Saturday, June 28, 2014

MTAKATIFU ANAANGUKA MARA 99 NA KUINUKA MARA 100



                       
                                            SIKUKUU YA PETRO NA PAULO MITUME
1. Mate 12: 1-11
2. 2 Timotheo 4: 6-8, 17-18
3.  Mathayo 16: 13 -19

Hayati Nelson Mandela aliwahi kukiri hivi: “Mimi sio mtakatifu, isipokuwa kama unamfikiria mtakatifu kuwa ni mdhambi ambaye anajaribu kila mara.” Kuna aliyesema baada ya kuungama dhambi zake kwa Mungu kuwa kabla ya kuungama alikuwa ni mdhambi anayeikimbilia dhambi sasa ni mdhambi anayeikimbia dhambi. “Kanisa sio Jumuiya ya wakamilifu, bali Jumuiya ya wadhambi,” alisema Papa Benedict XV, Kiongozi wa ngazi ya juu ya Kanisa Katoliki aliyestaafu. Ukweli huu unasemwa kwa namna nyingine na Billy Graham mhubiri maarufu: “Sote ni wadhambi. Kila mtu unayekutana naye popote duniani ni mdhambi.”  Wadhambi sio watu wakuchukia. “Chukia dhambi, mpende mdhambi,” alisema Mahatma Gandhi.  Kumchukia mdhambi badala ya dhambi ni jambo linaloshangaza. Lucius Annaeus Seneca alisema: “Watu wengi wana hasira, na sio dhidi ya dhambi, bali dhidi ya mdhambi,”
Mchungaji alimwambia mwana Kwaya: “watu hamsini wameniambia kuwa haujui kuimba hivyo nakufukuza kutoka kwenye kwaya.” Naye mwana kwaya alimjibu mchungaji: “Watu zaidi ya hamsini wamesema haujui kuhubiri hivyo nawe ufukuzwe kanisani.” Kuhubiri ni kipaji au karama. Kuimba ni kipaji au karama. Kinachotufanya watakatifu si kipaji au karama bali fadhila. Je kuna ukarimu katika kutumia hivyo vipaji? Je kuna unyenyekevu katika kutumia hivyo vipaji? Je kuna imani katika kutumia hivyo vipaji? Kuna upendo katika kutumia hivyo vipaji? Je kuna ujasiri katika kutumia vipaji hivyo. Bikira Maria mama wa Yesu alimpendeza Mungu kwa ubikira wake, lakini alibeba mimba kwa unyenyekevu wake. Mtakatifu Petro Kiongozi wa kwanza wa Kanisa alikuwa na kipaji cha uongozi, kipaji cha kuandika lakini kilichomfanya mtakatifu ni: ujasiri, upendo, unyenyekevu na ukarimu. Mtume Paulo alikuwa na kipaji cha kuhubiri, kuandika lakini kinachomfanya mtakatifu ni imani. Alisema mwenyewe: “imani nimeitunza.” Hawa watakatifu walikuwa watu wachangamfu. Kununa si sifa nzuri kwa watakatifu mtakatifu: “Mungu anilinde na watakatifu walionuna,” Mtakatifu Tereza wa Avila.
Mchungaji Hudson Taylor alisema: “Watu maarufu wote wa Mungu walikuwa watu wadhaifu.” Lakini Mungu aliwabadili wakawa watakatifu. Kanisa Katoliki Katika kitabu cha Maombi wakati wa sikukuu ya Mitume Watakatifu Petro na Paulo tarehee 29 Juni, hukiri udhaifu wa mtume Petro :  Ndugu wapenzi, Mungu alionyesha nguvu ya neema yake alipomwita Petro, mvuvi dhaifu, awe mwamba ambao juu yake alijenga kanisa lake..." Petro baada ya kujitazama alimwambia Yesu, “Ondoka kwangu  mimi mdhambi.” (Luka 5:8) Nabii Isaya alijitazama, Basi, mimi nikasema, “Ole wangu! Mimi nimeangamia, maana, midomo yangu ni najisi, na watu ninaoishi nao ni najisi kama mimi.” (Isaya 6:5) Mtume Paulo alipojitazama, alisema, “Maana mimi ni mdogo kabisa miongoni mwa mitume, na wala sistahili kuitwa mtume, kwa sababu nililidhulumu kanisa la Mungu.” (1 Wakorintho 15:9). Tunaposoma maisha ya hawa wadhambi waliogeuka kuwa watakatifu tutafakari ukweli huu: Biblia haikuandikwa ili kutufanya wasomaji bali watakatifu.
Simoni Petro baada ya kumkiri Yesu kuwa ni Masiya na Mwana wa Mungu baadaye Yesu alipoweka wazi mpango wake na sera yake ya kutufia msalabani Petro alimkemea Yesu naye Petro alikemewa akiambiwa rudi nyuma yangu shetani. Simoni Petro alishinda mtihani wa nadharia lakini hapa mtihani wa vitendo ulimshinda. Kuwa Masiya kivitendo ni kuwafia wengine. Mfalme alikuwa na shida ya moyo. Walitaka kumbadilishia moyo na kumpa moyo wa mtu mwingine. Lakini hapakuwepo na mtu aliyepata ajali. Hivyo akaitisha mkutano. Akaomba watu kama kuna anayeweza kunisaidia yaani kuwa tayari kufa kwa ajili yangu atoe moyo wake. Watu wote wakaamusha mikono. Akasema sasa nimchague nani. Akurusha unyoya wa ndege na kusema ukimwangukia mmoja wenu huyo ndiye atanipa moyo. Kila ulipokuwa unamkaribia mtu anaupuliza kwa hewa ya mdomoni unazidi kupaa angani. Walimpenda kwa maneno na sio kwa matendo.

