Wednesday, December 24, 2014

JE UNAKUMBUKWA?



                                                  
  


                                                     NOELI USIKU
1. Isa 9: 1-6
2. Tit 2: 11-14
3. Lk 2: 1-14


“Zawadi kubwa sana maishani ni kukumbukwa,” alisema Ken Venturi. Siku ya Krismasi tunampa zawadi kubwa sana mtoto Yesu zawadi ya kumkumbuka. Siku ya Krismasi tunampa zawadi kubwa sana Bikira Maria zawadi ya kumkumbuka. Siku ya Krismasi tunampa zawadi kubwa sana Mtakatifu Yozefu  zawadi ya kumkumbuka. Siku ya Krismasi tunalipa hori zawadi kubwa sana alipozaliwa mtoto Yesu zawadi ya kulikumbuka. Hatumkumbuki meneja wa Nyumba ya Wageni aliyewanyima nafasi. Tunasoma hivi katika Biblia: “Walipokuwa huko, siku yake ya kujifungua ikawadia, akajifungua mtoto wake wa kwanza wa kiume, akamvika nguo za kitoto, akamlaza horini kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni” (Luka 2: 6 -7). Kuna mambo saba ya kukumbukwa siku ya Krismasi.


Kwanza, Mtoto Yesu anapewa zawadi kubwa sana zawadi ya kukumbukwa. Kuna aliyemuuliza mtoto, “je umepata kile ulichohitaji katika Krismasi hii?” Mtoto alijibu sikupata kila nilichohitaji na kila nilichotegemea. Lakini hata hivyo siku ya leo siyo siku yangu ya kuzaliwa ni siku ya kuzaliwa Yesu Kristu.”  Ni vizuri watoto watambue kuwa Krismasi siyo siku yao ya kuzaliwa (labda kama mtoto alizaliwa tarehe 25/Desemba naye atakuwa anasherekea siku yake ya kuzaliwa) ni siku ya Kuzaliwa Yesu Kristu. Tatizo tunaweza kutekwa na kile kinachouzwa na kununuliwa tukamsahau yule aliyesababisha vitu vyenye maneno: “Heri ya Krismasi” viuzwe. Naye ni Yesu. Maneno ya kutakiana heri: Heri Krismasi; Baraka ya Krismasi; Furaha ya Krismasi yatukumbushe juu ya Yesu ambaye ni baraka kwa dunia. Kwa sababu yake kuna mabadiliko. Wafuasi wa Yesu wanafanya mengi ya maendeleo. Kuna Hospitali zimejengwa na madhehebu ya Kikristu. Vyuo vimejengwa kwa sababu Yesu alikuja. Inasikitisha kadi za Krismasi zinapokuwa hazina mchoro au “picha” ya Yesu. Krismasi bila Yesu ni bure.

Pili, Bikira Maria Mama wa Yesu anapewa zawadi kubwa sana ya kukumbukwa: Hakuna Krismasi bila Mama Maria Mama wa Yesu Kristo. “Hapa hakuwepo mkunga, hapakuwepo wasiwasi uliojaa huruma wa wanawake; alimvisha Yesu nguo za kitoto, yeye akiwa mama na mkunga,” alisema Mtakatifu Jerome. Ni kama “Mkunga” na “Nesi” katika Agano Jipya. Jambo kubwa na zuri sana ambalo baba anaweza kuwafanyia watoto ni kumpenda mama yao. Na jambo kubwa ambalo tunaweza kumfanyia Yesu mkombozi wetu ni kumpenda mama yake. Tuwaenzi wakina mama, tuwaheshimu wakina mama. Uchungu wa mwana aujuaye mzazi. Titi la mama li tamu, jingine halishi hamu. Mama ni mama ajapokuwa rikwama, hata akiwa na upungufu ni mama. Mama hamkani mwanawe japo awe kilema. Kuna watu ambao hutaka kulinganisha wakina mama. Mama wa Yesu hawezi kulinganishwa na mwanamke yeyote. Kuna Bwana mmoja aliyemwambia mke wake: “Chakula unachopika sio kitamu kama chakula mama yangu alikuwa anatupikia.” Mwanamke naye akamjibu: “Ni sawa, lakini hata mshahara wako ni mdogo ukilinganisha na mshahara baba yangu alikuwa anapata.”
Bikira Maria ni MAMA. Tafakari neno “MAMA.” Herufi ya Kwanza “M” inasimama badala ya Milioni ya vitu alivyokupa mama. “A” asante. Anastahili asante kwa mamilioni ya vitu alivyokupa. Waluhya wa Kenya wana methali isemayo: “Nyama choma haiwezi kuwa tamu sana ukasahau aliyeichoma.” Mama Maria anastahili asante kwa kukubali kumzaa mkombozi Yesu. “M” inasimama badala ya “Malezi” Mama analea mimba na analea mtoto. Mama Maria alilea mimba, mtoto Yesu akiwa tumboni. “A” inasimama badala ya “Adabu,” onyesha adabu kwa mama.

