Saturday, November 11, 2017

KUTOJIANDAA NI KUJIANDAA KUSHINDWA




                                                    
                         “Basi, kesheni, kwa sababu hamjui siku wala saa” (Mathayo 25: 13) jmggyt
  1. Hek 6: 12-16
  1. 1 Thes 4: 13-18
  1. Mt 25: 1-13

UTANGULIZI
Mafuta: Yanaweza kuwa na tafsiri nyingi. “Busara ni kama ufuta; unaukaanga kadiri unavyokula” (Methali ya Batoro, Uganda). Taa zetu hazina budi kuwa na mafuta. Mafuta ni busara. Kujiandaa ni busara. Pia mafuta yanaweza kueleweka kama upendo hai. Ndio huo unaoleta tofauti baina ya wanawali wapumbavu na wenye busara. Kadiri ya Mt. Augustino, “Mafuta yanamaanisha furaha.”  Kufuatana na ukweli huo, “Mungu wako, amekupaka mafuta, kwa mafuta ya furaha, kuliko wenzako” (Zaburi 45:8). Mafuta kuwekwa kwenye vyombo ni furaha iliyotunzwa moyoni na kwenye dhamiri.
Taa: Taa inaweza kuwa na tafsiri nyingi. Taa ni imani. Taa ni matendo mema. tKadiri ya Baba wa Kanisa Mt. Augustino:  “Taa wanazobeba mikononi ni matendo yao ambapo ilisemwa, ‘mwanga wenu uangaze mbele ya watu.’” (Mt 5:6).
Mabikira: Wanaojiandaa wanalinganishwa na mabikira watano wenye busara na wale ambao hawajiandai wanalinganishwa na mabikira wapumbavu.
Bwana harusi: Ni Yesu. Yesu anakuja namna mbili. Anapomchukua mtu mmoja. Namna ya pili atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu. Hakuna anayemjua mjumbe wa kifo atakuja lini. Ni busara kila tufanyalo katika maisha tujiulize, “Halafu?” Kama hadithi ya vijana wawili. Kijana mmoja alimuuliza mwingine. “Utafanya nini ukikua?” “Nitachukua somo la biashara.” “Halafu?” “Nitatafuta kazi.” “Halafu?” “Nitapata fedha nyingi kama mshahara.” “Halafu?” “Nitatafuta msichana nioe” “Halafu?” “Nitakuwa na watoto.” “Halafu?” “Nitawalea watoto” “Halafu?” “Nitakuwa babu?” “Halafu?” “Labda nitafanywa chifu.” “Halafu?” “Nitatawala watu.” “Halafu?” “Nitazeeka.” “Halafu?” ““Halafu?”, halafu, halafu, halafu usiulize zaidi ya hapo.” “Bila shaka uwe unafikiria kuwa siku moja utakufa.” Lakini tumaini linabaki kuwa kifo sio nukta, sio kikomo, bali ni alama ya mkato hadithi ya maisha inaendelea. Kutojiandaa ni kujiandaa Kutokuwa katika wateule. Jiandae.
MAHUBIRI YENYEWE
 “Ukinipa saa sita ili niukate mti, nitatumia saa nne za awali kulinoa shoka langu,” alisema  Abrahamu Lincoln (1809-1865). Hiyo ni busara. Hayo ni mafuta katika taa. Somo la meneno hayo ya Abrahamu ni kuwa kujiandaa kunatangulia mafanikio. Kwa kushindwa kujiandaa, unajiandaa kushindwa. Kuna mambo ambayo yanawafanya watu wasijiandae.
Kwanza ni kuwa katika eneo la faraja. Ili ni eneo ambapo watu wanajiona wako salama, wamefarijika. Hawataki kujisumbua. Kazi ya kweli ya kupigia debe ufalme wa mbinguni au maendeleo ni kuwasumbua waliofarijika na kuwafariji waliosumbuka. Lazima kutoka katika eneo la faraja ambalo linakufanya usifanye lolote la maana na kujiandaa.  Ili kuleta mabadiliko ni lazima kuvunja uzio na ukuta wa eneo la faraja inayokufanya kubweteka. Toka ndani ya sanduku. “Faraja ni mtego wako mkubwa na kutoka katika eneo la faraja ni changamoto yako kubwa,” alisema Manoj Arora. Katika Biblia tuna watu waliovunja ukuta wa eneo la faraja ni Musa: “ Kwa nguvu ya imani, Musa alipofikia utu uzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao” (Waebrania 11: 24). Musa alikuwa kwenye eneo la faraja la kuitwa mwana wa binti Farao. Mambo mawili yalimfanya  kuacha eneo la faraja: nayo ni nguvu ya imani na utu uzima.
Kuna nguvu ya imani. Katika kitabu cha maombi tunasali hivi: “Iliwalazimu wanawali kuwa na taa, yaani, imani: Utuangaze kutumia imani kama taa ya njia ya kweli katika maisha yetu ya kila siku.” Musa alitumia imani kama taa nasi tutumie imani kama taa.
Kuna utu uzima. Wanawali wapumbavu hawakutenda kama watu wazima. Kuna mwanaume alimuuliza mke wake utaweza kweli kwenda Dubai kuchukua mzigo wa biashara bila kusumbuliwa na wanaume huko? Mwanamke alimjibu mume wake: “Mimi ni mtu mzima.” Kuna kijana ambaye alihama kwa kaka yake akaanza kupanga nyumba. Kaka yake alimuuliza utaweza kuyamudu maisha. Alimjibu: “Mimi ni mtu mzima.” Ni utu uzima    ambao unakufanya kung’amua kuwa: mtegemea cha nduguye hufa akiwa maskini. Kuna kijana alikuwa anaenda kuanza masomo chuo kikuu, mzazi akamwambia tusindikize hadi Dodoma. Alimjibu mzazi: “Mimi ni mtu mzima. Hakuna haja ya kunisindikiza.” Mfalme alikuwa na mtumishi ambaye alimdharau na kumuona kama mtoto. Siku moja alimpatia fimbo akasema ukimuona mtu mzima ambaye hajiandai jua ni kama mtoto mpe fimbo hii. Mtumishi alizunguka hakumpata mtu wa namna hiyo. Siku moja alisikia mfalme yupo kitandani anaumwa sana kiasi cha kuchungulia kaburi. Alienda na kumuuliza: ukifa huko unakokwenda umeishajitengenezea marafiki? Mfalme alisema: “Hapana.” Mtumishi alimpa fimbo na kumwambia: “Wewe sio mtu mzima.”  

