo. Sherehe ya Leo ya wakatoliki inahusu utamaduni wa kushukuru. Waluhya wana methali isemayo, “Nyama choma haiwezi kuwa tamu ukamsahau aliyeichoma.” Methali hii inakazia kuwa na utamaduni wa kushukuru. Kama umepewa sio siri. Watu wanaona jinsi Mungu alivyokubariki na hivyo kwa mantiki hii wakatoliki wanaandamana hadharani kuonyesha shukrani yao
 Sherehe hii inapata nguvu kutoka katika maneno ya Biblia, “ Ndipo Wayahudi wakaanza kubishana kati yao: “Anawezaje huyu kutupa mwili wake, tule?’ Yesu akaambia, ‘Kweli nawaambieni, msipokula mwili wa mwana wa Mtu na kunywa damu yake, hamtakuwa na uhai ndani yenu.” (Yohane 6: 52-53) Jambo hili la kula mwili na kunywa damu ya Yesu lilizua utata mkubwa katika historia ya Kanisa Katoliki. Mwanzoni wakristu walishitakiwa kuwa ni watu wala watu. Ni kama Wayahudi waliojiuliza, “anawezaje huyu kutupa mwili wake?”
 Jambo hili linaeleweka hivi. Kama maji na madini yangekuwa na uwezo wa kusema yangeiambia mimea usipokunywa maji na kula madini hamtakuwa na uhai ndani yenu. Kama nyasi na maji vingekuwa na uwezo wa kusema vingewaambia wanyama kama ng’ombe na mbuzi msipokula majani na kunywa maji hamna uhai ndani yenu. Katika msingi huu kwa vile binadamu ana mwili na roho Yesu alisema msipokula mwili wangu na kunywa damu yangu hamtakuwa na uhai ndani yenu.  Kushiriki katika karamu ya Bwana ni muhimu.
Leo hii tunapewa changamoto ya kushiriki. Katika neno kushiriki tunapata neno ushirikiano. “Tunapomshukuru Mungu kwa kiokombe kile cha baraka, je, huwa hatushiriki damu ya Kristo? Na tunapoumega mkate, je, huwa hatushiriki mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate huo ni mmoja, sisi, ingawa ni wengi, tu mwili mmoja; maana sote twashiriki mkate huohuo.” (1 Wakorintho 10: 16-17) Basi kushiriki kwetu kusiishie Kanisani tushiriki katika Jumuiya Ndogo Ndogo. Tushiriki katika maendeleo ya Taifa.
Suala la sherehe ya leo na shukrani lina msingi wake katika Biblia. “Saa ilipotimia, Yesu akakaa kula chakula pamoja na mitume wake…Kisha akatwaa kikombe akashukuru, akasema, ‘Pokeeni, mgawanyiane…halafu akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa akisema, “Huu ni mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa kunikumbuka.” (Luka 22: 14-19) Yesu alishukuru alipochukua mkate na divai. Ekaristi inamaanisha shukrani na mkate na divai hutumika. Wakristu ambao wanashiriki kumbukumbu ya Karamu ya Mwisho ya Yesu kwa kuandamana leo wanakumbushwa kuwa na utamaduni wa kushukuru maana ndio kiini cha sherehe ya leo.
Hellen Keller ambaye alikuwa kipofu na kiziwi aliandika hivi: “Kila mara nimefikiria ingekuwa baraka kama kila mtu angekuwa kipofu na kiziwi kwa siku chache wakati wa siku zake za kwanza za utu uzima. Giza lingemfanya akiri uzuri wa mwanga; ukimya ungemfundisha furaha ya sauti.”  Kuna vitu ambavyo tunavyo lakini hatukiri uzuri wake na umuhimu wake mpaka tumevipoteza. “Hatuna budi kupata muda wa kutulia na kushukuru watu ambao wameleta tofauti katika maisha yetu,” alisema John F. Kennedy.
 Katika hadithi  za Aesop kuna hadithi juu ya mtumwa aliyeitwa Androcles ambaye alitoroka toka kwa Bwana wake na kukimbilia msituni. Alipokuwa akitangatanga alikutana na simba ambaye alikuwa amelala chini akinguruma na kutoa sauti ya uchungu. Mwanzoni alitaka kukimbia lakini aligundua simba hakumfukuzia. Alirudi nyuma na kumwendea. Alipomkaribia, simba alionyesha kwato zake au mguu wake ambao ulikuwa umevimba na ukitoa damu. Androcles aligundua palikuwepo na mwiba mkubwa ambao ulikuwa umeingia ndani na ulikuwa unamsababishia maumivu makali. Aliutoa mwiba huo na kuufunga vizuri mguu wa simba ambaye aliweza kusimama na kulambalamba mkono wa Androcles kama mbwa. Simba alimpeleke Androcles kwenye pango lake na kila siku alimletea nyama ya kula na kuweza kuishi. Lakini baadaye Androcles na Simba walikamatwa. Androcles alipewa adhabu ya kutupwa kwenye kibanda cha simba huyo ambaye siku nyingi aliwekwa kwenye kibanda bila chakula. Mfalme na watu wa ikulu ya mfalme walikuja kushuhudia simba akimrarua Androcles. Simba aliachiliwa kutoka katika kibanda chake na kumwendea huyo binadamu akinguruma. Alipomkaribia Androcles alimtambua na kuanza kulamba lamba mikono yake kama mbwa rafiki. Mfalme alishangaa alimuomba Androcles amueleze maana ya hayo yote. Androcles alimweleza mfalme kila kitu. Mtumwa alisamehewa na kuachwa huru  na simba aliachiliwa arudi msituni. Hayo ni matunda ya kutenda wema kwa Androcles na kushukuru kwa simba. Shukrani ni mtaji. Shukrani ina malipo.

