TAFAKARI 11/5/2017
(K)“ Watu na wakushukuru, Ee Mungu. Watu wote na wakushukuru”
(Zab 67:5)
Wakati wa raha jaribu kushukuru.
Zab 67 iliimbwa katika sikukuu ya shukrani baada ya mavuno (Kut23:24). Wakati
wa shida jaribu kushukuru. Katika shida Ayubu alimsifu Mungu: “Bwana alitoa, na
Bwana ametwaa; jina la Bwana litukuzwe” (Ayubu 1:21). Kusifu ni kushukuru. Maneno
“watu wote” yanabainisha wenye raha na wenye shida, wenye nacho na wasio nacho,
wagonjwa na wenye afya, walala hai na walalahoi, walalaheri na hohehahe,
wanaoteseka na wanaofurahi. Watu Wote
wamshukuru Mungu. Hata unapokosewa unajifunza kitu fulani, shukuru. “Msamaha wa
kweli ni pale unapoweza kusema, ‘Nashukuru kwa uzoefu huo,’” alisema Oprah
Winfret. Biblia inatwaambia: “Shukuruni katika kila jambo; maana hayo ni
mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu” (1 Wathesalonike 5: 18). Rick Warren
katika kitabu chake Maisha Yanayoongozwa
na Malengo alikuwa na haya ya kusema juu ya aya hiyo: “Mungu anakutaka
umshukuru kwamba atatumia matatizo yako kutimiza malengo yake.” Kutoshukuru ni kosa kubwa kuzidi kulipa
kisasi. “Kutoshukuru ni kosa la kudharauliwa zaidi ya kulipa kisasi, ambacho ni
kulipa baya kwa baya, wakati kutoshukuru ni kulipa baya kwa wema,” alisema
Mungu anapotoa hapimi kwa kijiko.
Tusimbanie shukrani. Waluhya wana methali isemayo, “Nyama choma haiwezi
kuwa tamu ukamsahau aliyeichoma.” Maisha yana baraka, usimsahau anayeleta
baraka-Mwenyezi Mungu. Yesu alipoomba kulisha wanaume 5,000 wanaojua kula
chakula Mungu Baba alimwongezea kuliko alivyokuwa ameomba wakakusanya mabaki
vikapu kumi na viwili. Bikira Maria alipoomba na kusema: Hawana divai.
Haikupatikana bora divai bali divai bora-grade one. Mfalme Solomoni aliomba
hekima, Mungu akamwongezea na mali. Yosefu aliomba kukumbukwa. Alikumbukwa na
zaidi alifanywa Waziri Mkuu. Huu ni mlipuko wa baraka. Kuna mzee fulani
aliyekuwa hakosi kuhudhuria adhimisho la Misa. Jumapili moja alihamua kupanga
matumizi yake. Aliweka shilingi elfu moja kwenye mfuko wa suruali kwa ajili ya
kutoa sadaka na shilingi 10,000/= aliziweka kwenye mfuko wa shati kwa ajili ya
matumizi madogo ya nyumbani. Wakati wa kutoa sadaka alitoa noti kwenye mfuko wa
shati bila kuitazama. Baadaye alienda dukani kununua sukari na mchele. Baada ya
kufunguwa bidhaa hiyo alipoingiza mkono wake kwenye mifuko alipata shilingi
1,000/=. Aimwomba samahani muuza dukani. Kwa kusononokea alienda nyumbani.
Baada ya dakika tano akiwa nyumbani alikuja mtu aliyemletea pesa hili kumaliza
deni lake la zamani laki tano. Mungu anapotoa hapimi kwa kilo. Kuna namna
nyingi za kuwashukuru unaokaa nao.
Kushukuru ni kuomba tena. “Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika
kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na
Mungu” (Filp 4:6). Kushukuru ni
kufanya haja zako zijulikane na Mungu. “Shukrani ni moyo wa kutegemea kupata
misaada siku za baadaye” (Sir Robert Walpole). “Hakuna kazi ambayo inahitaji kufanyika haraka kama kutoa shukrani”
(Mt. Ambrose). Tusishukuru kwa namna ya
kuomba miujiza ya ajabu. Kuna mtoto aliyefanya mtihani wa darasa la saba. Usiku
wakati wa sala za usiku alisikika akisema: “Mungu nakushukuru ulivyonisaidia
kujibu maswali naomba Mwanza ugeuke kuwa Mji Mkuu wa Tanzania.” Kushukuru si
kuomba kwa namna hiyo.
Kushukuru ni kuthamini. Mthamini mwenzako. Mungu wetu ni Mungu
anayethamini. “Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye
kuheshimiwa, nami nimekupenda” (Isaya 43:4). Wathamini watoto. Maua ya kesho
yako kwenye mbegu za leo. Kuna mwalimu
mmoja kila wanafunzi walipoingia darasani alisimama mlangoni akimwinamia kila
mwanafunzi alipoulizwa kwa nini anafanya hivyo, alisema sijui hawa woto
watakuwa wakina nani? Viongozi wangu wa kesho. Aliwathamini si jinsi
walivyo tu bali watakavyokuwa. Mwanamke mmoja alimuuliza mke wake: “Mbona kila
mara ninapoimba unatoa kichwa dirishani?” Mwanamke akasema: “Nataka majirani
wajue kuwa anayeimba vibaya sio mimi.”
Sala: Ee Yesu nisaidie kushukuru katika
shida na raha, katika magonjwa na afya, wakati wa vigelegele na wakati wa
kelele. Amina.