Saturday, December 13, 2014

JE UNA FURAHA?



                                               JUMAPILI YA 3 YA MAJILIO                                          

1. Isa 61: 1-2. 10-11
2.  1 Wath 5: 16 -24
3.  Yoh 1: 6-8. 19-28

Mungu wetu ni Mungu anayetaka uwe na furaha daima. Kufurahi ni wajibu. Una mawazo unayowawazia watu lakini Mungu anakuwazia mambo mazuri. Furahi kila wakati. Unafikiria watu Mungu anakufikiria. Furahi kila wakati. Tunapofanya tunaloweza, Mungu atafanya tusiloweza. Kwa namna hiyo tunaye Mungu anayeleta furaha. Furahi kila wakati. Jumapili hii katika Kanisa Katoliki inaitwa Jumapili ya Furaha. Furahi kwa kilatini “Gaudete.” Hatuna budi kufurahi sababu Yesu Kristo atazaliwa mioyoni mwetu siku ya Krismasi. Mtume Paulo anatushauri kwa msisitizo. ““Furahini kila wakati” (1 Wathesalonike 5:16). Pia mtume Paulo anasisitiza mahali pengine. “ Basi, furahini daima katika kuungana na Bwana! Nasema tena: furahini!” (Wafilipi 4:4).
 Wito ni furahi kila wakati. Katika insha moja iliandikwa kuwa mtoto anacheka mara 200 kwa siku. Mtu mzima anacheka mara 4 kwa siku. Kitabu cha mhubiri kinasema kuna wakati wa kucheka na wakati wa kulia. Kwa nini tofauti hii1. kubwa kati ya mtoto na mtu mzima? Furaha haitegemei mahali ulipo. Adamu na Eva walikuwa kwenye Bustani ya Eden, lakini baadaye hawakuwa na furaha baada ya kumkosea Mungu. Lucifer kadiri ya masimulizi ya maandiko matakatifu aliyekuwa mbinguni alimkosea Mungu na kukosa furaha. Alitumuliwa huko.  Alikuwa mbinguni hakuwa na furaha. Mtume Paulo anatualika, “Furahini kila wakati” (1 Wathesalonike 5:16). “Wanasema mtu anahitaji mambo matatu kuwa na furaha kweli katika dunia hii: nafsi  ya kupenda, kitu cha kufanya, na jambo la kutumainia,” alisema Tom Bodet.
Hakuna mtu anayependa Krismasi imkute kifungoni au jela. Taarifa ambazo huwa tunazipata toka zahanati na hospitalini ni kuwa wakati wa Krismasi wagonjwa wanapungua wadini. Hakuna ambaye anapenda Krismasi imkute wadini. Lakini ugonjwa haubishi hodi na hauna kalenda. Kipindi cha Krismasi ni kipindi cha kufurahi. Mtume Paulo anatukumbusha, “ Basi, furahini daima katika kuungana na Bwana! Nasema tena: furahini!” (Wafilipi 4:4). Krismasi inakaribia furahini. Mtume Paulo alipoandika barua kwa wafilipi mnamo mwaka 55 baada ya Kristo kuzaliwa alikuwa kifungoni. Licha ya kuwa katika matatizo alivaa vazi la furaha.
Daraja kati ya furaha na mateso sio ndefu. Wakati mwingine kuna furaha baada ya mateso. Kama tusemavyo, baada ya dhiki faraja. Kuna watu ambao wana furaha, wengine wana mateso. Baadhi ya watu wanakaa na kicheko na tabasamu utafikiri wana matangazo ya biashara ya dawa ya meno wanayotumia. Wengine wanakuwa na ndita za hasira usoni. Kuna ambao wanaambiwa usicheke uko kanisani. Kuna methali zinazobainisha ukweli huu: furaha ya mwenye meno, kibogoyo hashiriki, furaha ya kima mbwa hashiriki. Tofauti hizi zinatufanya tujiulize nini chemchemi ya furaha? Kwa wakatoliki Jumapili hii kabla ya Krismasi inaitwa Jumapili ya Furahi kwa kilatini “Gaudete.” Hatuna budi kufurahi sababu Yesu Kristo atazaliwa mioyoni mwetu siku ya Krismasi. Mtume Paulo anatushauri: “Furahini kila wakati. Salini bila kuchoka. Fanyeni shukrani katika yote” (1 Wathesalonike 5:16-18). Katika haya hii ya Biblia tunapata chemchemi ya furaha.
Kuthamini mtu na kushukuru kunaleta furaha. Unaposhukuru mtu ina maana unathamini zawadi yake naye unamthamini. Katika msingi huu unaweza kusema furaha yako ni furaha yangu. Furaha ya mwenzako iwe furaha yako. Katika msingi huu methali ya Kiswahili inasema, “Mzazi yeyote hufurahi amwonapo mtoto wake akicheka. Methali hii hutufunza kuwa mzazi yeyote humthamini mtoto. Kila mzazi hufurahi mwanawe anapoishi maisha ya furaha. Usipende pesa ukawatumia watu bali upende watu utumie pesa. Kwa maneno mengine thamini watu upate ya watu. Thamini watu upate furaha.