Hata unapokosewa unajifunza kitu fulani. “Msamaha wa kweli ni pale unapoweza kusema, ‘Nashukuru wa uzoefu huo,’” alisema Oprah Winfret. Biblia inatwaambia: “Shukuruni katika kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu” (1 Wathesalonike 5: 18). Rick Warren katika kitabu chake Maisha Yanayoongozwa na Malengo alikuwa na haya ya kusema juu ya haya hiyo: “Mungu anakutaka umshukuru kwamba atatumia matatizo yako kutimiza malengo yake.” Kusema kweli kutomthamini mwenzako ni kukufuru maana kushukuru ni kuthamini. Kutoshukuru ni kosa kubwa kuzidi kulipa kisasi. “Kutoshukuru ni kosa la kudharauliwa zaidi ya kulipa kisasi, ambacho ni kulipa baya kwa baya, wakati kutoshukuru ni kulipa baya kwa wema,” alisema William Jordan. Tujenge utamaduni wa kushukuru. Afrika yenye utamaduni wa kushukuru inawezekana.
Kushukuru ni kumsifu Mungu. Mungu kama amekujalia watoto, akili, utajiri, amani moyoni, jina jema, mke, mme, mshukuru ukimsifu. Zingatia maneno haya, “Mtukuzeni Bwana  pamoja nami, na tuliadhimishe jina lake pomoja .” (Zaburi 34:3) Mkumbuke Mungu. Hakuna haja ya kujidai sana sote ni “CHAKUPEWA.” “Nani amekupendelea wewe? Una kitu gani wewe ambacho hukupewa? Na ikiwa umepewa, ya nini kujivunia kana kwamba hukupewa?” (1 Wakorintho 4:7).   Kuna methali isemayo, “Aliyekupa wewe kiti ndiye aliyenipa mimi kumbi.” Na aliye na kidogo akitumie kupata kikubwa.
Kushukuru ni kuthamini zawadi uliyopewa. Kama Mungu ametupa zawadi ya amani, kushukuru ni kuthamini zawadi hiyo. Kama Mungu amekupa zawadi ya mke, shukuru ni kuthamini zawadi hiyo. Kama Mungu amekupa zawadi ya mme, shukuru ni kuthamini zawadi  yaani mme. Kama unamshukuru Mungu kwa kuwa Mkenya, basi itendee Kenya mambo mazuri. Kama unamshukuru Mungu kwa vile wewe ni mtanzania itendee Tanzania mambo mazuri.
Kushukuru ni kuomba tena. Ukipata shukuru. Kuna Baba mmoja ambaye alikuwa anatembea kando ya Bahari ya Indi na mtoto wake wa kiume. Mara wimbi likamchukua mtoto wake wa kiume lakini akaokolewa na mvuvi Msamaria mwema. Badala ya kushukuru Baba huyo alimuuliza mvuvi, “Mtoto wangu alikuwa na kofia umeiweka wapi?” Huo ni ukosefu wa shukrani. Sherehe ya Ekaristi ambayo inamaanisha shukrani ni changamoto kwa wakristu wote kuwa na moyo wa shukrani na sio na moyo wa punda. Shukrani ya punda ni mateke.