Jambo la pili  linalotufanya tusijiandae ni kusitasita. Kuna mtu ambaye alisema: “Kusitasita ni chanzo cha matatizo yangu yote. Hata hivyo sijui vizuri maana ya neno kusitasita kesho nitatazama maana yake kwenye kamusi.” Kutojiandaa ni kujiandaa kushindwa. Ngoja ngoja huumiza tumbo. Asubuhi ni wakati wa kuweka kipimo cha kasi utakayotumia. Kuna nguvu ya kufanya mambo mapema. Kuna mtu aliyeambiwa kuna ng’ombe dume watatu kwenye zizi, ukiweza kukamata mkia wa mmojawapo utapewa zawadi ya milioni mbili. Ng’ombe wa kwanza kujitokeza alikuwa mkali, macho makali, mnene na wa kutisha. Mtu huyo akaogopa kushika mkia wake. Wa pili kujitokeza alikuwa mkali zaidi na wa kutisha zaidi. Mtu huyo akangoja wa tatu. Wa tatu alikuwa amekonda, hana nguvu. Mtu huyo akasema nitashika mkia wa huyo. Bahati mbaya hakuwa na mkia. Alishindwa kufanya mambo mapema. Adui ya nguvu ya mapema ni kusitasita.
Jambo la tatu ambalo linatufanya tusijiandae ni mazoea mabaya. Kuna methali ya Tanzania isemayo, “Huwa nazaa watoto namna hii, aliuawa na mimba ya tisa.” Mazoea yanaweza kupofusha macho yetu, na kutufanya viziwi. Ukimtia chura kwenye maji moto ataruka ili atoke. Lakini ukimtia kwenye maji baridi na kupasha joto pole pole. Chura hatajua ni lini maji yamekuwa ya moto. Mazoea yanamfanya mtu hasishtuke.  Mazoe ya kutenda mema yatakusaidia.
Jambo la nne  linalotufanya tusijiandae ni inesha au ubaridi  au kingungumizi cha kuanza. “Watu wengi hushindwa kwa sababu hawaanzi. Hawaishindi inesha. Hawaanzi,” alisema Ben Stein. Jiulize umefikaje ulipo: kwa kuelea au kwa kupiga makasia. Kama ni kwa kuelea utakuwa hauna mwelekeo na dira. Kama kwa kupiga makasia ina maana unafanya kitu fulani. Palipo na inesha kuna kushindwa kuonesha hisia kali au shauku. Hakuna bashasha. Inesha ni kutofanya lolote. Kuna hadithi ya fisi aliyetoa kipande cha nyama kwenye sufuria. Kilikuwa ni cha moto. Kilimchoma midomo. Fisi wenzake wakamwambia, “Tema.” Akawajibu. “Niteme utamu.” Wakazidi kumshauri, “Meza.” Akawajibu, “Nimeze moto.” Huu ni ubaridi unaoletwa na kukosa uamuzi.
Kujiandaa ni kujiandaa kushinda. Mwanamke mmoja alikuwa akifanya kazi katika kiwanda cha kusindika nyama. Siku moja baada ya kumaliza kazi zake pale kiwandani alienda katika chumba chenye freezer (cold room) ambako nyama zilikuwa zikihifadhiwa kukagua baadhi ya bidhaa.​ Kwa bahati mbaya wakati yupo kwenye hicho chumba katika harakati za hapa na pale akausukuma mlango, ukajifunga. Hakukuwa na msaada wowote wa kuweza kuufungua mlango ule. Alianza kulia na kupiga kelele za kuomba msaada wa kufungiliwa, lakini kelele zake hazikuwa rahisi kusikika nje ya hicho chumba kidogo, na wafanyakazi wote pale kiwandani walikuwa wameishaondoka. ​Masaa mawili baadae akiwa katika hali ya kukaribia kukata roho kutokana na baridi kali iliyoko kwenye hicho chumba. ​Ghafla mlinzi wa geti la kiwanda hicho alifungua mlango alimokuwamo yule mwanamke.​ Alitahamaki kumkuta mwanamke yule katika hali ile mbaya.
Basi jitihada za kumpa huduma ya kwanza kumpeleka hospitali ikafuata. Baada ya kutolewa hospitalini alipata wasaa wa kumuuliza yule mlinzi ilikuwaje akafungua mlango wa cold room wakati ilikuwa si ratiba yake na vile vile ilikua si kazi yake? Maelezo ya yule mlinzi yakawa kama ifuatavyo:
​''Nimefanya kazi kwenye hiki kiwanda kwa miaka 38 sasa, mamia ya wafanyakazi wanatoka na kuingia kiwandani lakini wewe peke yako kati ya wote ndiye uliyekuwa ukithubutu kunisalimia asubuhi na kuniaga kila jioni unapoondoka kiwandani. Ulipokuja kazini asubuhi ulinisalimia kama kawaida na kunijulia hali. Lakini baada ya kazi na wafanyakazi kuanza kutoka kurudi, nilitegemea kusikia salamu yako, niliendelea kusubiri lakini cha ajabu mpaka watu wote wakawa wametoka na wewe sikuona sura yako. Nilianza kuingiwa na maswali mengi, na ndipo nikapata wazo la kuanza kuzunguka maeneo yote ya kiwanda na baadae chumba baada ya chumba. Na ndipo nilipokukuta kwenye chumba cha barafu.​ Funzo ni kuwa tenda mema kuna kesho. Ishi vizuri na kila mtu, mheshimu kila mtu bila kujali hadhi yake, ukubwa wala udogo wake, kwani hujui kesho atakua wapi katika kuwa sababu ya MSAADA kwako.
HITIMISHO: Maisha ya kikristo yanadai kazi, kuwa macho na kuwa tayari.

Saturday, August 12, 2017

AMINI MPAKA UNAAMINI


             



             Jumapili ya 19 ya Mwaka A



  “Ewe mwenye imani haba mbona uliona shaka” (Mathayo 14:31)



1. Fal 19:9a, 11-13a

2. Rum 9: 1-5

3.    Mt 14: 22-33



Kwanza kuamini mpaka kuamini ni kuonyesha au kutangaza nia. Penye nia pana njia. Mtume Petro alipoona Yesu anatembea juu ya maji alionesha nia ya yeye kutaka kutembea juu ya maji. Petro alimwambia Yesu: “Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji.” Petro alitangaza nia. Alionesha nia. Siku moja niliambatana na mchungaji kwenda kwenye yadi ya magari kumsaidia kuchagua gari zuri. Tulipofika pale tuliona magari mengi, tukaingia ndani na kuyakagua: Mark II, Toyota Corolla, Suzuki, Rava 4, Pick up, kutaja machache. Baada ya masaa mawili ya kukagua na kutazama nilimwambia, “Naomba tuchague sasa gari ambalo utanunua.”  Alinijibu: “Kusema kweli sina hata shilingi.” Nilimwambia: “Kwa nini usumbufu wote huu.” Alinijibu: “Namwonyesha Mungu nia yangu.” Onesha nia. Ukitaka kununua shamba hata kama huna hela, ulizia bei kwanza, kagua viwanja vilipo. Sala yetu iwe kama ya kijana mmoja kwenye Biblia, “Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu” (Marko 9: 24). Petro kwa upande mmoja alikuwa na kuamini na kwa upande mwingine alikuwa na kutoamini. Kutangaza nia tu hakutoshi.

Pili, kuamini mpaka unaamini si kutazama dhoruba imebeba nini mtazame anayeibeba dhoruba. Kwenye ziwa, Yesu haamrishi mawimbi kutulia ili kumwonesha Petro kuwa si ghadhabu ya upepo iliyomtia katika hatari bali ukosefu wa imani,” alisema Mtakatifu Yohane Chrysostomu. Tunasoma hivi katika Injili: “Lakini alipouona upepo akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana niokoe” (Mt 14: 30). Petro ana ujasiri na woga. Anaanza vizuri, anaona dhoruba na kuogopa. Anakosa imani. Usimwambie Yesu nina tatizo kubwa. Liambie tatizo Mungu wangu ni mkubwa nitashinda. Yesu anabeba makubwa kuliko dhoruba. Kuna hadithi juu ya mbwa na tembo. Wanyama wote walibeba mimba wakati ule ule. Baada ya miezi mitatu mbwa alijifungua. Na baada ya miezi mitatu mingine alibebea mimba na kujifungua tena. Mara ya tatu alibeba mimba na kujifungua. Hapo tembo hajajifungua. Mbwa akamuuliza tembo: "Una hakika umebeba mimba ?" Tembo akamwambia mbwa : "Mimi nimebeba tembo sikubeba kambwa kadogo. Mtoto wangu anapozaliwa anatingisha ardhi. Akipita barabarani watu wanangoja apite na wanamstaajabia."  Yesu amebeba makubwa. Usijisumbue na kesho imebeba nini. Shughulika na anaye ibeba kesho



Tatu, kuamini mpaka unaamini kunahitaji hatua ya kwanza. Ukitembea kwa imani piga hatua ya kwanza. “Imani ni kupanda ngazi ya kwanza hata kama hauoni ngazi zote,” alisema mchungaji Dk. Martin Luther King Jr. Unapopiga hatua ya kwanza umeamini mpaka ukaamini. Petro alimjibu Yesu: “Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji.” Akasema, Njoo. Hakusema maneno mengi bali: N-j-o-o. Petro alishindwa kutembea kwa imani juu ya bahari. Alikuwa na imani ya kumtoa kwenye mtumbwi hakuwa na imani ya kumfanya atembee juu ya bahari. Walau alijaribu kupiga hatua ya kwanza. .



Wana wa Israeli walipovuka bahari ya shamu inasemekana maji hayakutoa nafasi iliyowazi kwanza mpaka mtu mmoja alipoingia majini na kupiga hatua ya kwanza. Kwa macho ya mwili huyu mtu aliona maji. Kwa macho ya imani aliona njia kavu baharini. Yesu alipowambia wakoma kumi waende wajioneshe kwa makuani. Walikuwa hawajapona walipona walipokuwa wanapiga hatua kwenda mbele. Kwa kuona walikuwa bado na ukoma lakini walitembea kwa imani. Walipokuwa wanatembea walitakasika, walipona. Mungu anapoona umepiga hatua, anajua kuwa mtu huyu anatembea kwa imani. “Imani si kujaribu kuamini jambo bila ya kuzingatia ushahidi: imani ni kujaribu kufanya jambo bila kuzingatia matokeo,” alisema Sherwood Eddy.