 Tatu, Mtakatifu Yozefu anapewa zawadi kubwa sana ya kukumbukwa: Jina Yozefu  linatokana na neno la kiebrania lenye maana: na aniongezee mwingine. Papa Leo XIII alikuwa na haya ya kusema juu ya Mtakatifu Yozefu, “Mtoto aliyekuwa anatishiwa na wivu wa mfalme alimkinga asiuawe na alimtafutia mahali pa kukimbilia; katika shida za safari na katika makali ya ukimbizi alikuwa daima mwenzi na msaada, mtetezi wa Bikira na Yesu.” Yozefu anakumbukwa kama baba mwema. Changamoto kwa wanaume ni kukumbukwa na watoto kama baba mwema. “Natumaini nakumbukwa na watoto wangu kama baba mwema,” alisema Orson scott Card.
Nne, Nguo za kitoto alizovikwa Yesu zinapewa zawadi kubwa ya kukumbukwa: Siku ya Krismasi tunazipa zawadi kubwa sana nguo za kitoto alizovikwa mtoto Yesu, tunazikumbuka. “Yeye aliyevisha dunia yenye uzuri wa aina mbalimbali alivikwa nguo za kawaida za kitani, ili tuweze kupokea vazi zuri sana; yeye ambaye vitu vyote vimafanyika, mikono yake na miguu  vinakunjwa ili mikono yetu iinuliwe kwa kila kazi tuifanyayo, na miguu yetu iongozwe katika njia ya amani,” alisema Baba wa Kanisa Bede. Tukumbuke vazi tulilovishwa tulipobatizwa.

Tano, Horini alipowekwa mtoto Yesu panapewa zawadi kubwa sana ya kukumbukwa: “Anafungiwa mahali padogo pa hori baya, ambaye kiti chake kilikuwa mbinguni, ili atupe chumba cha kutosha katika furaha za ufalme wa mbinguni. Yeye  ambaye ni mkate wa mbinguni analazwa horini, ili atushibishe kama wanyama walivyokuwa wanashibishwa,” alisema Baba wa Kanisa Bede. Kuingia horini ilibidi mtu kuinama, ishara ya unyenyekevu. Alitaka watakaoingia waingie kwa mtindo wa unyenyekevu. Horini alipozaliwa Yesu alizungukwa na wanyama. Kwa wayahudi wanyama kama ilivyo kwa Wamasai walikuwa ni ishara ya utajiri. Bwana Yesu alizungukwa na ishara ya utajiri kuonesha alikuja kututajirisha. Katika kupambana na umaskini ni vizuri hilo likasisitizwa vinginevyo tunaweza kuwaprogramu watu kuwa maskini (Umaskini wa kiroho ni muhimu lakini ulalahoi si muhimu). Ingawa watakatifu wengi wametokea “Slum” hatuwezi “kuendekeza” slums ili tuwapate watakatifu.