Saturday, June 14, 2014

MAFIGA MAWILI HAYAIVISHI CHUNGU



                                                 
                                                         SHEREHE YA UTATU MTAKATIFU
1.       Kut 34: 4b -6. 8-9
2. 2 Kor 13: 11 -13
3.  Yn 3: 16 -18

Mungu wetu ni mkubwa. Yuko katika nafsi tatu: Baba Mwana na Roho Mtakatifu. Ana nguvu. Nakubaliana na Andrew Guzalds aliyesema: “Kuna nguvu zaidi katika neno moja kutoka kwa Mungu kuliko maneno yote ya adui yakiwekwa pamoja.” Ukiwa na Mungu huko upande wa wengi. Sala yako iwe hii: “Nakuomba ee Bwana wangu, ufuatane nasi” (Kutoka 34:9). Tafakari hadithi hii: Binti alimuaga mama yake, “naenda matembezi na marafiki zangu.” Mama yake akamwambia: “Mungu awe nawe katika Safari yako.” Kwa dharau na kiburi binti akajibu “mh mama gari imejaa labda huyo Mungu akae kwenye buti kama anaweza. Kwa kasi akawasha gari wakaondoka. Njiani wakapata ajali mbaya wote wakafa walitambuliwa tu kwa mavazi waliyovaa! Polisi walipofungua buti wakakuta mayai trey 2 yakiwa salama kabisa! Unajua kwa nini? Wewe Mungu umemweka wapi?
Kuna methali ya Wahaya wa Bukoba isemayo: “Fanya urafiki na mkubwa anamaliza kabisa tatizo la kukosa kitoweo.” Mungu mmoja katika nafsi tatu ni mkubwa fanya urafiki naye. “Kuna utupu au ombwe lenye sura ya Mungu katika kila mtu ambalo linaweza kujazwa na Mungu,” alisema Blaise Pascal.
Mungu wetu Mkubwa hata siku moja usimwambie kuwa dhoruba yako ni kubwa, tatizo lako ni kubwa bali iambie dhoruba: Mungu wangu ni mkubwa ni nafsi tatu, Mungu mmoja. Ukiwa na imani kwa Mungu mmoja nafsi tatu, utaiondoa milima. Lakini ukiwa na hofu milima itakuondoa. Uwe mwondoaji wa milima kwa kuamini katika Utatu Mtakatifu na kwa kusali hivi: “Nakuomba ee Bwana wangu, ufuatane nasi” (Kutoka 34:9).
Mafiga mawili hayaivishi chungu.Ni methali ya Kiswahili. Mafiga mawili hayawezi kukiivisha chungu; lazima yawe matatu. Tutakapo kufanikiwa lazima tuwe tayari kushirikiana na wenzentu.  Katika mtazamo huu wazee wetu walituachia busara: kidole kimoja hakivunji chawa. Jiwe moja haliinjiki chungu. Kuna kitendawili cha Wafipa wa Tanzania kisemacho: Tatu tatu mpaka Ulaya. Jibu ni mafiga. Haya ni mawe matatu. Ndoa inahitaji watatu: mme, mke na Mungu. Kwa kumuungiza Mungu kwenye ndoa, ndoa inadumu. Ni katika msingi huu tunasema: Familia inayosali pamoja hudumu pamoja. Umoja huu wa Utatu ni muhimu.  “Kwa kuungana tunasimama; kwa kugawanyika tunaanguka,” alisema John Dickson. Tafakari methali ya Tanzania isemayo: Mkono mmoja haulimi shamba.
