Jumapili ya 19 ya Mwaka A
“Ewe mwenye
imani haba mbona uliona shaka” (Mathayo 14:31)
1. Fal 19:9a, 11-13a
2. Rum 9: 1-5
3. Mt 14:
22-33
Kwanza kuamini mpaka kuamini ni
kuonyesha au kutangaza nia. Penye nia pana njia. Mtume Petro alipoona Yesu anatembea
juu ya maji alionesha nia ya yeye kutaka kutembea juu ya maji. Petro alimwambia Yesu: “Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru
nije kwako juu ya maji.” Petro alitangaza nia. Alionesha nia. Siku moja
niliambatana na mchungaji kwenda kwenye yadi ya magari kumsaidia kuchagua gari
zuri. Tulipofika pale tuliona magari mengi, tukaingia ndani na kuyakagua: Mark
II, Toyota Corolla, Suzuki, Rava 4, Pick up, kutaja machache. Baada ya masaa
mawili ya kukagua na kutazama nilimwambia, “Naomba tuchague sasa gari ambalo
utanunua.” Alinijibu:
“Kusema kweli sina hata shilingi.” Nilimwambia: “Kwa nini usumbufu wote huu.”
Alinijibu: “Namwonyesha Mungu nia yangu.” Onesha nia. Ukitaka kununua shamba
hata kama huna hela, ulizia bei kwanza, kagua viwanja vilipo. Sala yetu iwe
kama ya kijana mmoja kwenye Biblia, “Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu”
(Marko 9: 24). Petro kwa upande mmoja alikuwa na kuamini na kwa upande mwingine
alikuwa na kutoamini. Kutangaza nia tu hakutoshi.
Pili, kuamini mpaka unaamini si kutazama dhoruba imebeba
nini mtazame anayeibeba dhoruba. “Kwenye ziwa, Yesu haamrishi mawimbi
kutulia ili kumwonesha Petro kuwa si ghadhabu ya upepo iliyomtia katika hatari
bali ukosefu wa imani,” alisema Mtakatifu
Yohane Chrysostomu. Tunasoma hivi katika Injili: “Lakini alipouona upepo
akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana niokoe” (Mt 14: 30). Petro ana ujasiri na
woga. Anaanza vizuri, anaona dhoruba na kuogopa. Anakosa imani. Usimwambie Yesu
nina tatizo kubwa. Liambie tatizo Mungu wangu ni mkubwa nitashinda. Yesu
anabeba makubwa kuliko dhoruba. Kuna hadithi juu ya mbwa na tembo. Wanyama wote
walibeba mimba wakati ule ule. Baada ya miezi mitatu mbwa alijifungua. Na baada
ya miezi mitatu mingine alibebea mimba na kujifungua tena. Mara ya tatu alibeba
mimba na kujifungua. Hapo tembo hajajifungua. Mbwa akamuuliza tembo: "Una
hakika umebeba mimba ?" Tembo akamwambia mbwa : "Mimi
nimebeba tembo sikubeba kambwa kadogo. Mtoto wangu anapozaliwa anatingisha
ardhi. Akipita barabarani watu wanangoja apite na wanamstaajabia." Yesu amebeba makubwa. Usijisumbue na kesho
imebeba nini. Shughulika na anaye ibeba kesho
Tatu, kuamini mpaka unaamini kunahitaji hatua ya kwanza. Ukitembea kwa imani piga hatua ya kwanza.
“Imani ni kupanda ngazi ya kwanza hata kama hauoni ngazi zote,” alisema
mchungaji Dk. Martin Luther King Jr. Unapopiga hatua ya kwanza umeamini mpaka
ukaamini. Petro alimjibu Yesu: “Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya
maji.” Akasema, Njoo. Hakusema maneno mengi bali: N-j-o-o. Petro alishindwa
kutembea kwa imani juu ya bahari. Alikuwa na imani ya kumtoa kwenye mtumbwi
hakuwa na imani ya kumfanya atembee juu ya bahari. Walau alijaribu kupiga hatua
ya kwanza. .
