Saturday, September 27, 2014

KUSEMA NA KUTENDA



                                                
                                          JUMAPILI YA 26 YA MWAKA A

1. Ezekieli 18: 25 -28
2. Wafilipi 2: 1-11au Wafilipi 2: 1-5
3.  Mathayo 21: 28 -32
UTANGULIZI
Matendo yanapozungumza maneno si kitu. Sisi tunajiendesha kama watoto. Tunasema  ndiyo, lakini hatufanyi kitu, pengine tunakataa kwanza na baadaye tunajuta na kutimiza tunayoambiwa. Tumuombe Mungu katika adhimisho la leo atuepushe na mazoea ya kutamka maneno ya ndiyo ndiyo bila kutimiza kwa matendo.
MAHUBIRI YENYEWE
Mgeni  mmoja alitembelea nchi ya Poland enzi za ukomunisti. Alioneshwa maeneo mengi na mwanachama  wa chama tawala. Mgeni alimuuliza mwanachama huyo, “Je, wewe ni mkatoliki?” Mwanachama huyo alijibu, “Naamini lakini sitendi.” Mgeni baadaye alimuuliza, “Je, wewe ni mkomunisti?” Ofisa huyo alitabasamu na kujibu, “Natenda, lakini siamini.” Dini ya Kikristu inawadai wanachama wake kusema na kutenda yaani kuhubiri maji  na kunywa maji na si kuhubiri maji na kunywa divai. “Jibu fupi ni kutenda,” alisema Lord Herbert. Ahadi ni mawingu kutumiza ahadi ni mvua. Haitoshi kuahidi lazima kutenda. “Tendo ni lugha ya kushawishi,” alisema William Shakespeare.
Neno zuri ni zuri, tendo zuri ni zuri zaidi. Kwa msingi huo matendo yana kauli kuliko maneno. Maneno matupu hayajengi ghorofa. Si kwa kusema asali asali utamu unaingia mdomoni. Utukufu hauji kwa kuuita. Ni methali ya Kenya. Matendo yanapozungumza maneno si kitu. Kuna methali ya Kiafrika isemayo, “Sikusikii matendo yako yananipigia kelele.” Kwa matendo yake tunamjua mtu. Watu wote wanaweza kuzungumza lakini si watu wote wanaweza kutenda. “Neema haitolewi kwa wale ambao huzungumzia juu ya imani yao lakini kwa wale ambao wanaishi imani yao,” alisema  Mt. Gregory.
Injili ya leo inatupa umuhimu wa matendo. Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; akamwendea yule wa kwanza, akasema, ‘Mwanangu, leo nenda kafanye kazi katika shamba la mizabibu,’ Akajibu akasema, ‘Naenda, Bwana; asiende. Akamwendea yule wa pili, akasema vilevile. Naye akajibu akasema, ‘Sitaki; baadaye akatubu, akaenda. Je, katika hao wawili ni yupi aliyefanya mapenzi ya babaye?” Wakamwambia, “Ni yule wa pili.” Basi Yesu akawaambia, “Amin, nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu” (Mathayo 21: 28 – 31). “Tunachoweza kujifunza katika mfano huu Bwana aliwazungumzia wale ambao wanaahidi kidogo au hawaahidi chochote lakini katika matendo wanafanya makubwa na dhidi ya wale ambao wanaahidi makubwa lakini hawafanyi lolote kati ya wale ambao wameaahidi,”  alisema Origen Baba wa Kanisa.
Baba wa Kanisa Jerome alikuwa na haya ya kusema, “Mungu anazungumza kwanza kwa watu wa mataifa kupitia kanuni ya maumbile; ‘Nenda kafanye kazi katika shamba langu la mizabibu;’ ni kusema, ‘Mtendee mwenzako kama unavyotaka akutendee’ (Tobiti 4:16). Alijibu kwa majivuno , ‘Sitaki.’  Kumbe aliyesema nitaenda baadaye akwenda ni wayahudi wasio waaminifu. Mzabibu ni taifa teule la Israeli (Isa 5:1). Mwenye shamba ni Mungu. Watumwa wake ndio manabii. Mwanae ndiye Yesu. Wakulima wauaji ndiyo wayahudi wasio waaminifu. Watu wengine watakaoaminishwa shamba la mizabibu ni watu wa mataifa yaani wapagani.