Siku zilizopita nilipokea ujumbe katika simu wenye maneno haya: “Kuna siri gani katika namba 3? Shetani alimjaribu Yesu mara 3. Yesu alianguka na msalaba mara 3. Petro alimkana Bwana Yesu mara 3. Jogoo aliwika mara 3. Yesu alifufuka si ku ya 3. Wanawake walienda kaburini siku ya 3 nao walikuwa 3. Matanga huanuliwa siku ya 3. Mafiga ya kupikia huwa 3. Mashindanoni namba za ushindi ni 3. Nyakati zinagawanyika mara 3: wakati uliopita, uliopo na ujao. Wazo, neno na tendo vinakamilisha uwezo wa binadamu navyo ni vitatu. Kuna nafsi 3 katika sarufi: Mimi, Wewe na Yeye. Nafsi za Mungu ni 3: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Nini maana ya 3? Namba tatu ni namba ya ukamilifu na utimilifu. Namba tatu inawakilisha kitu kizima, cha kweli na kamilifu. Inadokeza uimara, uthabiti, uhakika.
Jumapili ya leo wakatoliki kote duniani wanasherehekea Sherehe ya Utatu Mtakatifu. Inahusu imani kuwa Mungu ni mmoja katika nafsi tatu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Ni kama mafiga matatu. Wakatoliki hubatizwa kwa jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu na wala sio kwa majina ya Baba na Mwana na Roho Mtakatifu. Hapa hakuna suala la hesabu za kujumlisha ambapo moja kujumlisha na moja kujumlisha na mojo ni tatu. Ikumbukwe kuwa moja kuzidisha na moja kuzidisha na moja  ni moja. Hapa hatuingizi hoja ya mahesabu. Ieleweke hivi mimi ukisoma makala yangu kwenye gazeti unaniita mwandishi wa makala maalum (columnist), kanisani waumini wananiita padre, chuoni wanafunzi wananiita mwadhiri. Hatuko watatu ni mmoja.
Katika kufanikisha mambo kuna nguvu ya wingi au nguvu ya namba. Tunaona nguvu ya wingi katika uumbaji. “Mungu akasema: Tumfanye mtu kwa mfano wetu, afanane nasi” (Mwanzo 1:26). Ni Utatu  Mtakatifu uliosema “tumfanye mtu,” katika kitabu cha Mwanzo. Inavyoonekana hata mwanzoni mwa Injili Utatu Mtakatifu ulisema, “tumkumboe mtu.” Ili kufanikisha mambo. Ili kufanikiwa lazima kufikiria katika msingi wa “sisi.”  Nafsi tatu zinafikiria katika msingi wa sisi. Nakubaliana na Ralph Chaplain Yusufu aliyesema: “Hauwezi ukawa na usalama, hata ukijaribu namna gani; kama haufikiri kwa msingi wa “sisi” badala ya mimi.” Lorii Myers alikuwa na mawazi hayo aliposema: “Sisi ni sawa na nguvu.”
Kutatua tatizo la kutozaa la Abrahamu na Sara palikuwepo na nguvu ya namba au nguvu ya umoja. “Mgeni akamwambia, ‘Nitarudi kwako mwaka ujao, wakati huu; na hapo mkeo Sara atakuwa na mtoto wa kiume” (18: 10). Sara na Abrahamu walikuwa wamezeeka lakini kwa Mungu hakuna lisilowezekana. Abrahamu alitembelewa na utatu mtakatifu. Tafakari vizuri haya hizi: “Bwana akamtokea Abrahamu” (Mwanzo 18: 1); “Akainua macho akaona watu watatu wamesimama mbele yake” (Mwanzo 18:2). Ni Bwana mmoja halafu watu watatu. Kutatuliwa tatizo la kutozaa ni ufunuo wa uwepo wa Mungu katika nafsi tatu. Tunahitaji nguvu ya Utatu Mtakatifu tufanikiwe ambayo inaelezwa katika somo la pili: “Neema ya Bwana Yesu Kristo, na upendo wa Mungu Baba, na Ushirika wa Roho Mtakatifu viwe nanyi nyote” (2 Kor 13:13).