Ng’ombe licha ya kuwa na miguu minne huanguka. Ni methali ya wanandi. Kama mambo ni hivyo itakuwaje mtu mwenye miguu miwili. Methali hii inatufundisha kuwa binadamu hukosea. Lakini upo uwezekano wa kusahihisha makosa. Kuanguka chini si kushindwa. Kushindwa ni kutoamka toka chini, “Kwa maana mwenye haki huanguka mara saba akaondoka tena” (Mithali 24:16). Mtakatifu ni yule anayeanguka mara 99 na kuamka mara 100. Mwana mpotevu alianguka lakini aliamka toka chini, “Utukufu wetu wa juu haupo katika kutoanguka kamwe, bali kuamka ghyflukila tunapoanguka” (Oliver Goldsmith).

Lakini tuna adui anayefurahi tunapoanguka. Adui huyo ni shetani tusimfurahishe. “Usifurahie maafa yangu ewe adui yangu! Nikianguka, nitainuka tena; nikiwa gizani, Mwenyezi – Mungu ni mwanga wangu” (Mika 7: 8). Sio shetani anayecheka na kufurahi tunapoanguka hata adui zetu wengine ambao ni mawakala na mawikili wake. Hata watakatifu walikuwa na adui kama hao wakawashinda kwa kushirikiana na neema za Mungu kama tusomavyo katika misale ya waumini: “Watakatifu tunaowaheshimu leo walikuwa binadamu kama sisi, na pengine wapo tuliowaelewa. Wao walishinda adui za roho zetu kwa kutumaini neema za Mungu.”    
Binadamu huanguka. Hoja si kuanguka hoja ni kuinuka. Maneno haya yazame moyoni mwako. “Nikianguka nitainuka.” Unapoanguka, unapotenda dhambi unakuwa gizani. Lakini Mungu ni mwanga wako. Mwanga wa Mungu ni neema ya utakaso tunayopata tukitubu. Kumbuka hoja si namna unavyoanza hoja ni namna unavyomaliza. Mwanampotevu alianza vibaya akamalizia vizuri. Biblia yasema, “Mtu mwema huanguka mara nyingi lakini huinuka, lakini mtu mwovu huangamizwa na janga” (Methali 24:16).
Ni kweli mtakatifu ni yule anayeanguka mara 99 na kuinuka mara 100. Udhaifu wa Musa ulikuwa hasira. Lakini Mungu alimgeuza kuwa “mtu mpole kuliko wote duniani” (Hesabu 12:3). Udhaifu wa Ibrahimu ulikuwa ni woga. Mara mbili alidai mke wake alikuwa ni dada yake. Mungu alimgeuza jasiri na kumfanya baba wa imani. Daudi mzinzi alifanywa kuwa mtu aupendezaye myo wa Bwana. Yohane mwenye majivuno mmojawapo wa wana wa ngurumo akawa mtume wa upendo. Udhaifu wa Gidioni ilikuwa ni kutojiamini akawa mtu shujaa. Saulo muuaji aligeuzwa kuwa mtangazi Injili akawa Paulo. Simoni dhaifu akawa Petro mwamba. Nakubalina na maneno ya Mtakatifu Yohane Paulo II: “Sisi sio jumla ya udhaifu wetu na kushindwa kwetu. Ni jumla ya upendo wa baba kwetu na uwezo wetu wa kweli wa kuwa sura ya mwanawe.”
