Saturday, September 27, 2014

KUSEMA NA KUTENDA



                                                
                                          JUMAPILI YA 26 YA MWAKA A

1. Ezekieli 18: 25 -28
2. Wafilipi 2: 1-11au Wafilipi 2: 1-5
3.  Mathayo 21: 28 -32
UTANGULIZI
Matendo yanapozungumza maneno si kitu. Sisi tunajiendesha kama watoto. Tunasema  ndiyo, lakini hatufanyi kitu, pengine tunakataa kwanza na baadaye tunajuta na kutimiza tunayoambiwa. Tumuombe Mungu katika adhimisho la leo atuepushe na mazoea ya kutamka maneno ya ndiyo ndiyo bila kutimiza kwa matendo.
MAHUBIRI YENYEWE
Mgeni  mmoja alitembelea nchi ya Poland enzi za ukomunisti. Alioneshwa maeneo mengi na mwanachama  wa chama tawala. Mgeni alimuuliza mwanachama huyo, “Je, wewe ni mkatoliki?” Mwanachama huyo alijibu, “Naamini lakini sitendi.” Mgeni baadaye alimuuliza, “Je, wewe ni mkomunisti?” Ofisa huyo alitabasamu na kujibu, “Natenda, lakini siamini.” Dini ya Kikristu inawadai wanachama wake kusema na kutenda yaani kuhubiri maji  na kunywa maji na si kuhubiri maji na kunywa divai. “Jibu fupi ni kutenda,” alisema Lord Herbert. Ahadi ni mawingu kutumiza ahadi ni mvua. Haitoshi kuahidi lazima kutenda. “Tendo ni lugha ya kushawishi,” alisema William Shakespeare.
Neno zuri ni zuri, tendo zuri ni zuri zaidi. Kwa msingi huo matendo yana kauli kuliko maneno. Maneno matupu hayajengi ghorofa. Si kwa kusema asali asali utamu unaingia mdomoni. Utukufu hauji kwa kuuita. Ni methali ya Kenya. Matendo yanapozungumza maneno si kitu. Kuna methali ya Kiafrika isemayo, “Sikusikii matendo yako yananipigia kelele.” Kwa matendo yake tunamjua mtu. Watu wote wanaweza kuzungumza lakini si watu wote wanaweza kutenda. “Neema haitolewi kwa wale ambao huzungumzia juu ya imani yao lakini kwa wale ambao wanaishi imani yao,” alisema  Mt. Gregory.
Injili ya leo inatupa umuhimu wa matendo. Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; akamwendea yule wa kwanza, akasema, ‘Mwanangu, leo nenda kafanye kazi katika shamba la mizabibu,’ Akajibu akasema, ‘Naenda, Bwana; asiende. Akamwendea yule wa pili, akasema vilevile. Naye akajibu akasema, ‘Sitaki; baadaye akatubu, akaenda. Je, katika hao wawili ni yupi aliyefanya mapenzi ya babaye?” Wakamwambia, “Ni yule wa pili.” Basi Yesu akawaambia, “Amin, nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu” (Mathayo 21: 28 – 31). “Tunachoweza kujifunza katika mfano huu Bwana aliwazungumzia wale ambao wanaahidi kidogo au hawaahidi chochote lakini katika matendo wanafanya makubwa na dhidi ya wale ambao wanaahidi makubwa lakini hawafanyi lolote kati ya wale ambao wameaahidi,”  alisema Origen Baba wa Kanisa.
Baba wa Kanisa Jerome alikuwa na haya ya kusema, “Mungu anazungumza kwanza kwa watu wa mataifa kupitia kanuni ya maumbile; ‘Nenda kafanye kazi katika shamba langu la mizabibu;’ ni kusema, ‘Mtendee mwenzako kama unavyotaka akutendee’ (Tobiti 4:16). Alijibu kwa majivuno , ‘Sitaki.’  Kumbe aliyesema nitaenda baadaye akwenda ni wayahudi wasio waaminifu. Mzabibu ni taifa teule la Israeli (Isa 5:1). Mwenye shamba ni Mungu. Watumwa wake ndio manabii. Mwanae ndiye Yesu. Wakulima wauaji ndiyo wayahudi wasio waaminifu. Watu wengine watakaoaminishwa shamba la mizabibu ni watu wa mataifa yaani wapagani.