NEEMA YA BWANA YESU KRISTU
Mt. Gregory wa akizungumzia juu ya ubatizo alisema ni: “Neema: kwani hutolewa hata kwa wahalifu.” Ukweli kuwa neema hutolewa hata kwa waalifu ni ukweli ambao tunauona msalabani. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo ilitolewa kwa mwizi Dismasi. Tunahitaji neema ili kufanikiwa. George W. Bush aliwahi kusema: “Naamini katika neema, kwa sababu nimeiona; katika amani kwa sababu nimeionja; katika msamaha, kwa sababu nimehuitaji.” Neema ya Bwana Yesu inaonjeka. Ili kuonja neema ya Bwana wetu Yesu lazima kushirikiana nayo. Kuna ambaye alitaka kushinda bahati nasibu ya Kampuni ya Simu ya Tigo. Kila mara aliomba kushinda. Alisali kwa Bwana wetu Yesu Kristu. Usiku alitokewa katika ndoto. Yesu alimwambia: nataka ushinde lakini nunua vocha. Alitaka naye atoe mchango wake. Ni lazima kushirikiana na neema ya Mungu.

UPENDO WA MUNGU BABA
Kilichojaa hufurika. Ni methali ya Watanzania. Mungu Baba amejaa upendo na unafurika. “Kwa maana  jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amsadikiye asipotee, bali awe na uzima wa milele (Yn 3:16). Martin Luther aliita haya hii: “Injili katika mfano mdogo.” Upendo wa Mungu unajieleza katika kumtuma Mwana wake wa Pekee. Kutoa ni matokeo ya upendo. Unaweza kupenda bila kutoa. Lakini hauwezi kupenda bila kutoa.
Hata katika matatizo kuna upendo wa Mungu. Methali ya Kiyiddishi inasema yote: “Yule ambaye Mungu anampenda anamwaadhibu.” Mateso yanaweza kuwa sehemu ya upendo wa Mungu. “Mungu alikuwa na Mwana mmoja bila dhambi, lakini hakuwa na yeyote bila mateso,” alisema Mt. Augustini. Kuna kijana mdogo ambaye alimuua bata wa baba yake. Mkubwa wa kijana huyo akasema: Chochote ninachotaka unifanyie utanifanyia, vinginevyo nitakushitaki kwa Baba kuwa uliua bata. Siku ilifuata kijana mkubwa alikuwa na zamu ya kuosha vyombo. Akamwambia mdogo aoshe vinginevyo alisema: nitakushitaki kuwa ulimuua bata. Alikuwa na zamu ya kuosha nguo akamwambia mdogo asipoosha nguo atamshitaki kwa baba yake.  Mambo yaliendelea hivyo mpaka mtoto mdogo alipoamua kwenda kuripoti kwa baba yake kuwa alimuua bata. Baba alimwambia nilikuona ulipofanya tendo hilo. Nilingoja uje kwangu usiwe mtumwa wa kaka yako. Niliishakusamehe. Huu ni mfano wa upendo wa Mungu Baba.
USHIRIKA WA ROHO MTAKATIFU
Kama hewa ilivyo kwa mwili wa binadamu ndivyo Roho Mtakatifu alivyo katika maisha ya kiroho. Roho Mtakatifu yupo nyuma ya pazia anafanya mambo. Anaunganisha pointi, matukio anapanga kalenda. Omba kuwa na ushirika naye. Tutumie mafiga haya matatu: Neema, Upendo na Ushirika.

HITIMISHO
Tunahuitaji Utatu Mtakatifu. Tuuiige. Tujifunze kufanya mambo kwa pamoja. “Sala usafiri kwa haraka tunaposali pamoja.” Ni methali ya Kilatini.

Counter

You are visitor since April'08