FURAHA IPO KATIKA KUPENDA NA KUPENDWA
Nafsi ya kwanza ya kupenda ni Mungu. Katika hili Mtakatifu Augustini alisema, “Hatutulii tutatulia katika Mungu.” Katika Mungu kuna furaha kamili. Kupendwa na Mungu ni furaha. Kumpenda Mungu ni furaha. Mungu huyu amejificha kati yetu. Yohane anasema, “katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi” (Yohane 1: 26). Katika Yesu Kristo Mungu amevaa ubinadamu wetu. Mungu wetu ni “Mungu aliyejificha.” Lakini anatufanyia makubwa nyuma ya pazia. Ni kama Mwandishi wa maisha ya mtu mwingine. Haonekani katika kitabu lakini anafanya mambo mengi. Kuna watoto ambao walikuwa wanacheza mchezo wa kujificha. Mtoto mmoja alipojificha hawakwenda kumfichua. Alipotoka kwenye maficho akakuta wanaendelea na mchezo mwingine. Mungu amajificha. Amejificha katika viumbe vyake mpaka watu tunachoka kumtafuta. Tunaambiwa “katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi” (Yohane 1: 26). Yupo kati ya wagonjwa. Yupo kati ya maskini. Yupo kati ya wageni.
Kutulia katika Mungu ni chemchemi ya furaha. Mtakatifu Augustini wa Hippo Afrika ya Kaskazini alisema, “Wewe umetufanya kwa ajili yako mwenyewe na mioyo yetu haitulii mpaka inapotulia ndani yako.” Tutakuwa na furaha kamili na ya kweli tutakapotulia katika Mungu, katika kutimiza mapenzi na amri za Mungu. Andika mipango yako kwa kalamu ya mtI Mungu mwenyewe ana mfutio. Msemo wetu uwe Bwana akipenda au msemo maarufu wa kiarabu Inshallah. Inatupasa kusema, “Bwana akipenda tutakuwa wazima bado na kufanya hiki na hiki” (Yakobo 4:15). Chemchemi ya furaha kamili haitokani na matukio yanatokea au mazingira tuliyomo. Inatoka katika Mungu anayekuwa ndani mwetu. Kutulia katika Mungu kunahitaji unyenyekevu. Kuna kijiji kimoja kilivamiwa na watu wakatili kuna mtoto wa miaka kama kumi na mawili ambaye alikuwa mlemavu wa miguu. Hivyo wazazi walipokimbia hakuwa na uwezo wa kukimbia walimwambia akae kama amekufa hivi. Hivyo aliachama. Maadui walipofika walishangaa usafi wa meno yake wakasema huyu amekufa lakini ana meno mazuri na masafi sijui anatumia dawa gani. Mtoto huyu akasema, “Natumia colgate.” Majivuno yalimuingiza hatarini wakajua hajafa. Nyenyekea ule vya Mungu na watu. Kukiri hali ya kumtegemea Mungu ni msingi wa furaha. Mungu ni nguvu yako. Mungu ni ngome yako.
Nafsi ya pili ya kupenda ni mtu mwingine au watu wengine. Kupendwa na watu ni furaha. Kupenda watu ni furaha. Ya mwisho ni nafsi yako. Kuwapenda wengine kama ambavyo unajipenda ni furaha.