Mfano huu ni mfano juu ya watoto wabaya wawili. Ni mtoto yupi kati ya hao wawili angekuwa mtoto wa kuigwa au mfano wa kuigwa? Yule anayesema hapana ya herufi kubwa mbele ya baba yake au yule anayesema ndiyo. Jibu ni kuwa hayupo hata mmoja wa kuigwa. Mtoto ambaye ni mfano wa kuigwa ni yule anayesema ndiyo na kuweka katika matendo. Yesu alisema: “Si kila mtu aniambiaye :Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni, bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni” (Mathayo 7:21).  
Maneno “umefanya vizuri” ni mazuri zaidi kuliko maneno  “umesema vizuri.”  Ni maneno ya Benjamini Franklin (1709-1790) mmojawapo wa Waasisi wa Amerika, mwandishi na mwanadiplomasia. Mwanasiasa huyu alitaka kusema matendo yana kauli kuzidi maneno. Maneno haya yanabainisha maana ya methali au msemo wa Kenya: Kusema na kutenda. Haitoshi kusema kunahitajika kutenda pia. “Muwe watimizaji wa neno, si wasikiaji tu; kama sivyo, mnajidanganya wenyewe” (Yakobo 1:22). Dini ni ya matendo.
Haitoshi kusema tu lazima tutende. Kunda kijana aliyemtumia mchumba wake ujumbe wa simu wenye maneno haya: “Nakupenda sana kiasi cha kupanda mlima mrefu kwa ajili yako. Nakupenda sana kiasi cha kuweza kuogelea kwenye mto TANA kwa ajili yako. Ninaweza kupitia katikati ya moto kwa ajili yako. Naweza kunyeshewa mvua kwa ajili yako. Naomba tukutane kesho saa nane kama mvua haitanyesha.” Maneno hayo ni mazuri lakini ni maneno matupu bila matendo. Kwa nini baadaye kijana anaogopa mvua.
Wanandoa siku ya kufunga ndoa wanaulizwa juu ya upendo: Padre kwanza anamuuliza Bwana arusi: F. unampokea F. awe mke wako, tena waahidi kuwa mwaminifu kwake, katika taabu na raha, katika magonjwa na afya, umpende na kumheshimu siku zote za maisha yako?” Kisha padre anamuuliza bibi arusi; F. unampokea F. awe mume wako, tena waahidi kuwa mwaminifu kwake, katika taabu na raha, katika magonjwa na afya, umpende na kumheshimu siku zote za maisha yako?” Jibu ambalo hutolewa huwa ndiyo. Hiyo ni kusema kunabaki kutenda.
Ukisema mimi ni “memba” au muumini wa Kanisa. Jambo hilo liweke katika matendo. “Memba” au mwenye hisa ni mmojawapo wa wamiliki wa kampuni au chama. Wewe kama ni “memba” jua Kanisa ni lako. Jenga chako. Lakini “Asiyekujua hakuthamini.” Lijue Kanisa. Kanisa lina mafiga matatu: padre, mtawa na mlei. Mafiga mawili hayaivishi chungu. Kazi yote hawezi kuaachiwa padre na mtawa. Mafiga mawili hayaivishi chungu. Mlei ujue Kanisa ni lako. Mtawa ujue Kanisa ni lako. Padre ujue Kanisa ni lako.
Ukiimba wimbo wa “Mkristu miye niko salama…” Wimbo huo ukauweke katika matendo. Lisaidie Kanisa. Shilingi moja na shilingi mia moja zilikuwa na mazungumzo. Shilingi moja iliuliza, “Wewe shilingi elfu moja ya Kenya (17,000/= Tshs) umetembelea sehemu zipi?” Shilingi mia moja ya Kenya ilijibu, “Nimetembelea mabenki yote. Nimekuwa sehemu za starehe zote, hoteli kubwa kubwa, nimekukaa sana supermarket, nimelala mara nyingi Dubai, China. Jew ewe shilingi moja unakaa wapi?” Shinlingi moja ilijibu. “Mimi nitafute kwenye makanisa ya Kanisa la Peter Claver, Consolata, Yohane Mbatizaji.” Ukristo ni matendo. LISAIDIE KANISA LIKUSAIDIE. Kama unajiita mkristu lazima kuhudhuria vikao, adhimisho la ibada ya misa, mikutano ya Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristu. “Watu wangapi wanahudhuria katika Kanisa lako?” Mchungaji mmoja alimuuliza mwingine.” Mchungaji alifikiria kidogo halafu alijibu, “60 wapo kila mara, 250 C na E.” “Nini maana ya C na E?” Mchungaji alitaka kujua. “Maana yake ni Christmasi na ‘Easter” yaaani Paska.
Kupenda ni kitenzi. Upendo ukibaki ni nomino ni nomino dhahania. Upendo husipotolewa hudumaa na ukitolewa unakua. Tutoe upendo kwa waliotuzunguka baadaye upendo upae kuwaendea wengine. Kuna mtoto aliyemuuliza mama yake, “Tupo hapa duniani kwa ajili ya nini?” Mama alimjibu, “Tupo hapa kwa ajili ya kuwapenda wengine.” Na mtoto akazidi kudadisi, “ Wengine wapo kwa ajili ya nini?” Kuna watu wanafikiri wapo kwa ajili ya kupendwa na si kupenda. Mungu ametuumba kwa ajili ya kupenda na kupendwa. Upendo ambao haujawekwa katika vitendo ni kama ujumbe wa simu ulioandikwa lakini ukasahau kuutuma. Ni kama barua ambayo umeandika ukasahau kuipeleka posta. Upendo ukibaki ni jina tu au nomino tu ni nomino dhahania lakini lazima uwe kitenzi-kupenda ni kitenzi.