Nne, kuamini mpaka unaamini ni kutumaini kuwa Yesu atajitokeza. Katika kilele cha dhoruba Yesu alijitokeza. Katika kilele cha hatari, katika upeo wa wasiwasi Yesu alijitokeza. Anakuja wakati ambapo hategemewi kabisa. Mitume walifikiri ni mzuka wakauotea mbali. Yesu ni Mkombozi wakubariki. Ni Mkombozi tunayeweza kumkimbilia. Alifanya kile ambacho binadamu hawezi kufanya. Alitembea juu ya maji. Vile ambavyo hatuwezi kufanya tumuachie yeye. Wakati tunapozama kwenye bahari ya matatizo tulie kwa sauti: “Bwana utuokoe !”



Kuna mtu ambaye aliota ndoto alikuwa anatembea kando ya bahari kwenye mchanga. Akiwa na furaha alipotazama nyuma aliona nyayo za watu wawili. Wakati wa shida na matatizo alipotazama nyuma aliona nyayo za mtu mmoja. Alimuuliza Yesu: maana yake nini? Yesu alimwambia kuwa wakati wa furaha wanakuwa pamoja wanaambatana pamoja. Mtu huyo alidadisi: “Mbona wakati wa shida naona nyayo zangu peke yangu?” Yesu alimwambia kuwa wakati wa shida anakuwa amembeba mgongoni. Ndiyo maana anaona nyayo za mtu mmoja.



Tano, kuamini mpaka kuamini ni kuwa na sala za mishale wakati wa hatari. Hizi ni sala fupi. Sala fupi hufika mbinguni (Methali ya Kidachi). Petro alilia kuomba msaada kwa maneno machache tu: “Bwana, Niokoe!” (Mt 14:30). Ilikuwa sala tosha na ya kueleweka. Sala fupi inaweza kutolewa wakati wowote mahali popote. Mbali na sala rasmi na ndefu; tujitahidi kutunga sala zetu baada ya kuona ile ya petro, jaribu hii kabla kuanza safari, “Bwana, tusaidie tusafiri vema.” Unapokuwa na hasira sema: “Bwana, nisaidie niwe mvumilivu,” unapokuwa na mambo mengi ya kufanya, Sali: “Bwana, panga siku yangu.” Jaribu hii unapokuwa mezani “Ahsante Bwana kwa chakula hiki.”“Tusisali sala ndefu, zinazotutoa nje lakini tusali sala fupi iliyo na mapendo kamili. Tusali kwa niaba ya wasio sali.  Tuwakumbuke, kama tunataka kuweza kupenda, lazima tuweze kusali!”(Mama Teresa wa Calcutta). Kuna ambao radi ikipiga wanasali: “Yesu na Maria.” Kuna wengine wanasema kile kilichojaa moyoni: “Panya amedondokea kwenye sufuria.”

Saturday, July 15, 2017

MAMBO YOTE HAYAHUSU UDONGO, BALI YANAMHUSU MPANDAJI PIA


2017 Julai 16 Jumapili ya 15

“Mpanzi alikweda kupanda mbegu” (mathayo 13:3)
Alexander Maclaren aliandika: “Mfano wa mpanzi, ni wa kihistoria na wa kinabii. Unaeleza uzoefu halisi wa Kristo, na unabashiri juu ya watumishi wake.” Mafanikio au kushindwa, uzuri au ubaya, mpanzi Yesu Kristo au Mungu wetu, usikate tamaa. Yesu akiwa amejaa neema  anaonesha jitihada za kusonga mbele kila mara, bila kuwa na mawazo ya kukata tamaa. Changamoto kwetu, tunapaswa kuwa kama Baba yetu wa mbinguni Mpanzi Mkuu. Lazima tuungane nae tuanze kupanda mbengu za injili zaidi na pasipo kubagua. “Unaposikia maneno, mpanzi alitoka akaenda kupanda mbegu, usifikirie kwamba ni marudio.  Mpanzi anatoka  mara nyingi kwa malengo mbalimbali; kama  kulima, kung’oa magugu, kutoa miiba au kazi nyingine yoyote, lakini mtu huyo alienda moja kwa mojakupanda. Ni jambo lilitokea kwa mbegu? Robo tatu ziliharibika, na robo moja ilibakia; lakini siyo zote kwa namna ile, lakini kwa utofauti fulani, na alivyopanda nyingine zilianguka njiani” (Mt. Yohane Krisostomu)

Shetani anatumia mbinu ifuatazo kunyakua kilichopandwa moyoni yaani neno la Mungu.  Shetani anatumia mbinu ya kutoona. Mwenye macho haambiwi tazama. Yaani mtu akiwa na haja na kitu ni juu yake kukishughulikia. Hauwezi kungoja kuletewa mambo mazuri. “Penye miti hakuna wajenzi.” Ndivyo isemavyo methali ya Kiswahili. Ni kama watu hawaoni hiyo miti. Kuna vitu ambavyo vinaweza kumfanya mtu hasione. Mazoea huleta dharau, lakini mazoea huleta upofu. Tunaambiwa, “Kutazama mtatazama, lakini hamtaona.” (Mathayo 13: 14) Chuki bila sababu au maamuzi mbele yaweza kumfanya mtu hasione mfano Nathanaeli. “Naye Nathanaeli akamwuliza Filipo, “Je, kitu chema chaweza kutoka Nazareti?” (Yohane 1: 46) Ukabila unaweza kumfanya mtu asione zuri kutoka kabila fulani. Ubaguzi wa rangi unaweza kumfanya mtu hasione jambo zuri kutoka watu wa rangi tofauti na yake, ingawa damu yao wote ni nyekundu.

Mbinu  nyingene  ya shetani ya kuondoa mbegu iliyopandwa moyoni ni kuleta shaka au mashaka. Shetani aliwaletea Adamu na Eva mashaka katika sura ya nyoka kama tunavyosoma katika Biblia.  “Basi nyoka akamwambia huyo mwanamke, “Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, msile matunda ya miti yote ya bustani?” (Mwanzo 3: 1) Shetani alimletea Yesu  mashaka, “Ikiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe nikate.” (Mathayo 4: 3)  Maneno ati, eti na ikiwa ni maneno ya kuonyesha au kueleza shaka au wasiwasi juu ya jambo.  Mashaka utengeneza milima ambayo imani inaweza kuhamisha. Sala ya mtu mwenye mashaka iko hivi, “Ee Mungu – kama yupo Mungu kweli okoa roho yangu kama nina roho kweli.Amina.”

 Kuondoa hofu ni mbinu ambayo shetani hutumia kuondoa mbegu iliyopandwa moyoni. Watu hukimbia kumkwepa nyoka na nyoka hukimbia kukwepa watu.” Hiyo ni methali ya Yoruba. Inatufunulia juu ya woga na hofu. Shetani alimuondolea hofu Eva. “Nyoka akamwambia mwanamke, ‘Hakika hamtakufa.” (Mwanzo 3:4)  Shetani alipomjaribu Yesu alitaka kumwondolea hofu, “Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, ‘Atakuagiza malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.” (Mathayo 4: 6) Shetani alimuondolea hofu kwa kutumia Biblia. Shetani anaweza kukuondolea hofu kwa kutumia Biblia vibaya. Kuna watu wanaofanya ulevi kuwa halali kwa kutumia maneno ya Paulo kwa Timotheo, “Usinywe maji tu, bali unywe divai kidogo kwa ajili ya tumbo lako, kwani unaugua mara kwa mara.” (1 Timotheo 5: 23) Mtume Paulo wa Tarsus hapingi kunywa divai bali anapendekeza kiasi katika neno kidogo. Anapinga ulevi. Lakini kifungu hiki kinaweza kutumiwa vibaya kuendekeza tabia ya ulevi.

 Sala: Mpendwa Yesu, ulipanda Neno la Mungu kwa mapendo, uvumilivu, juhudi na bila kuchoka, nisaidie kukuiga wewe uliye mpanzi wa Neno la Mungu. Amina.

