TAFAKARI 8/5/2017
“Nalikuwa katika
mji wa Yafa nikiomba, roho yangu ikazimia, nikaona maono” (Matendo 11: 5)
Usipojipogramu
watu wabaya watakuprogramu. Mungu asipokuprogramu watu wabaya wanaweza
kukuprogramu. Mungu alimprogramu Simoni Petro kupitia ndoto au maono. “Jambo
hili lilitendekea mara tatu” (Matendo 10:16). Mungu anatuprogramu mara nyingi.
Mungu alitaka Petro abadili mtazamo wake: Kutoka Mungu wa Israeli kwenda Mungu
wa mataifa yote. Kutoka kukumbatia waliotahiriwa kwenda kwenye kukumbatia
wasiotahiriwa. Kutoka kula nyama ya wanyama walio safi hadi kula nyama ya
wanyama najisi kama nguruwe. Huenda
Mungu atakuletea maono kama Petro lakini unaweza kupiga picha kichwani ya mambo
mazuri. Unaweza kujiprogramu.
Kuna kitendawili
kisemacho: “Nimelala usiku natazama filamu.” Jibu ni ndoto. Hatuna budi kuwa na
filamu ya maisha tunayoyataka akilini mwetu.
“Ni muda muafaka wa kuishi maisha ambayo umeyafikiria,” alisema Henry James.
Fikiria utakapokuwa kesho. “ Tuko tulivyo na tulipo kwa sababu kwanza
tulipafikiria,” Donald Curtis. Kuna mambo kadhaa ya kuzingatia.
Kuwa na picha akilini. Unataka
kununua gari, kuwa na picha ya gari hilo akilini. Unataka kuoa, kuwa na picha
ya arusi akilini mwako. Unataka kujenga nyumba, kuwa na picha akilini mwako ya
nyumba unayoipenda. “Roho haiwezi
kufikiri bila picha,” alisema Aristotle. Tunaweza kusema mtu hawezi kufikiri
bila picha. Naye John Holland alisema, “Roho haiwezi kuzungumza bila picha.”
Mtu hawezi kuzungumzia mipango yake bila picha. Ukizungumzia duka unalotaka
kulianzisha kuwa na picha. Ukizungumzia taasisi unayotaka kujenga kuwa na picha
akilini mwako.“ Badili sura za picha kwenye kichwa chako ziendane na maono
kwenye moyo wako,” alisema mtu fulani. “Piga picha ya kitu unachokitaka
akilini, kione, kihisi, kiamini. Fanya picha ya kitu hicho kichwani mwako, na
anza kukijenga,” alisema Robert Collier. “Kupiga picha akilini ni kuona lile
ambalo halipo, ambalo halionekani – ndoto.
Kupiga picha akilini kusema kweli na kutengeneza uongo unaonekana. Uongo
unaonekana, hata hivyo una namna ya kuwa ukweli wa mambo,” alisema Peter
McWilliams.
Fikiri kama kwamba unachokitaka kipo. “Kuleta jambo katika maisha
yako, fikiria kama kwamba tayari lipo,” alisema Richard Bach. Yapigie msitari
maneno “kama kwamba” ni maneno muhimu. “Umba maono ya unayetaka kuwa na baadaye
ishi katika picha hiyo kama kwamba ni kweli,” alisema Arnold
Schwarzenegger. Ishi kama kwamba
lisilowezekana linawezekana. “Watu wa kawaida huamini tu katika linalowezekana.
Watu wasio wa kawaida hupiga picha si ya lile ambalo linawezekana au
linayamkinika bali lile ambalo haliwezekani. Na kwa kupiga picha ya lile
lisilowezekana wanaanza kuliona kama linalowezekana,” alisema Cherie Carter-Scott.
Badili
unachokiona. “Toa mawazo yako, maneno yako na macho
kwenye mambo yalivyo, na yaweke tu kwenye namna ambavyo unataka mambo yawe,”
alisema Che Garman. “Mtu anaweza kupokea lile ambalo anaona anapokea,”
alisema Florence Scovel Shinn. “Lazima uone kitu vizuri akilini kabla ya
kukifanya,” Alex Morrison.
Kuna faida nyingi za kuwa na picha ya unachokitaka
akilini. Kwanza, picha ya unachokitaka inakupa
matumaini. “Ukiwa na maono kwa ajili ya maisha yako hilo linakuwezesha kuishi
kwa matumaini badala ya hofu zako,” alisema Stedman Graham. Pili, ni kupiga
hatua kimaendeleo. Hatua ya kimaendeleo
inategemea upeo wako ulivyo. Upeo wako ukiwa chini hutabaki chini. Upeo wako
ukiwa juu utakuwa juu kweli. “Mtu anaweza kukua kiasi ambacho upeo wake unamruhusu,”
alisema John Powell. Watu wenye upeo wa juu sana si wa kawaida. Tatu,
kunasaidia kufanikiwa. Ukweli huu
unabainishiwa na methali ya kichina: “Dunia ni ya wale ambao wanavuka madaraja
mengi katika kufikia kwao kabla ya wengine hawajaona hata daraja moja.” Nne,
kupiga picha akilini kunasisimua, na kuleta ari mpya. “Kila dakika, kila saa,
piga picha kichwani namna unavyotaka uwe. Sisimukia WEWE mpya,” alisema, Thomas
D Willhite. Picha akilini ni kichocheo cha kutenda. "Picha inazaa shauku. Unakusudia
lile ambalo umelipigia picha ya akilini,” alisema J. G. Gallimore. “Naota kwa
hiyo nakuwa hivyo,” Cheryl Grossman.