Saturday, September 13, 2014

UKIUBEBA VIZURI MSALABA MSALABA UTAKUBEBA



                          
                                               SIKUKUU YA KUTUKUKA MSALABA
                                                        JUMAPILI YA 24 YA MWAKA A
“Hakuna msalaba, hakuna Mkristo,” alisema  Profesa Mchungaji Daniel Deutschlander wa Ujerumani. Msalaba ni kitambulisho cha mkristo. “Muumini yeyote ambaye hajaukabili msalaba, bado hajawa mfuasi wa Kristo,” alisema  S. E. Entsua-Mensah mchungaji anayeishi Kumasi Ghana. Msalaba unavyotumika hapa haumaanishi mti bali mateso, matatizo, shida, udhia, karaha, sononeko, huzuni na maumivu. Binadamu naye anaweza kuwa msalaba licha ya kuwa neema. Mtoto anaweza kuwa msalaba kwa mzazi. Mke anaweza kuwa msalaba kwa mumewe. Mume anaweza kuwa msalaba kwa mke wake. Wajibu kwa umma na kwa Mungu ni msalaba. “Daima imani hubaki kuwa jambo la msalaba,” ameandika hivyo Papa Francis Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki kwa sasa katika kitabu chake Furaha ya Injili.  Kuna mke wa mtu alipata ujumbe kwenye simu ya mkono toka kwa mpango wa kando au nyumba yake ndogo uliosema hivi:”Nimekuacha tangia leo.” Mwanamke huyo akaanza kulia. Mme wako akamuuliza: “Ni ujumbe gani huo uliosoma halafu unaanza kulia.” Mwanamke akasema: “Ni ujumbe kuhusu namna ya kupika.” “Sasa kuna jambo la kukufanya ulie?” Mwanamke akasema: “Nimefikia kwenye sehemu ya kukata vitunguu. Na unajua vitunguu vinafanya mtu atoke machozi.” Usanii wa namna hiyo ni msalaba. Mwanamke wa namna hiyo ni msalaba.
Wasafiri nao wanaweza kuwa msalaba. Methali ya Kiswahili inasema yote: Msafiri kafiri. Kuna mtu amenitumia ujumbe huu kwenye simu ya mkononi: “Jamaa alikuwa kwenye daladala (Matatu) pembeni kuna dada mrembo kaka. Kamlia timing kwa muda kisha halafu akamuuliza ‘Samahani dada unaitwa Google?” Dada akamjibu: “Hapana, kwa nini umedhani naitwa hivyo?” Jamaa: “Una kila kitu ninachokitafuta.” Msafiri mwenzako anaweza kuwa msalaba.
Swali linabaki tubebeje msalaba? Tusiubebe kwa manung’uniko. Wana wa Israel baada ya Mungu kuwatendea miujiza walipopata na matatizo walinung’unika: “Njiani watu wakakata tamaa. Wakawanung’unikia Mungu na Musa. ‘Kwa nini mmetutoa Misri tuje tufe huku jangwani? Maana huku hakuna mkate wala maji; tumechoka na chakula hiki dhaifu!” (Hesabu 21: 4-5). Chakula walikuwa nacho lakini walikiita dhaifu.  “Maelekeo yetu tukiwa kwenye mateso ni kumgeukia Mungu. Ni kuwa na hasira na kuwa wakali na kuikunjia mbingu ngumi na kusema, ‘Mungu, haujui mateso yanavyofanana! Uelewi! Hauna wazo lolote juu ya yale ninayoyapitia. Uelewi ni kwa kwa kiwango gani inahumiza.’ Msalaba ni njia ya Mungu ya kuondoa mashitaka yetu, visingizio na hoja zetu kwake. Msalaba ni Mungu anachukua mwili na damu na kusema, ‘Na mimi pia,” alisema Mchungaji Rob Bell (Alizaliwa mwaka 1970. Alitajwa mwaka 2011 na gazeti  la Time Magazine la Amerika kuwa ni mmoja kati ya watu 100 duniani wenye ushawishi mkubwa).
“Mateso yanatualika kuweka maumivu yetu katika mikono mikubwa. Katika Kristu tunamwona Mungu akitutesekea. Na kutualika kushiriki katika upendo wa Mungu unaoteseka kwa ajili ya ulimwengu unaohumiza . Maumivu yetu madogo na yanayotuzidi nguvu ya maisha yetu yanaunganishwa kwa ukaribu sana na maumivu makubwa ya Kristo. Mateso yetu ya kila siku yanatia nanga katika mateso makubwa na kwa hiyo kuna matumaini makubwa,” alisema Padre  Henri J.M. Nouwen