Saturday, July 1, 2017

MSALABA UNABEBEKA




Jumapili ya 13

 “asiyepokea msalaba wake akanitafuta, hafai kwangu.”(Mathayo 10:38)
“Msalaba unamaanisha hakuna maangamizi ya meli baharini bila matumaini; hakuna giza bila mapambazuko; hakuna dhoruba bila bandari,” alisema Papa Mt.Yohane  Paulo II. “Kwa kuchukua msalaba, haimaanishi kitu kingine chochote zaidi ya kwamba tunapaswa kupokea na kuteseka kwa sababu ya  maumivu, mambo yanayopingana, mateso na kujikatalia tunavyopitia,” alisema Mtakatifu Francis wa Sales. Inabidi tubebe misalaba yetu badala ya kuiongelea tu. Tarehe 25 Oktoba 1970 Papa Paul VI aliwatangaza  watakatifu mashahidi40 wa Kiingereza. Alexander Briant alijitengenezea kimsalaba kidogo wakati wa kufungwa kwake jela na siku ya kuuwawa kwake alikishikilia mikononi mwake wakati wa hukumu ya kifo inatolewa.Walimyanganya kimsalaba chake, lakini alimwambia jaji: “Unaweza kukichukua toka mikononi mwangu na  si kutoka  moyoni mwangu.”  Msalaba juu ya Golgotha ​​hauwezi kukubadilisha wewe kama si haukusimikwa moyoni mwako. 

Msalaba ni mzigo lakini unabebeka kwa vile ni mzigo mwepesi. “Ukiubeba msalaba ipasvyo, msalaba utakubeba,” alisema Thomas à Kempis. Watoto ni misalaba lakini wanabebeka. Mzazi akiwabeba vyema nao baadaye watoto watambeba, akiisha zeeka hana nguvu watamtunza kama aliwaandalia vizuri maisha ya kesho. Kuna mtoto wa miaka kumi na miwili alikuwa amembeba mdogo wake wa mwaka mmoja. Alipoulizwa na jirani kama ni mzito. Mtoto alijibu, “Si mzito kwa vile ni ndugu yangu.” Siku moja rafiki wa baba aliyekuwa na watoto wanne alimuuliza, “Kwa nini unawapenda watoto wako?” Baba huyo alifikiria kwa dakika  na kupata jibu moja ambalo angelitumia, “Kwa sababu ni wangu.”  Watoto wanapendwa na wanapendeka. Wanabebeka kwa vile wanapendwa. Nao watoto wanawajibu kama isemavyo, ukibebwa bebeka.

Yesu alisema, “Mtu akitaka kuwa mfuasi wangu, ajikane mwenyewe, lazima ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate” (Luka 9: 23). “Msalaba unabebwa kwa namna mbili: mwili kwa kujinyima na moyo unapoguswa na huruma” alisema Mtakatifu Gregori. Mzazi anajinyima mambo mazuri ya mwili kama kujipamba, mafuta, chakula kizuri, sehemu nzuri ya kukaa ili mtoto wake asome shule kwa namna hiyo anaubeba msalaba. Mzazi akifikiria maisha ya mbele anawaonea watoto wake huruma aubeba msalaba.  Mungu hakupi msalaba wa kubeba unaozidi uwezo wako. “Msalaba Mungu anaokutumia ameutathimini kwa macho yake yanayojua yote, ameuelewa kwa akili yake ya kimungu, ameujaribu na haki yake yenye hekima, umeupa joto kwa mikono yake ya upendo, ameupima kwa mikono yake kujua kuwa haupitilizi ukubwa hata kwa inchi moja na haupitilizi uzito hata kwa ratili moja, “ alisema Mtakatifu Francis de Sales. Wajibu ni msalaba lakini unabebeka: wajibu wako kwa umma, kwa familia, kwa Mungu na kwako wewe ni msalaba lakini unabebeka.

Msalaba unabebwa kila siku.  Lakini si kila siku ni kila saa. “Na sisi, kwa nini tumo hatarini kila saa? Siku kwa siku nipo taabani” (1 Wakorintho 15:30-31). Inavyoonekana ni jambo gumu kufa kila siku kuliko kufa mara moja. Ina maana kila mara unatoa sadaka ya kitu fulani iwe hata muda wako kwa ajili ya wengine. Mfanyakazi ofisini anabeba msalaba wake wa kazi kila saa. Anaporudi nyumbani kama ana wazazi wa kuwatimizia aja zao anafanya hivyo, kama ana mwenzi wa ndoa anamjali, kama ana watoto anasikiliza shida zao. Ni kila siku karibu ni kila saa kuubeba msalaba.

Sala: Ee Bwana wetu Yesu Kristo nisaidie ili hamasa na nguvu zangu vitoke kwenye kujikatalia na msalaba. Amina.

Saturday, June 10, 2017

MAFIGA MAWILI HAYAIVISHI CHUNGU


SHEREHE YA UTATU MTAKATIFU
"Neema ya Bwana Yesu Kristo, na upendo wa Mungu Baba, na Ushirika wa Roho Mtakatifu viwe nanyi nyote” (2 Kor 13:13).
Mafiga mawili hayawezi kukiivisha chungu; lazima yawe matatu. Tutakapo kufanikiwa lazima tuwe tayari kushirikiana na wenzentu.  Nafsi tatu za Utatu Mtakatifu zinashirikiana. 
Jumapili ya leo wakatoliki kote duniani wanasherehekea Sherehe ya Utatu Mtakatifu. Inahusu imani kuwa Mungu ni mmoja katika nafsi tatu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Ni kama mafiga matatu. Wakatoliki hubatizwa kwa jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu (Mt 28: 19) na wala sio kwa majina ya Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.  Katika kufanikisha mambo kuna nguvu ya wingi au nguvu ya namba. Tunaona nguvu ya wingi katika uumbaji. “Mungu akasema: Tumfanye mtu kwa mfano wetu, afanane nasi” (Mwanzo 1:26). Ni Utatu  Mtakatifu uliosema “tumfanye mtu,” katika kitabu cha Mwanzo.  Ili kufanikiwa lazima kufikiria katika msingi wa “sisi.”  Nafsi tatu zinafikiria katika msingi wa sisi. Nakubaliana na Ralph Chaplain Yusufu aliyesema: “Hauwezi ukawa na usalama, hata ukijaribu namna gani; kama haufikiri kwa msingi wa “sisi” badala ya mimi.” Lorii Myers alikuwa na mawazo hayo aliposema: “Sisi ni sawa na nguvu.”
 Tunahitaji nguvu ya Utatu Mtakatifu tufanikiwe ambayo inaelezwa na mtume Paulo: “Neema ya Bwana Yesu Kristo, na upendo wa Mungu Baba, na Ushirika wa Roho Mtakatifu viwe nanyi nyote” (2 Kor 13:13).
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo:  Bwana wetu Yesu Kristo anatoa neema  hata kwa wahalifu.” Ukweli kuwa neema hutolewa hata kwa waalifu ni ukweli ambao tunauona msalabani. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo ilitolewa kwa mwizi Dismasi. Tunahitaji neema ili kufanikiwa. Neema ya Bwana Yesu inaonjeka. Ili kuonja neema ya Bwana wetu Yesu lazima kushirikiana nayo. Kuna ambaye alitaka kushinda bahati nasibu ya Kampuni ya Simu ya Tigo. Kila mara aliomba kushinda. Alisali kwa Bwana wetu Yesu Kristu. Usiku alitokewa katika ndoto. Yesu alimwambia: nataka ushinde lakini nunua vocha. Alitaka naye atoe mchango wake. Ni lazima kushirikiana na neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.
Upendo wa Mungu Baba: Kilichojaa hufurika. Ni methali ya Watanzania. Mungu Baba amejaa upendo na unafurika. Tunakiri upendo huu kwa sala ya shangwe “Abba! Baba! (Warumi 8:15.  Upendo wa Mungu Baba unajieleza katika kumtuma Mwana wake wa Pekee. “Kwa maana  jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amsadikiye asipotee, bali awe na uzima wa milele (Yn 3:16). Haya  hii ni  “Injili katika mfano mdogo.” Kutoa ni matokeo ya upendo. Unaweza kupenda bila kutoa. Lakini hauwezi kupenda bila kutoa.
Ushirika wa Roho Mtakatifu: Somo la pili lionaongelea ushirika huu: “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu” (   Warumi 8:16     ). Kama hewa ilivyo kwa mwili wa binadamu ndivyo Roho Mtakatifu alivyo katika maisha ya kiroho. Anatutia ujasiri. Roho Mtakatifu yupo nyuma ya pazia anafanya mambo. Anaunganisha pointi, matukio anapanga kalenda. Omba kuwa na ushirika naye. Tutumie mafiga haya matatu: Neema, Upendo na Ushirika. Tunahuitaji Utatu Mtakatifu. Tuuiige. Tujifunze kufanya mambo kwa pamoja. “Sala usafiri kwa haraka tunaposali pamoja.” Ni methali ya Kilatini
Sala: Ee Bwana wetu Yesu nisaidie niige Utatu Mtakatifu katika kushirikiana na wengine.  Amina.