Wana wa Israeli walipovuka bahari
ya shamu inasemekana maji hayakutoa nafasi iliyowazi kwanza mpaka mtu mmoja
alipoingia majini na kupiga hatua ya kwanza. Kwa macho ya mwili huyu mtu aliona
maji. Kwa macho ya imani aliona njia kavu baharini. Yesu alipowambia wakoma
kumi waende wajioneshe kwa makuani. Walikuwa hawajapona walipona walipokuwa
wanapiga hatua kwenda mbele. Kwa kuona walikuwa bado na ukoma lakini walitembea
kwa imani. Walipokuwa wanatembea walitakasika, walipona. Mungu anapoona umepiga
hatua, anajua kuwa mtu huyu anatembea kwa imani. “Imani si kujaribu kuamini jambo bila ya kuzingatia ushahidi: imani ni
kujaribu kufanya jambo bila kuzingatia matokeo,” alisema Sherwood Eddy.
Nne,
kuamini mpaka unaamini ni kutumaini kuwa Yesu atajitokeza. Katika kilele cha dhoruba Yesu alijitokeza.
Katika kilele cha hatari, katika upeo wa wasiwasi Yesu alijitokeza. Anakuja
wakati ambapo hategemewi kabisa. Mitume walifikiri ni mzuka wakauotea mbali.
Yesu ni Mkombozi wakubariki. Ni Mkombozi tunayeweza kumkimbilia. Alifanya kile
ambacho binadamu hawezi kufanya. Alitembea juu ya maji. Vile ambavyo hatuwezi
kufanya tumuachie yeye. Wakati tunapozama kwenye bahari ya matatizo tulie kwa
sauti: “Bwana utuokoe !”
Kuna mtu ambaye aliota ndoto alikuwa anatembea kando
ya bahari kwenye mchanga. Akiwa na furaha alipotazama nyuma aliona nyayo za
watu wawili. Wakati wa shida na matatizo alipotazama nyuma aliona nyayo za mtu
mmoja. Alimuuliza Yesu: maana yake nini? Yesu alimwambia kuwa wakati wa furaha
wanakuwa pamoja wanaambatana pamoja. Mtu huyo alidadisi: “Mbona wakati wa shida
naona nyayo zangu peke yangu?” Yesu alimwambia kuwa wakati wa shida anakuwa
amembeba mgongoni. Ndiyo maana anaona nyayo za mtu mmoja.
Tano, kuamini mpaka kuamini ni
kuwa na sala za mishale wakati wa hatari. Hizi ni sala fupi. Sala fupi
hufika mbinguni (Methali ya Kidachi). Petro alilia kuomba msaada kwa maneno
machache tu: “Bwana, Niokoe!” (Mt 14:30). Ilikuwa sala tosha na ya
kueleweka. Sala fupi inaweza kutolewa wakati wowote mahali popote. Mbali na
sala rasmi na ndefu; tujitahidi kutunga sala zetu baada ya kuona ile ya petro,
jaribu hii kabla kuanza safari, “Bwana, tusaidie tusafiri vema.” Unapokuwa na
hasira sema: “Bwana, nisaidie niwe mvumilivu,” unapokuwa na mambo mengi ya
kufanya, Sali: “Bwana, panga siku yangu.” Jaribu hii unapokuwa mezani “Ahsante
Bwana kwa chakula hiki.”“Tusisali sala ndefu, zinazotutoa nje lakini tusali
sala fupi iliyo na mapendo kamili. Tusali kwa niaba ya wasio sali. Tuwakumbuke, kama tunataka kuweza kupenda,
lazima tuweze kusali!”(Mama Teresa wa Calcutta). Kuna ambao radi ikipiga
wanasali: “Yesu na Maria.” Kuna wengine wanasema kile kilichojaa moyoni: “Panya
amedondokea kwenye sufuria.”