FURAHA IPO KATIKA MATENDO MEMA
Furaha ipo katika kufanya kitu fulani hasa kutenda wema. “Furaha sio kitu ambacho kimetengenezwa tayari. Kinatoka katika matendo yako,” alisema Dalai Lama XIV. Matendo yanayozungumziwa ni matendo mema. Mtume Paulo anazidi kutuasa, “Kagueni yote: yaliyo mema yashikilieni. Mabaya ya kila namna yaepukeni” (1 Wathesalonike 5: 22). “Ukifanya mambo mazuri, watu watakushitaki kuwa una nia ya kujinufaisha iliyofichika, fanya mazuri vyovyote vile. Kama umefanikiwa,utajipatia marafiki ambao sio wa kweli na maadui kweli, fanikiwa vyovyote vile. Zuri utakalofanya leo litasahuliwa kesho, fanya jambo zuri vyovyote vile. Ukweli na uwazi vinaweza kukufanya udhuriwe. Kuwa mkweli na muwazi  vyovyote vile.  Watu wakubwa wa kike na kiume wenye mawazo makubwa wanaweza wanaweza kushushwa na watu wadogo wa kiume na kike wenye mawazo madogo. Fikiria makubwa vyovyote vile. Watu huwapenda watu wanaoonewa lakini huwaiga washindi tu. Pigania wanaoonewa vyovyote vile. Unachotumia  miaka mingi kujenga kinaweza kuharibiwa usiku mmoja. Jenga kwa vyovyote vile. Watu wanahitaji msaada kweli lakini wanaweza kukushambulia kama ukiwasaidia. Wasaidie vyovyote vile. Ipe dunia zuri ulilonalo utakabiliana na upinzani. Ipe dunia zuri kwa vyovyote vile,” aliandika Kent M. Keith. Katika kuwasaidia wengine kuna furaha. Kuna methali ya Kichina isemayo, “Ukitaka furaha kwa saa, lala. Ukitaka furaha kwa mchana wote, nenda kuvua. Ukitaka furaha kwa mwaka mmoja urithi mali. Ukitaka furaha kwa maisha yako yote, saidia mtu.”

FURAHA IPO KATIKA MATUMAINI
Kuwa na jambo la kutumainia kunaleta furaha. Mgonjwa akiwa kwenye chumba cha kungojea daktari wakimwambia kuwa daktari atakeyemtibu ni daktari bingwa, anakuwa na matumaini na matumaini hayo yanamletea furaha. Sasa hivi wakristu wanatumainia baraka na neema za Krismasi jambo kubwa zaidi Yesu azaliwe katika mioyo yao.  Lakini katika mateso na shida tunaweza kuwa na furaha. “Ni vigumu kusahau maumivu, lakini ni vigumu zaidi kukumbuka utamu. Hatuna makovu ya kuonesha furaha. Tunajifunza machache kutoka kwenye amani,” aliandika Chuck Palahniuk katika Diari yake.

FURAHA IPO KATIKA MAWAZO CHANYA
“Sio kile ulichonacho, au cheo ulichonacho au mahali ulipo panakufanya uwe na furaha. Ni kile unachofikiria juu yake,” aliandika Dale Carnegie. Furaha inakutwa katika kusema ndiyo ikawa ndiyo kweli na hapana ikawa hapana kweli. “Furaha ni pale unachofikiria, unachokisema na unachokitenda vinapatana kikamilifu,” alisema Mahatma Gandhi. Zaidi ya hayo furaha ni suala la mtazamo chanya.
GHARAMA YA FURAHA
Tukumbuke kuwa furaha inapatikana kwa gharama. Wanaoenda kupanda kwa machozi. Watavuna kwa kelele za shangwe. “Tunapotaka kuifikia furaha ya kweli kwa bei rahisi, tutaikuta imefungwa kama kitu cha bei rahisi,” aliandika  David Roberts katika kitabu chake, “The Grandeur and Misery of Man, 1955. Vya bei rahisi huenda visilete furaha. Ni katika msingi huu Yesu alisema anayetaka kunifuata ajitwike msalaba wake anifuate.
KUSHIRIKISHANA FURAHA
Furaha ni kamili unapowashirikisha wengine. “Furaha ndilo jambo pekee ambalo linaongezeka mara mbili unapowashirikisha wengine,” alisema Albert Schweitzer. Maneno hayo yalikwekwa namna nyingine na Ralph Ingersoll, “Njia ya kuwa na furaha ni kuwafanya wengine wawe na furaha.” “Furaha ni ya kweli tu wengine wanapoishiriki,” alisema Jon Krakauer
FURAHA IPO KATIKA FADHILA
Furaha ipo katika kuwa na fadhila. Unataka kuwa na furaha kuwa mpole. “Kwa kila dakika unayokasirika unapoteza sekunde sitini za furaha,” alisema Ralph Waldo Emerson. Unataka kuwa na furaha, kuwa na kiasi. Unataka kuwa na furaha kuwa na shukrani. Kiasi ni chemchemi ya furaha. Kiasi ni fadhila inayoratibu mvuto wa furaha. Fadhila inakuwa katikati. Furaha ni kituo cha njiani kati ya mengi sana na machache sana. Mfano unyenyekevu upo katikati ya majivuno na kujidhalilisha ambako ni kujinyenyekesha kupita kiasi. Ukarimu upo katikati ya uchoyo na kutapanya hovyo. Kutapanya hovyo ni ukarimu uliozidi mipaka. “Majonzi yanaweza yakajishughulikia yenyewe, lakini kupata thamani yote kabisa ya furaha lazima uwe na mtu wa kugawana naye,” alisema Mark Twain.

Counter

You are visitor since April'08