Wednesday, May 10, 2017

KATIKA SHIDA NA RAHA, JARIBU KUSHUKURU



TAFAKARI 11/5/2017

(K)“ Watu na wakushukuru, Ee Mungu. Watu wote na wakushukuru” (Zab 67:5)

Wakati wa raha jaribu kushukuru. Zab 67 iliimbwa katika sikukuu ya shukrani baada ya mavuno (Kut23:24). Wakati wa shida jaribu kushukuru. Katika shida Ayubu alimsifu Mungu: “Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana litukuzwe” (Ayubu 1:21). Kusifu ni kushukuru. Maneno “watu wote” yanabainisha wenye raha na wenye shida, wenye nacho na wasio nacho, wagonjwa na wenye afya, walala hai na walalahoi, walalaheri na hohehahe, wanaoteseka na wanaofurahi.  Watu Wote wamshukuru Mungu. Hata unapokosewa unajifunza kitu fulani, shukuru. “Msamaha wa kweli ni pale unapoweza kusema, ‘Nashukuru kwa uzoefu huo,’” alisema Oprah Winfret. Biblia inatwaambia: “Shukuruni katika kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu” (1 Wathesalonike 5: 18). Rick Warren katika kitabu chake Maisha Yanayoongozwa na Malengo alikuwa na haya ya kusema juu ya aya hiyo: “Mungu anakutaka umshukuru kwamba atatumia matatizo yako kutimiza malengo yake.”  Kutoshukuru ni kosa kubwa kuzidi kulipa kisasi. “Kutoshukuru ni kosa la kudharauliwa zaidi ya kulipa kisasi, ambacho ni kulipa baya kwa baya, wakati kutoshukuru ni kulipa baya kwa wema,” alisema William Jordan. Tujenge utamaduni wa kushukuru. Tanzania yenye utamaduni wa kushukuru inawezekana.

Mungu anapotoa hapimi kwa kijiko. Tusimbanie shukrani. Waluhya wana methali isemayo, “Nyama choma haiwezi kuwa tamu ukamsahau aliyeichoma.” Maisha yana baraka, usimsahau anayeleta baraka-Mwenyezi Mungu. Yesu alipoomba kulisha wanaume 5,000 wanaojua kula chakula Mungu Baba alimwongezea kuliko alivyokuwa ameomba wakakusanya mabaki vikapu kumi na viwili. Bikira Maria alipoomba na kusema: Hawana divai. Haikupatikana bora divai bali divai bora-grade one. Mfalme Solomoni aliomba hekima, Mungu akamwongezea na mali. Yosefu aliomba kukumbukwa. Alikumbukwa na zaidi alifanywa Waziri Mkuu. Huu ni mlipuko wa baraka. Kuna mzee fulani aliyekuwa hakosi kuhudhuria adhimisho la Misa. Jumapili moja alihamua kupanga matumizi yake. Aliweka shilingi elfu moja kwenye mfuko wa suruali kwa ajili ya kutoa sadaka na shilingi 10,000/= aliziweka kwenye mfuko wa shati kwa ajili ya matumizi madogo ya nyumbani. Wakati wa kutoa sadaka alitoa noti kwenye mfuko wa shati bila kuitazama. Baadaye alienda dukani kununua sukari na mchele. Baada ya kufunguwa bidhaa hiyo alipoingiza mkono wake kwenye mifuko alipata shilingi 1,000/=. Aimwomba samahani muuza dukani. Kwa kusononokea alienda nyumbani. Baada ya dakika tano akiwa nyumbani alikuja mtu aliyemletea pesa hili kumaliza deni lake la zamani laki tano. Mungu anapotoa hapimi kwa kilo. Kuna namna nyingi za kuwashukuru unaokaa nao.

Kushukuru ni kuomba tena. “Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu” (Filp 4:6).  Kushukuru ni kufanya haja zako zijulikane na Mungu. “Shukrani ni moyo wa kutegemea kupata misaada siku za baadaye” (Sir Robert Walpole). “Hakuna kazi ambayo inahitaji kufanyika haraka kama kutoa shukrani” (Mt. Ambrose). Tusishukuru kwa namna ya kuomba miujiza ya ajabu. Kuna mtoto aliyefanya mtihani wa darasa la saba. Usiku wakati wa sala za usiku alisikika akisema: “Mungu nakushukuru ulivyonisaidia kujibu maswali naomba Mwanza ugeuke kuwa Mji Mkuu wa Tanzania.” Kushukuru si kuomba kwa namna hiyo.

Kushukuru ni kuthamini. Mthamini mwenzako. Mungu wetu ni Mungu anayethamini. “Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda” (Isaya 43:4). Wathamini watoto. Maua ya kesho yako kwenye mbegu za leo. Kuna mwalimu mmoja kila wanafunzi walipoingia darasani alisimama mlangoni akimwinamia kila mwanafunzi alipoulizwa kwa nini anafanya hivyo, alisema sijui hawa woto watakuwa wakina nani? Viongozi wangu wa kesho. Aliwathamini si jinsi walivyo tu bali watakavyokuwa. Mwanamke mmoja alimuuliza mke wake: “Mbona kila mara ninapoimba unatoa kichwa dirishani?” Mwanamke akasema: “Nataka majirani wajue kuwa anayeimba vibaya sio mimi.”

Sala: Ee Yesu nisaidie kushukuru katika shida na raha, katika magonjwa na afya, wakati wa vigelegele na wakati wa kelele. Amina.

Monday, May 8, 2017

WAKIWA NA MASHAKA NA UKRISTO WAKO, WEMA NA KAZI ZAKO VIKUSHUHUDIE


“Huko Antiokia, ndiko kwa mara ya kwanza, wafuasi waliitwa Wakristo” (Matendo 11:26)

“Kama tungetenda kama wakristo kweli, pansigekuwepo na watu ambao si wakristo,” alisema Mt. Papa Yohane XXII.  Ni katika mtazamo huo huo, Soame Jenyns alisema: “Kama nchi za kikristo zingekuwa nchi za kikristo, pasingekuwepo na vita.”  Kama ungekamatwa kwa kuwa mkristo, je pangekuwepo na ushahidi wa kutosha wa kukutia hatiani? Je, kuna ushahidi gani wa kuwa wewe ni mkristo. Mkristo kama mshumaa lazima atulie wakati huo huo anawaka mapendo. Mkristo anaonesha ukristo. Ukristo: “Ni wema nyumbani. Katika biashara ni ukweli. Katika jamii ni adabu. Kazini ni kutenda haki. Kwa wenye shida ni huruma. Ni msaada kwa wadhaifu. Upinzani dhidi ya waovu. Ni imani kwa wenye nguvu za kimaadili. Ni ‘msamaha’ kwa wakosefu. Ni furaha kwa waliofanikiwa. Ni uchaji na imani kwa Mungu,” alisema mtu fulani. Ukristo ni kuwa mkristo pale ulipo. Usipokuwa mkristo pale ulipo huwezi kuwa mkristo popote. Wanafunzi walioitwa wakristo walikuwa kwanza wakristo Antiokia.

Mtoto wa miaka minne alimuuliza mama yake: “Hivi mama Yesu unayenielezea habari zake kira mara ni mwema kama wewe? Mama alimjibu: “ Yesu ni mwema sana mimi najitahidi kumuiga.” Mtoto alijibu: “Kama ni hivyo nitampenda.” Wema ni sifa ya kuwa mkristo. Tunaambiwa juu ya mkristo Barnaba: “Barnaba alikuwa mtu mwema na mwenye kujaa Roho Mtakatifu na imani. Kundi kubwa la watu lilivutwa kwa Bwana” (Matendo 11:24).