Mfano huu ni mfano juu ya watoto wabaya wawili. Ni mtoto yupi kati ya hao wawili angekuwa mtoto wa kuigwa au mfano wa kuigwa? Yule anayesema hapana ya herufi kubwa mbele ya baba yake au yule anayesema ndiyo. Jibu ni kuwa hayupo hata mmoja wa kuigwa. Mtoto ambaye ni mfano wa kuigwa ni yule anayesema ndiyo na kuweka katika matendo. Yesu alisema: “Si kila mtu aniambiaye :Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni, bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni” (Mathayo 7:21).  
Maneno “umefanya vizuri” ni mazuri zaidi kuliko maneno  “umesema vizuri.”  Ni maneno ya Benjamini Franklin (1709-1790) mmojawapo wa Waasisi wa Amerika, mwandishi na mwanadiplomasia. Mwanasiasa huyu alitaka kusema matendo yana kauli kuzidi maneno. Maneno haya yanabainisha maana ya methali au msemo wa Kenya: Kusema na kutenda. Haitoshi kusema kunahitajika kutenda pia. “Muwe watimizaji wa neno, si wasikiaji tu; kama sivyo, mnajidanganya wenyewe” (Yakobo 1:22). Dini ni ya matendo.
Haitoshi kusema tu lazima tutende. Kunda kijana aliyemtumia mchumba wake ujumbe wa simu wenye maneno haya: “Nakupenda sana kiasi cha kupanda mlima mrefu kwa ajili yako. Nakupenda sana kiasi cha kuweza kuogelea kwenye mto TANA kwa ajili yako. Ninaweza kupitia katikati ya moto kwa ajili yako. Naweza kunyeshewa mvua kwa ajili yako. Naomba tukutane kesho saa nane kama mvua haitanyesha.” Maneno hayo ni mazuri lakini ni maneno matupu bila matendo. Kwa nini baadaye kijana anaogopa mvua.
Wanandoa siku ya kufunga ndoa wanaulizwa juu ya upendo: Padre kwanza anamuuliza Bwana arusi: F. unampokea F. awe mke wako, tena waahidi kuwa mwaminifu kwake, katika taabu na raha, katika magonjwa na afya, umpende na kumheshimu siku zote za maisha yako?” Kisha padre anamuuliza bibi arusi; F. unampokea F. awe mume wako, tena waahidi kuwa mwaminifu kwake, katika taabu na raha, katika magonjwa na afya, umpende na kumheshimu siku zote za maisha yako?” Jibu ambalo hutolewa huwa ndiyo. Hiyo ni kusema kunabaki kutenda.
Ukisema mimi ni “memba” au muumini wa Kanisa. Jambo hilo liweke katika matendo. “Memba” au mwenye hisa ni mmojawapo wa wamiliki wa kampuni au chama. Wewe kama ni “memba” jua Kanisa ni lako. Jenga chako. Lakini “Asiyekujua hakuthamini.” Lijue Kanisa. Kanisa lina mafiga matatu: padre, mtawa na mlei. Mafiga mawili hayaivishi chungu. Kazi yote hawezi kuaachiwa padre na mtawa. Mafiga mawili hayaivishi chungu. Mlei ujue Kanisa ni lako. Mtawa ujue Kanisa ni lako. Padre ujue Kanisa ni lako.
Ukiimba wimbo wa “Mkristu miye niko salama…” Wimbo huo ukauweke katika matendo. Lisaidie Kanisa. Shilingi moja na shilingi mia moja zilikuwa na mazungumzo. Shilingi moja iliuliza, “Wewe shilingi elfu moja ya Kenya (17,000/= Tshs) umetembelea sehemu zipi?” Shilingi mia moja ya Kenya ilijibu, “Nimetembelea mabenki yote. Nimekuwa sehemu za starehe zote, hoteli kubwa kubwa, nimekukaa sana supermarket, nimelala mara nyingi Dubai, China. Jew ewe shilingi moja unakaa wapi?” Shinlingi moja ilijibu. “Mimi nitafute kwenye makanisa ya Kanisa la Peter Claver, Consolata, Yohane Mbatizaji.” Ukristo ni matendo. LISAIDIE KANISA LIKUSAIDIE. Kama unajiita mkristu lazima kuhudhuria vikao, adhimisho la ibada ya misa, mikutano ya Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristu. “Watu wangapi wanahudhuria katika Kanisa lako?” Mchungaji mmoja alimuuliza mwingine.” Mchungaji alifikiria kidogo halafu alijibu, “60 wapo kila mara, 250 C na E.” “Nini maana ya C na E?” Mchungaji alitaka kujua. “Maana yake ni Christmasi na ‘Easter” yaaani Paska.
Kupenda ni kitenzi. Upendo ukibaki ni nomino ni nomino dhahania. Upendo husipotolewa hudumaa na ukitolewa unakua. Tutoe upendo kwa waliotuzunguka baadaye upendo upae kuwaendea wengine. Kuna mtoto aliyemuuliza mama yake, “Tupo hapa duniani kwa ajili ya nini?” Mama alimjibu, “Tupo hapa kwa ajili ya kuwapenda wengine.” Na mtoto akazidi kudadisi, “ Wengine wapo kwa ajili ya nini?” Kuna watu wanafikiri wapo kwa ajili ya kupendwa na si kupenda. Mungu ametuumba kwa ajili ya kupenda na kupendwa. Upendo ambao haujawekwa katika vitendo ni kama ujumbe wa simu ulioandikwa lakini ukasahau kuutuma. Ni kama barua ambayo umeandika ukasahau kuipeleka posta. Upendo ukibaki ni jina tu au nomino tu ni nomino dhahania lakini lazima uwe kitenzi-kupenda ni kitenzi.

Counter

You are visitor since April'08