Ubebe kwa uvumilivu na subira bila kutarajia matokeo ya mara moja. Papa Francis amekuwa na haya ya kusema katika kitabu chake Furaha ya Injili: “Shauku inayokithiri iliyopo leo hii kuhusu matokeo ya mara moja inawafanya wahudumu wa uchungaji waone vigumu kuvumilia jambo lolote linaloonekana kama vile linakosa makubaliano, lina uwezekano wa kushindwa, kuna maoni ya upinzani, ni msalaba.” Jani la chai likiwa kwenye maji moto linabadili rangi ya maji. Badili mambo kwa uvumili wako. Huko ni kubeba vizuri msalaba. Stempu haitoki kwenye bahasha mpaka bahasha imemfikia mlengwa. Huu ni mfano wa kubeba msalaba kwa uvumilivu.  Yesu hakushuka toka msalabani.
Ubebe bila kukata tamaa na kwa upole. Papa Francis ameandika hivi katika kitabu chake, Furaha ya Injili:  “Pamoja na kutambua unyonge wetu kwa uchungu mkubwa, ni lazima tusonge mbele bila kukata tamaa, tukizingatia kile ambacho Bwana alimwambia Mtakatifu Paulo: “Neema yangu inakutosha, maana nguvu yangu hufanywa kuwa kamilifu katika udhaifu’ (2 Kor 12:9). Daima ushindi wa Kikristo huwa ni msalaba, lakini ni msalaba ambao wakati huo huo ni bendera ya ushindi inayobebwa kwa upole wenye guvu dhidi ya mashumbulizi ya uovu.” Tumebebe msalaba kwa upole na matumaini.  Kuubeba vizuri msalaba ni kufikiria juu ya wengine badala ya kufikiria juu ya mateso yako tu. “Ingawa Yesu alikuwa katika mateso msalabani, alifikiria juu ya kuwaombea watesaji wake, kutunzwa kwa mama yake, kuratibisha wokovu wa mwizi,” alisema Thomas Dubay. Akili yako unapoiweka kwenye mateso ya wengine inasaidia kubeba vyema ya kwako. “Msalaba ni mahali ambapo mbingu inakutana na dunia na neema inalipuka. Msalaba sio mahali ambapo Yesu anakabili mateso yetu tu, bali anakuwa mateso yetu ili kubadilisha dunia,” alisema Mchungaji Matt Farlow wa Kanisa la New Wine, New Wineskins. Tubebe msalaba kwa hekima tukitafuta suluhisho la matatizo. Tubebemsalaba kwa upole hasira haisahidii. Tubebe msalaba kwa imani. Tubebe msalaba kwa uvumilivu tukitafuta suluhisho la matatizo.
NYOKA  WA  SHABA  AL IYEINULI WA NA MWANA WA MTU AL IYEINULIWA
Kuna kitendawili kisemacho: “Viwili vyafanana”. Jibu ni Meli na Pasi. Viwili vyafanana ni nyoka wa shaba aliyeinuliwa, aliyetundikwa na Mwokozi aliyeinuliwa. “Kama vile Musa alivyomwinua juu nyoka wa shaba kule jangwani, naye Mwana wa mtu atainuliwa juu vivyo hivyo ili kila anayemwamini awe na uzima wa milele. (Yohane 3:14) Mwinjili Yohane hueleza nyoka wa shaba kama mfano wa
Kristo aliyeinuliwa msalabani. Tunasoma hivi katika kitabu cha hesabu, “Watu wakamnung’unikia Mungu, na Musa, “Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu”. Bwana akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa. Watu wakamwendea Musa, wakasema, “Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung’unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa Bwana atuondolee nyoka hawa”. Basi Musa akawaombea watu. Bwana akamwambia Musa, “Jifanyie nyoka wa shaba ukamuweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa aitazamapo ataishi. Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti; hata ikiwa nyoka amemuuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi” (Hes.21 :4-9).
UFANANO
Nyoka wa shaba hakuwa wa sumu, ingawa alikuwa na sura ya nyoka. Ingawa Yesu alionekana kama mnyang’anyi, alionekana kama mdhambi hakuwa na dhambi. “Hapakuwa na hila kinywani mwake” (Isaya 53:9). Kama nyoka wa shaba alivyoinuliwa Yesu aliinuliwa msalabani. Aliyemtazama nyoka alipona. Majeraha ya sumu yalitibiwa. Yesu anatibu majeraha ya dhambi. Ingawa nyoka wa shaba alikuwa ni nyoka lakini ni wa shaba. Yesu alikuwa mtu lakini ni Mungu,ni Mungu mtu.