Sifa nyingine ya mkristo ni kuwatia wengine moyo. Barnaba maana yake mwana wa kutia moyo. Alimtia moyo Paulo. Mtu akinunua pikipiki mtie moyo. Usiseme, “Inafanana na yangu.” Ukaishia hapo. Mtu akinunua nguo nzuri mpongeze. Usiseme, “Nilinunua kama hii mwaka 1970.” Mwanafunzi anayepata maksi za chini, mtie moyo. Dante Gabriel Rossetti mshairi na mchoraji maarufu wa karne ya 19 alitembelewa na mzee fulani. Mzee huyo alikuwa amebeba picha na michoro mbali mbali ambazo alitaka zihakikiwe ili kujua kama ni mizuri. Rossetti alizitazama kwa makini sana. Baada ya kuziangalia chache alisema ukweli kuwa michoro si mizuri. Mgeni huyo alisikitika sana. Alitoa michoro mingine na kumwambia kuwa imechorwa na kijana mwanafunzi. Rosseti alizitazama na kuchangamka na kuwa na furaha na kusema, “Michoro hii ni mizuri. Kijana huyo aliyezichora ana kipaji kikubwa. Apewe kila msaada na kutiwa moyo katika wito wake wa kuwa mchoraji. Kijana huyo ni nani? Ni mtoto wako?” Mzee alijibu. “Siyo mtoto wangu ila ni mimi miaka arobaini iliyopita. Kama miaka hiyo ningesikia maneno mazuri kama haya ningekuwa mchoraji mzuri sana. Hata kama watu hawakutii moyo jitie moyo. Kuna mwanafunzi ambaye alikuwa hapendwi na wenzake. Aliitwa Siima. Hata walimtania kuwa hata kivuli chake hakimpendeki hakiko tayari kumfuata. Siku moja alikuwa anaadhimisha Siku yake ya Kuzaliwa. Alijua kuwa hakuna atakayemwandikia kadi ya pongezi. Alifanya kitu fulani. Wenzake walipokuja kumtembelea na kumkejeli walikuta kadi kumi na mbili. Walishangaa. Walipozisoma zikuwa zote zinatoka kwa mtu mmoja. Kutoka kwa Siima kwenda kwa Siima.

Kazi zako zikushuhudie. “Kazi ninazofanya mimi kwa jina la Baba yangu zinanishuhudia” (Yohane 10:25). Watu walikuwa wamemuuliza Yesu kama ndiye Kristo. Kazi zake za huruma zilimshuhudia. Wewe kama ni mkristo kazi zako zikushuhudie. Matendo ya huruma yakushuhudie. Wewe kama ni daktari wa binadamu, kazi zako zikushuhudie. Wewe kama ni mwalimu kazi zako zikushuhudie. Wewe kama ni mwanasiasa kazi zako zikushuhudie. Pilato alipoambiwa kuwa kuna watu wanasema anaimba vibaya. Alijibu, “Nitafanya mazoezi na kuimba vizuri hakuna atakayewaamini.” Kazi zako zifanye watu wasiamini mabaya yanayosemwa juu yako. Kuna watu waliosema  vibaya juu ya Bwana Yesu alipokuja anakula na kunywa tofauti na Yohane Mbatizaji lakini kazi zake nzuri zilimshuhudia.

Sala: Ee Bwana Yesu nisaidie niwe mkristo kweli, niwe sauti ambayo kwayo utazungumza,niwe moyo ambao kwao utapenda, niwe mikono ambayo kwayo utasaidia. Amina.

 

JIPROGRAMU NA MWACHE MUNGU AKUPROGRAMU



TAFAKARI 8/5/2017

“Nalikuwa katika mji wa Yafa nikiomba, roho yangu ikazimia, nikaona maono” (Matendo 11: 5)

Usipojipogramu watu wabaya watakuprogramu. Mungu asipokuprogramu watu wabaya wanaweza kukuprogramu. Mungu alimprogramu Simoni Petro kupitia ndoto au maono. “Jambo hili lilitendekea mara tatu” (Matendo 10:16). Mungu anatuprogramu mara nyingi. Mungu alitaka Petro abadili mtazamo wake: Kutoka Mungu wa Israeli kwenda Mungu wa mataifa yote. Kutoka kukumbatia waliotahiriwa kwenda kwenye kukumbatia wasiotahiriwa. Kutoka kula nyama ya wanyama walio safi hadi kula nyama ya wanyama najisi kama nguruwe.  Huenda Mungu atakuletea maono kama Petro lakini unaweza kupiga picha kichwani ya mambo mazuri. Unaweza kujiprogramu.

Kuna kitendawili kisemacho: “Nimelala usiku natazama filamu.” Jibu ni ndoto. Hatuna budi kuwa na filamu ya maisha tunayoyataka akilini mwetu.  “Ni muda muafaka wa kuishi maisha ambayo umeyafikiria,” alisema Henry James. Fikiria utakapokuwa kesho. “ Tuko tulivyo na tulipo kwa sababu kwanza tulipafikiria,” Donald Curtis. Kuna mambo kadhaa ya kuzingatia.

Kuwa na picha akilini. Unataka kununua gari, kuwa na picha ya gari hilo akilini. Unataka kuoa, kuwa na picha ya arusi akilini mwako. Unataka kujenga nyumba, kuwa na picha akilini mwako ya nyumba unayoipenda.  “Roho haiwezi kufikiri bila picha,” alisema Aristotle. Tunaweza kusema mtu hawezi kufikiri bila picha. Naye John Holland alisema, “Roho haiwezi kuzungumza bila picha.” Mtu hawezi kuzungumzia mipango yake bila picha. Ukizungumzia duka unalotaka kulianzisha kuwa na picha. Ukizungumzia taasisi unayotaka kujenga kuwa na picha akilini mwako.“ Badili sura za picha kwenye kichwa chako ziendane na maono kwenye moyo wako,” alisema mtu fulani. “Piga picha ya kitu unachokitaka akilini, kione, kihisi, kiamini. Fanya picha ya kitu hicho kichwani mwako, na anza kukijenga,” alisema Robert Collier. “Kupiga picha akilini ni kuona lile ambalo halipo, ambalo halionekani – ndoto.  Kupiga picha akilini kusema kweli na kutengeneza uongo unaonekana. Uongo unaonekana, hata hivyo una namna ya kuwa ukweli wa mambo,” alisema Peter McWilliams.

Fikiri kama kwamba unachokitaka kipo.  “Kuleta jambo katika maisha yako, fikiria kama kwamba tayari lipo,” alisema Richard Bach. Yapigie msitari maneno “kama kwamba” ni maneno muhimu. “Umba maono ya unayetaka kuwa na baadaye ishi katika picha hiyo kama kwamba ni kweli,” alisema Arnold Schwarzenegger.  Ishi kama kwamba lisilowezekana linawezekana. “Watu wa kawaida huamini tu katika linalowezekana. Watu wasio wa kawaida hupiga picha si ya lile ambalo linawezekana au linayamkinika bali lile ambalo haliwezekani. Na kwa kupiga picha ya lile lisilowezekana wanaanza kuliona kama linalowezekana,” alisema Cherie Carter-Scott.

Badili unachokiona. “Toa mawazo yako, maneno yako na macho kwenye mambo yalivyo, na yaweke tu kwenye namna ambavyo unataka mambo yawe,” alisema  Che Garman.  “Mtu anaweza kupokea lile ambalo anaona anapokea,” alisema Florence Scovel Shinn. “Lazima uone kitu vizuri akilini kabla ya kukifanya,” Alex Morrison.

Kuna faida nyingi za kuwa na picha ya unachokitaka akilini.  Kwanza, picha ya unachokitaka inakupa matumaini. “Ukiwa na maono kwa ajili ya maisha yako hilo linakuwezesha kuishi kwa matumaini badala ya hofu zako,” alisema Stedman Graham. Pili, ni kupiga hatua kimaendeleo.  Hatua ya kimaendeleo inategemea upeo wako ulivyo. Upeo wako ukiwa chini hutabaki chini. Upeo wako ukiwa juu utakuwa juu kweli. “Mtu anaweza kukua kiasi ambacho upeo wake unamruhusu,” alisema John Powell. Watu wenye upeo wa juu sana si wa kawaida. Tatu, kunasaidia kufanikiwa.  Ukweli huu unabainishiwa na methali ya kichina: “Dunia ni ya wale ambao wanavuka madaraja mengi katika kufikia kwao kabla ya wengine hawajaona hata daraja moja.” Nne, kupiga picha akilini kunasisimua, na kuleta ari mpya. “Kila dakika, kila saa, piga picha kichwani namna unavyotaka uwe. Sisimukia WEWE mpya,” alisema, Thomas D Willhite. Picha akilini ni kichocheo cha kutenda. "Picha inazaa shauku. Unakusudia lile ambalo umelipigia picha ya akilini,” alisema J. G. Gallimore. “Naota kwa hiyo nakuwa hivyo,” Cheryl Grossman.