Sita, Bethlehemu alipozaliwa Yesu panapewa zawadi kubwa sana ya kukumbukwa. Hapo pamejengwa Kanisa. Bethlehemu maana yake ni nyumba ya mkate. Yeye aliyejitambulisha kama Mkate alizaliwa mahali penye maana ya Nyumba ya Mkate. “Ee Bethlehemu nchini Yudea, wewe si mdogo kamwe kati ya miji maarufu ya Yudea; maana kwako atatokea kiongozi atakayewaongoza watu wangu Israeli” (Mathayo 2: 6). Changamoto: “Kama Kristu anazaliwa mara elfu moja Bethlehemu na si katika moyo wako, umepotea milele yote,” alisema Angelus Silesius (1624-1677). Umuhimu wa mtu si mahali anapokaa na mahali anapotokea, au mahali alipozaliwa. Baraka Obama Rais wa Amerika ametokea Kijiji cha Kogelo huko Kisumu lakini sasa ni Rais wa Amerika. Hakutoka New York. Hakutokea Tel Aviv. Hakutokea London. Yesu hakutokea jiji la Yerusalemu. Alizaliwa Bethlehemu. Alitokea Nazareti, kijiji kilichodharauliwa sana kama tunavyosoma katika Biblia “Naye Nathanaeli akamwuliza Filipo, “Je kitu chema chaweza kutoka Nazareti?” Filipo akamwambia, “Njoo uone” (Yohane 1: 46).
Saba, usiku mtulivu na mtakatifu unapewa zawadi kubwa sana ya kukumbukwa. Kipindi cha Krismasi unaimbwa wimbo ambao umevuta nyoyo za watu “Silent Night” ambao umetafsiriwa kwa Kiswahili: Usiku mkuu! Usiku Mtakatifu! Uko utulivu; Bikira amezaa Mwana, Mtoto Mtakatifu ni Bwana; Alale amanini, Alale amanini.” Wimbo huu unazungumzia ukimya, utulivu, ukuu na utakatifu wa usiku alipozaliwa Yesu. Utulivu huu na ukimya huo ni wito wa kuwa na utamaduni wa kuwa kimya na kutulia. Wakati wa vita ya kwanza ya dunia Krismasi ya mwaka 1914 vikosi vyote vilivyokuwa vinapigana viliweka silaha chini na kuimba wimbo wa “Silent Night.” Kelele za bunduki zilisimamishwa. Lakini pongezi ingekuwa kama kelele hizo zingesimamishwa siku zote na sio usiku tu wa Krismasi. Utamaduni wa kutochafua hewa kwa kelele lisiwe suala la Krismasi tu. “Tunahitaji kumtafuta Mungu, na hapatikani katika kelele na kutotulia. Mungu ni rafiki wa ukimya. Tazama viumbe – miti, maua, nyasi vinakua katika ukimya; tazama nyota, mwezi na jua vinafanya mambo katika ukimya.. Tunahitaji ukimya kuweza kugusa nyoyo za watu,” alisema Mama Tereza wa Calcutta.
Kila mtu ajiulize anakumbukwa kwa lipi na atakumbukwa kwa lipi. Tenda wema huende zako wema hauozi. Tunasoma katika Biblia. “Habari kuhusu tukio hilo iliandikwa katika kitabu cha kumbukumbu mbele ya mfalme” (Esta 2:23). Matendo yako mazuri yataandikwa katika kitabu cha “Guiness” cha Mungu.
Kijana mwenye umri wa miaka kumi na nane alienda karibu na Ghala la Dawa na kutoa kreti ya soda aitumie kufikia kwenye sanduku la kupigia simu. Alisimama juu ya kreti ya soda na kubonyeza vitufe (buttons) za namba saba. Mmiliki wa Ghala ya Dawa alisikiliza mazungumzo: Kijana alisema, “Mama unaweza kunipa kazi ya kukata nyasi kwenye uwanja wako? Mama huyo alijibu, “Tayari nina mtu anayekata nyasi katika uwanja.” Kijana alisema, “Mama nitaka nyasi kwenye uwanja nusu ya gharama ya mtu anayekata nyasi katika uwanja wako.” Mama huyo alijibu, “Ninaridhika na kazi anayoifanya mfanyakazi wangu.” Kijana akionesha uvumilivu alisema, “Mama, nitafagia njia na vinjia katika eneo lako lote bure.”  Mama huyo alijibu kwa mkato, “Hapana, nashukuru.” Akiwa amevaa tabasamu, kijana huyo alimaliza mazungumzo. Mmiliki wa Ghala ya Dawa alisema, “Kijana nimependa mtazamo wako juu ya kazi nataka nikupe kazi.” Kijana alijibu kwa ufupi, “Hapana, nashukuru.” Mmiliki wa Ghala ya Dawa alimjibu, “Lakini ulikuwa unaomba sana upewe kazi.” Kijana alisema, “Nilikuwa nataka kujua kipimajoto cha kazi kikoje, kama mama ninayemfanyia kazi anaridhika na ananikumbuka kama mchapakazi.” Ndugu utakumbukwa kama Yozefu – Mfanyakazi? Ndugu utakumbukwa kama Bikira Maria – Mama mkimya aliyeweka yote moyoni? Ndugu utakumbukwa kama mtoto Yesu aliyekua katika umbo na hekima?


Counter

You are visitor since April'08