TOFAUTI
Zipo tofauti kati ya nyoka wa shaba aliyeinuliwa na Yesu aliyeinuliwa. Jukwaa la nyoka aliyeinuliwa ni jangwa. Jukwaa la Yesu aliyeinuliwa ni Kalvari. Watazamaji upande wa nyoka wa shaba ni wana wa Israeli. Upande wa Yesu aliyeinuliwa ni dunia nzima. Jamii yote ya binadamu inamtazama Yesu msulubiwa. Wana wa Israeli waliomtazama nyoka aliyeinuliwa walitibiwa kimwili baadaye, miaka kupita, siku kupita walikumbwa na kifo cha kawaida. Kifo hakina kalenda na hakuna atakayesahaulika. Yesu aliyeinuliwa hatibu tu magonjwa ya kimwili na ya kiroho pia. Yeyeanatoa maisha ya milele.
KUTAZAMA NI KUSADIKI
“Kutazama” katika Injili ya Yohane kuna maana ya kusadiki. Kumtazama Yesu aliyeinuliwa ni kumsadiki. “Watamtazama yeye waliyemchoma” (Yohane 19:37). Akida wa kirumi ni mfano wa wapagani waliomsadiki Yesu kwa kumtazama. “Basi yule akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la nchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu” (Mt. 27:54). Kuamini siyo kutaja maneno ya kanuni ya imani bali kuyaishi.
 MATATIZO NI MSALABA
 Katika nchi yangu kwanza unakwenda gerezani halafu unakuwa rais baadaye,” alisema Hayati Nelson Mandela aliyeaga dunia akiwa na umri wa miaka 95. Wajibu wa Hayati Nelson Mandela kwa umma na uzalendo vilikuwa ni msalaba. Aliuchukua msalaba huu ukamchukua hadi ikulu. Kuna upande mzuri wa msalaba kama matatizo. Ni katika msingi huu Yesu alisema: “Mtu asiyechukua msalaba wake na kunifuata, hanistahili” (Mathayo 10: 36). “Huwezi kukwepa msalaba, popote unapokimbilia; popote unapokwenda, kila mara utaukuta. Ukiuchukua msalaba kwa kuupenda, utakuchukua na kukupeleka unapopatamani: yaani kule ambapo patakuwa na mwisho wa mateso, ingawa hapa hakuna mwisho wa mateso. Ukiuchukua bila kupenda, unaufanya uwe mzigo kwako kuchukulika…ukiuutupa kwa nguvu msalaba mmoja bila shaka utakutana na mwingine labda mzito zaidi,” alisema Thomas รก Kempis.
Picha ya matatizo kama msalaba tunaipata katika sala ya Kanisa Katoliki ambayo husaliwa Ijumaa Kuu na kipindi cha Kwaresima: “Ee Yesu mkarimu, mimi pia ninao msalaba wangu: jirani zangu, mwenzangu wa ndoa, watoto, wazazi wangu, kazi zangu, joto, baridi,   njaa,   kiu,,, vishawishi, magonjwa na matatizo mengine ya maisha, wajibu wangu kwa Mungu, kwa umma na kwa Kanisa hayo yote ni msalaba. Unipe ukarimu wako ee Yesu, niyapokee bila kunung’unika na kuyabeba vema.”
Mwenzako wa ndoa anaweza kuwa msalaba. Kuna mwanaume aliyemsikia mchungaji anahubiri juu ya maneno ya Yesu: anayetaka kuwa mfuasi wangu abebe msalaba wake na anifuate. Mwanaume alipofika nyumbani alimbeba mke wake. Akampitisha sebuleni, bafuni, jikoni, barazani. Mwanamke alishangaa na kusema: ulinibeba siku ya kufunga ndoa. Mchungaji amefundisha nini Kanisani unanibeba namna hii leo hii. Mwanaume huyo alisema: mchungaji amefundisha tubebe misalaba yetu.  
Usijitengenezee msalaba. Kuna misalaba ya kujichongea. Kujiingiza kwenye mambo ya watu wengine, sio kwa sababu ya Yesu. Ukisikia mwanamke anasema sitaolewa tena na mwanamme huyu. Usiijiingize katika ugomvi wao na kuanza kuchochea. Ni kama kusema shuka kutoka kwenye msalaba wa ndoa. Ukipata matatizo huko umejiingiza kwenye ndoa ya watu si kujenga bali kubomoa. Ndugu wakigombana chukua jembe ukalime wakipatana chukua kapu ukavune. Usichochee ugomvi kati ya ndugu wakipatana watakugeuka na wewe utakuwa umejichongea msalaba. Wasaidie kupatana. Usichochee mafarakano. Kuwa na kiburi ni kujitengenezea msalaba. Kutukana watu ni kujitengenezea msalaba.  