Saturday, May 6, 2017

UMENISHAWISHI NAMI NIMESHAWISHIKA

 
                                JUMAPILI YA 4 YA PASAKA
“Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kasha wawe nao tele” (Yohana 10:10).
 Yesu Mchungaji Mwema amekufia endelea kushawishika kumfuata. Yesu kama mchungaji mwema anakujua kwa jina endelea kushawishika kumfuata.  Katika tafakari ya leo tutatumia maneno ya nabii Yeremia: “Ee Bwana umenishawishi nami nimeshawishika” (Yeremia 20:7). Kuna mambo yanayowashawishi watu wamfuate Yesu mchungaji mwema. Katika wito wowote kuna ushawishi na kushawishika.  Katika wito uliomo muombe Bwana Yesu akusaidie kuendelea kushawishika kudumu isije ikasemwa, tulipiga ngoma haukucheza, tuliomboleza haukulia.
  1. UPENDO UPEO
    Upendo upeo ni upendo katika kiwango cha mwisho cha upendo. Ni upendo wa mtu kumfia mwingine. Upendo upeo unaelezwa hivi: “Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo” (Yohana 10:11). Katika Injili ya leo upendo upeo unaelewa hivi: “Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kasha wawe nao tele” (Yohana 10:10). Upendo upeo wa Yesu unashawishi na tunashawishika. Unatuvuta na tunavutiwa. Kuvuta ni kuleta mvuto. Msalaba unatuvuta kwa Yesu. Nakubaliana na John R.W.Stott aliyesema, “Msalaba ni moto uwakao ambapo moto wa upendo wetu unawashwa, na hatuna budi kukaribia sana ili cheche zake zitufikie.” Kama mchungaji mwema atoavyo uhai wake kwa ajili ya kondoo Yesu alitufia msalabani. Upendo wa namna hii unavuta. Yeye alisema: “Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu” (Yohana 12: 32). Pale pale msalabani kilimvuta askari Yule aliyemchoma Yesu mkuki akawa Mtakatifu Longinus. Longinus maana yake mkuki. “Basi Yule akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la nchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu” (Mathayo 27: 54). Kifo cha Yesu msalabani kiliwavuta akida na wale aliokuwa pamoja naye. Kifo cha Yesu msalabani kinatosha kwa wote kutukomboa lakini umuhimu wake ni kwa wale tu ambao wanakubali zawadi yake hii. Yaani wale wanaovutiwa au kushawishika. Wahaya wa Tanzania wana methali isemayo: Kitu kisichojitingisha ni jiwe. Kifo cha Yesu msalabani kina ushawishi.
    Upendo upeo unadai upendo kwa jirani. Diogenes alikuwa amesimama kwenye kona mtaani siku moja huku akicheka kama mwehu. “ Jambo gani linakufanya ucheke ?” Mpita njia alimuuliza. Unaona jiwe hilo katikati ya njia? Tangia nije hapa asubuhi watu wamekuwa wakijikwaa na kulaani jiwe. Lakini hakuna aliyejisumbua kulitoa ili wengine wasijikwae. Yesu kwa kuwa ni mchungaji ambaye si mtu wa mshahara ametuondolea vikwazo njiani, huu ni upendo upeo.    
  2. JINA KUBWA
    Jina la Yesu ni Jina Kubwa. Kwa kawaida jina huvuta watu. Watunzi mashuhuri wa vitabu huwa hawatangulizi jina la kitabu au kichwa cha kitabu bali jina lao linaandikwa kwa herufi kubwa kuzidi kichwa cha kitabu sababu jina tu linavuta ni “brand.” Watu huwa wanatafuta jina la mtunzi mashuhuri hata bila kujali ameandika nini. Jina la Yesu ni “brand.”  Petro anatwaambia “Jueni ninyi nyote na watu wote  wa Israeli ya kuwa  kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye  ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu…wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina lingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo!” (Mate 4:10-12). Petro alikua anajibu swali hili: “Kwa nguvu gani na kwa jina la nani ninyi mmefanya haya?” (Mate 4:7). Rais wa nchi akiingia hapa tulipo tutasimama kumpa heshima. Lakini Yesu Kristo akiingia hapa tulipo tutapiga magoti kumwabudu. YESU KRISTO ni JINA KUBWA.  Fanya urafiki naye. YESU TOSHA
  3. AHADI ZA KWELI
    Mungu akiahidi anatenda. Mungu akiahidi atafanya. Yesu alihaidi kuwa atafufuka na kweli alifufuka kama Petro anavyotwaambia katika somo la leo: “…ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu” (Mate 4: 10). Ahadi za kweli zinashawishi. Yesu ametushawishi nasi tumeshawishika. Yesu hatoi ahadi hewa. Watu wanavutwa na ahadi za kweli. Kuna aliyeshinda nishani huko Ulaya na kupewa hati ya kusafiri bure kwenye treni kwa kipindi cha miaka kumi. Alitembea amevaa hati ndogo ya kusafiri bure ikininginia shingoni hata siku moja hakusafiri kwa kutumia treni. Mungu ametupa ahadi nzuri. Ametupa kama hati za kusafiri bure. Je tunatumia ahadi za Mungu. Je tunachukua ahadi hizo. Mungu akiahidi anatenda. Yesu akiahidi anatenda. Yesu anashawishi kwa ahadi za kweli. 
    Sala: Ee Bwana wetu Yesu Kristo, nisaidie nishawishike kukufuata kila mara isije ikasemwa, tulipiga ngoma haukucheza, tuliomboleza haukulia. Amina.

Saturday, April 22, 2017

JE VIDONDA VYAKO NI VIDONDA VYA HURUMA?


  JUMAPILI YA HURUMA YA MUNGU (JUMAPILI YA 2 YA PASAKA)

“Tia kidole chako humu, tazama mikono yangu, lete mkono wako na kuutia katika ubavu wangu na usikose imani” (Yohane 20: 27)

“Bwana anatuonesha kupitia Injili, vidonda vyake. Ni vidonda vya huruma. Ni kweli; vidonda vya Yesu ni vidonda vya huruma,” alisema Papa Francis katika mahubiri yake Jumapili ya Huruma ya Mungu mwaka 2015. Yesu alipofuka vidonda vitano vilikuwa ni utambulisho wake. Yesu aliwaonesha mitume wake mikono yake na ubavu wake, walitambua kuwa ni yeye. “Yesu anatualika kutazama vidonda hivi, kuvigusa kama Thomasi alivyofanya, kuponya kutoamini kwetu. Licha ya hayo yote, anatualika kuingia kwenye fumbo la vidonda hivi, ambalo ni fumbo la upendo wake wa huruma,” alisema Papa Francis. Vidonda hivi vilibaki kama makovu si kumbukumbu ya ukatili kumbukumbu ya ukombozi. Yesu ametukomboa kwa huzuni na mateso. Utabiri wa nabii Isaya unasema ukweli wote, “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu…na kwa kupigwa kwake sisi tumepona” (Isaya 53:5). Yesu alibaki na makovu yake kama alama ya ushindi na utukufu. “Nikaona Mwanakondoo amesimama kati ya kiti cha enzi na wenye uhai wanne waliozungukwa na wazee. Alionekana kama amechinjwa” (Ufunuo 5:6). Kuonekana kama amechinjwa kunabainisha makovu yake makubwa matano. Tukiyatazama kwa miwani chanya ni makovu ya kushinda vita dhidi ya uovu. Tukiyatazama kwa miwani hasi ni makovu ya ukatili.

Wachimba migodi wana vidonda vya kubeba mizigo wana “taji la miiba”  na makuli na wabebaji mizigo. Wawindaji wana vidonda miguuni, vidonda vya huruma, wakitafuta riziki ya familia. Fundi seremala wana vidonda vya kuchomwa na misumari. Wakati wa kuandikisha watu kwenye daftari la kudumu la wapiga kura iligundulika kuwa katika jamii za wakulima na wapiga kokoto alama za vidoleni zilishatoweka sababu ya matendo ya huruma kutafuta riziki kwa ajili ya wanafamilia. Kuna makovu ya huruma kwenye viganja.  Mafundi wa magari vidole vyao vina makovu ya huruma wakitafuta riziki za wanafamilia. Wakati wa kuandikisha wapiga kura kwenye daftari ya kudumu, iligundulika tulivyosikia kwenye vyombo vya habari kuwa watu wengine alama za vidoleni zilikwishafutika sababu ya shughuli za kilimo. Hayo ni makovu ya huruma kwa nafsi zao na huruma kwa wanafamilia wakiwatafutia lishe bora. Kuna watawa na mapadre ambao wana makovu kwenye magoti sababu ya tendo la huruma la kuwaombea wazima na wafu.