Kadili tumbili anavyopanda juu ndivyo makalio yanazidi kuonekana. Binadamu kadili anavyopanda katika ngazi vya vyeo vya jamii kasoro zake ndogo zinaonekana haraka. Mfalme Daudi naye aliingia katika kapu hilo hilo . Alitenda kosa na Bathsheba, baada ya kukemewa na nabii Nathani aliomba msamaha. Zaburi yote ya 51 katika Biblia ni Zaburi ya kuomba msamaha. “Nihurumie, Ee Mungu, kadiri ya fadhili zako; ufutilie mbali makosa yangu, kadiri ya wingi wa huruma yako” (Zaburi 51:1). Baada ya kutubu na kumgeukia Mungu na kuishi maisha mazuri aligeuka na kuwa  mtakatifu. Mifano hiyo ni ushahidi tosha kuwa mtakatifu ni mdhambi aliyeanguka lakini akainuka na kumgeukia Mungu. Lakini ukweli huo si tiketi ya kumkosea Mungu na kusema nitainuka. Haujui utakufa namna gani? Ajali huenda isikupe muda wa kumgeukia Mungu. Kumbe wakati uliokubalika ni sasa. Amua, inuka, achia.
Wenye afya hawamhitaji daktari bali wagonjwa. Yesu alikuja kuwaita wenye dhambi wapate kutubu.  Ukweli huu utufanye tutubu, tujute.  “Wafuate watakatifu, kwa sababu wale ambao uwafuata watakuwa watakatifu,” alisema Papa Mtakatifu Clement I. Orodha ya watakatifu ambao ni mifano ya kuigwa haifanyi kanisa liwe jumba la makumbusho la watakatifu bali ni mwaliko wa kuishi vizuri na kuwaiga. “Kanisa ni hospitali ya wadhambi  na sio nyumba ya makumbusho ya watakatifu,” alisema Pauline Phillips. Mwaliko wa kujitakatifuza ni mwaliko ambao unavuka ubinafsi. Mbinguni hauendi peke yako. “Jitakatifuze na utaitakatifuza jamii,” alisema Francis wa Assis. Leo Kanisa Katoliki linafanya Sikukuu ya Mitume Petro na Paulo. “Tunawaenzi, kuwaheshimu, na kuwapenda mitume zaidi ya watakatifu wengine, kwa sababu walimtumikia Mungu kwa uaminifu zaidi na kwa sababu walimpenda kwa ukamilifu zaidi,” alisema Mtakatifu Ignatius.  Yote yakishasemwa ukweli unabaki. Tukianguka tusimame.
Kama utakavyokumbuka Mtakatifu Paulo alikuwa ameshikilia nguo za Stefano akitazama alivyokuwa anapigwa mawe. Stefano aliwaombea wote na Paulo akiwemo wakati huo ni Saulo. Sala hizo zilikuwa na nguvu. Baadaye,  Saulo akawa Paulo. Muuaji akawa Mchungaji. Mwangamizaji akawa Muuokoaji. Adui wa Kanisa akawa rafiki wa Kanisa. Alitubu. Kila mdhambi ni mtakatifu mtarajiwa ambaye hajasimamishwa kwenye barabara iendayo Damascus. Kuna Askofu aliyetoa kichekesho kuwa Mitume Petro na Paulo walishindwa kuishi vizuri pamoja duniani Kanisa likawaunganisha pamoja katika Sikukuu ya Leo kwa vile wanaishi pamoja vizuri huko mbinguni. Tukumbuke hawa mababa ni nguzo za imani yetu. Tuwaige katika mazuri yao ambayo ni mengi kuliko kasoro zao. Kila mtu ni dhahabu inayohitaji kusafishwa. Kweli mtakatifu ni yule anayeaanguka mara 99 na kuinuka mara 100 tunamuita mtakatifu.

Counter

You are visitor since April'08