Kuna kijana wa miaka thelathini aliyemua baba yake na mama yake. Baada ya kutolewa hukumu aliulizwa kama anaweza kujitetea. Aliomba kupunguziwa miaka akiota hoja yeye ni  mwana yatima hana baba wala mama. Huu ni msalaba wa kujitakia sio kwa sababu ya Yesu. Kuna aina mbili za misalaba: msalaba wenye Yesu Kristu na msalaba usio na Yesu Kristo.  Msalaba wenye Yesu ni pale ambapo unatazama matatizo yako kwa kutumia miwani ya Yesu yaani hakuna Jumapili ya Paska bila Ijumaa Kuu. Ripoti kwa Yesu matatizo yako. Mweke Yesu katika matatizo yako. Msalaba usio na Yesu ni pale ambapo unashindwa kuripoti matatizo yako kwa Yesu. Haubebi mtazamo wa Yesu wa Ijumaa Kuu kwanza Jumapili ya Paska baadaye.
Matatizo ni m\salaba. Kuna ishara ya msalaba. Matatizo yanaweza kuwa ishara ya mafanikio siku za mbeleni. Dalili ya mvua ni mawingu. Dalili ya mafanikio inaweza kuwa matatizo. Kabla ya kufika bandarini kuna mawimbi makali na makubwa. Unaweza kuwa mtu mwema lakini ukateseka. Kwa nini watu wema huteswa na wengine au na jirani. Jirani yako anaweza kuwa msalaba. Sababu ni kuwa watu wema wanafanya mambo mazuri tofauti na wengine. Watu kama hawakuelewi watakutesa. Utendaji kazi wa watu wema unawaibisha wavuvi. Watu katika ofisi wakiamua kubadili  mambo ofisini na wewe haushiriki watakutukana. Watu wema ni kikwazo kwa mipango ya watenda maovu. Utasikia watu wanasema ficha ficha, fulani amekuja. Watu wema hawabadili misimamo yao. Mfano wa Danieli. Mfalme alitaka Danieli abadili msimamo wake. Hakubadili. Alitupwa katika shimo la simba. Lakini kwa mihujiza Mungu alimtoa. Ukiubeba msalaba vizuri utakubeba. Mwanamke anamkataa bosi na kumwambia mme wangu ananitosha na kuniridhisha. Ofisini mwanamke huyo anateswa sababu ya msimamo wao, kwa sababu ya jina la Yesu. Aliapa Kanisani kwa jina la Yesu. Akibeba vizuri msalaba. Msalaba utambeba.


Saturday, September 6, 2014

UJIPENDE USIJEPENDELEE



                                              
                                        JUMAPILI YA MSAMARIA MWEMA
                                    Jumapili ya 23 ya Mwaka A
1. Ezekieli 33: 7-9
2. Woroma 13: 8-10
3. Mathayo 18: 15-20