Mama aliyejifungua kwa njia ya operesheni ana makovu ya huruma. Ni huruma kwake na ni huruma kwa mtoto. Siku moja kuna mtoto wa miaka kumi na miwili aliyekuwa anaogelea mtoni. Mamba akashika miguu yake kwa meno. Mama yake aliyekuwa karibu akashikilia mikono kwa nguvu zake zote, hata kucha zikatoboa mikono ya mtoto. Bahati nzuri palikuwepo na mwindaji karibu. Alimpiga huyo mamba risasi, mamba alimwachia mtoto. Mtoto alipokuwa anauguza majeraha aliyasifia majeraha aliyokuwa nayo mikononi ni majeraha aliyopata sababu ya huruma ya mama, aliyemshikilia mpaka kucha za mama zikatoboa sehemu za mikono yake.

Kuna vidonda ambavyo si vya huruma: kuchubuka kwa sababu ya ulevi, kuchubuka kwa sababu ya hasira. Siku moja huko Afrika ya Kusini Gandhiji alikuwa anasafiri kwenye treini daraja la kwanza kinyume cha sheria. Polisi mzungu alitaka kumwondoa toka daraja la kwanza Gandhiji. Lakini Gandhiji aliona si haki alikataa. Mambo yalipofikia hatua hii polisi alikasirika na kumpiga kwa teke. Akijizuia kumtukana Gandhiji alijibu: “Ndugu, umehumiza mguu wako?” Polisi aliposikia swali hilo aliona aibu. Kama mguu wa polisi ulihumia kwa kumpiga teke Gandhiji, hicho hakikuwa kidonda cha huruma.

 

Bwana wetu Yesu Kristo alipofufuka alikuwa na makovu ya vidonda vya mwilini bila shaka alikuwa na makovu ya vidonda vya moyoni. Tunajifunza kwake mtazamo chanya. Alifufuka na makovu kama ishara ya ushindi na si ishara ya ukatili. Huo ni mtazamo chanya. Kuwa na mtazamo chanya ni tiba ya vidonda vya moyoni.                

MILANGO ILIYOFUNGWA NI BARAKA YA HURUMA KATIKA SURA YA BALAA

                JUMAPILI YA HURUMA YA MUNGU (JUMAPILI YA 2 YA PASAKA)

“(Yesu), akasimama katikati, ingawa milango ya chumba walimokaa wafuasi ilikuwa imefungwa kwa kuwaogopa wayahudi” (Yohane 20: 19). 

 “Mungu anapokupa mwanzo mpya, unaanza na mwisho. Mshukuru kwa milango iliyofungwa. Mara nyingi  inatuelekeza kwenye milango sahihi!” alisema mwanamke wa imani. Mlango wa ualimu wa Baba wa Taifa Julius Kambarage Nyerere ulipofungwa ukamwelekeza kwenye mlango wa urais. Naye Joyce Meyer alikuwa na haya ya kusema, “Usimwombe Mungu tu kufungua milango, lakini pia muombe Mungu kufunga milango ambayo inahitaji kufungwa.” Mlango wa ualimu kwa Baba wa Taifa ulihitaji kufungwa. “Leo funga baadhi ya milango. Si kwa sababu ya majivuno, kutokuwa na uwezo, au ubabe, lakini ni kwa sababu tu haikupeleki popote,” alisema Paul Coelho. 

Kwa mtu anayeomba kazi mlango uliofungwa ni ishara ya kukataliwa au kucheleweshwa lakini inaweza kuwa baraka katika sura ya balaa. Kwa milango iliyofungwa kwa sababu ya woga inaweza kuwa baraka katika sura ya balaa. Yesu alipouawa Ijumaa Kuu wafuasi wake baadaye waliingia chumbani na kufunga milango ya chumba. Milango iliyofungwa iliwawezesha mitume kufaidi tendo la huruma la kufundisha wajinga.

Tunasoma katika Injili ya Yohane. “(Yesu), akasimama katikati, ingawa milango ya chumba walimokaa wafuasi ilikuwa imefungwa kwa kuwaogopa wayahudi” (Yohane 20: 19).  “Yesu alingoja mpaka wote wamekusanyika: na milango imefungwa, ili kuonesha kuwa namna alivyoingia kwenye chumba ndivyo alivyoweza kufufuka jiwe likiwa juu ya kaburi,” alisema Baba wa Kanisa Theophilo. Milango iliyofungwa ilisaidia kama nyenzo za kufundishia somo la ufufuko. Yesu alifufuka wakati jiwe liko juu. Liliviringishwa na malaika sio kwa sababu Yesu apite bali mitume na wanawake wafuasi wa Yesu waweze kushuhudia kuwa amefufuka.

Milango iliyofungwa ilimtenga Thomasi, hakuwa na mitume. Aliporudi na kuambiwa kuwa Bwana Yesu amewatokea hakuamini. “Kutoamini kwa Thomasi (Yoh 11:6; 14:5; 20:24.26-29; 21:2) kumeleta faida zaidi kwenye imani yetu kuliko imani ya wafuasi wengine. Anavyomshika Kristo na kusadikishwa, kila mashaka yanaondolewa na imani yetu inaimarishwa. Hivyo mfuasi aliyekuwa akitia mashaka, aligusa madonda ya Yesu na kugeuka kuwa shahidi wa ukweli wa ufufuko” (Mt Gregori Mkuu). Tukumbuke kuwa kufundisha ni tendo la huruma, na ni baraka. Ni kweli milango iliyofungwa ni baraka ya huruma katika sura ya balaa.

Tendo la Yesu kuingia kwenye chumba wakati milango imefungwa ni somo juu ya ubikira wa Bikira Maria, baada ya kumzaa Yesu Kristo, alibaki bikira. “Milango iliyofungwa haikuzuia mwili ambapo umungu ulikaa. Aliweza kuingia bila milango kuwa wazi, ambaye alizaliwa bila kuharibu ubikira wa mama yake,” alisema Mt. Augustini. Tukumbuke kuwa kufundisha ni tendo la huruma, na ni baraka. Ni kweli milango iliyofungwa ni baraka ya huruma katika sura ya balaa.

 

“Mlango mmoja unapofungwa mwingine unafunguliwa; lakini mara nyingi tunatazama kwa kujutia mlango uliofungwa na hatuoni mlango ambao umefunguliwa kwa ajili yetu,” alisema Alexander Graham Bell. Mwanzoni mtume Thomasi aliutazama sana mlango uliofungwa wa Yesu wa Ijumaa Kuu na kuchelewa kuuona mlango uliokuwa wazi wa Yesu Kristo wa Pasaka.

Soichiro Honda wakati alipoomba kupewa kazi katika Kampuni ya Toyota Motors, baada ya kusailiwa hakupewa kazi. Mlango ulikuwa umefungwa. Lakini alitazama mlango uliofunguliwa. Tatizo la kukosa kazi katika kampuni hiyo lilikuwa ni alama ya mkato na si nukta. Alianzisha kampuni yake mwenyewe na kuanza kutengeneza baisikeli zenye injini ndogo. Leo hii Honda ni kampuni kubwa ya kutengeneza pikipiki na magari. Soichiro Honda alisema: “Mafanikio yanawakilisha asilimia moja ya kazi yako ambayo inatokana na asilimia tisini na tisa zinazoitwa kushindwa.” Kifaranga kwenye yai kinapopambana na ukuta wa yai uliokizunguka kitoke ukikionea huruma ukakisaidia kutoka unakinyima nafasi adimu ya kujiimarisha.

Mlango uliofungwa ni baraka ya huruma katika sura ya balaa.  Lakini Yesu hauzuiliwi na milango iliyofungwa. Kuna methali ya Tanzania isemayo, “Baraka ni baridi hata uwe umefunga mlango inaingia.” Yesu naye anaingia kwenye milango iliyofungwa. Mlango wa kupata kazi kama umefungwa Yesu anaweza kukusaidia kuingia. Mlango wa kupata mchumba kama umefungwa Yesu anaweza kukusaidia kuingia. “Naamini , ukiendelea kuamini, ukiendelea kutumaini, ukiendelea kuwa na mtazamo sahihi, na kama una shukrani, utamuona Mungu anafungua milango mipya,” alisema Mchungaji Joel Osteen.

 

Counter

You are visitor since April'08