“Msiwiwe na mtu chochote, isipokuwa kupendana…Mpende jirani yako kama nafsi yako…” (Woroma 13: 8-10)
Mama anayenyonyesha mtoto akiamua kunyonya titi lake mwenyewe na kunywa maziwa ya mtoto jambo hilo halikubaliki. Ni kujipendelea. Mama huyo amejipenda kupita mipaka ya kujipenda. Jambo la msingi ujipende lakini usijipendelee. Kumsaidia mtu hakumaanishi kutojijali au kutojitunza. Anayejihukumu husema yeye ni mzuri wa sura. Hizo ni methali za Afrika ambazo zinasisitiza umuhimu wa kujipenda. Inashangaza kuona kuwa fundi seremala licha ya kutengeneza viti vya kukalia yeye hana kiti hata kimoja nyumbani. Huyo hajipendi. Mtengeneza vyungu vya udongo vya kupikia yeye anakula chakula kutumia kipande cha chungu kilichovunjika. Huyo hajipendi. Itashangaza kuona kuwa mjenzi wa nyumba nzuri sana yeye ana nyumba ya makuti ambayo inaweza kuanguka wakati wowote.
 Jambo la katikati ni kujipenda. Jambo baya kulia kabisa ni kujipendelea, uchoyo, ubinafsi na umimi. Ni kujipendelea kupita kiasi. Jambo baya kushoto kabisa ni kutojipenda, kutojijali, kutojitunza. Kujipendelea ni kujifikiria wewe mwenyewe tu. Kutojipenda ni kujipunguzia heshima au hadhi. Kutojipenda ni kujidhalilisha. Mtu ambaye hajipendi ni mtu ambaye anajidanganya yeye mwenyewe.
Kuna methali isemayo: Watu wanajilamba vidole (sababu ya kutoshiba) wewe unasema mbwa wangu aitwaye simba hajala. Ni methali ambayo inaelimisha umuhimu wa kumtanguliza kwanza binadamu mwenye shida kama mwenye njaa. Njaa ina matokeo mabaya mengi. Mtu mwenye njaa ni mtu mwenye hasira. Ni methali yaw a Igbo wa Nigeria. Utamu haumalizi njaa. Ni methali ya Kenya. Kuna mwanaume mmoja alimwambia mke wake: Haupiki chakula kizuri kama mama yangu.” Naye mwanamke alijibu: “hauna fedha kama baba yangu.” Anayepika vizuri anapika alivyoletewa. Pengine chanzo cha ugomvi huo ni njaa.
Ni mtu mbaya ambaye ni mzuri tu kwa ajili yake tu. Ni ujumbe ambao tunaupata kutoka katika methali ya Haiti isemayo: wewe ni mbaya, kama ni mzuri kwa ajili ya nafsi yako tu. Methali hii inambainisha mtu anayejipendelea. Hatuna budi kujipenda. Kumsaidia mtu hakumaanishi kutojijali. Ni methali ya Mamprussi. Wakati kuna watu wanakula na kusaza kuna ambao wanalala usiku wakiwa na matumbo matupu. “Njaa ni aibu kubwa katika dunia ya leo,” alisema Baba Mtakatifu Yohani Paulo wa II. Biblia yasema “Msiwiwe na mtu chochote, isipokuwa kupendana…Mpende jirani yako kama nafsi yako…” (Woroma 13: 8-10). Tuna deni la kuwalisha wenye njaa. Kuwalisha wenye njaa ni kuwapenda. Baba Mtakatifu Francis, siku ya kuzindua kampeni dhidi ya njaa duniani tarehe 10/12/2013 alisema hivi: “Naalika taasisi zote ulimwenguni, makanisa na kila mtu mmoja, kama familia moja, kuzungumza kwa sauti kuwatetea wale wote wanaoteseka kimya kimy kwa NJAA, ili sauti yetu kubwa iwe kishindo kinachoweza kuutikisa ulimwengu.” Kadiri ya tafiti zilizofanyika, njaa inaua mtu mmoja kila sekunde tano duniani.
Ulimwengu una mali za kumtosha kila mtu, lakini hauna mali za kuwatosha wanaojipendelea. Ni katika mtazamo huo naweza kusema ulimwengu una chakula cha kumtosha kila mtu lakini hauna chakula cha kuwatosha wanaojipendelea. Naye Baba Mtakatifu Francis amekuwa na haya ya kusema: “Ni jambo la kuiabisha na kuleta huzuni kubwa kufahamu kwamba watu wengi duniani wanateseka kwa njaa wakati ulimwengu unacho chakula cha kutosheleza kulisha kila mtu. Hali ya watu kutokuwa na nafasi sawa ya kupata chakula ndiyo kiini cha janga la njaa duniani. Hali hii inazidi kuwa mbaya wakati mashirika makubwa yanapoficha chakula ili kipande bei, kuhamasisha ukulima wa mazao ya kuzalisha nguvu za kuendesha mitambo ya machine kama ‘jatorpher,’ utupaji wa chakula kinachofaa kwa matumizi ya binadamu na ugumu wa kufikia masoko. Haki ya kupata chakula inalinda haki ya msingi ya binadamu ya kutokuwa na njaa.”
 Bwana Yesu alipofanya muujiza wa kuongeza mikate mitano na samaki wawili na kulisha umati wa watu zaidi ya elfu tano watu waliposhiba aliwaambia wanafunzi wake, “Kusanyeni vipande vilivyobaki visipotee bure.” Maneno hayo ni changamoto kwetu kukusanya chakula kinachobaki kisipotee bure maana kuna ambao wanaenda vitandani matumbo matupu.
Nakumbuka sala ya mkristu moja nilipoalikwa katika sherehe ya kuanza  mwaka mpya. Chakula kilikuwa kingi na cha kila aina, yaani meza ilikuwa imechafuka. Mwenyeji wetu alisali hivi, “Baba wa Mbinguni nakushukuru kwa mambo matatu:chakula, hamu ya kula, na watu wakula chakula hiki. Kuna watu wenye hamu ya kula lakini hawana chakula, kuna ambao wana chakula lakini hawana hamu ya kula, kuna ambao wana chakula na hamu ya kula lakini hawana watu wa kula chakula…”Walioathirika na baa la njaa wana hamu ya chakula na watu wa kula chakula lakini shida ni uhaba wa chakula. Unapowasaidia wenye njaa unajipenda maana unajiwekea pointi mbinguni. Unaposhindwa kuwasaidia wenye njaa unajipendelea.
“Si rahisi kuzungumzia amani pale ambapo watu wanateseka kwa sababu ya njaa,” alisema Papa Benedict XVI wakati pia akishutumu wingi wa fedha unaotumika katika kununulia silaha. Ujumbe huu Baba Mtakatifu aliutoa alipozungumza na maafisa wa ubalozi siku ya Jumatatu tarehe 9 mwezi wa Januari 2006.
TUMEUMBWA KUPENDA NA KUPENDWA
 Mtu anaweza kulipa deni la dhahabu, lakini mtu huyo atakufa akiwa katika deni la upendo milele yote. Ndivyo isemavyo methali ya Malaya. Ukiwa unadaiwa shilingi elfu kumi unaweza kulipa lakini sio rahisi kulipa deni la upendo la mke wako, baba yako, mama yako, mme wako, mtoto wako au  mfadhili wako. Licha ya ukweli huo tumeumbwa kupenda na kupendwa. Katika Biblia tuna amri mbili za upendo. Amri ya kwanza ya upendo ni: Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa akili zako zote na kwa roho yako yote. Na  amri ya pili ya upendo ni mpende jirani yako kama unavyojipenda (Mathayo 22: 34 -40).

 Usipopenda unakuwa haujatimiza mojawapo la lengo la kuumbwa kwako. Kama kitabu hakiwezi kusomwa au kosomeka hakijatimiza lengo la kuandikwa kwake. Kama kengele haitoi sauti inapogongwa imeshindwa kufukia malengo ya kutengenezwa kwake. Kama chakula hakiwezi kuliwa au hakiliki hakijafikia lengo la kupikwa kwake. Hivyo hivyo kama binadamu hawezi kupenda na kupendwa ameshindwa kufikia lengo la kuumbwa kwake.

Hasiyekujua hakuthamini. Hatuwezi kumpenda Mungu kama hatumjui. Tunamjua Mungu kupitia mambo mengi. Tukisoma vitabu vitakatifu tunamjua Mungu. Hauwezi kumpenda jirani yako kama haumjui. Asiyekujua hakuthamini. Kuna mtu aliyeaniambia, “Padre usinitambulishe kwa huyo jamaa. Maana nataka kuendelea kumchukia. Nikimjua nitampenda.” Nilichukua nafasi hiyo kuelezea athari na matokeo ya chuki. Chuki humchoma anayeitunza.
Ukimjua Mungu utampenda. Kuna fundi aliyekuwa juu sana ya jengo alitaka mafundi chini wampandishie matofari. Alitupa chini shilingi ishirini toka juu. Fundi aliyekuwa chini aliokota pesa hiyo na kuweka mfukoni hakutazama juu. Alitupa tena “mbao,” fundi mwingine akaiokota bila kutazama juu. Baadaye alitupa jiwe dogo likamgonga fundi mmoja chini. Fundi huyo alitazama juu kwa vile alihumizwa kidogo. Mungu anaweza kutuletea mateso kwa vile anataka kututumia ujumbe Fulani. Mateso hayo yanaweza kuwa ni alama ya upendo. Mama umunywesha mtoto wake dawa chungu ili apone kwa sababu anampenda mtoto wake. Tukijua kuwa Mungu wetu ni Mungu wa namna hiyo tutampenda.
Amri ya pili ya upendo inasema, “Mpende jirani yako kama nafsi yako.” Ni lazima kujipenda na sio kujipendelea ili uweze kuwapenda wengine kama unavyojipenda. Kula chakula ni kujipenda lakini kula robo tatu ya chakula na kumwachia mwenzako aliye na tumbo kama wewe na hamu kama wewe robo tu ya chakula ni kujipendelea. Kuwa na ardhi ni kujipenda, lakini kuwa na ardhi kama jimbo zima la uchaguzi ni kujipendelea.



Counter

You are visitor since April'08